Matokeo chanyA+ online




Thursday, December 3, 2020

WIZARA YA ARDHI YAWAFUATA WANANCHI KATIKA MITAA


Afisa kutoka kitengo cha Kodi Wizara ya Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Massaga Malunde (kulia) akimuelimisha mkazi wa Mtaa wa Maganga jijini Dodoma Abraham John wakati wa zoezi kuhamasisha ulipaji kodi ya pango la ardhi na utoaji huduma za sekta ya ardhi katika mitaa. (PICHA ZOTE NA MUNIR SHEMWETA WIZARA YA ARDHI)

Mkuu wa Kitengo cha Kodi Wizara ya Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Dennis Masami amesema katika kuhamasisha ulipaji kodi ya ardhi na tozo nyingine zinazohusiana na sekta hiyo nchini Wizara imeanza utaratibu wa kumilikisha ardhi kwenye mitaa mbalimbali nchini kwa lengo la kusogeza huduma karibu na wananchi.

Kwa kuanzia huduma imeanza kutolewa kwenye mtaa wa Maganga kata ya Mkonze katika jiji la Dodoma ambapo timu ya Watendaji wa sekta ya ardhi ilikuwa Ofisi ya Mtendaji Kata kwa lengo la kuhamasisha ulipaji kodi na utoaji huduma za sekta ya ardhi ikiwemo kumilikisha wananchi ardhi.

 

Mkuu wa Kitengo cha Kodi Wizara ya Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Dennis Masami akikagua utendaji kazi wa watendaji wa sekta ya ardhi kwenye Ofisi ya Mtendaji kata ya Mkonze jijini Dodoma jana wakati wa zoezi la kuhamasisha ulipaji kodi ya pango la ardhi na utoaji huduma za sekta ya ardhi katika mitaa. 

Mkuu wa Kitengo cha Kodi Wizara ya Ardhi Dennis Masami jana akiwa katika zoezi la kuhamasisha ulipaji kodi ya pango la ardhi na tozo nyingine zinazohusiana na sekta hiyo kwa nchi nzima alitembelea Mtaa wa Maganga ilipo Ofisi ya Mtendaji Kata ya Mkonze Dodoma na kujionea utendaji kazi ambapo alionesha kuridhishwa kasi ya ulipaji kodi na umilikishaji ardhi kwenye mtaa huo.

Akizungumza katika ofisi ya Mtendaji alisema, sasa Wizara ya Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi imeona umuhimu wa kushusha huduma za ardhi katika ngazi ya mitaa kwa kushirikisha watendaji wa mitaa ili kusaidia utoaji elimu na ukusanyaji maduhuli ya serikali kwa upande wa kodi ya ardhi.

 

 

Watendaji wa sekta ya ardhi katika jiji la Dodoma wakitoa huduma katika ofisi ya Mtendaji kata ya Mkonze jijini Dodoma jana wakati wa zoezi la kuhamasisha ulipaji kodi ya pango la ardhi na utoaji huduma za sekta ya ardhi katika mitaa.

Aliongeza kwa kusema, watendaji wa Kata nchini ni muhimu katika kuhamasisha wamiliki wa ardhi kulipa kodi ya ardhi kwa kuwa wako karibu na wananchi na wizara imeona ni vizuri ikawatumia kwa ushirikiano na watendaji wa sekta ya ardhi katika halmashauri za wilaya na majiji ili kurahisisha zoezi hilo.

Kwa mujibu wa Masami, Wizara ya Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi, mbali na watendaji wake kushiriki kutoa elimu kuhusiana na umuhimu wa kulipa kodi ya ardhi na huduma nyingine zinazohusiana na ardhi pia watahakikisha wamiliki wa ardhi wanaofika wanapatiwa Ankara za malipo na kulipia papo hapo kwa taasisi za kibenki ambazo zitakuwepo katika mitaa husika.

Watendaji wa sekta ya ardhi katika jiji la Dodoma wakiwa kazini katika ofisi ya Mtendaji kata ya Mkonze jana wakati wa zoezi la kuhamasisha ulipaji kodi ya pango la ardhi na utoaji huduma za sekta ya ardhi kwenye mitaa.
 

Mkuu wa Kitengo cha Kodi Wizara ya Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Dennis Masami (aliyesimama kushoto) akisisitiza jambo kwenye ofisi ya Mtendaji Kata Mkonze jijini Dodoma jana wakati wa zoezi la kuhamasisha kulipa kodi ya ardhi na utoaji huduma za sekta ya ardhi katika mitaa. Wa tatu kulia ni Mtendaji Kata ya Mkonze Antony Rugayurala.

Na Munir Shemweta, WANMM DODOMA

‘’Zoezi la kusogeza huduma za ardhi kwenye mitaa litawapunguzia gharama wananchi na kuwafanya kuiona serikali inawajali, kupeleka watendaji kumi kwa ajili ya kuhudumia watu mita tano katika mtaa inasaidia sana kwani hawatakuwa na ulazima wa kuzifuata huduma mbali’’ alisema Masami.

