Matokeo chanyA+ online




Monday, September 21, 2020

TARI YAANZA KWA KASI UTOAJI MAFUNZO KWA VITENDO KUINUA UBORA WA ZAO LA KOROSHO



Mratibu wa Kitaifa wa Zao la Korosho kutoka Kituo cha Utafiti wa Kilimo TARI Naliendele, Dkt.Geradina Mzena, akitoa mada kwenye mafunzo ya kilimo bora cha korosho yaliyotolewa jana kwenye ukumbi wa Halmashauri ya Mji Mdogo wa Gairo kwa Maafisa Ugani na Wakulima kutoka Halmashauri 7 za  Mkoa wa Morogoro. 

 

Mtafiti Mwandamizi na Mdhibiti wa visumbufu vya wadudu na magonjwa kwenye zao la korosho, kutoka Tari- Naliendele  Dkt.Wilson Nene, akitoa mada kwenye mafunzo hayo.

Mtafiti  kutoka Tari- Naliendele Programu ya Zao la Korosho, Kasiga Ngiha, akitoa mada kuhusu Agronomia ya korosho.


Washiriki wakiwa katika mafunzo hayo.

Mkuu wa Kituo cha Morogoro kutoka Bodi ya Korosho, Luseshelo Silomba akizungumza kwenye mafunzo hayo.


Mafunzo yakiendelea.

Afisa Kilimo wa Wilaya ya Gairo, Eunice Kyungai akizungumza kwenye mafunzo hayo.

Washiriki wakiwa katika mafunzo hayo.

Afisa Kilimo na Mratibu wa Zao la Korosho Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Morogoro,Isabella Chilumba akizungumza. 


Mafunzo yakiendelea.


Mjadala ukiendelea.

Washiriki wakiwa kwenye mafunzo hayo.
Mkulima Elizabeth Senyagwa kutoka Gairo,  akishiriki moja ya mjadala  kwenye mafunzo hayo kwenye mafunzo hayo.

Afisa Kilimo wa Wilaya ya Kilosa, Elina Dastan, akizungumza kwenye mafunzo hayo.

Afisa Kilimo Abilah Samli kutoka Kilosa akizungumza kwenye mafunzo hayo.

Mkulima kutoka Dumila, Samwel Dede akishiriki moja ya mjadala  kwenye mafunzo hayo.

Godwin Myovela na Dotto Mwaibale.

Taasisi ya Utafiti wa Kilimo Nchini (TARI) kupitia Kituo chake cha Naliendele kimewataka wakulima wote wa zao la korosho kubadilika na kuanza kulima kilimo cha biashara kwa kuzingatia 'agronomia' stahiki ili kuongeza tija na ubora wa zao hilo.

Sambamba na hilo kituo hicho kimetoa angalizo kwa wakulima na wadau wa korosho kuhakikisha wanaepuka udanganyifu wowote wanapohitaji huduma ya mbegu bora ya zao hilo, badala yake wawasiliane na Maafisa Kilimo wa eneo husika ili kupata maelezo ya namna ya upatikanaji wake .

Mratibu wa zao hilo kitaifa kutoka Kituo cha Utafiti wa Kilimo Tari Naliendele Dkt.Geradina Mzena aliyasema hayo  kwenye ukumbi wa Halmashauri ya Mji Mdogo wa Gairo jana wakati   akifungua mafunzo ya kilimo bora cha zao la korosho kwa maafisa ugani na wakulima kutoka Halmashauri 7 za Mkoa wa Morogoro.

"Tari Naliendele hatuuzi mbegu kwa fedha taslimu, lazima uwe na namba ya malipo 'control number' na  endapo ukiuziwa mbegu na mtu yeyote kwa fedha taslimu ujue umeibiwa. Korosho ni zao la kudumu, lina mfumo wake na kamwe usijaribu kupanda mbegu usiyoijua." alisema Mzena.

Alisema mbegu bora ya zao hilo na aina zake huzalishwa na Kituo cha Utafiti wa Kilimo cha Tari Naliendele pekee na sio kwingineko, hivyo wakulima wanapaswa kuwa makini ili kwa pamoja kuweza kuinua ubora wa zao hilo na kujihakikishia uwepo wa soko lake kitaifa na kimataifa.

