Matokeo chanyA+ online




Wednesday, July 7, 2021

WAZIRI MKENDA ATUA SIMIYU//AZINDUA KAMPENI YA KITAIFA YA KUONGEZA UZALISHAJI NA TIJA KATIKA ZAO LA PAMBA


Waziri wa Kilimo Mhe Prof. Adolf Mkenda akisisitiza jambo wakati Akizindua kampeni ya Kuongeza Tija katika zao la Pamba iliyofanyika Kijiji cha Kijereshi Wilaya ya Busega Mkoani Simiyu tarehe 4 Julai 2021. (Picha Zote Na Mathias Canal, Wizara ya Kilimo)
Waziri wa Kilimo Mhe Prof. Adolf Mkenda akikata utepe kuashiria kuzindua kampeni ya Kuongeza Tija katika zao la Pamba iliyofanyika Kijiji cha Kijereshi Wilaya ya Busega Mkoani Simiyu tarehe 4 Julai 2021.
Waziri wa Kilimo Mhe Prof. Adolf Mkenda akisisitiza jambo wakati alipotembelea na kukagua shamba darasa la Pamba wakati wa uzinduzi wa kampeni ya Kuongeza Tija katika zao la Pamba iliyofanyika Kijiji cha Kijereshi Wilaya ya Busega Mkoani Simiyu tarehe 4 Julai 2021.
Balozi wa Pamba Tanzania Ndg Agrey Mwanri akitoa elimu kwa wakulima wa Pamba kuhusu namna bora ya kulima, kupanda kwa kufuata mistari kabla ya kumkaribisha mgeni rasmi-Waziri wa Kilimo Mhe Prof. Adolf Mkenda kuzindua kampeni ya Kuongeza Tija katika zao la Pamba iliyofanyika Kijiji cha Kijereshi Wilaya ya Busega Mkoani Simiyu tarehe 4 Julai 2021.
Mkurugenzi Mkuu wa Bodi ya Pamba Ndg Marco Mtunga akitoa ufafanuzi juu ya dhamira ya Bodi kuhakikisha Tija inaongezeka kwenye zao la Pamba mbele ya mgeni rasmi-Waziri wa Kilimo Mhe Prof. Adolf Mkenda kabla ya kuzindua kampeni ya Kuongeza Tija katika zao la Pamba iliyofanyika Kijiji cha Kijereshi Wilaya ya Busega Mkoani Simiyu tarehe 4 Julai 2021.
Sehem ya wananchi wa Wilaya ya Busega wakifuatilia maelezo ya wataalamu kuhusu namna bora ya kulima zao la Pamba kabla ya rasmi-Waziri wa Kilimo Mhe Prof. Adolf Mkend kuzindua kampeni ya Kuongeza Tija katika zao la Pamba iliyofanyika Kijiji cha Kijereshi Wilaya ya Busega Mkoani Simiyu tarehe 4 Julai 2021.

Na Mathias Canal, Wizara ya Kilimo-Simiyu

“Tija ya zao la pamba kwa sasa ni kilo 200 hadi 300 kwa ekari. Taarifa nilizonazo, tunaowakulima wanozingatia kanuni 10 za kilimo bora cha pamba na tija yao ni kati ya kilo 1,000 na 1,200 kwa ekari. Tanzania ina fursa kubwa ya kuongeza uzalishaji wa pamba kutoka wastani wa tani 300,000 hadi tani 1,000,000”      

Waziri wa Kilimo Mhe Prof. Adolf Mkenda ameyasema hayo tarehe 5 Julai 2021 wakati Akizindua kampeni ya Kuongeza Tija katika zao la Pamba iliyofanyika Kijiji cha Kijereshi Wilaya ya Busega Mkoani Simiyu.

“Kwa lengo la kufikia lengo la kuzalisha tani 1,000,000 ifikapo mwaka 2025 kama ilivyoainishwa kwenye ilani, leo ni siku muhimu sana. Nimezindua kampeni ya kuongeza tija katika zao la pamba. Wizara iliona ni muhimu kuendesha kampeni kabambe ya kuwahamasisha wakulima wa pamba kuzingatia kanuni 10 za kilimo bora cha pamba” Amekaririwa Waziri Mkenda

Amesema Kwa kuwa pamba inazalishwa katika Mikoa 17 nchini, hivyo Wakuu wa Mikoa na viongozi wote katika ngazi mbalimbali, wanapaswa kuunga mkono juhudi hizo ikiwemo Wabunge kusaidia kuelimisha wananchi katika maeneo yao ili kilimo cha pamba kiwe mkombozi wa maisha wakulima na watanzania kwa ujumla wake.