Mmoja wa wananchi waliofika kupata huduma kwenye mtaa wa Maganga Benadicta Kimario aliipongeza Wizara ya Ardhi kwa uamuzi wake wa kusogeza huduma karibu na wananchi na kuelezea uamuzi huo kuwa utasaidia kuondoa kero waliyokuwa wakiipata kufuata huduma ya kumilikishwa na huduma nyingine katika ofisi za mjini.

‘’Mimi nikiwa mjini nilipata taarifa kuwa Wizara imesogeza huduma kwenye mtaa hivyo nikaona nije kuonana na wahusika maana nina kiwanja nataka kuanza kujenga na hapa nimeonana na wahusika na kuhudumiwa, kwa kweli zoezi hili ni zuri sana’’ alisema Benedicta.

 

TANESCO YAWAPANDISHA KIZIMBANI WATU SABA KWA KUINGILIA MIUNDOMBINU YA UMEME

Shirika la umeme Tanzania ( TANESCO) limewapandisha kizimbani watu sita katika mahakama ya hakimu mkazi Kisutu jijini Dar es Salaam Desemba 2, 2020 kwa tuhuma za kuingilia miundombinu ya umeme na kulisababishi Shirika hasara ya shilingi milioni sita.(6,000,000). 

Watuhumiwa hao ni pamoja na Boniphace Emmanuel, Elitruda Ancelim, Twalib Ibrahim, Mwarami Omary, Vumilia Sultani Kaambi, James Joseph na Haidary Islamy.

Hata hivyo upande wa mashtaka umesema upelelezi bado unaendelea na haukuwa na kipingamizi katika kutolewa dhamana ambapo hakimu anayesikiliza kesi hiyo alisema kila mshtakiwa anapaswa kulipa shilingi milioni moja na kuwa na mdhamini mmoja baye sharti awe mtumishi wa Umma.

Kesi imehairishwa hadi tarehe 16.12.2020.

Baadhi ya watuhumiwa hao wakisindikizwa na polisi kwenye mahakama ya hakimu mkazi Kisutu jijini Dar es Salaam leo Desemba 2, 2020.

Wednesday, December 2, 2020

PINDA:KILIMO PEKEE NDICHO KITAONDOA UMASIKINI TANZANIA


Katibu wa Chama cha Wachumi Kilimo Tanzania (AGREST) Dkt. Betty Waized akitoa salamu za Chama hicho na malengo ya mkutano huo kabla ya kumkaribisha Mgeni rasmi kwaajili ya ufunguzi. 
Waziri Mkuu Mstaafu wa Tanzania Mizengo Pinda akitoa nasaha zake mbele ya Wataalamu hao wa Uchumi Kilimo wakati akifungua rasmi mkutano huo wa 12 wa Kisayansi wa  Chama hicho mjini Dodoma.
Profesa. Aida Isinika akimkabidhi Pinda zawadi maalumu iliyotolewa na chama hicho kama kumbukumbu.
Mkutano ukiendelea.
Mkutano ukiendelea.
Mkutano ukiendelea.
Wanachama wa AGREST na Mgeni rasmi Mizengo Pinda mara baada ya ufunguzi wa mkutano huo wa 12 wa kisayansi.

Washiriki wa mkutano wakifuatilia hotuba za ufunguzi.
Washiriki wa mkutano wakifuatilia hotuba za ufunguzi. 


Na Calvin Gwabara, Dodoma


Imeelezwa kuwa Tanzania haitaweza kuondoa umasikini wala kupiga kasi ya Kim aendelee kwa Wananchi wake endapo swala la Kilimo Bora na cha kisasa halitapewa kipaumbele na Serikali, Watafiti na wadau wengine wa kilimo.

Hayo yamesemwa na Waziri Mkuu Mstaafu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Mizengo Pinda wakati akifungua Kongamano la Kisayansi la Chama cha Wachumi Kilimo Tanzania (AGREST) lenye Mada kuu isemayo “Kuondoa vizuizi katika biashara ili kushanirisha biashara ya mazao ya Kilimo na mifumo ya chakula baina ya nchi za Afrika”lililofanyika mkoani Dodoma.

Pinda alisema pamoja na mabadiliko yanayoendelea katika shughuli za kiuchumi za watanzania katika maeneo ya vijijini zaidi ya asilimia 60 ya wananchi wanategemea kilimo lakini ni ukweli kwamba  wanaotegemea kilimo bado ni masikini kwa kiasi kikubwa wanategemea mazao ya chakula kama chanzo muhimu cha kipato cha kaya.

“ Juhudi za nchi  yetu za kuendeleza viwanda kwa kiasi kikubwa zinategemea uzalishaji na biashara ya mazao ya kilimo na hasa mazao ya chakula hivyo mada kuu ya kongamano hili ni muhimu sana katika ustawi wa Wananchi wengi ambao wanategemea moja kwa moja Kilimo cha mazao hayo au wale wanaofanya shughuli katika mnyororo wa thamani wa mazao hayo”  alisisitiza Pinda.

