Matokeo chanyA+ online




Tuesday, January 19, 2021

RAIS MAGUFULI ASHUHUDIA UTIAJI SAINI MKATABA WA MADINI YA NICKEL NA UWEKAJI JIWE LA MSINGI KIWANDA CHA MAZIWA KARAGWE

Waziri wa Madini Mhe. Dotto Biteko na Msajili wa Hazina Bw. Athumani Mbuttuka (wa tatu toka kushoto walioketi) pamoja na wanasheria wakishuhudia Mwanasheria Mkuu wa Serikali Dkt Adelardus Kilangi na Makamu wa Rais wa Kampuni ya LZ NICKEL LIMITED ya Uingereza Bw. Chris Von Chritierson wakitia saini makubaliano ya pamoja ya ushirikiano kati ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Kampuni hiyo katika uchimbaji wa madini ya Nickel katika mgodi wa Kabanga wilayani Ngara mkoa wa Kagera

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli akishuhudia Msajili wa Hazina Bw. Athumani Mbuttuka akibadilishana nyaraka na Makamu wa Rais wa Kampuni ya LZ NICKEL LIMITED Bw. Chris Von Christierson baada ya kutiliana saini makubaliano ya ushirikiano katika uchimbaji wa madini ya Nickel huko Kabanga katika Wilaya ya Ngara mkoani Kagera kwenye hafla iliyofanyika katika ukumbi wa Shule ya Sekondari ya Bukoba mjini Bukoba  Jumanne Januari 19, 2021

Msajili wa Hazina Bw. Athumani Mbuttuka akionesha nyaraka akiwa na Makamu wa Rais wa Kampuni ya LZ NICKEL LIMITED Bw. Chris Von Christierson  (katikati) na afisa wa kampuni ya LZ NICKEL LIMITED baada ya kutiliana saini makubaliano ya ushirikiano katika uchimbaji wa madini ya Nickel huko Kabanga katika Wilaya ya Ngara mkoani Kagera kwenye hafla iliyofanyika katika ukumbi wa Shule ya Sekondari ya Bukoba mjini Bukoba Jumanne Januari 19, 2021

Katibu Mkuu wa Wizara ya Mifugo na Uvuvi Profesa Elisante Ole Gabriel akimtambulisha Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt John Pombe Magufuli kwa Mkurugenzi wa kampuni ya Kahama Fresh Bw. Jossam Ntageki wakati wa hafla ya uwekaji wa jiwe la msingi mradi wa ujenzi wa kiwanda cha kusindika maziwa na vyakula vya mifugo cha
Kahama Fresh mjini Karagwe  Jumanne Januari 19, 2021
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt John Pombe Magufuli akiwa na viongozi wengine akisikiliza maeleo ya mradi wa ujenzi wa kiwanda cha kusindika maziwa na vyakula vya mifugo cha Kahama Fresh mjini Karagwe kabla ya kuweka jiwe la msingi la mradi huo utaondeshwa na mwekezaji mzawa Bw. Jossam Ntangeki leo Jumanne Januari 19, 2021
 Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt John Pombe Magufuli akiwa pamoja na Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Mashimba Ndaki akiweka jiwe la msingi la mradi wa ujenzi wa kiwanda cha kusindika maziwa na vyakula vya mifugo cha Kahama Fresh mjini Karagwe unaoendeshwa na mwekezaji mzawa Bw. Jossam Ntangeki  Jumanne Januari 19, 2021
 Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt John Pombe Magufuli akiwa Mkurugenzi wa kampuni ya Kahama Fresh Bw. Jossam Ntageki baada ya kuweka jiwe la msingi la mradi wa ujenzi wa kiwanda cha kusindika maziwa na vyakula vya mifugo cha Kahama Fresh mjini Karagwe baada ya kuweka jiwe la msingi la mradi huo utaondeshwa na mwekezaji huyo mzawa Jumanne Januari 19, 2021


Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli akizungumza na wageni mbalimbali waliohudhuria hafla fupi ya utiaji saini Mkataba kati ya Serikali na Kampuni ya Lz Nickel limited kwa ajili ya uchimbaji wa madini hayo Ngara mkoani Kagera  tarehe 19 Januari 2021

 

 Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli  akiwashukuru Wananchi na kuwaaga mara baada ya hafla ya utiaji saini Mkataba kati ya Serikali na Kampuni ya Lz Nickel limited kwa ajili ya uchimbaji wa madini hayo mkoani Kagera  tarehe 19 Januari 2021


Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli akizungumza na wananchi wa Kyaka Misenyi mkoani Kagera wakati akielekea Wilayani Karagwe.

 


 Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli akizungumza na Wanafunzi wa Shule ya Sekondari Bukoba iliyopo Bukoba mjini mkoani Kagera muda mfupi mara baada ya kushuhudia utiaji saini wa Mkataba wa makubaliano kati ya Serikali na Kampuni ya LZ Nickel limited  tarehe 19 Januari 2021.

 

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli akiwa katika picha ya pamoja na Wanafunzi wa Shule ya Sekondari Bukoba mara baada ya kuzungumza nao.

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli akiagana na Wanafunzi wa Shule ya Sekondari Bukoba mara baada ya kuzungumza nao.

Sehemu ya Wananchi wa Kyaka Wilayani Misenyi wakimsikiliza Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli wakati aliposimama kuwasalimia  tarehe 19 Januari 2021

 

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli  tarehe 19 Januari, 2021 ameshuhudia utiaji saini wa mikataba ya uwekezaji kati ya Serikali ya Tanzania na kampuni ya LZ Nickel Limited juu ya uchimbaji wa madini ya Nickel yaliyopo Kabanga katika Wilaya ya Ngara Mkoani Kagera.

Hafla ya utiaji saini mikataba hiyo imefanyika Mjini Bukoba na kuhudhuriwa na viongozi mbalimbali wakiwemo Mawaziri na Naibu Mawaziri, Katibu Mkuu Kiongozi Mhe. Balozi John Kijazi, Balozi wa Uingereza hapa nchini Mhe. David William Concar, Makatibu Wakuu na Naibu Makatibu Wakuu, Mwanasheria Mkuu wa Serikali Prof. Adelardus Kilangi, viongozi wa Dini, viongozi wa vyama vya siasa na viongozi wa Mkoa wa Kagera wakiongozwa na Mkuu wa Mkoa huo, Brig. Jen. Marco Gaguti.

Kwa upande wa Tanzania mkataba huo umesainiwa na Waziri wa Madini Mhe. Doto Biteko na Msajili wa Hazina Bw. Athuman Mbuttuka na kwa upande wa LZ Nickel waliotia saini ni Makamu Mwenyekiti Bw. Chris Von Christierson na Mtendaji Mkuu Bw. Chris Showalter.

Serikali ya Tanzania na LZ Nickel Ltd zimekubaliana kuunda kampuni ya ubia iitwayo Tembo Nickel Corporation Limited ambayo itamiliki kampuni 2 ambazo ni Tembo Nickel Mining Company Ltd ambayo itajihusisha na uchimbaji wa madini ya Nickel huko Kabanga na kampuni ya Tembo Nickel Refinery Company Limited itakayojihusisha na usafishaji wa madini huko Kahama, Shinyanga.

Akizungumza baada ya kushuhudia utiaji saini wa mikataba hiyo, Mhe. Rais Magufuli amempongeza Prof. Palamagamba Kabudi (Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki) na timu aliyoiongoza kufanya majadiliano na kampuni ya LZ Nickel Ltd ambapo makubaliano yaliyofikiwa yameiwezesha Tanzania kuwa mwanahisa kwenye uwekezaji huo pamoja na kupata manufaa mbalimbali yakiwemo kugawana faida kwa 50/50, kodi na manufaa mengine kama inavyoelekezwa na sheria mbalimbali ikiwemo sheria mpya ya madini ya mwaka 2017.

