Na.WAMJW-Nairobi
Tanzania
na Kenya wamekubaliana ndani ya wiki nne zijazo kufanyia kazi
changamoto kubwa nne katika eneo la kupima wasafiri UVIKO 19.
Makubaliano
hayo yamefanyika leo kwenye mkutano wa pamoja baina ya Mawaziri wa Afya
wa Tanzania Dkt. Dorothy Gwajima na Waziri wa afya nchini Kenya Sen.
Mutahi Kagwe mjini Nairobi.
Moja ya makubaliano ya kufanyia kazi
changamoto hizo ni pamoja na kushusha gharama za upimaji wa UVIKO-19 kwa
wasafiri wanaoingia na kutoka katika nchi hizo mbili ili kuchochea
masuala ya biashara na utalii baina na nchi hizo mbili.
Nchi hizo
pia zimekubaliana kufanyia kazi changamoto ya kulipisha fedha kipimo
cha haraka cha Corona (PCR) kwa wasafiri wanaotumia njia ya barabara
ikiwemo kuona uwezekano wa kushusha kwa kiasi kikubwa gharama hizo kwa
wasafiri wanaotumia ndege.
Kwa upande wa madereva wanaosafirisha
mizigo na bidhaa muhimu wamekubaliana kufanyia kazi uwezekano wa
kutokutozwa gharama kwa kipimo cha Corona ili kupunguza mzigo kwa
wasafirishaji ikiwa ni njia ya kuchochea uchumi kwa nchi hizo mbili.
Aidha
Tanzania na Kenya wamekubaliana kuona uwezekano wa kutumia mifumo ya
kielektroniki kwa ajili ya kufuatilia afya za wasafiri pamoja na
kudhibiti wasafiri wasio kuwa waaminifu kwa kugushi vyeti hivyo
wanapopita mipakani.
Hata hivyo katika mkutano huo Mawaziri hao
wamekubaliana kufanyia kazi mpango wa kuvitambua vyeti vya upimaji
vinavyotolewa na mamlaka za afya za nchi hizo mbili, pamoja na
kubadilishana taarifa zinazohusu masuala ya afya ili kuimarisha udhibiti
wa magonjwa mbalimbali yanayowaathiri wananchi wa pande hizo mbili
ikiwemo Malaria, Polio na Corona.
Akiongea wakati wa mkutano na
Waandishi wa Habari Waziri wa Afya Dkt. Gwajima amesema kuwa tatizo la
ugonjwa wa Corona ni la dunia nzima hivyo lazima kuangalia ni namna
gani halitowadhuru sana ili uchumi na ustawi wa jamii na nchi uendelee
kwa kuweka makubaliano ya kuishi kwa Amani kama watu wanaoishi katika
kijiji kimoja cha afrika mashariki.
Dkt. Gwajima amesema ugonjwa
huo uliowafika hauwezi kuwaacha iwapo kutakuwa hakuna suluhu ya pamoja
ya kuudhibiti kwani hadi sasa ugonjwa huu umetufundisha mengi na
viongozi wa nchi zote mbili wamekuwa wakitoa maono mengi. Hivyo, kama
Mawaziri wenye dhamana kwa kushirikiana na wataalam watahakikisha
wanatafsiri dhamira ya viongozi wakuu wa nchi ili kuja na uhalisia.
Aliongeza
kuwa janga hilo ni kubwa hivyo ni lazima kuendelea kushirikiana katika
kudhibiti na kuzuia anuai mpya za ugonjwa wa Corona kwa pamoja kwani
miundombinu ya uchumi inashuka katika nchi zetu na kwa jamii pia.
"Baada
ya kutokea janga hilo wasafiri na madereva walikua wanatakiwa kuendelea
kusafirisha abiria,mizigo na bidhaa muhimu hivyo kubwa ni lazima kuweka
jitihada ili kuwarahisishia wananchi kuendelea na shughuli za uchumi na
maisha kwa usalama kwa ushirikiano baina ya nchi zetu hizi”.
Naye
Waziri wa Afya nchini Kenya Sen.Mutuhi Kagwe amesema kwamba Tanzania
na Kenya ni majirani wa muda mrefu hivyo vyovyote watakacho fanya
hawawezi kuwaacha majirani zao ambao ni Tanzania.
Katika
kukabiliana na Corona Waziri Kagwe amesema lazima kujifunza kuishi nao
hivyo ni jambo la kuelewa kwamba hakuna nchi itakayokuwa na nguvu bila
kushirikiana.
“Sisi ni wamoja lazima tuendelee kujisaidia
wenyewe Katika mapambano haya na vile vile kwenye Malaria,Polio kwa
wananchi wetu mipakani” Alisisitiza.
Aliongeza kwamba nchi hizo mbili zina mashirikiano ya muda mrefu katika maeneo na sio tu masuala ya afya tu, hivyo wataimarisha ushirikiano hata katika maeneo mengine.
No comments:
Post a Comment