Alisema kuwa taarifa zilizopo zinaonyesha kuwa biashara ya mazao ya kilimo baina ya nchi za Afrika kwa sasa ni chini ya asilimia 20 huku ikikadiriwa kuwa tunakosa mapato Dola bilioni 30 kwa Mwaka kwa kutoboresha mazingira ya Biashara yetu ya Kilimo baina yetu wakati maeneo mengine nje ya Vara la Afrika yakifanya vizuri.

Pinda aliongeza kuwa kwa muongo mmoja na nusu Tanzania imeweza kupanda kutoka nafasi ya 10 Mwaka 2007 hadi kufikia nafasi ya 7 kama muuzaji mkubwa wa mazao ya kilimo ndani ya Afrika na kwamba muelekeo huo ni mzuri ingawa kuna mengi ya kufanya hasa ukilinganisha na uwezo na rasilimali zilizopo nchini.

Hata hivyo waziri mkuu huyo mstaafu alibainisha kuwa tafiti zinaonyesha kuwa

vikwazo visivyo kodi vinakwamisha zaidi biashara kuliko vikwazo vya kikosi na kwamba taarifa zilizopo zinaonyesha kuwa vikwazo visivyo kodi ni tatizo kubwa San katika kufanya biashara baina ya nchi za Afrika kuliko nchi zilizo nje ya Afrika.

“ Ni imani yangu kuwa katika kongamano hili mtajadili namna bora ya kutoka katika mzunguko au mkwamo huu” alisema Pinda.

Hata hivyo  Pinda alisema kwakuwa kilimo bodo kinaajiri watu wengi kuimarika kwa bishara ya mazao ya Kilimo kutaimarisha ajira za watu wengi na kufanya Kilimo kiwe ni ajira yenye kuvutia hasa vijana kwani benki ya dunia inakadiria hadi kufikia mwaka 2022 kutakuwa na watu bilioni 1.6 wanaohitaji ajira na Afrika pekee ni vijana milioni 25 wanaohitaji ajira kila mwaka.


“ Mimi binafsi ni muumuni wa kuwa maendeleo ya jamii ya jamii yoyote yanategemea sana matumizi ya taarifa za kutafiti ambazo zitasaidia wafanya maamuzi kuchukua Mrengo sahihi hivyo naamini Kongamano hili la wana AGREST mtajadili namna bora ya kutoka katika mzunguko huu ili Tanzania na Afrika kwa ujumla ziweze kunufaika katika biashara ya mazao na bidhaa za chakula” alisema Pinda.

Aliongeza kuwa Serikali ya CCM inayoongozwa na Rais John Magufuli ina nia njema kabisa ya kuhakikisha kuwa Tanzania inashirikiana na wadau wote katika kuhakikisha Kilimo kinaendelea na kuondoa changamoto zinazojitokeza lakini lazima wajue kwamba Serikali pekee haiwezi kuziondoa bila wataalamu kushirikiana na Serikali.

“ Nikipongeze Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo (SUA) kupitia wataalamu wake wabobevu na mahiri Kwani tunashuhudia kazi zinazofanywa na nanyi na Taasisi zingine katika kukuza shughuli za utafiti na ubunifu hapa nchini” alipongeza Pinda.

Awali akizungumza kabla ya kumkaribisha mgeni rasmi katibu wa chama hicho Dkt. Betty Waized  alisema kuwa lengo kuu la AGREST ni kusaidia kuchochea maendeleo na matumizi ya Elimu ya Uchumi Kilimo na biashara nchini Tanzania na mikutano hiyo ndio njia mojawapo ya kufikia lengo hilo ni kupitia mikutano hiyo ya kisayansi ambayo wanajadili na kubadilishana mambo muhimu ya uchumi kilimo na kusambaza kwa jamii kubwa zaidi.

Alisema mkutano huu wa 12 kisayansi wa AGREST ni fursa nzuri ya maandalizi ya mijadala  mkutano wa Mifumo ya chakula unaotarajiwa kufanyika mwaka 2021 ambao unalenga kuboresha mbinu za mifumo ya hakika hapa nchini.

“ Tanzania imeingia kwenye uchumi wa kati na  lengo ni ifikapo mwaka 2025 tunahitaji kampuni za kibiashara za kushindana ambazo zitakazofanya kazi kibunifu kwa mifumo ya chakula ambayo inafanya kazi kwa wote” alisema Dkt. Waized.

Alibainisha kuwa mkutano huo wa kisayansi pamoja na mambo mengine unalenga kujibu maswali ya aina gani ya mifumo ya sera inahitajika kusukuma mfumo endelevu wa chakula kwenye bara letu hasa Tanzania.

Katibu huyo wa AGERST alisema mkutano huo umevutia washiriki 80 kutoka sehemu mbalimbali za Tanzania wakiwakilisha wanataaluma, watafiti, maafisa wa Serikali, mashirika yasiyo ya kiserikali na washiriki binafsi ambapo zaidi ya tafiti za kisayansi 30 zitawasilishwa.

