Waziri
Mkuu, Kassim Majaliwa akiwapungia wananchi wakati alipowasili katika
eneo la Karema wilayani Tanganyika kuweka jiwe la Msingi la ujenzi wa
Bandari, Julai 4, 2020. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu)
Waziri
Mkuu, Kassim Majaliwa akizungumza na wananchi baada ya kuweka jiwe la
msingi la ujenzi wa bandari ya Karema wilayani Tanganyika, Julai 4,
2020.
Waziri
Mkuu, Kassim Majaliwa ameiagiza Kampuni ya Xiamen Ongoing Construction
Group inayojenga Bandari ya Karema kwa gharama za zaidi ya sh. bilioni
47 ifanye kazi usiku na mchana na kukamilisha ujenzi huo kwa wakati ili
kuimarisha biashara kati ya Tanzania na Congo.
Pia,
Waziri Mkuu ametoa muda wa siku 21 kwa Mamlaka ya Bandari Tanzania
(TPA), Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), Idara ya Uhamiaji, Jeshi la
Polisi, Wizara ya Madini na wawe wameanza kutoa huduma katika eneo la
Ikola ili kuhudumia wageni wanaotoka Congo.
Alitoa
agizo hilo jana jioni (Jumamosi, Julai 04, 2020) baada ya kuweka jiwe
la msingi la ujenzi wa Bandari ya Karema inayojengwa kwenye ziwa
Tanganyika katika kata ya Karema wilayani Tanganyika, Katavi. Alisema
mkandarasi anatakiwa ahakikishe mradi huo unakamilika haraka.
Waziri
Mkuu alisema mradi huo unalenga kuongeza tija katika shughuli za
kibandari kwenye ukanda wa Ziwa Tanganyika ndani na nje ya nchi na
kwamba utaongeza fursa za kibiashara nchini na pia utakuwa chachu ya
kukuza uchumi pamoja na kuboresha huduma za usafiri kwa wananchi.
“Tumeamua
kujenga bandari hii ambayo itawezesha meli zaidi ya moja kupakia na
kushusha abiria na mizigo kwa wakati mmoja. Hii ni Serikali ya kuahidi
na kutekeleza na ni Serikali ya kusikia na kutenda na ndio maana halisi
ya falsafa ya Rais Dkt. John Pombe Magufuli ya Hapa Kazi Tu.”
Kwa
upande wake, Mwakilishi wa Mkurugenzi Mkuu wa TPA Mhandisi Dkt. Baraka
Mdima alisema mradi huo unahusisha ujenzi wa gati kubwa la kufungia meli
lenye urefu wa mita 150 pamoja na kingo ya kuzuia mawimbi makali,
uchimbaji wa kuongeza kina cha lango la kuingilia bandarini na sehemu ya
kugeuzia meli.
Alisema
eneo jinguine ni ujenzi wa miundombinu ya bandari ikiwemo mgahawa,
jengo la kupumzikia abiria, majengo ya ofisi, eneo la sakafu ngumu kwa
ajili ya kuhifadhia makasha pamoja na miundombinu ya Zimamoto na Tehama.
Mradi huo utazingatia ujumuishi wa Reli ya Kisasa (SGR).
“Mradi
unajengwa kwa miezi 24 na kukamilika kwa bandari ya kisasa ya Karema,
kutaboresha shughuli za kiuchumi katika mkoa wa Katavi na Tanzania kama
kusafirisha watu na bidhaa katika maeneo ya mwambao wa Ziwa Tanganyika
na nchi jirani za Congo, Burundi na Zambia.”
Kadhalika,
Waziri Mkuu alimuagiza Mkuu wa Mkoa wa Katavi, Juma Homera aendelee na
operesheni ya kuwasaka watu wote wanaomiliki silaha kinyume cha
sheria.“Watu wote wanaomiliki silaha bila ya kuwa na vibali watafuwe
popote walipo na wachukuliwe hatua za kisheria.”
Awali,
Waziri Mkuu alizungumzia upatikanaji wa umeme katika wilaya ya
Tanganyika, alisema Serikali ya Awamu ya Tano inayoongozwa na Rais Dkt.
John Pombe Magufuli imedhamiria kufikisha huduma ya umeme katika vijiji
vyote nchini, hivyo waendelee kuwa na subira.
“Rais
wetu Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli anataka kuona kila nyumba ya
Mtanzania inawaka umeme na amepunguza gharama za kuunganisha umeme
kutoka sh. 380,000 hadi sh. 27,000 ili kila mwananchi aweze kumudu
gharama hizo.”
Waziri
Mkuu aliongeza kuwa licha ya gharama za kuunganishiwa umeme kupunguzwa,
pia wananchi hatolazimika kulipia gharama za nguzo pamoja na gharama za
fomu za maombi ya kuunganishiwa umeme kwani tayari zimeshalipiwa na
Serikali.
No comments:
Post a Comment