Kaimu Katibu wa Tume ya Utumishi wa Walimu Tanzania (TSC), Moses Chitama ametaja makosa sugu yanayofanywa na baadhi ya walimu nchini kuwa ni utoro, ulevi pamoja na kujihusisha kimapenzi na wanafunzi.
Aliyasema hayo Januari 5 mwaka huu, wakati akiwasilisha mada kuhusu maadili, katika Mkutano wa Pili wa Umoja wa Walimu Wakuu wa Shule za Msingi Tanzania Bara, uliofanyika jijini Dodoma.
Chitama alifafanua kuwa, TSC ikiwa ni Mamlaka ya Nidhamu kwa Walimu nchini, imebaini kuwa makosa hayo matatu ndiyo yanaongoza kuripotiwa kwa sasa, miongoni mwa makosa kadhaa yanayohusiana na utovu wa nidhamu katika kada husika.
Aliendelea kueleza zaidi kuwa, kwa kulitambua hilo, Tume imekuwa ikitumia mbinu mbalimbali katika kuhakikisha suala hilo linatokomezwa ikiwemo kutoa elimu kwa wahusika na kuchukua hatua kali za kinidhamu kwa wanaothibitika kutenda makosa hayo.
Aidha, Kaimu Katibu Chitama alitumia jukwaa hilo kukemea vikali walimu wenye tabia hiyo na kuwataka kuacha mara moja huku akisisitiza kuwa Serikali kupitia Tume husika, haitawavumilia.
Alisema kuwa walimu ndiyo chanzo kikuu cha maendeleo ya nchi kwani ndiyo wamepewa dhamana ya kuwalea kiakili na kimwili watoto, ambao wanategemewa na Taifa kuja kuwa viongozi na wataalamu katika nyanja mbalimbali, hivyo wanapaswa kutimiza wajibu wao ipasavyo.
“Ninyi walimu msiposimamia maadili ya taaluma yenu pamoja na maadili ya watoto mnaowafundisha, tutakuwa na Taifa bovu, lililokosa mwelekeo na lenye mmomonyoko wa maadili.
Mkurugenzi kutoka Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI), anayesimamia Elimu ya Awali na Msingi, Susan Nussu, akisisitiza kuhusu maadili ya walimu, wakati wa mkutano wa pili wa Umoja wa Walimu Wakuu wa Shule za Msingi Tanzania Bara (hawapo pichani), uliofanyika jijini Dodoma, Januari 5, 2021.
Akitoa takwimu, Chitama alibainisha kuwa, katika kipindi cha miaka mitano (2016 – 2020), jumla ya walimu 9,819 walifunguliwa mashauri na waajiri wao, ambapo 5,441 kati yao walifukuzwa kazi.
Aidha, alieleza kuwa, katika kipindi hicho, walimu 1,803 walipewa maonyo na makaripio, 520 walipunguziwa mishahara, 244 walisimamishiwa nyongeza ya mishahara na 403 waliteremshwa vyeo.
Kwa upande mwingine, alisema walimu 149 walilipwa fidia na wengine 438 kuachiwa huru.
Akihitimisha, Kaimu Katibu Chitama aliwataka walimu kuwachukulia wanafunzi kama watoto wao wa kuzaa hivyo wawatendee sawa na wanavyotendea familia zao.
Sehemu ya Wajumbe wa Mkutano wa Pili wa Umoja wa Walimu Wakuu wa Shule za Msingi Tanzania Bara (hawapo pichani), wakifuatilia mada mbalimbali zilizokuwa zikiwasilishwa wakati wa mkutano huo uliofanyika jijini Dodoma, Januari 5, 2021.
Na Veronica Simba
Akizungumza katika Mkutano huo, Mkurugenzi kutoka Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI), anayesimamia Elimu ya Awali na Msingi, Susan Nussu, aliwasisitiza walimu kujiepusha na masuala ya udanganyifu wa mitihani katika shule zao.
Alisema wengi hutenda kosa hilo kwa tamaa ya kujitafutia sifa ya ufaulu katika shule zao lakini akawataka kukumbuka kuwa kitendo hicho huwaponza wanafunzi wao kwa kuwasababishia kufutiwa matokeo.
Aidha, aliwataka Walimu Wakuu wa Shule za Msingi kuacha tabia ya kuwapanga walimu wazembe na wavivu kufundisha madarasa ya awali badala yake wawapange walimu wenye weledi ili waweze kuwajengea watoto msingi mzuri wa elimu.
Mkutano huo wa Pili wa Umoja wa Walimu Wakuu wa Shule za Msingi Tanzania, uliongozwa na kaulimbiu isemayo uongozi na usimamizi makini wa elimu, utaimarisha Tanzania katika uchumi wa kati.
No comments:
Post a Comment