“ Mkutano huu pia unawapa nafasi  wanasayansi  wachanga kupata uzoefu namna ya kuandaa na kuwasilisha tafiti zao za kisayansi” alisema Waized.

Katika mkutano huo wanachama hao walimpatia Pinda zawadi mbalimbali ikiwemo Kinyago cha mnyama Tembo pamoja vitenge kwa ajili yake na mke wake lakini pia AGREST walitoa zawadi kwa mwana AGREST mkongwe kwenye chama chao zawadi ambayo ilikwenda kwa Profesa, Aida Isinika kutoka Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo (SUA).


NDAHANI APONGEZA UFANISI VETA SINGIDA...AWAFUNDA WAHITIMU


Kaimu Afisa Vijana Mkoa wa Singida ambaye ni mgeni rasmi wa Mahafali ya 31 VETA-Singida, Frederick Ndahani akihutubia sherehe za mahafali hayo juzi.

Wahitimu wakijiandaa kuingia ukumbini.

Wazazi na baadhi ya walimu wakishiriki sherehe hizo.
Wazazi na baadhi ya walimu wakishiriki sherehe hizo.
Wanachuo wa VETA Singida-wakifuatilia matukio ya sherehe hizo.

Baadhi ya wahitimu wakiwa kwenye picha ya pamoja.

Sherehe zikiendelea ndani ya ukumbi.


Baadhi ya wahitimu wakiwa kwenye picha ya pamoja.

Mkuu wa Chuo cha Veta-Singida, Paul Batoleki akimpongeza mmoja wa wahitimu.

Ndahani akikabidhi vyeti kwa wahitimu.

Mgeni rasmi akiwa kwenye karakana ya Ufundi Bomba.

Mratibu wa Chama cha Waandishi wa Habari Mkoa wa Singida (Singida Press), Domician Mwalusito (kulia) na Katibu wa chama hicho Revocatus Gervas wakiwa na mmoja wa wahitimu kwenye mahafali hayo.



Na Godwin Myovela, Singida


KAIMU Afisa Vijana mkoani hapa Frederick Ndahani amepongeza umahiri wa mafunzo na mifumo ya kiteknolojia inayotumika kutoa mafunzo ya nadharia na vitendo kwa vyuo vya VETA nchini, huku akiwataka wahitimu wake kutumia stadi za mafunzo hayo katika kulifikisha Taifa kwenye uchumi wa juu.

Ndahani alitoa pongezi hizo jana wakati akihutubia Sherehe za Mahafali ya 31 ya kuhitimu Mafunzo ya Ufundi Stadi VETA Singida.

"Tafsiri ya kuhitimu kwenu leo maana yake ni kuongeza tija kwa taifa letu na kuzidi kutatua changamoto ya upungufu wa ajira hususani kwa vijana," alisema.

Alisema ili kuikwamua nchi katika sekta mbalimbali serikali imejiwekea mikakati kadhaa ya utekelezaji, ikiwemo kuhuisha uwiano wa viwango vya mafunzo vyenye ujuzi wa juu yaani (Engineers), ujuzi wa kati (Technicians) na mafundi wa kazi za mikono (Artisans) kwa uwiano wa 1:5:25.

"Nawasihi tumieni ujuzi na umahiri mlioupata kwenye kujiajiri ili kujikwamua na wimbi la umasikini. Funguo ya mafanikio kwanza ni kuwa na ujuzi na maarifa, pili ni tabia na tatu ni vitendo," alisisitiza Ndahani.

Sanjari na kupongeza juhudi za serikali kupitia VETA Singida- kwa kuchagiza maendeleo ya vijana kiuchumi, Ndahani alitoa wito kwa wakurugenzi kuwatumia wahitimu wa vyuo hivyo na vijana wengine katika ujenzi wa miradi inayotumia 'Force Account'.

Alisema mfumo huo ulianzishwa na kutolewa maelekezo na Rais John Magufuli kwa maksudi, lengo likiwa ni kuwasaidia mafundi waliopo mitaani kupata ajira kupitia miradi hiyo.

Imeelezwa kwamba mfumo wa makandarasi umekuwa ukiwaumiza mafundi kwa kuwakosesha fursa mbalimbali hususani vijana wa kundi la kazi za mikono, huku baadhi ya Mabaraza ya Halmashauri na Wakurugenzi wakishindwa kusimamia ipasavyo.

"Niwasihi sana wakurugenzi kuwatumia sana vijana wa taifa hili wakiwemo hawa wanaopita kwenye mikono ya VETA katika ujenzi wa miradi hii ambayo kwa sasa ipo kila kona ya nchi" alisema Mgeni rasmi wa mahafali hayo Ndahani, ambaye pia ni Kaimu Afisa Vijana Mkoa wa Singida.

Kwa upande wake, mwenyeji wa mahafali hayo, Mkuu wa Chuo cha Veta-Singida, Paul Batoleki, alisema kupitia mahafali hayo, jumla ya wanachuo 156 wamehitimu fani mbalimbali kwa Ngazi ya Pili na Tatu.

