Matokeo chanyA+ online




Monday, August 3, 2020

WAZIRI KAIRUKI AHIMIZA MATUMIZI YA MITANDAO YA KIJAMII KUFIKISHA TAARIFA ZA FEDHA NA UCHUMI KWA WANANCHI

Na. Peter Haule na Farida Ramadhani, WFM, Simiyu

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia Uwekezaji, Mhe. Angellah Kairuki amehimiza kutumia lugha rahisi na mitandao ya kijamii kufikisha taarifa za masuala ya uchumi na fedha kwa wananchi.

Rai hiyo ameitoa alipotembelea Banda la Wizara ya Fedha na Mipango, katika Maonesho ya Nanenane Kitaifa yanayofanyika katika Viwanja vya Nyakabindi, Mkoani Simiyu.


Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia Uwekezaji, Mhe. Angellah Kairuki, akizungumza jambo na Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano Serikalini, Wizara ya Fedha na Mipango, Bw. Benny Mwaipaja, baada ya kutembelea Banda la Wizara ya Fedha na Mipango, katika Maonesho ya Nanenane yanayofanyika Kitaifa, viwanja vya Nyakabindi Mkoani Simiyu.


Mhe. Kairuki alisema kuwa ni vema Kampuni za simu za mikononi, tovuti na mitandao mingine ya kijamii ikatumika kupeleka toleo la Bajeti ya Wananchi kulingana na mahitaji husika ili kuwafikia wananchi wengi zaidi.

Pia ameitaka Mamlaka ya Udhibiti wa Manunuzi ya Umma (PPRA) kusimamia taasisi za umma kuhakikisha zinatoa fursa kwa makundi maalum kushiriki katika zabuni za umma kama ambavyo sheria ya ununuzi wa umma inavyoeleza.

Mamlaka ya Masoko ya Mitaji na Dhamana wametakiwa kuongeza kampuni zilizo jiorodhesha kwenye Soko la Hisa kutoka kampuni 27 ili idadi hiyo ilingane na idadi ya kampuni zilizosajiliwa kwenye Wakala wa Usajili wa Biashara na Leseni-BRELA, zinazofikia zaidi ya elfu nane ili sekta ya masoko ya mitaji na dhamana yawe chachu ya kukuza uchumi wa nchi.


Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia Uwekezaji, Mhe. Angellah Kairuki (kulia), akiangalia machapisho mbalimbali kuhusu Deni la Serikali, alipotembelea Banda la Wizara ya Fedha na Mipango, katika Maonesho ya Nanenane yanayofanyika Kitaifa, viwanja vya Nyakabindi Mkoani Simiyu.

Ameipongeza Wizara ya Fedha na Mipango kwa kazi nzuri ya kuandaa mipango ya kitaifa na usimamizi wa Sera za Bajeti na Fedha na kuwataka wataalam wa Wizara hiyo kuongeza juhudi zaidi ili kuiwezesha nchi kufanikisha malengo yake ya kuwahudumia wananchi wake.

Akimwongoza kutembelea Banda la Wizara ya Fedha na Mipango katika Viwanja vya Nyakabindi, Bariadi, mkoani Simiyu, Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano Serikalini wa Wizara hiyo, Bw. Benny Mwaipaja, alimweleza Waziri Mheshimiwa Angellah Kairuki, kwamba Wizara ya Fedha na Mipango inatambua mchango mkubwa unaotolewa na Sekta ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi katika kukuza pato la Taifa.


Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia Uwekezaji, Mhe. Angellah Kairuki, (kulia) akisoma chapisho la Bajeti ya Wananchi alipotembelea Banda la Wizara ya Fedha na Mipango, katika Maonesho ya Nanenane Kitaifa, viwanja vya Nyakabindi Mkoani Simiyu.

Aidha alisema kuwa Serikali kupitia Wizara ya Fedha na Mipango, imefuta kodi zenye kero zipatazo 105 katika sekta ya kilimo, mifugo na uvuvi ili kuongeza tija kwa wakulima na kuwawezesha kuzalisha mazao kwa wingi.

Aidha alisema kupitia taasisi zake za Wizara imetoa mchango mkubwa katika kukuza masuala ya ushirika na mikopo kwa wananchi ambapo amesema Taasisi yake ya Self Microfinance pekee, imewekeza zaidi ya shilingi bilioni 36.3 kwa vikundi vya wajasiliamali nchini kote.


Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano Serikalini, Mamlaka ya Udhibiti wa Manunuzi ya Umma (PPRA) Bw. Mcharo Mrutu (kulia) akielezea mchakato wa Zabuni za Umma wakati Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia Uwekezaji, Mhe. Angellah Kairuki (kushoto), alipotembelea Banda la Wizara ya Fedha na Mipango, katika Maonesho ya Nanenane Kitaifa, viwanja vya Nyakabindi Mkoani Simiyu, katikati ni Waziri wa Kilimo, Mhe. Japhet Hasunga.

Bw. Mwaipaja alibainisha kuwa taasisi za elimu ya juu zilizopo chini ya Wizara ya Fedha na Mipango kikiwemo Chuo cha Usimamizi wa Fedha (IFM) na Taasisi ya Uhasibu Tanzania (TIA) zimetoa mchango mkubwa katika kuhakikisha kuwa tafiti zinazofanywa na vyuo hivyo zinakidhi mahitaji ya kuisaidia jamii hususani katika kuandaa maandiko ya miradi pamoja na huduma za ushauri.

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia Uwekezaji, Mheshimiwa Angellah Kairuki, alikuwa amemwakilisha Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Majaliwa Kassim Majaliwa, kwenye siku ya Ushirika, wakati wa Maonesho ya siku ya Wakulima Nanenane katika viwanja vya Nyakabindi mkoani Simiyu.


Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia Uwekezaji, Mhe. Angellah Kairuki (katikati), Waziri wa Kilimo Mhe. Japhet Hasunga, wakiwa katika picha ya pamoja na baadhi ya Watumishi wa Wizara ya Fedha na Mipango baada ya kutembelea Banda la Wizara ya Fedha na Mipango, katika Maonesho ya Nanenane yanayofanyika Kitaifa, viwanja vya Nyakabindi Mkoani Simiyu.

No comments:

Post a Comment