Na Stephano Mango, Namtumbo
Wannachi kutoka katika koo 16 wa Kijiji cha Mchomoro kilichopo katika Halmashauri ya Wilaya ya Namtumbo Mkoani Ruvuma wamemuomba Waziri wa ardhi , nyumba na maendeleo ya makazi William Lukuvi kuingilia kati utatuzi wa mgogoro wa ardhi yao zaidi ya heka 700 kati yao na Mkuu wa Wilaya hiyo Mstaafu Luckness Amlima ili waweze kuendelea na shughuli zao za kimaendeleo kuliko mateso ambayo wanayapa hivi sasa ya kufunguliwa kesi kila wanapoenda katika mashamba yao.
Wakizungumza na waandishi wa habari waliofika katika kijiji hicho jana wawakilishi wa koo 16 zenye familia zaidi ya 68 walisema kuwa mgogoro huo umedumu kwa zaidi ya miaka mitano sasa na kwamba viongozi wa kijiji na Wilaya wamekuwa wakipuuzia mgogoro huo kwa sababu zao binafsi hali ambayo inaashiria kuwa ni kumpendelea mkuu huyo wa Wilaya mstaafu kwa kuwa alisaidiwa na baadhi ya viongozi kujimilikisha maeneo hayo kinyume na utaratibu
Akizungumza kwa niaba ya koo hizo Rashid Malamaye alisema kuwa mkuu huyo wa Wilaya amevamia katika maeneo yao ya asili ambayo wao walikuwa wanayatumia kwa shughuli za kilimo na ufugaji toka miaka mingi lakini cha kushangaza kwa sasa wanataka kudhulumiwa mashamba yao na mkuu huyo mstaafu
Malamaye alisema kuwa katika mashamba hayo kulikuwa na nyumba za nyasi lakini zimechomwa moto, mazao ya muda mrefu aina ya minazi, machungwa,migomba na mihogo lakini cha kushangaza mazao hayo yamefyekwa bila wao kujulishwa na kuwekwa walinzi ambao wamekuwa wakiwapiga wananchi ambao wanakwenda katika mashamba hayo na kuwafungulia mashataka mbalimbali kwa lengo la kuwanyanyasa
“Tumeshtushwa sana na kitendo hicho cha uharibifu wa mazao yetu na uvamizi wa mashamba hayo ambayo yapo katika maeneo ya mihane katika kitongoji cha Nyerere na mwekezaji ambaye aliwahi kuwa mkuu wa Wilaya bila sisi wenye maeneo kujulishwa na hata tulipolalamika kwenye uongozi wa kijiji na Wilaya hakuna hatua zinazochukuliwa dhidi yake”alisema Malamaye
Naye Issa Languka alisema kuwa mara baada ya kutokea kwa uvamizi huo walitoa taarifa katika uongozi wa kijiji na kwenye uongozi wa Chama cha Mapinduzi lakini majibu waliyoyatoa kuwa mwekezaji huyo yupo kihalali bila kufafanua sheria ipi au mkutano gani wa hadhara ambao ulihalarisha mwekezaji huyo kupewa heka zaidi ya 700 na kijiji kinyume na sheria za ardhi
Languka alisema kuwa inasikitisha sana kuona kuwa viongozi wa kijiji badala ya kulinda raia na mali zao wao wamekuwa chanzo cha kutengeneza migogoro kinyume na kiapo chao cha uadilifu ambacho waliapa na mara kadhaa wamekuwa wakitoa taarifa za uongo kuhusu mgogoro huo
Alifafanua kuwa hali iliyopo kwasasa sio nzuri kwani wenye mashamba wamekuwa wakienda kufanya shughuli zao wanakamatwa na kufunguliwa kesi mbalimbali katika kituo cha polisi Wilaya ya Namtumbo hali ambayo inazidisha uhasama kati ya wananchi na mwekezaji huyo.
Alisema kuwa kutokana na kitendo hicho tumemwandikia Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma Christine Mdeme kumjulisha madai yetu ili aweze kuchukua hatua stahiki kwani mwenendo wa viongozi wa Wilaya ya Namtumbo dhidi ya mgogoro husika hauridhishi na hatuna imani nao kwani ni zaidi ya mwaka wa nne sasa wameshindwa kuukomesha.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa kijiji hicho Said Mohamed Mkalela alikili kuwepo kwa mgogoro huo na kusema kuwa hatua zinaendelea kuchukuliwa ingawa wananchi hao wamekuwa wakikosa imani kutokana na kuchelewa kumalizika kwa mgogoro huo
Mkalela alisema kuwa wao waliingia madarakani mwaka 2019 lakini nyaraka zinaonyesha mwekezaji huyo alipata eneo la heka 40 kihalali toka mwaka 2016 katika maeneo ya namambigi na sio mihane, lakini hatua za kutatua mgogoro huo zinaendelea ingawa wananchi wanateseka.
Naye Mkuu wa Wilaya mstaafu Luckness Amlima alipotafutwa ili kuelezea mgogoro huo alisema yeye hautambui mgogoro huo bali waulizwe viongozi wa kijiji husika na sio yeye kwani yeye amepewa na viongozi wa kijiji hicho kwa kufuata utaratibu waliokubaliana
Amlima alipotakiwa kusema kuwa ni eneo lipi ambalo alipewa kisheria lakini aliendelea kusema kuwa yeye na wenzake 16 waliomba mashamba na walipewa na mkutano wa kijiji mwaka 2017 lakini yeye haelewi kuwa ni wapi ambapo alikabidhiwa hivyo wanao weza kujibu malalamiko hayo ni viongozi wa vijiji
Kwa upande wake Katibu Tawala wa Wilaya hiyo aden Nchimbi alikiri kuusikia mgogoro huo na kuagiza wahusika kwa kushirikiana na Afisa ardhi wa Halmashauri kukutana na kuumaliza mgogoro huo ili kuwaondolea kero wananchi
Kwa upande wake Mbunge wa Jimbo la Namtumbo Vita Kawawa alipotafutwa ili aweze kuzungumzia mgogoro huo alisema atafutwe baadae kwani kwasasa yupo kwenye shughuli za Bunge.
No comments:
Post a Comment