Waziri Mkuu Kassim Majaliwa amesema
Serikali haijamlazimisha na wala haitamlazimisha mwananchi kuchanjwa
chanjo ya ugonjwa wa UVIKO 19, hivyo amewataka Watanzania wapuuze
upotoshaji unaosambazwa kupitia mitandao ya kijamii.
"Hakuna
aliyelazimishwa kuchanja chanjo hiyo na wala hakuna mahali palipoandikwa
kwamba lazima wananchi wachanjwe. Chanjo ni hiari tusipotoshane kwa
sababu hakuna Serikali inayoweza kuandaa mpango wa kuwaangamiza wananchi
wake."
Waziri Mkuu ameyasema hayo leo (Jumanne, Julai 27, 2021)
wakati akizungumza na wananchi wa wilaya ya Ruangwa kwenye mkutano wa
hadhara uliofanyika katika kijiji cha Nandagala ambapo amewasisitiza
waendelee kuchukua tahadhari na kujikinga na UVIKO 19.
Mheshimiwa
Majaliwa amesema Serikali imeleta chanjo hiyo ili kutoa fursa kwa
Watanzania watakaohitaji kuchanjwa kwa ajili ya kujikinga na ugonjwa wa
UVIKO 19 waweze kuipata kwa ukaribu na urahisi zaidi na si vinginevyo.
Kadhalika,
Mheshimiwa Majaliwa amewasisitiza Watanzania waendeleze tabia ya kunawa
mikono mara kwa mara na maji safi yanayotiririka na sabuni, watumie
vitakasa mikono pamoja na kuvaa barakoa zilizothibitishwa na mamlaka
husika.
Mbali na maelekezo hayo, Pia Waziri Mkuu amesema ni vema
kwa sasa wananchi wakajiepusha na mikusanyiko isiyokuwa ya lazima na
inapolazimu basi wazingatie kukaa umbali wa mita moja au zaidi kutoka
mtu mmoja hadi mwingine lengo likiwa ni kujikinga na UVIKO 19.
Mheshimiwa
Majaliwa amesema wananchi wanatakiwa wafanye mazoezi ya mara kwa mara
kulingana na afya zao pamoja na mazingira yanayowazunguka, pia amewasihi
wazingatie lishe bora.
Katika hatua nyingine, Mheshimiwa
Majaliwa amewahakikishia wananchi wa wilaya ya Ruangwa kwamba Serikali
imedhamiria kumaliza tatizo la upatikanaji wa huduma ya maji safi na
salama katika wilaya yao na Tanzania kwa ujumla, hivyo waendelee
kuiamini Serikali yao.
Waziri Mkuu amesema Serikali inatekeleza
kampeni ya kumtua mama ndoo kichwani ili kuhakikisha wananchi wote
nchini wanapata huduma hiyo karibu na maeneo yao ya makazi. Amewataka
waendelee kuiamini Serikali yao kwa sababu imedhamiria kuwatumikia.
Amesema
tatizo la maji wilayani Ruangwa linaenda kuwa historia kwa sababu
Serikali inatekeleza ujenzi wa mradi wa maji wa Mbwinji ambao unatoa
maji Ndanda hadi Ruangwa. “Mradi huu mkubwa utapunguza tatizo la
upatikanaji wa maji wilayani Ruangwa.”
Kwa upande wake, Waziri wa
Maji Jumaa Aweso amemuhakikishia Waziri Mkuu kwamba atasimamia ipasavyo
kuhakikisha mradi wa maji wa Mbwinji-Ruangwa unakamilika kwa wakati ili
wananchi wa wilaya hiyo waweze kuondokana na tatizo la upatikanaji wa
maji safi na salama.
Aweso amesema Serikali ya Awamu ya Sita
inayoongozwa na Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan imedhamiria kumaliza
tatizo la upatikanaji wa huduma ya maji safi na salama katika maeneo
yote nchini, amewaomba wananchi waendelee kuwa na subra.
No comments:
Post a Comment