Matokeo chanyA+ online




Wednesday, November 18, 2020

RAIS WA ZANZIBAR DK. HUSSEIN MWINYI AMETOA MUDA WA MIEZI MITATU KWA UONGOZI WA WIZARA YA AFYA KUREKEBISHA KASORO ZA KIUTENDAJI

 



Rais wa  Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk. Hussein Ali Mwinyi ametoa muda wa miezi mitatu kwa uongozi wa Wizara ya Afya kurekebisha kasoro za kiutendaji zinazosababisha kutokuwepo  ufanisi katika utoaji wa huduma bora kwa wagonjwa.

Dk. Mwinyi ametoa kauli hiyo  wakati alipofanya ziara ya kushtukiza katika Hospitali ya Rufaa ya Mnazi mmoja, alipofika kuangalia utoaji wa huduma kwa wagonjwa katika maeneo na vitengo  tofauti  vya Hospitali hiyo.

Alisema kwa kiwango kikubwa mambo mengi yanahitaji kufanyiwa marekebisho, akibainisha kuwepo changamoto mbali mbali za kiutendaji na hivyo kuzorotesha uapatikanaji wa huduma bora kwa wagonjwa.

Alisema analenga kuchukua hatua za kiutawala dhidi ya watendaji wasiowajibika kazini na kusababisha wananchi kulalamika kutokana na ukosefu wa huduma, pamoja na kupewa lugha zisizordhisha kutoka kwa wauguzi na watendaji wengine  wa Hospitali hiyo.

Aidha, Dk. Mwinyi alisema pamoja na Serikali kuipatia fedha za kutosha Hospitali hiyo kila mwezi, kumekuwepo changamoto za ukosefu wa vifaa muhimu kwa wagonjwa ikiwemo magodoro, dawa na vifaa vya maabara, hivyo akautaka Uongozi wa Hospitali hiyo kubadilika na kuondokana na utendaji wa mazowea.

Alisema pale Serikali inapotoa fedha kwa ajili ya ununuzi wa dawa na hatimae wagonjwa wakakosa dawa hizo, ni dhahiri kuwa kuna tatizo mahala hapo.

No comments:

Post a Comment