Alizitaja fani hizo kuwa ni pamoja na Mifugo, Ufundi Magari, Uchomeleaji, Useremala, Ujenzi, Ushonaji, Umeme, na Ufundi Bomba, huku pia kukiwa na fani nyingine ya Uhazili na Kompyuta inayofundishwa chuoni hapo ambayo hata hivyo haikuwa na muhitimu kwenye mahafali hayo.

Batoleki alipongeza serikali kupitia Mamlaka hiyo ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi Stadi nchini kwa kutenga jumla ya shilingi milioni 340 Kwa ajili ya ujenzi wa madarasa na maabara chuoni hapo kwa fani ya ufugaji wa wanyama.

Awali, kupitia risala yao, wahitimu hao Kwa kuzingatia ongezeko la tija chuoni hapo wameiomba serikali kutatua uhaba uliopo wa baadhi ya vitabu vya masomo ya fani.

Changamoto nyingine ni mamlaka ziangalie uwezekano wa kuwagharamia wanafunzi wawapo kwenye mafunzo kwa vitendo, hasa kwenye maeneo ya viwanda ambako wengi hujikuta wakifanya 'fields' zao katika mazingira magumu.

"Tunaomba pia tuongezewe walimu wa masomo ya muambata mfano 'LifeSkills' lakini kubwa serikali iangalie uwezekano wa kutuongezea vifaa kulingana na teknolojia za kisasa ili kuongeza tija na ufanisi,"  alisema Rais Mstaafu wa Chuo hicho, Elisha Ezekiel.

Mkoa wa Singida una jumla ya viwanda 1,805 ambapo kati yake kiwanda kikubwa ni 1, kati 10, vidogo 309 na vidogo sana 1,485 hatua ambayo imeendelea kupanua wigo wa fursa za ajira hususani kwa makundi ya vijana na wanawake kulingana na fani mbalimbali walizonazo.


Tuesday, December 1, 2020

REPPSI TANZANIA WAHIMIZA UPENDO KWA WATU WANAISHI NA VVU



Mkurugenzi wa REPPSI Edwick Mapalala akiwa katika maonyesho ya siku ya ukimwi katika viwanja vya Posta, Kijitonyama
 
Mkurugenzi wa REPPSI Edwick Mapalala akiwa na baadhi ya vijana katoka maonyesho ya siku ya ukimwi katika viwanja vya Posta, Kijitonyama

Mwandishi wetu, Dar es Salaam.

Mkurugenzi Mkazi wa Shirika  Regional Psychosocial Support Initiative (REPPSI), Edwick Mapalala ameikumbusha jamii kuongeza upendo na kuendelea kutokomeza unyanyapaa kwa watu wanaoishi na Virusi vya Ukimwi (VVU).

Amesema kuwalinda, kuwathamini na kuwajali watu wanaoishi na VVU hasa vijana kutasaidia kuwapunguzia msongo wa mawazo wale ambao hawajaikubali afya yao, na hivyo kuikubali na kushiriki katika kukuza uchumi wa Taifa.
Mapalala amesema hayo wakati akitoa salamu za REPPSI, Shirika linalojihusisha na malelezi, makuzi na msaada wa Kisaikolojia kwa watoto kuhusu siku ya Ukimwi Duniani.

“Hii ni siku ya kutafakari kuhusu maambukizi ya VVU, waliopima na kujua afya zao waendelee kuwa waaminifu kwenye utumiaji wa dawa, wasiopima wapime ili wajitambue na wale wasio na maambukizi waendelee kujilinda. Pia tuwakumbuke waliopoteza maisha yao kwa VVU,” amesema Mapalala.

Akizungumzia mradi wa Ready Plus, unaowahusu vijana wanaoishi na VVU Mapalala amesema wengi wamejikubali, wanajiamini na wanaendeleza ndoto zao za kimaisha baada ya kupatiwa elimu sahihi kuhusu VVU
.
“Na nitoe wito kwa jamii, tuendelee kuwalea vijana wetu kwa upendo, tusiwakatishe tamaa kwa sababu wanaweza kufikia ndoto,” amesema Mapalala.

Hata hivyo ameipongeza Serikali ya Tanzania kwajitihada kubwa katika kupambana na VVU.
Mwisho

AIRTEL YAJA NA OFA YA SIKUKUU WATEJA KUPEWA DABO DATA


Dar es Salaam

Kampuni ya simu za Mkononi Airtel Tanzania leo imetangaza kuzindua ofa ya Airtel Smartphone Dabo Data kwa wateja wote wa simu aina ya Smartphone kwa msimu huu wa sikukuu.

Pia ofa hii itawanufaisha Wateja wote wa sasa wa Airtel wanyempango wa kubadilisha simu au Smartphone mpya kwa kujipatia Dabo Data kwa bando za wiki na mwezi kwa miezi sita ijayo yaani nusu mwaka.

