Matokeo chanyA+ online




Thursday, April 21, 2022

NENDENI MKAISHANGILIE SIMBA, AFRIKA KUSINI NI SALAMA - WAZIRI MCHENGERWA

 Na. John Mapepele


Waziri wa Utamaduni, Sanaa na Michezo. Mhe Mohamed Mchengerwa amewatoa hofu  mashabiki  wa soka wanaotaka kwenda Afrika Kusini kuishangilia Timu ya Simba katika mchezo wa raundi ya pili robo fainali ya Mashindano ya Kombe la Shirikisho  barani Afrika kuwa watakuwa salama.

Mhe. Mchengerwa ametoa kauli hiyo leo Aprili 21, 2022 kwenye Uwanja wa Taifa jijini  Dar es Salaam alipokuwa akiongea na Vyombo vya Habari.

"Niseme tu kwamba sisi kama Serikali tunafuatilia  kwa karibu usalama wa timu na hivi ninavyoongea nimemteua Msaidizi wangu Mkurugenzi wa Michezo ili aweze kuniwakilisha kusimamia hili" amefafanua Mhe. Mchengerwa

Aidha, Mhe. Mchengerwa amesema watanzania na waafrika Kusini ni ndugu wa muda mrefu hivyo ni mategemeo kuwa  hakutakuwa na jambo lolote linaloweza kuhatarisha usalama.
 
Ameeleza kuwa  katika mechi hiyo Timu ya Simba inakwenda kushindana  siyo kushiriki ili kuliwakilisha taifa  ambapo amewataka wachezaji kucheza kwa weledi na ari  kubwa ili ipige hatua katika hatua inayofuata hatimaye irudishe kombe nyumbani.

Akizungumzia kuhusu kuzisaidia timu za taifa,  Mhe. Mchengerwa tayari Serikali imeshatoa fedha kwa ajili ya kufanya maandalizi kwenye makambi yote  ya timu hizo.

Pia, amesema dhamira ya taifa  ni kushiriki kwenye Mashindano ya  Kombe la Mataifa ya Afrika (AFCON) na kuratibu mashindano hayo hapa hapa nchini.

Amesema tayari Serikali inafanya maandalizi hayo kwa kuandaa timu bora zitakazofuzu  na kuandaa miundombinu ya michezo hiyo.

Katika hatua nyingine Mhe. Mchengerwa amesema kutokana na kuendelea kufanya vizuri, Tanzania imekuwa miongoni mwa nchi nane Afrika ambazo kombe la dunia litapita ambapo hapa nchini linatarajia kufika mwisho wa mwazi huu.



No comments:

Post a Comment