Aidha Mtafiti huyo na Mgunduzi wa zao hilo Dkt.Mzena alisema ili kubaini kama mbegu ya korosho husika ina ubora ni sharti idadi ya punje za korosho ziwe chini ya 200 kwa kilo moja na sio zaidi ya hapo.

Mratibu huyo kitaifa alifafanua kwamba kilo moja ya zao hilo inaposheheni punje zaidi ya 200 hudhihirisha wazi kuwa ubora wa mbegu hiyo una mashaka na mkulima husika anapaswa kufika Tari Naliendele ili kupatiwa mbegu mbadala zenye ubora.

Hata hivyo akizungumza mbele ya wakulima na maafisa ugani, Mzena ambaye pia ni Mratibu wa  Utafiti na Ubunifu kutoka Kituo cha Tari Naliendele alibainisha kuwa pamoja na mambo mengine korosho ambayo hulimwa na takribani watanzania laki 283 nchini ina faida kubwa katika kuongeza kipato cha kaya na kuondoa umasikini.

Alisema Mtanzania yeyote atakayelima korosho ndani ya mikoa rafiki takribani 17 inayostawisha zao hilo ni dhahiri atajipatia pesa za kutosha kutokana na ukweli kwamba zao hilo lina nguvu na utajiri mkubwa, tofauti na mazao mengine. Kikubwa ni kuzingatia kanuni bora za kilimo.

"Korosho haijawahi kukosa soko la uhakika, na zaidi inamfumo wa soko linaloeleweka unaoitwa stakabadhi ghalani na kukuwezesha kukopesheka kupitia taasisi za fedha." alisema.

Mzena alisisitiza kwa wale walio mbali na vituo vya Tari wakihitaji huduma ya mbegu bora wamuone Afisa ugani wa eneo lake ili hatimaye awasiliane na Tari Naliendele ili kuepuka hasara ya mkulima kuuziwa mbegu na viuatilifu feki.

"Mbegu za zao hili la kimkakati na aina zake zinazozalishwa na kituo chetu zinavumilia ukame, magonjwa, visumbufu vya wadudu na zinatoa mazao mengi." alisema Mzena.

Kwa upande wake Mtafiti mwingine wa zao hilo wa kituo hicho Kasiga Ngiha alisema kwa sasa wataalamu wa kituo hicho wanapita maeneo mbalimbali nchini kutoa elimu ya kuongeza ubora na uzalishaji wa zao la korosho kwa tija na ustawi.

Mtafiti Mwandamizi na Mdhibiti wa visumbufu vya wadudu na magonjwa kwenye zao hilo, Dkt.Wilson Nene alisema kituo hicho kinatoa mafunzo hayo lengo ni kuwawezesha wakulima na maafisa ugani kuwatambua wadudu waharibifu, magonjwa na namna ya kukabiliana nayo ili kufikia shabaha tarajiwa kutoka tani laki tatu zinazozalishwa kwa sasa kufikia tani milioni 1 ifikapo  2023.

" Korosho inafaida nyingi ikiwemo baada ya kusindika tunazalisha bidhaa kama korosho karanga, na bibo lake hutumika kutengeneza bidhaa ya juisi, mvinyo, ethanol na malisho ya mifugo." alisema Nene.

Alisisitiza kimsingi mafunzo hayo yanalenga kutoa teknolojia ya mbinu bora na za kisasa za uzalishaji wa zao la korosho kwa kuzingatia wapi mkulima atapata mbegu bora, namna ya kuandaa shamba, kuchimba mashimo, kupanda na kupalilia hatimaye mavuno yake.

Kituo  cha Tari Naliendele pamoja na mambo mengine kimepewa majukumu ya kitaifa ya kutafiti, kustawisha na kuongeza tija na thamani kwenye mazao ya korosho na mbegu jamii ya mafuta-ikiwemo ufuta, karanga na alizeti. 

No comments:

Post a Comment