- Kayanga ni miongoni mwa mji 28 iliyonufaika na sh. tril. 1.2 za miradi hiyo
Mjumbe
wa Kamati Kuu ya Halmashauri Kuu ya Taifa ya Chama cha Mapinduzi (CCM)
Kassim Majaliwa amesema Serikali imetekeleza miradi ya maji 1,423
ikiwemo mradi wa kupeleka maji kwenye miji 28 unaotekelezwa kwa sh.
trilioni 1.2.
“Kayanga
imepata sh. bilioni 58, ni miongoni mwa miji 28 iliyopata fedha za
mradi wa maji kitaifa ambao unajumuisha mikoa mingi,” amesema.
Ametoa
kauli hiyo leo (Jumanne, Septemba 29, 2020) wakati akizungumza na
wakazi wa kata ya Kayanga, katika mikutano uliofanyika kwenye uwanja wa
Changarawe, wilayani Karagwe, mkoani Kagera.
Mjumbe
wa Kamati Kuu, Kassim Majaliwa, akiwahutubia wananchi wa Kata ya
Kayanga, wilayani Karagwe, katika mkutano wa kampeni, uliyofanyika
uwanja wa Changarawe, Septemba 29, 2020. (Picha Eliud Rwechungura)
Mgombea
Ubunge wa Jimbo la Karagwe, Innocent Bashungwa akipiga magoti ya
kuwaomba wananchi wa jimbo la Karagwe kupigia kura wagombea wote wa
Chama Cha Mapinduzi katika Uchaguzi mkuu utakaofanyika oktoba 28, 2020,
katika mkutano wa kampeni, uliyofanyika uwanja wa Changarawe, Septemba
29, 2020. (Picha Eliud Rwechungura)
Mjumbe
wa Kamati Kuu, Kassim Majaliwa, akiwakabidhi nakala ya Ilani ya
Uchaguzi ya Chama Cha Mapinduzi ya 2020-2025 Mgombea Ubunge wa Jimbo la
Karagwe, Innocent Bashungwa (kushoto) na Mgombea Udiwani Kata ya
Kayanga, Germanus Byabusha (katikati), katika mkutano wa kampeni,
uliyofanyika uwanja wa Changarawe, Septemba 29, 2020. (Picha Eliud
Rwechungura)
Mjumbe
wa Kamati Kuu, Kassim Majaliwa, akiwahutubia mamia ya wananchi wa Kata
ya Kayanga, wilayani Karagwe, katika mkutano wa kampeni, uliyofanyika
uwanja wa Changarawe, Septemba 29, 2020. (Picha Eliud Rwechungura)
Mikoa
inayohusika na mradi huo miji yake kwenye mabano ni Tanga
(Handeni/Korogwe, Muheza na Pangani); Njombe (Njombe, Wanging’ombe na
Makambako); Kagera (Kayanga); Mtwara (Nanyumbu na Makonde); Singida
(Manyoni); Ruvuma (Songea); Tabora (Sikonge, Urambo-Kaliua); Mbeya
(Rujewa na Chunya); Kigoma (Kasulu); Lindi (Kilwa Masoko); Mara (Mugumu,
Rorya/Tarime); Geita (Geita na Chato); Singida (Singida Mjini na
Kiomboi); Katavi (Mpanda); Dodoma (Chamwino na Chemba); Iringa
(Mafinga); na Morogoro (Ifakara).
Aidha, Mheshimiwa Majaliwa amewataka watanzania wamchague Dkt. John Pombe Magufuli kwa sababu anatoka katika chama ambacho kina mikakati inayotokana na mawazo ya wananchi.
"Dkt.
Magufuli anatoka kwenye Chama ambacho kina utaratibu katika kuendesha
nchi, chama ambacho kinaratibu kero za wananchi, ambacho kinasikiliza wananchi mpaka ngazi ya chini," amesema.
Ametoa
wito huo leo (Jumanne, Septemba 29, 2020) wakati akizungumza na wakazi
wa kata ya Nkwenda, akiwa njiani kuelekea Isingiro wilayani Kyerwa,
mkoani Kagera.
"Tumemjaribu
na amefanya mambo makubwa katika wizara alizoziongoza na ndiyo maana
namleta kwenu Dkt. Magufuli na kumuombea miaka mingine mitano ili alete
maendeleo zaidi."
Mheshimiwa
Majaliwa ambaye yuko mkoani Kagera kumuombea kura mgombea Urais kwa
tiketi ya CCM, Dkt. Magufuli alitumia fursa hiyo kumnadi mgombea ubunge
wa jimbo la Kyerwa, Bw. Innocent Bilakwate, mgombea udiwani wa kata ya
Nkwenda, Bw. Edward Katunzi na wagombea wa CCM wa kata za jirani.
Amesema
CCM ni chama kinachoongozwa na Ilani ya Uchaguzi na kuna mambo
yamethibitika katika ilani inayoishia 2020. "Leo tunaleta kitabu kingine
cha Ilani ya 2020 - 2025. Kama tuliweza kufanya makubwa ndani ya miaka
mitano na kile kitabu kidogo, je huko tuendako itakuwaje?"
Akiwa Isingiro kwenye
mkutano wa hadhara, Mheshimiwa Majaliwa alisema Serikali ilibadilisha
sheria tangu mwaka 2017 na ikazuia uuzaji wa madini ya bati nje ya nchi
kwa kutumia njia za panya.
"Sheria
inatutaka tutenge ekari kadhaa kwa ajili ya wachimbaji wadogo. Leo hii
ekari 38,000 zimetolewa kwa wachimbaji wadogo wa madini mbalimbali. Pia
tumeanzisha masoko ya madini 26 na vituo vidogo 28 vya kuuzia madini,"
alisema.
Akifafanua
kuhusu vitambulisho vya Taifa, Mheshimiwa Majaliwa alisema Tanzania ni
nchi ya amani na wengi wanatamani kuja kuishi nchini.
Alisema
wilaya za Kyerwa, Karagwe na Missenyi ni za mipakani kwa hiyo zina
changamoto za uhamijai na masuala ya kiraia. "Ndiyo maana Serikali
inakuwa makini katika uhakiki. Tutaimarisha usimamizi ili kila Mtanzania
apate kitambulisho.”
Pia
amewaonya maafisa wanaohusika na utaoaji vitambulisho vya uraia ambao
wanapokea hongo na kuwapa vitambulisho hivyo watu wasiostahili.
Wakati huohuo, Mheshimiwa
Majaliwa amempokea aliyekuwa mgombea ubunge wa jimbo la Karagwe kupitia
Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Bw. Princepius Rwazo
ambaye ameamua kurejea CCM.
Akizungumza
kwenye mkutano huo, Bw. Rwazo alisema alikuwa mgombea ubunge kwenye
uchaguzi mkuu uliopita na aliisumbua sana CCM lakini sasa ameamua
kurejea kwani ameona mazuri yanayofanywa na Chama hicho.
"CCM
imejibu kiu zetu, kimekuwa kama chama cha upinzani, na wapinzani sasa
wamelala. Nimerudi CCM, sihitaji cheo chochote, shida yangu ni kujiunga
na watu wanaochapa kazi. Nitamuunga mkono Dkt. Magufuli na ndugu yangu
Bashungwa," alisema na kushangiliwa.
Mheshimiwa Majaliwa anaendelea za ziara yake katika wilaya za Karagwe na Missenyi.