Airtel inapozindua Ofa hii ya shamrashamra za mwisho wa Mwaka Wateja wengine wa smartphone kwa sasa wanaweza kujiunga na mtandao wa Airtel ili kufurahi ofa hii. Ofa hii ni pale mtu mtumiaji wa simu aina ya smartphone anapotumia mtandao wa Airtel kwa mara ya kwanza kwenye simu yake. Ofa hii inatoa fursa kwa wateja kufurahia huduma yenye kasi ya Airtel 4G inayopatikana nchini kote Tanzania.  

 Ofa ya Dobo Data inampa mteja mara mbili kwa kila bando analonunua ikiwa ni ya wiki au mwezi kwa kipindi cha miezi sita yaani Nusu Mwak. Ili kujipatia ofa hii, mteja wa smartphone anatakiwa kupiga *149*99#, changua 5 (intaneti) kisha 6 (Smartphone ofa) ili kujiunga. Baada ya kujiunga kikamilifu, mteja atapata ofa mara mbili ya bando lolote atakalo nunua iwe ni kwa siku saba au mwezi kwa miezi sita ijayo kuanzia siku ambayo amejiunga.

Muda wa ukomo wa Airtel Smartphone Dabo Data ni sawa na ule ambao bando imenunuliwa na bonasi ya data kwa wale tu waliojiunga na ofa hii. 

 Ezekiel Kahatano, Mkuu wa kitengo cha Data na Masoko Airtel Tanzania anasema, “Dhamira yetu siku zote ni kuwapa wateja wetu huduma bora ambayo inaendana na Maisha ya sasa ya kidigitali. Kwa maana hiyo, leo tunatangaza kuzindua ofa ya Airtel Smartphone Dabo Data, ambayo inawapa wateja unafuu kwenye kupata huduma bora ya Airtel 4G. Wakati tunakaribia msimu wa sikukuu, hii itawapa wateja wetu fursa ya kuendelea kuunganishwa na familia, marafiki na wadau wote kote nchini.

Kwa upande wake, Meneja Mawasiliano Airtel Tanzania Jackson Mmbando anasema;

 “Ninachukua fursa hii kuwaomba wateja pamoja na watumiaji wa smartphone kujiunga na mtandao wa Airtel ili kufurahi ofa hii kwa WIKI na MWEZI kwa bando za intaneti kwa Nusu Mwaka. Tunaamini ya kwamba wakati wa kipindi hiki cha msimu wa sikukuu wateja wetu wanahitaji uhuru wa kuwasiliana na marafiki, familia na wafanya biashara wenzao na kwa hivyo huduma hii inawapa uhuru ule wanaohitaji”.

Kuzindulia kwa ofa hii ya Smartphone data ambayo inampa bonua ya asilimia mia moja mteja inaonyesha ni kwa kiwango ngani tunavyothamini wateja wetu. Tuna Imani kuwa huduma hii itawapa hamasa wale ambao sio watumiaji wa smartphone kuanza kutumia na hivyo kukuza Maisha ya kidigitali kwa Watanzania.

WAZIRI MKUU KASSIM MAJALIWA: VIFO VITOKANAVYO NA UKIMWI VIMEPUNGUA NCHINI

Waziri Mkuu Kassim Majaliwa amesema uimarishaji wa huduma za tiba ikiwemo matumizi ya dawa za kufubaza virusi vya ukimwi (ARVs) umechangia kupunguza vifo vitokanavyo na UKIMWI kutoka vifo vya watu 85,000 mwaka 2001 hadi kufikia vifo 21,529 mwaka 2019.

Waziri Mkuu ameyasema hayo leo (Jumanne, Desemba Mosi, 2020) katika maadhimisho ya Siku ya UKIMWI Duniani yaliyofanyika Kitaifa katika uwanja wa Mandela Manispaa ya Moshi, Mkoani Kilimanjaro. Kaulimbiu ya maadhimisho hayo kwa mwaka huu ni ‘Mshikamano wa Kimataifa, Tuwajibike Pamoja.’

Waziri Mkuu amesema mbali na kupungua kwa vifo hivyo, pia maambukizi mapya ya UKIMWI nayo yamezidi kupungua kutoka watu 130,000 mwaka 2001 hadi kufikia watu 68,484 mwaka 2019, hivyo ametoa wito kwa wadau wote katika mapambano ya ugonjwa huo waongeze jitihada.

“Mafanikio yote haya yametokana na kuendelea kuimarika kwa huduma za tiba ikiwemo matumizi ya dawa za kufubaza VVU (ARVs) na afua za kinga zinazohusisha tohara ya kitabibu kwa wanaume na kuzuia maambukizo ya VVU kutoka kwa mama kwenda kwa mtoto.”


Amesema Tanzania imefanikiwa kufikia malengo ya tisini tatu (90:90:90) hasa katika 90 ya pili na ya tatu. “Kwa kujikumbusha tu, ni kwamba tisini tatu zinalenga kuhakikisha kuwa asilimia 90 ya WAVIU wanajua hali zao; asilimia 90 ya wanaojua hali zao wanaanza kutumia dawa za kufubaza mapema na asilimia 90 ya walioanza dawa za kufubaza VVU kinga zao za mwili zinaimarika ifikapo mwaka 2023.”

