Katibu Mkuu wa Wizara ya Madini, Profesa Simon Msanjila amesema kuwa katika kipindi cha mwaka 2020 Sekta ya Madini ilikua kuliko sekta nyingine huku ikiongoza pia kwa kuliingizia Taifa fedha za kigeni
Profesa
Msanjila ameyasema hayo leo tarehe 27 Aprili, 2021 kwenye ufunguzi wa
kikao cha pili cha baraza la wafanyakazi wa Tume ya Madini ambalo
linajumuisha Wajumbe kutoka Makao Makuu, Ofisi za Maafisa Madini Wakazi
wa Mikoa, Kamishna wa Kazi, Viongozi wa TUGHE ngazi ya Taifa, Mkoa na
Tawi la Tume ya Madini.
Alisema kuwa, tangu kuanzishwa kwa Wizara
ya Madini, mchango wa Sekta ya Madini kwenye Pato la Taifa umeendelea
kukua kwa kasi na kusisitiza kuwa lengo la Wizara ni kuhakikisha mchango
wa Sekta ya Madini kwenye Pato la Taifa unafikia asilimia 10 ifikapo
mwaka 2025.
Alisema kuwa, Wizara ya Madini imeweka mikakati
mbalimbali ili kuhakikisha wananchi wote wananufaika na rasilimali za
madini ikiwa ni pamoja na kuongeza kasi ya utoaji wa leseni za madini
kwa wachimbaji wadogo wa madini, ushirikishwaji wa watanzania kwenye
sekta ya madini, wawekezaji kutoa huduma za jamii kwenye maeneo yenye
shughuli za uchimbaji wa madini na uanzishwaji wa masoko na vituo vya
ununuzi wa madini nchini.
Katika hatua nyingine, Profesa Msanjila
akielezea mafanikio ya Sekta ya Madini, tangu kuanzishwa kwa Wizara ya
Madini alisema kuwa kasi ya utoaji wa leseni imeongezeka ambapo katika
kipindi cha mwezi Julai 2020 hadi Machi, 2021, Wizara kupitia Tume ya
Madini ilitoa leseni za madini 8709 na uanzishwaji wa Ofisi za Maafisa
Madini Wakazi wa Mikoa na Maafisa Migodi Wakazi ili kusogeza huduma
karibu na wananchi.
Profesa Msanjila aliendelea kutaja mafanikio
mengine kuwa ni pamoja na uanzishwaji wa masoko ya madini 39 na vituo
vya ununuzi wa madini 50 ili kuhakikisha wachimbaji wadogo wa madini
wanapata masoko ya uhakika ya madini yao, kuimarika kwa udhibiti wa
utoroshaji wa madini kupitia ujenzi wa ukuta wa Mirerani na kuimarisha
ulinzi kwenye viwanja vya ndege na mipakani na usimamizi dhabiti wa
mazingira kwenye shughuli za uchimbaji wa madini nchini.
Aidha,
aliwapongeza watendaji wa Tume ya Madini wakiongozwa na Mwenyekiti wa
Tume wa Madini, Profesa Idris Kikula, kwa usimamizi mzuri uliopelekea
mafanikio ya Wizara ya Madini na kusisitiza kuwa Wizara ya Madini
itaendelea kutatua changamoto zilizopo.
"Ninafahamu kabisa zipo
changamoto zilizopo kwenye usimamizi wa Sekta ya Madini hususan kwenye
ukusanyaji wa maduhuli, masoko ya madini na vituo vya madini
vilivyoanzishwa, kama Wizara tunaendelea kuzitatua pamoja na kuweka
mazingira mazuri ya kazi ikiwa ni pamoja na ujenzi wa Ofisi za Maafisa
Madini Wakazi wa Mikoa, ununuzi wa vifaa vya kazi na maboresho ya
maslahi ya watumishi.
Naye Mwenyekiti wa Tume ya Madini, Profesa
Idris Kikula akizungumza kwenye ufunguzi wa baraza hilo alimshukuru Rais
wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan kwa kuaminiwa
na kuteuliwa tena kuendelea kuisimamia Tume ya Madini kwenye utekelezaji
wa majukumu yake.
Aidha, aliishukuru Wizara ya Madini kwa
maboresho ya ofisi za Tume ya Madini mikoani pamoja na ujenzi wa jengo
la makao makuu ya Tume ya Madini jijini Dodoma ambapo ujenzi wake
unatarajiwa kukamilika mapema Januari, 2022.
Naye Kaimu Katibu
Mtendaji wa Tume ya Madini, Mhandisi Yahya Samamba akizungumza kupitia
mahojiano maalum na waandishi wa habari alieleza kuwa lengo la kikao cha
pili cha baraza la wafanyakazi lilikuwa ni kujadili changamoto za
utendaji kazi pamoja na kuzipatia ufumbuzi, kupitia bajeti kwa mwaka wa
fedha 2021-2022 na kupewa mafunzo mbalimbali.
Aliongeza kuwa yeye kwa kushirikiana na menejimenti ya Tume ya Madini amejipanga kuhakikisha Sekta ya Madini inaendelea kukua kwa kasi kwa kufuata sheria na kanuni za madini kwa ubunifu na uzalendo wa hali ya juu.
No comments:
Post a Comment