Katibu Mkuu wa Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano (Sekta ya Ujenzi), Arch. Elius Mwakalinga (WaKwanza kulia), akikagua barabara ya Rusumo- Lusahunga (KM 92), mkoani Kagera, alipofika mkoani humo kuangalia maendeleo yake.
Katibu
Mkuu wa Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Masiliano, anayeshughulikia Sekta
ya Ujenzi, Mbunifu Majengo, Elius Mwakalinga, ametoa siku Tatu kwa
Uongozi wa Wakala wa Barabara Tanzania (TANROADS) mkoa wa Kagera
kuhakikisha wanakamilisha ukarabati wa barabara ya Rusumo - Lusahunga
(KM 92) ambayo imekuwa kero kubwa kwa wasafirishaji wa mizigo ya ndani
na nje ya nchi.
Akizungumza wakati wa ukagauzi wa barabara hiyo, mkoani Kagera,
Mwakalinga, amemtaka Kaimu Meneja wa Mkoa huyo na wasaidizi wake
kuhakikisha wanafanya kazi usiku na mchana kuanzia leo ili kuruhusu
magari ambayo yameshindwa kupita kuendelea na safari zake kutokana na
ubovu wa barabara hiyo.
Katibu Mkuu wa Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano (Sekta ya Ujenzi), Arch. Elius Mwakalinga, akitoa maelekezo kwa Kaimu Meneja wa Wakala wa Barabara (TANROADS) Mkoa wa Kagera, Mhandisi Jackson Lwerengera, alipofika mkoani humo kukagua barabara ya Rusumo- Lusahunga (KM 92) ili kujionea maendeleo yake.
“Nadhani Meneja umenielewa, nataka ndani ya siku Tatu kama ulivyoahidi barabara hii iwe inapitika, na hakikisheni mnafanya kazi usiku na mchana kuanzia leo ili mkamilishe kazi hii”, amesema Mwakalinga.
Aidha, Mwakalinga ameongeza kuwa barabara hiyo inatakiwa kuwa yenye viwango bora kutokana na umuhimu wake katika uchumi wa nchi, na hivyo kumuelekeza Mkurugenzi wa barabara wa Sekta hiyo Mhandisi Hussein
Mativila, kuhakikisha wanatazama kwa jicho la pekee na kuzipa kipaumbele barabara zote ambazo zinaunganisha nchi yetu na nchi jirani.
Kaimu Meneja wa Wakala wa Barabara (TANROADS) Mkoa wa Kagera, Mhandisi Jackson Lwerengera, akifafanua jambo kwa Katibu Mkuu wa Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano (Sekta ya Ujenzi), Arch. Elius Mwakalinga (Kulia), alipofika mkoani humo kukagua barabara ya Rusumo- Lusahunga (KM 92) ili kujionea maendeleo yake.
Mwakalinga, amefafanua kuwa barabara hiyo imetengewa kiasi cha shilingi Bilioni 12.5 ambazo ni kwa ajili ya kuwekewa lami ambapo kwa kuanza ameelekeza utekelezaji wa fedha hizo uanze kwa kurekebisha vipande vilivyoharibika sana.
Kwa upande wake Kaimu Meneja wa (TANROADS) Mkoa wa Kagera, Mhandisi Jackson Lwerengera, amemhakikishia Katibu Mkuu huyo kukamilisha ukarabati wa barabara hiyo ndani ya siku alizowaagiza.
Amesema kuwa TANROADS Mkoa huo ulitekeleza kazi za dharura chini ya matengenezo ya muda maalumu katika barabara hiyo ambapo kilometa 6.7 kwa sehemu ya Kwanza na Kilometa 7.1 za sehemu ya pili zimekamilika.
Ukarabati wa barabara ya Rusumo- Lusahunga (KM 92) ukiendelea ambapo unatarajiwa kukamilika hivi karibuni.
Magari ya mizigo yakipita katika moja ya vipande vinavyokarabatiwa katika barabara ya Rusumo- Lusahunga (KM 92) ambapo ukarabati wake unatarajiwa kukamilika hivi karibuni.
PICHA NA WUUM
Mhandisi Lwerengera, ameeleza baadhi ya changamoto kuwa barabara hiyo
kuchelewa kufanyiwa matengenezo makubwa kutokana na ongezeko kubwa la
magari ambalo linahitaji tabaka la zege ya lami badala ya lami nyepesi
ambayo ndiyo iliyopo na inayotumika kwa marekebisho ya sasa.
Barabara hiyo ambayo ina historia ya miaka 35 tangu ilipojengwa
imekuwa ni kiungo kikubwa katika masuala ya kiuchumi kati ya nchi yetu
na nchi jirani za Rwanda, Burundi na Congo (DRC) kutokana na wafanya
biashara wengi kutumia barabara hiyo kusafirisha mizigo yao.
Imetolewa na Kitengo cha Mawasiliano Serikalini, Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano.
No comments:
Post a Comment