Waziri Mkuu ametumia fursa hiyo kutoa wito kwa wadau mbalimbali wa masuala ya mapambano dhidi ya VVU na UKIMWI, waongeze jitihada hususani katika kuhamasisha upimaji wa VVU ili wafikie lengo la 90 ya kwanza.

Hata hivyo, Waziri Mkuu ametoa siku 30 kwa kila mkoa uliowahi kufanya maadhimisho hayo uhakikishe kuwa unawasilisha taarifa yake Tume ya Kudhibiti Ukimwi Tanzania ndani ya mwezi mmoja kuanzia leo (Jumanne, Desemba Mosi, 2020).


Vilevile, Waziri Mkuu ametoa agizo kwa TACAIDS, Wizara ya Afya na wadau wote wa kudhibiti VVU na UKIMWI nchini, wajipange vizuri kubaini na kufanyia kazi maeneo mbalimbali ya uwekezaji yenye gharama nafuu katika kudhibiti VVU/UKIMWI lakini yatakayoleta matokeo makubwa.

Katika hatua nyingine, Waziri Mkuu amewasihi vijana wajitambue na kuthamini maisha yao kwa kujikinga na maambukizi mapya ya VVU kwa kuwa wao ni nguvu kazi na Taifa linawategemea. “Na wale wanaoishi na VVU waendelee kutumia dawa za ARV kwa ufuasi sahihi bila kuacha ili waweze kufubaza VVU na kuimarisha afya zao.”

“Vijana ni kundi linalokabiliwa sana na changamoto ya maambukizi mapya ya VVU nchini. Takwimu za maambukizi mapya ya VVU zinaonesha kwamba asilimia 40 ya maambukizi hutokea kwa vijana na katika hao asilimia 80 ni vijana wa kike.”

Amesema kwa mujibu wa takwimu hizo, ni dhahiri kuwa kundi la vijana, na hasa wa kike, lipo kwenye hatari kubwa zaidi ya kupata maambukizi mapya kutokana na sababu mbalimbali ikiwemo kuanza ngono katika umri mdogo.

“Hali hii husababisha mhusika kuwa na mahusiano ya mapenzi na watu wengi hadi anapofikia utu uzima, hivyo, kujiweka katika hatari ya kupata maambukizi ya VVU. Nawaasa vijana, msijihusishe na mapenzi katika umri mdogo. Ili vijana muweze kutimiza ndoto au malengo yenu katika maisha; ni lazima muwe na subira.”

Waziri Mkuu amesema sababu nyingine ya vijana hao wadogo wa kike kuwa na mahusiano ya kingono na wanaume wenye umri mkubwa ni kuvutika na vishawishi kama vile pesa na zawadi ndogondogo. “Kwa mara nyingine, natoa rai kwa wanaume wenye umri mkubwa kuachana na tabia ya kujihusisha na mapenzi na wasichana wadogo. Niwakumbushe tena, Serikali haitasita kuchukua hatua kali za kisheria kwa yeyote atakayebainika.”

Mapema, mara baada ya kuwasili kwenye eneo hilo, Waziri Mkuu alitembelea baadhi ya mabanda ya maonesho, ambapo kupitia mabanda hayo, amejionea utoaji wa huduma za elimu, uhamasishaji na upimaji wa Virusi vya UKIMWI (VVU) na magonjwa mengine yasioambukiza. Amesema amevutiwa na huduma zinazotolewa kwenye mabanda hayo.

Naye, Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro, Dkt. Anna Mghwira alisema kiwango cha maambukizi ya UKIMWI katika mkoa wa Kilimanjaro kimeendelea kupungua kutoka asilimia 7.3 mwaka 2004 hadi kufikia asilimia 2.6 mwaka 2017. “Kiwango hiki kipo chini ya wastani wa maambukizi Kitaifa ambacho ni asilimia 4.8.”

“Hata hivyo kiwango cha maambukizi kimkoa kuwa chini ya wastani wa Kitaifa haimaanishi kuwa tuko salama; hivyo sote tunapaswa kuongeza juhudi za pamoja ili tufikie lengo la maambukizi sifuri ifikapo 2030.”

Alisema licha ya mafanikio hayo, pia wanakabiliwa na changamoto kubwa ya utoaji huduma ya tiba na mafunzo kwa baadhi ya WAVIU kutokuwa na ufuasi mzuri wa dawa pindi hali zao kiafya zinapoonekana kuimarika, hivyo aliwataka watu walioanza kutumia ARV, wazingatie ufuasi wa dawa.

Kwa upande wake, Balozi wa Marekani nchini, Dkt. Donald Wright aliipongeza Serikali ya Tanzania kwa jitihada zake za kupambana na UKIMWI ikiwa ni pamoja na kuhakikisha kuwa watu wote wanaoishi na virusi hivyo wanapata dawa, na kuahidi kuwa Serikali yake itaendelea kushirikiana na Tanzania.