Waziri Mkenda amesema kuwa kilimo kinakabiliwa na tatizo kubwa la tija kuwa ndogo sana karibu katika kila zao. Hali hiyo inasababisha pato la mkulima kuwa chini.

”Wizara yangu imelitambua tatizo hili la msingi na kwamba tuna jukumu kwanza la kuuelimisha umma na wakulima kwa ujumla juu ya umuhimu wa kuangalia pato la mkulima kama kigezo cha ufanisi katika shughuli zote za kilimo. Pili tuna wajibu wa kuweka mazingira sahihi ili kila mkulima nchini wa zao lolote abadili maisha yake kutokana na shughuli yake. Hivyo, kwa nafasi ya pekee niwapongeze Wadau wa Pamba kuwa wa kwanza kutekeleza maono ya Wizara ya Kilimo katika kuongeza tija” Amesema Waziri Mkenda

Waziri wa Kilimo amesem akuwa Kipato cha mkulima kinategemea kiasi mkulima anachozalisha kwa ekari, ubora wa zao na bei ambayo soko liko tayari kulipa. Mkulima yoyote ana uwezo wa kupata tija kubwa na kuzalisha zao bora. “Muda umefika wa viongozi na wakulima kuelewa kwamba tija ikiwa kubwa kwa bei yoyote itakayokuwepo sokoni, pato litakuwa kubwa” Amesisitiza

Waziri Mkenda amesema kuwa ili kilimo kiweze kutoka kwenye tija ndogo, suala la kuboresha utoaji wa huduma za ugani ni la lazima. Katika mwaka huu wa fedha jumla ya Pikipiki 1,500 zitanunuliwa na kusambazwa katika mikoa mbalimbali baada ya kutosheleza Mikoa ya Dodoma, Singida na Dodoma.

Amesema kuwa kuwa Lengo ni kufanya vizuri katika Mikoa 3 ili mwaka ujao kujipima kiasi cha mafanikio na kuongeza nguvu kuifikia mikoa mingine; ikiwa ni pamoja na Maafisa Ugani kupatiwa mafuta  ili kuwawezesha kutekeleza majukumu yao; na Ili kuimarisha usimamizi vyombo vya usafiri vitafungiwa GPS.

Kwa upande wake Balozi wa Pamba Tanzania Ndg Geofrey Mwanri akizungumza wakati wa uzinduzi huo amesema kuwa ili tija iweze kuongezeka kwenye zao la Pamba ni lazima wakulima Kubadili vipimo vya kupandia kutoka 90x40cm na kuwa 60x30cm ambapo idadi ya mimea kwa ekari itaongezeka kutoka 22,222 hadi 44,400. Mabadiliko yanafanyika baada ya kukamilika kwa utafiti uliofanywa na TARI Ukiriguru na kuonesha ongezeko kubwa la tija kufikia kilo 1,000 kwa ekari.

Mwanri amesema kuwa wakulima wanapaswa Kusomba samadi na kusambazwa mashambani ili kurutubisha udongo ambapo wakulima wa pamba wanapaswa kuondokana na matumizi ya jembe la palizi la kukokotwa na wanyamakazi. Hatua hii itarahisisha palizi kufanyika kwa saa 2 kwa ekari badala ya siku 7 kwa jembe la mkono;

Kwa upande wake Mkurugenzi Mkuu wa Bodi ya Pamba  Ndg Marco Mtunga amesema kuwa Bodi ya Pamba imejipanga Kuimarisha huduma za ugani, Kusambaza kamba za kupandia katika wilaya zote ili kuwezesha wakulima wa pamba kuzingatia vipimo vipya vya upandaji; na Pembejeo zote ikiwemo mbegu, viuadudu, vinyunyizi kusambazwa kwa wakati.

Ameongeza kuwa katika maeneo yote ya usukumani na mikoa inayolima Pamba wakulima hawana tatizo la nguvu kinachokosekana ni maarifa machache yanayopatikana kwenye kilimo cha Pamba.

Hata hivyo amewapongeza wakulima wa Pamba kote nchini kwa kuitikia mwito wa serikali wa kuhakikisha uzalishaji unaongezeka katika msimu wa mwaka 2020/2021 hivyo amewaomba wananchi kuitikia tena mwito wa serikali kuhakikisha kuwa uzalishaji na tija unazidi kuongezeka.


No comments:

Post a Comment