Matokeo chanyA+ online




Wednesday, June 9, 2021

EPUKENI MAPUNGUFU KATIKA KUSIMAMIA MIRADI ILI KUONDOKANA NA HOJA ZA UKAGUZI


Na Anthony Ishengoma-Shinyanga

Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga Dkt. Philemon Sengati amezitaka Halmashauri za Mkoa wa Shinyanga kuhakikisha zinakuwa na miradi inayozingatia masharti ya kitaalamu ikiwemo usanifu, michoro na taratibu za manunuzi zilizowekwa na Serikali ili kuepukana na hoja za ukaguzi.

Dkt. Sengati amesema hayo leo Katika Manispaa ya Kahama alipokaribishwa kwa mara ya kwanza na wadau mbali mbali kutoka Wilaya ya Kahama na kuwataka watendaji na viongozi katika Wilaya hiyo kuwa na fikra za kimapinduzi zitakazo sukuma maendeleo ya mkoa na Taifa kwa ujumla.

Dkt. Sengati pia amewataka viongozi wa Halmashauri kuweka katika mipango yao miradi yote inayoibuliwa na Halmashauri ili miradi hiyo isije kuonekana na miradi hewa lakini pia kuwataka watendaji hao kuhakikisha wanatenga fedha kwa ajili ya masuala ya lishe.

Aidha Dkt. Sengati amekumbusha kuwa Halmashauri zimekuwa zikijisahau kutenga sh.1000 kwa ajili ya mipango ya lishe au kutenga fedha lakini fedha izo zimekuwa hazipelekwi kama inavyokusudiwa na hivyo kusababisha masuala ya lishe nchini kushindwa kupimika.

‘’Fedha nyingi zinaenda kwenye posho na kwenye mambo ya kiuendeshaji na bahati mbaya baadhi ya Taasisi zimekuwa hazitekelezi miradi yenye mashiko kwa kipindi cha mwaka mzima’’. Aliongeza Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga Dkt. Philemon Sengati.

Naye Katibu Tawala Mkoa wa Shinyanga Dkt. Batlida Buriani amewapongeza Wilaya ya Kahama kwa ujenzi wa shule nyingi na kuongeza kuwa hiyo haitoshi bali juhudi za kuhakikisha ufaulu unaongezeka zinatakiwa ili kuhakikisi kasi ya ujenzi wa shule katika Wilaya ya Kahama.

Adha Dkt. Buriani ameongeza kuwa Wilaya hiyo inapaswa kuangazia upya suala la ugonjwa wa ukumwi ambapo Wilaya ya Kahama haijafanya vya kutosha kuhakikisha maambukizi ya Ukimwi yanapungua.

Mkuu wa Wilaya ya Kahama Bw. Anamlingi Macha amesema wachimbaji wadogo wadogo wamekuwa na mchango mkubwa katika uchumi wa Halmashauri za Wilaya ya Kahama ambapo kwa mwaka wa fedha 2020/21 jumla ya kilo takribani elfu 1.7 zilitokana na wachimabaji wadogo.

Naye Mwenyekiti wa Baraza la Wazee Wilaya ya Kahama Mzee Wilfred Bilago amesema Wilaya ya Kahama imekuwa ikifanya vizuri katika kuhakikisha wazee wilayani humo wanapatiwa huduma za Bima ya Afya iliyoboreshwa.

Mkuu wa mkoa wa Shinyanga pamoja na Katibu Tawala wa Mkoa huo wako katika Wilaya ya Kahama kwa ajili ya kukutana na wadau wa Wilaya hiyo lakini pia kukutana na viongozi na baadhi ya wananchi wa Wilaya hiyo.



No comments:

Post a Comment