NA MWANDISHI WETU IRINGA
Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa
Dkt.Philip Mpango amewataka baadhi ya viongozi wanaochangia katika
uharibifu wa mazingira na vyanzo vya maji kuacha mara moja ili kunusuru
Taifa dhidi ya athari za uharibifu zinazojitokeza hivi sasa.
Makamu wa Rais amesema hay oleo tarehe 19 Desemba 2022 wakati
akifungua Kongamano la Wahariri na Wadau wa Uhifadhi Mazingira na
Utunzaji wa Vyanzo vya Maji linalofanyika katika Ukumbi wa Masiti mkoani
Iringa. Amesema ni vema viongozi kuachana na maslahi binafsi ili kunusuru
mito yote kwani madhara kwa jamii ya watanzania ni makubwa zaidi.
Makamu wa Rais amesema ni lazima kushirikiana na kuwa na jitihada za
pamoja baina ya serikali, dini, sekta binafsi, vyombo vya Habari pamoja na
vyama vya siasa katika kupambana na uharibifu wa Mazingira nchini.
Halikadhalika Makamu wa Rais amewaasa Waandishi wa Habari kuendelea
kutumia ushawishi walionao katika jamii kuihamasisha jamii kuhusu utunzaji
wa mazingira na kuziagiza taasisi za Serikali kuhakikisha zinawashirikisha
Waandishi wa Habari na Vyama mbalimbali vya Wanahabari vinavyojitoa
kushirikiana na Serikali katika kukabiliana na athari za uharibifu wa mazingira.
Pia amewasihi wahariri na waandishi kuandika habari na taarifa za kuelimisha
umma za kiuchunguzi na kuepukana na kuandika habari bila kufanya tafiti za
kutosha au kujiridhisha hivyo kupelekea habari za upotoshaji hapa nchini.
Makamu wa Rais amewaasa wahariri na wanahabari wote kwa ujumla kuwa
wazalendo na kulinda taswira na maslahi ya nchi kwa kuepuka kuwa mstari
wa mbele katika kutetea mambo yanayohujumu taifa.
Amewataka kujiepusha
na kupokea fedha, mali au vishawishi vingine kutoka kwa watu wachache
wenye jeuri ya pesa au madaraka ili kupindisha ukweli wa mambo kinyume
na maslahi ya taifa au wananchi wengi wanyonge wasio na sauti.
Pia ametoa wito kwa wanahabari wito kusaidia kuelimisha jamii kuhusu fursa
zitokanazo na utunzaji wa mazingira ikiwemo biashara ya Kaboni, inayofanyika
kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi duniani hususan, kwa kupunguza
gesijoto. Amesema biashara hiyo ni fursa ambayo itachangia katika pato la
Taifa na kuimarisha suala zima la uhifadhi wa mazingira.
Makamu wa Rais amewasihi kutumia Kongamano hilo kufanya mijadala ya
kina ya kujenga na kupata maazimio ambayo pamoja na mambo mengine,
yatajumuisha hatua mbalimbali zitakazochukuliwa katika kuongeza juhudi za
kuhabarisha umma kuhusu utunzaji na ulinzi wa mazingira hususan katika
Vyanzo vya Maji.
Kwa upande wake mwenyekiti wa Kituo cha Wanahabari Watetezi wa
Rasilimali na Taarifa (MECIRA) amesema wanahabari watetezi wa rasilimali
kwa umoja wao watahakikisha wanashiriki katika mapambano ya kuhakikisha
wanalinda na kuhifadhi na kutetea rasilimali za nchi ikiwemo suala la
mazingira. Aidha ametoa wito kwa mamlaka za usimamizi kuwasimamia
watendaji waliopewa dhamana ya ulinzi wa vyanzo vya maji ili waweze
kutimiza wajibu wao na kuepukana na athari za uharibifu zinazojitokeza hivi
sasa.
Wanahabari hao watetezi wa Rasilimali wamesema wameshuhudia mto Ruaha
ukifikisha siku 130 bila kutiririsha maji licha ya maji hayo kuwepo katika
chanzo cha mto ambao huzuiliwa na baadhi ya wananchi wachache
wanaofanya shughuli mbalimbali za kilimo jirani na mto huo.
Kongamano hilo linaratibiwa na Kituo cha Wanahabari Watetezi wa Rasilimali
na Taarifa (MECIRA) kwa kushirikiana na Jukwaa la Wahariri nchini na
linashirikisha wanahabari, wadau wa mazingira, viongozi wa serikali, dini,
vyama vya siasa pamoja na viongozi wa vyombo vya ulinzi na usalama.
No comments:
Post a Comment