Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar Mh. Othman Masoud Othman ametoa
kauli hio tarehe 04/03/2021 alipokuwa akizungumza na Waumini wa Dini
ya kiislamu waliojitokeza katika Hitma (Dua) ya kumuombea Marehemu
Maalim Seif Sharif Hamad aliefariki dunia mwezi uliopita.
Dua hio
iliyoandaliwa na Uongozi wa Chama cha ACT Wazalendo Mkoa wa Mjini
Kichama ilifanyika katika Mskiti wa Muembe Tanga Wilaya ya Mjini Mkoa wa
Mjini Magharib Unguja, ambapo pia ilihudhuriwa na viongozi wa wakuu wa
Chama cha ACT Wazalendo pamoja na viongozi wa Kiserikali.
Akimkaribisha
Makamu wa kwanza wa Rais wa Zanzibar kwa niaba ya Chama cha ACT
Wazalendo Makamu M/Kiti wa Chama hicho kwa upande wa Zanzibar Mh. Juma
Duni Haji amesema Maalim alikuwa anawapenda sana Wazanzibari na alikuwa
na lengo kubwa la kuwaunganisha, sasa kwavile ameshatangulia na
kwasababu ameshapatikana kiongozi mwengine Mh. Othman basi wampe
mashirikiano na wawe pamoja nae, nahii ndio njia ya kumuenzi Maalim
Seif.
Mh.Othman amesema sio jambo rahisi kuvaa viatu vya
Marehemu Maalim Seif ila kwasababu Wazanzibari ni wamoja na wanaamini
katika ushirikiano itakuwa rahisi kwake kufanikisha majukumu yake.
Mh.
Othman amesema Maalim Seif alikuwa ni muumini wa umoja na mshikamano
hivyo Wananchi kwa pamoja wakisimamia misingi hio watakuwa wamemtendea
haki, na kwake ni faraja.
”Jambo muhimu kuliko yote ni kusimamia
Umoja na Mshikamano baina yetu, kwani hilo ndio jambo kubwa ambalo
Kiongozi wetu Maalim Seif alikuwa analihubiri, hivyo njia adhwimu ya
kumuenzi ni kukiendeleza alichokiacha” Amesema Mh.Othman
Makamo
wa Kwanza wa Rais amesisitiza tena kwa kusema kwahakika ni ngumu kuwa
kama Maalim Seif, kwani Maalim ni Kitabu kilichokamilika na amefanya
mengi sana enzi za uhai wake, lakini jambo kubwa linalompa moyo na
faraja nikwamba wapo viongozi wenzake ambao anaamini watashikamana na
kushirikiana ili kuhakikisha mambo yanakwenda sawa, kwani Wazanzibari
kwa sasa wanapigania mustakbali wa Nchi yao, na katika hilo Mungu hutia
baraka na nguvu.
Mh. Othman amesema “kwasasa Wazanzibari
tumepata fursa ya kuwa na Rais ambae amejipambanua katika kuikwamua
Zanzibar kutoka hapa ilipo sasa, hivyo ipo haja mahususi Wananchi wote
kwa pamoja kutazama mbele na kuisaidia Nchi yetu ili tuweze kukwamuka
kwa kumuunga mkono Mh.Rais na Serikali kwaujumla’’
No comments:
Post a Comment