Matokeo chanyA+ online




Friday, January 8, 2021

SERIKALI IMEANZA UJENZI WA DARAJA LA CHAMKOROMA LILILOHARIBIWA NA MVUA


Serikali imeanza ujenzi wa daraja la Chamkoroma linalounganisha wilaya ya Mpwapwa na Kongwa ambalo liliharibiwa na mvua na kupelekea uwepo wa changamoto ya usafiri na hivyo kurudisha nyuma uchumi wa mwananchi mmoja mmoja na halmashauri kwa ujumla.

Daraja hilo lipo ndani ya barabara ya Pandambili-Mlali -Mpwapwa hadi Ngh'ambi inayojengwa kwa gharama ya Sh Bilioni 1.1 na mkandarasi Bahati Investment.


Akizungumza Januari 7,2020 wilayani Kongwa ikiwa ni muendelezo wa ziara yake ya kikazi ya kukagua maeneo yaliyoharibiwa na mvua Mkuu wa Mkoa wa Dodoma Dkt Binilith Mahenge amemtaka mkandarasi kujenga njia ya mbadala ndani ya siku mbili Ili  kuwawezesha wananchi kupita wakati ujenzi wa daraja ukiendelea.

 "Daraja hili ni muhimu Sana katika kukuza uchumi wetu,kuharibika kwake kumezuia shughuli za kiuchumi kwa wananchi kuendelea,niwapongeze Wakal wa Barabara Tanzania (TANROADS) Mkoa wa Dodoma kwa usimamizi lakini niwaombe mumsimamie mkandarasi huyu ili akamilishe kwa wakati,,na njia mbadala isizidi siku mbili iwe imekamilika,"alisema.


 

Dkt Mahenge amewasisitiza TANROADS kumsimamia mkandarasi ili daraja lijengwe kwa kiwango kuendana na thamani ya pesa iliyotolewa na liweze kukamilika kwa muda uliowekwa.

"Wekeni structure ambayo wataalam mtaridhika nayo,unapojenga kitu kisichokuwa na ubora haikudumu na baada ya muda fulani kinaharibika na hivyo kuzuia fedha ambazo zingetumika kwingine,naomba mjiridhishe na kile ambacho kitafanyika hapa ili kiwe Cha uhakika,"alisisitiza Dkt Mahenge.


Amewashauri pindi wanapoanza mradi wowote wakae na wenyeji wa eneo husika ili kupewa historia ya eneo na hivyo kuepuka kurudia kufanya kazi Mara mbili endapo itaharibika.

"Wataalam jiongezeni, Mhandisi unapotekeleza mradi wowote lazima ujiulize sana endapo Kuna mvua na vitu vingine,ndio maana tunasema unapofika kwenye eneo pata historia ya eneo husika,mnapokwenda ku design bila ya kujua chochote Cha eneo hilo ndio inatokea muda mfupi mradi unaharibika,"aliongeza

Kwa upande wake Mkuu wa wilaya hiyo Dkt Suleiman Serera amewakumbusha wananchi suala la upandaji wa miti ili kuzuia wingi wa maji unaoharibu miundombinu ya barabara


"Hivi karibuni nilifanya kikao hapa na kuhimiza suala la utunzaji wa mazingira Ili kuokoa miundombinu yetu,tukipanda miti kwa wingi maji yanayopita hapa hayatakuja kwa kasi hadi kupelekea uharibifu wa miundombinu,"alisema Dkt Serera.

Akizungumza katika ziara hiyo Kaimu Meneja wa TANROADS mhandisi Salome Kabunda amesema wanachofanya kwa Sasa ni kuona namna ya kuzuia maji ili yasiweze kuleta uharibifu zaidi wakati huu ambapo kazi inaendelea.


"Kazi hii tunayoifanya ipo kwenye uwezo wa mkandarasi na ndani ya wiki tatu au mwezi mmoja mkandarasi ameahidi kukamilisha daraja hili,na tuahidi kuwa tutamsimamia ili akamilishe kwa wakati,"alisema.

Awali diwani wa kata ya Chamkoroma Saimon Binde amesema tatizo lililopo ni uharibifu mkubwa wa mazingira unaofanywa na wananchi.

"Hapa Kuna wananchi wamejimilikisha ardhi mlimani huko,wanalima wanafanya uharibifu wa kukata misitu na hivyo kumaliza misitu iliyopo na kupelekea eneo hili kwa kiasi kikubwa kuharibiwa na mvua,"alisema.


Ziara ya Dkt Mahenge ilianzia kwenye kukagua barabara ya Kongwa mjini inayojengwa kwa kiwango cha lami ambapo amemuelekeza mkandarasi Mtuvilo Traders anayejenga barabara hiyo kufanya marekebisho kwa kuweka makaravati ili kuzuia maji kujaa barabarani na kuingia katika makazi ya watu.

No comments:

Post a Comment