Na WAMJW - Dodoma
Kuelekea
Siku ya Mtoto wa Afrika, Serikali inatarajia kuzindua Makao ya Taifa ya
Malezi na Makuzi ya Watoto yaliyojengwa katika Kata ya Kikombo, jijini
Dodoma.
Akizungumza leo na Waandishi wa Habari jijini Dodoma,
Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia ,Wazee na Watoto, Dkt Dorothy
Gwajima amesema Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe.
Dkt. Isdor Mpango atazindua makao hayo wakati wa Maadhimisho ya Siku ya
Mtoto wa Afrika yatakayofanyika tarehe 16 mwezi huu.
Dkt.
Gwajima amesema lengo la kujengwa kwa makao hayo ni kutatua changamoto
za makao ya Taifa ya awali yaliyokuwa Kurasini Dar es Salaam za ufinyu
wa maeneo ya shughuli mbalimbali ikiwemo michezo, bustani, ujasiriamali
na ufugaji kutofanyika sawasawa hivyo kufanya hali ya lishe na uchumi
kuwa duni.
" Ujenzi huu ni sehemu ya utekelezaji wa mpango wa
Taifa wa Kimkakati wa kuwatambua, kutengamanisha na kuwaunganisha na
familia watoto wanaoishi katika mazingira hatarishi, pia ni utekelezaji
wa maagizo ya Mhe. Rais kuwa watoto wanaotunzwa kwenye makao waandaliwe
mapema kadri inavyowezekana kuwaunganisha na familia ili kuwawekea
msingi wa malezi" alisema Dkt. Gwajima.
Ameongeza pia watoto
wanatakiwa kukaa kwenye makao kwa muda tu na wakiisha kuimarika
warejeshwe kwenye makazi ya kawaida iwe ya kambo au kuasili ili waishi
kawaida katika familia.
Dkt. Gwajima amesema, uzinduzi huo
utaambatana na uzinduzi wa vituo vya Jamii vya malezi, Makuzi na
Maendeleo ya awali ya watoto pamoja na Baraza la Taifa la Watoto hapo
tarehe 14 mwezi huu.
Aidha, Dkt. Gwajima ametoa rai kwa wazazi na
jamii kwa ujumla kuhakikisha wanatimiza jukumu la malezi ya watoto wao
na kuwa, hatua ya kulelewa katika makao iwe ni ya mwisho baada ya hatua
zote kushindikana.
Mradi wa Ujenzi wa Makao ya Watoto Kikombo,
umetekelezwa kwa Ushirikiano kati ya Serikali kupitia Wizara ya
Afya,Maendeleo ya Jamii,Jinsia ,Wazee na Watoto na Shirika la ABBOT
Fund Tanzania na Makao hayo yana uwezo wa kuhudumia watoto 250 kwa
wakati mmoja na hadi sasa watoto wanaohudumiwa katika Makao hayo ni 28.
Wednesday, June 9, 2021
SERIKALI KUZINDUA MAKAO YA TAIFA YA WATOTO WAISHIO MAZINGIRA HATARISHI
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment