Na Faraja Mpina, WMTH, Dodoma
Waziri wa Mawasiliano na Teknolojia ya Habari Dkt. Faustine Ndugulile
ameiagiza Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) kwa kushirikiana na
Baraza la Ushauri la Watumiaji wa Huduma za Mawasiliano (TCRA-CCC)
kuboresha vitengo vyao vya mawasiliano ili kuongeza kasi ya kutoa elimu
kwa umma kuhusu matumizi sahihi ya huduma za mawasiliano kwa kuzingatia
haki na wajibu pamoja na matumizi sahihi ya simu janja na mtandao.
Dkt. Ndugulile amezungumza hayo mbele ya waandishi wa habari baada ya
kikao chake cha kazi cha Wizara na taasisi zilizo chini ya Wizara hiyo
cha kujadili na kufanya mapitio ya taarifa za mapato na matumizi za
taasisi hizo kwa robo ya tatu ya mwaka wa fedha 2020/2021 Kilichofanyika
katika Ukumbi wa Hazina jijini Dodoma.
Aidha Dkt. Ndugulile
ameziagiza taasisi hizo kuboresha mifumo ya wananchi kutolea malalamiko
yanayohusu huduma za mawasiliano na kushughulikia malalamiko hayo kwa
wakati na taarifa ya malalamiko hayo itakuwa ni ajenda ya kudumu katika
vikao vya kila robo mwaka baina ya Wizara hiyo na taasisi zake.
Ameongeza kuwa elimu kwa umma ikitolewa kwa kiwango kinachojitosheleza
kitapunguza baadhi ya malalamiko ya wananchi kwa mfano malalamiko ya
vifurushi vya data kuisha haraka ambapo kwa namna moja ama nyingine
inasababishwa na settings za simu janja kuruhusu programu zake
kujiboresha zenyewe (automatic Updating).
“Kuna mambo ambayo ni
muhimu wananchi kuyafahamu kwa mfano matumizi makubwa ya data
yanayosababishwa na settings za simu janja ambazo zinaruhusu baadhi ya
programu kujiboresha zenyewe nazo zinachangia vifurushi vya data kuisha
haraka”, alizungumza Dkt. Ndugulile
Aliongeza kuwa Serikali
inatengeneza mazingira wezeshi ya kuhakikisha mawasiliano yanafika kwa
wananchi wote lakini kumekuwa na changamoto ya baadhi ya watu kutokuwa
na matumizi sahihi ya huduma hii, hivyo wananchi wanahitaji kuelemishwa
ili kuhakikisha wanajua wajibu wao na haki zao na kuwa na matumizi
sahihi ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA).
Akizungumzia kikao cha Wizara na taasisi zilizo chini ya Wizara hiyo cha
mapato na matumizi Dkt. Ndugulile amesema kuwa lengo ni kusimamia
nidhamu na matumizi ya fedha za taasisi hizo badala ya kusubiri mpaka
mwisho wa mwaka CAG aje kuhoji.
“Sisi kama Wizara tunajipanga kuhakikisha fedha zinazopatikana zinaelekezwa katika kute
keleza majukumu ya msingi ya Wizara na taasisi zake ikiwa ni pamoja na kwenda kutekeleza miradi ya maendeleo.
Dkt.
Ndugulile amezielekeza taasisi zilizo chini ya Wizara yake kutolea
ufafanuzi maeneo ambayo yaliguswa katika taarifa ya CAG na kama kuna
hoja zozote ziliyojitokeza zijibiwe kikamilifu na kuwasilishwa ndani ya
wiki ijayo na taasisi ambazo hazikuwasilisha hesabu zao kwa CAG watoe
maelezo kwa nini hawakuziwasilisha kwa mujibu wa taratibu za Serikali
Naye Naibu Waziri wa Wizara hiyo Mhe. Kundo Mathew amezitaka taasisi
zilizo chini ya Wizara hiyo kufanya kazi kwa ushirikiano kwa kutambua
kuwa Wizara inayowasimamia ipo makini kuhakikisha taasisi hizo
zinatimiza wajibu wake wa kuhudumia wananchi na yeye kama msaidizi wa
Waziri mwenye dhamana atashirikiana na Katibu Mkuu wa Wizara hiyo na
Naibu wake kuhakikisha kuwa Wizara na taasisi zake zinafanya kazi zenye
ubora na kwa wakati ikiwa ni pamoja na kuandaa taarifa zinazojitosheleza
bila kusubiri maelekezo.
Kikao hicho kilihudhuriwa na Katibu
Mkuu wa Wizara hiyo Dkt. Zainab Chaula, Naibu wake Dkt Jim Yonazi,
Wakuu wa taasisi za Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA), Shirika la
Mawasiliano Tanzania (TTCL), Tume ya Taifa ya Tehama (ICTC), Shirika la
Posta Tanzania (TPC), Mfuko wa Mawasiliano kwa Wote (UCSAF) na Baraza la
Ushauri la Watumiaji wa Huduma za Mawasiliano (TCRA-CCC), Menejimenti
ya Wizara pamoja na baadhi ya watendaji wa taasisi zake.
No comments:
Post a Comment