Mhe. Rais Magufuli ameelezea kufurahishwa kwake na hatua iliyofikiwa katika uchimbaji wa madini ya Nickel kutoka Kabanga kwa kuwa mradi huo haukuwa umetekelezwa kwa kipindi kirefu cha tangu mwaka 1976/79 ulipofanyiwa utafiti na kubaini kuwepo mashapo makubwa ya Nickel tena yenye ubora wa daraja la kwanza.

Amepongeza mpango wa kujenga mtambo wa kusafisha madini (Smelter) huko Kahama ambao amesema utasaidia madini yote yanayochimbwa kujulikana, mfano uchimbaji wa Nickel huambatana na madini mengine kama vile Cobalt.

Mhe. Rais Magufuli ameiagiza Wizara ya Madini kuhakikisha mradi huu unatekelezwa haraka ili wananchi wa Ngara na Kahama waweze kunufaika.

Akiwa njiani kwenda Karagwe, Mhe. Rais Magufuli amewasalimu wananchi wa Kyaka katika Wilaya ya Misenyi ambapo amewaahidi kupanua kituo cha afya cha Kyaka na kuwa Hospitali, na ameeleza kutofurahishwa na kasi ya utekelezaji wa mradi wa maji wa Kyaka unaotarajiwa kugharimu shilingi Bilioni 15.1 na ambao umefikia asilimia 30 ya utekelezaji.

Mhe. Rais Magufuli ameagiza ndani ya kipindi cha miezi 13 ya mradi huo, uwe umekamilika vinginevyo mkandarasi na viongozi wanaosimamia watachukuliwa hatua.

Wakati huo huo, Mhe. Rais Magufuli ameweka jiwe la msingi la ujenzi wa kiwanda cha kusindika maziwa na kusindika chakula cha mifugo (Kahama Fresh) kilichopo Karagwe.

Kiwanda hicho ambacho kitakuwa na uwezo wa kusindika lita 10,000 kwa siku na kitazalisha ajira 400 kinamilikiwa na Mtanzania Jossam Ntangeki ambaye anawekeza shilingi Bilioni 9 ikiwemo shilingi Bilioni 2.7 alizopata mkopo kutoka Benki ya Maendeleo ya Kilimo (TaDB).

Mhe. Rais Magufuli amempongeza Bw. Ntangeki kwa uwekezaji huo na ametoa wito kwa Watanzania kujitokeza kuwekeza katika ufugaji na uzalishaji wa maziwa kwa kuwa mahitaji ya maziwa kwa Tanzania ni makubwa kuliko uzalishaji uliopo licha ya kuwa nchi ya pili kwa idadi kubwa ya mifugo barani Afrika.

Ameiagiza Wizara ya Mifugo na Uvuvi kuhakikisha Kampuni ya Ranchi za Taifa (NARCO) inaongeza mifugo katika ranchi zake zote, na kwa maeneo ambayo haiyatumii wapewe wafugaji wengine na kwa gharama nafuu.

Mhe. Rais Magufuli ameagiza Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi kutangaza haraka zabuni za ujenzi wa kilometa 60 za barabara ya lami ya kuanzia Karagwe kwenda Ngara, kilometa 50 za kuanzia Kyerwa kwenda Karagwe na barabara ya Nyakahura – Rusumo ambazo zimeainishwa katika Ilani ya Uchaguzi Mkuu ya CCM ya mwaka 2020/25.

Amemuagiza Meneja wa TANROADS Mkoa wa Kagera Mhandishi Andrew Kasamwa kukamilisha ujenzi daraja la Kitengule katika mto Kagera ifikapo Juni 2021 vinginevyo atachukua hatua kwa kuwa ujenzi wa daraja hilo umecheleweshwa kwa miaka 3.


No comments:

Post a Comment