Picha ya pamoja |
Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Mhe. January Makamba amekutana na kufanya mazungumzo na Waziri wa Mambo ya Nje wa India, Mhe. Dkt.Subrahmanam Jaishankar ikiwa ni maandalizi ya ziara ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan atakayoifanya nchini humo kuanzia tarehe 8 hadi 11 Oktoba 2023. Katika mazungumzo yao yaliyofanyika hivi karibuni jijini New Delhi, viongozi hao pamoja na mambo mengine wamelezea matarajio yao ya kuimarika zaidi kwa ushirikiano kati ya Tanzania na India kupitia ziara hiyo ya kihistoria. Kwa upande wake , Mhe. Makamba amemshukuru mwenyeji wake kwa kumkaribisha nchini humo lakini pia kwa maandalizi mazuri ya ziara ya Mhe. Rais Dkt. Samia nchini humo. Kadhalika, Mawaziri hao walibadilishana taarifa kuhusu ushirikiano uliopo baina ya nchi hizi mbili na kukubaliana kuongeza jitihada ili kufikia malengo ya pamoja ya kuinua kuwango cha biashara na uwekezaji kati ya nchi hizi mbili na kuhakikisha ushirikiano uliopo unazaa matokeo tarajiwa. Mhe. Rais Dkt. Samia anatarajiwa kuwasili India tarehe 8 Oktoba 2023 kwa ziara ya kitaifa ya siku tatu. Wakati wa ziara hiyo kutashuhudiwa ubadilishanaji wa mikataba mbalimbali ya ushirikiano katika sekta za uwekezaji, uchukuzi, afya, maji na nyingine nyingi. Ziara hiyo pamoja na mambo mengine inalenga kuimarisha ushirikiano kati ya Tanzania na India hususan kwenye maeneo ya kimkakati na manufaa kwa Tanzania ikiwemo afya, maji, elimu uchumi wa buluu, teknolojia, kilimo, na biashara na uwekezaji. |
No comments:
Post a Comment