Umoja wa waalimu wa Hedhi Salama kwa shule za msingi
mkoani Rukwa wamepania kuhakikisha wanapunguza fikra potofu kuhusu suala la
hedhi kwa wasichana wanaovunja ungo pamoja na kukomesha utoro kwa wananfunzi wa
kike wanaoona aibu kuhudhuria shule pindi wanapopata hedhi kwa kutoa elimu
sahihi ya suala la hedhi mashuleni.
Azma hiyo imekuja baada ya waalimu hao kupewa mafunzo
yanayohusu namna ya kutengeneza pedi kwa kutumia aina mbalimbali za vitambaa
pamoja na kukabiliana na wanafunzi wanaoona aibu ama fedheha pindi wanapopata
hedhi wakiwa shuleni na hivyo kuwarahisishia Maisha yao wanapokuwa shuleni huku
wakiwahamasisha kuendelea kuhudhuria shuleni ili wasiachwe nyuma kimasomo.
Aida Mwanauta
ni mwalimu wa Hedhi Salama kutoka Shule ya Msingi Ilambila, Wilayani Kalambo, aliishukuru
serikali kwa kuwapatia mafunzo hayo muhimu kwani changamoto wanazokumbana nazo
ni nyingi na mafunzo hayo yamamsaidia kujua namna ya kuwasaidia wasichana hao
pindi wanapokuwa katika hedhi kutokana na wanafunzi wengi kutokuwa na ufahamu
wa kutosha juu ya namna ya kukabilina na hali hiyo.
Baadhi ya Waalimu kutoka halmashauri ya wilaya ya Kalambo wakionesha
vyeti vyao baada ya kupatiwa mafunzo ya Hedhi Salama wakiwa katika
picha ya pamoja na Mratibu wa Mradi wa SWASH Mkoa Matinda Mwinuka
(aliyechuchumaa kushoto) na Mwezeshaji Jesca Lwiza (aliyechuchumaa
kulia)
“Kuna mwanafunzi anakuja shuleni hajui ni namna gani anaweza
akajistiri, mwingine anatoka nje anakimbia, huko nje anachukua hata makaratasi,
majani kwaajili ya kujistiri ambayo inaweza ikamletea matatizo baadaye, kwahiyo
katika semina hii tumejifunza mambo mbalimbali, tumejua ni mambo gani ambayo
unaweza ukamfundisha mtoto, akajua jinsi ya kujihifadhi akiwa shuleni na
hatimae akawa anasoma na asiwe mtoro shuleni, na kujiona ni sawa na wengine,”
Alisema.
Nae, Mwalimu Victoria Tanganyika alisema kuwa mafunzo
hayo yamemsaidia kujua vifaa vinavyotumika kutengeneza pedi za kike na namna ya
kuvitekeza pamoja na kujua mazungumzo anayotakiwa kufanya na matoto ili kumshawishi
aweze kujiamini na kushiriki katika
michezo na masomo katika mazingira ya shule.
Kwa upande wake Mwalimu Clifonsia Remidio ameiomba
serikali kuendelea kutumia njia mbalimbali za vipeperushi na kutoa semina kwa
waalimu wengi zaidi wanaotoa huduma ya hedhi salama mashuleni ili kuweza
kuwasaidia wanafunzi wa kike ambao wamekuwa wakipata tabu kusoma wanapokuwa
katika kipindi cha hedhi.
“kuna vitu vingi tulikuwa hatuvifahamu, kuna wakati
mwingine hata kama mimi mwalimu nimeshasoma lakini bado nitaona aibu kuenenda
kumuelekeza yule mwanafunzi, lakini ameshatuelekeza mwezeshaji tumepata mwanga
mzuri pia nimefurahi kwasababu hili suala linashirikisha pande zote mbili,
upande wa waalimu wa kiume na upande wa waalimu wa kike pia kwamba tuwasaidie Watoto
wanaposikia ile hali ya mabadiliko ya mwili,”Alisema.
Aidha, Mwezeshaji wa mafunzo hayo ya Hedhi Salama, Mwalimu
Jesca Lwiza alisema kuwa mafunzo hayo yanalenga kutoa elimu ya hedhi salama kwa
wanafunzi ili kupunguza utoro mashuleni na kuongeza kuwa wanategemea kuona
mabadiliko makubwa ya mahudhurio shule kwa shule ambazo waalimu wake wamehudhuria
mafunzo hayo.
“Kuna ukimya ambao upo katika masuala ya hedhi salama,
wanafunzi wanakosa elimu sahihi, lakini pia wanakosa namna ya kujiamini
wanapokuwa katika masomo na wakati mwingine shuleni hakuna vyumba maalum vya
kujihifadhi wanapokuwa katika hedhi, kwa kulitambua hilo tumeona serikali namna
ilivyoweza kuwezesha kwa kuwapa mafunzo waalimu lakini imeweza kuboresha miundombinu
iliyopo mashuleni kwa kuweka vyumba hivyo,” Alisema.
Wakati akifungua mafunzo hayo Kaimu Katibu Tawala Mkoa
wa Rukwa Winnie Kijazi alisisitiza kuwa tafiti zilizofanyika zimeonesha kuwa
wasichana wengi hawana taarifa za awali kuhusu hedhi za pia walipata hedhi ya
kwanza pasipo kuwa na uelewa wa kutosha kuhusu mabadiliko ya miili yao hivyo
mafunzo hayo yamelenga kuwajengea uwezo waalimu kufikisha elimu katika shule.
“Tafiti
zinaonesha kuwa bado kuna fikra zisizo sahihi kuhusu masuala ya hedhi hususani
miiko na unyanyapaa inayosababisha wasichana na wanawake kushindwa kushiriki
kikamilifu katika shughuli za maendeleo na kijamii na wanafunzi wa kike kukosa
baadhi ya siku za masomo na wengine kuacha shule wanapokuwa kwenye hedhi.
Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania kwa kulitambua hilo imeweka jitihada kuhakikisha kuwa fursa za elimu
zinapatikana kwa makundi yote,” Alieleza.
Halikadhalika mratibu wa mradi wa School
Water Sanitation and Hygiene (SWASH) Mwalimu Matinda Mwinuka aliwaasa waalimu
kuhakikisha shule zinakuwa na vyombo maalum kwaajili ya walemavu pamoja na
vyumba kwaajili ya wasichana kubadili pedi za hedhi pindi wanapokuwa katika
hali hiyo nasio kutumia vyoo vya kawaida ambavyo havina mazingira mazuri ya kubadilishia
vifaa vyao.
“Kuna shule moja fundi kaweka shule
maalum, anasema kuwa kile ndio chumba maalum, walemavu wataingia humo humo,
hedhi salama wataingia humo humo, ametoboa tundu na kuweka ‘pipe’ anasema Watoto
wa kike wakishaingia humu ndimo watatumbukiza vile vitu vyao yaani ni vitu vya
ajabu kwakweli.”
Mradi huo unatekelezwa katika
halmashauri tatu za Mkoa wa Rukwa kwa muda wa miaka minne huku kwa mwaka wa
fedha 2019/2020 Mkoa ulipewa kiasi cha Shilingi 578,486,955.63/= kwaajili ya
utekelezaji wa mradi huo unaofadhiliwa na Benki ya Dunia na kutekelezwa katika
mikoa 17 na Halmashauri 86 za Tanzania Bara ukiwa na lengo la kuboresha mazingira
ya kufundishia, kujenga vyoo bora shuleni na kuweka miundombinu ya maji safi na
salama.