Awali, Mwenyekiti wa Baraza la Watu Wanaoishi na Virusi vya UKIMWI (NACOPHA), Bibi Leticia Mourice alitumia fursa hiyo kuiomba Serikali, asasi za kiraia, taasisi za dini na vyombo vya habari viendelea kutoa elimu ya makuzi, kubadili tabia na hofu ya Mwenyezi Mungu kwa vijana, wazazi na walezi ili kuwaepusha na matendo hatarishi.

“Hatua kali zichukuliwe dhidi ya ukandamizaji na udhalilishaji wa aina yoyote ya haki kwa watoto na vijana. Pia, viongozi wa dini, kwa kuzingatia misingi ya imani zetu, tushikamane kuelimishana na kuongoza jamii ya waumini kupiga vita unyanyapaa dhidi ya VVU.”

MBUNGE WA BUYUNGU ATOA MSAADA WA MABATI 300 KUSAIDIA SHULE ZA SEKONDARI


 Mbunge wa Jimbo la Buyungu mkoani Kigoma kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM), Aloyce Kamamba (katikati kushoto), akikabidhi bati moja kati ya 300 kwa ajili ya ujenzi wa shule za sekondari jimboni humo.
Mkuu wa wilaya ya Kakonko, Kanali Hosea Ndagala (kushoto) akikabidhiwa mifuko ya saruji 100 na Kampuni ya Ujenzi ya Nyanza Road kwa ajili ya ujenzi wa Shule ya Sekondari Kanyonza
Moja ya madarasa ya shule za sekondari jimboni humo.

 Na Mwandishi Wetu, Kigoma.

Mbunge  wa Jimbo la Buyungu mkoani Kigoma kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM), Aloyce Kamamba, amekabidhi mabati 300 yenye thamani ya sh.milioni 9 ikiwa ni utekelezaji wa ahadi yake aliyoitoa wakati wa kampeni.

Akizungumza katika hafla ya kukabidhi mabati hayo, Kamamba alisema ni utekelezaji wa ahadi yake aliyoitoa wakati wa kampeni ya kutatua changamoto mbalimbali.

"Niliahidi kutatua changamoto mbalimbali za wananchi katika jimbo letu na nimeanza na changamoto za miundombinu kwa kununua mabati  300 kwa ajili ya ujenzi wa shule zetu" alisema Kamamba.

Alisema mabati hayo yatapelekwa kujenga miundombinu katika shule tatu za sekondari katika jimbo hilo.

Alizitaja shule hizo kuwa ni Sekondari ya  Kanyonza iliyopo Kata ya Kanyonza ambayo itaipata mabati 100, Shule ya Sekondari Kakonko ambayo nayo itaipata mabati 100 na Shule ya Sekondari ya Ushindi iliyopo Kata ya Kasuga.

Mkuu wa wilaya ya Kakonko, Kanali Hosea Ndagala akikabidhiwa mifuko ya saruji 100 na Kampuni ya Ujenzi ya Nyanza Road kwa ajili ya ujenzi wa Shule ya Sekondari Kanyonza ikiwa ni maandarizi ya kupokea  wanafunzi wapya wa kidato cha kwanza  Januari 2021 aliushukuru uongozi wa kampuni hiyo na kumpongeza mbunge huyo kwa kuanza kwa kasi kutekeleza ilani ya uchaguzi ya chamsingi hicho ya 2020/ 2025.

"Nikupongeze mheshimiwa mbunge kwa kuanza kutekeleza ilani ya chama chetu na sisi kama Serikali tutakupa ushirikiano wa kutosha" alisema.

Mwananchi wa Kata ya Kasanda, Alexander Madebwa amemshukuru mbunge huyo kwa juhudi za maendeleo alizoanza kuzifanya hasa katika kuboresha miundombinu upande wa elimu.

Mkazi wa Kata ya Kanyoza  Shetiel Juma amempongeza mbunge wao kwa hatua hiyo aliyoianza ambayo inaleta natumaini mapya kwa wananchi wa jimbo hilo.

Katibu wa CCM Wilaya ya Kakonko, Abdul Kambuga Amempongeza  mbunge huyo kwa kuanza kwa kasi utekelezaji wa Ilani ya chama hicho na kuwa kasi hiyo inawafanya wananchi kuwa na imani na Serikali inayoongozwa na chama hicho chini ya Rais Dkt.John Magufuli.

MBUNGE MALEMBEKA ATOA PIKIPIKI KWA MASHEHA

Mbunge wa viti maalum (CCM)  Mkoa wa Kaskazini Unguja,Angelina Adamu Malembeka amesema kuna umuhimu wa masheha wa mkoa huo kupatiwa vitendea kazi ili kurahisisha kazi zao katika maeneo yao ya kazi.

Kauli hiyo ameitoa jana wakati akikakabidhi pikipiki 12 kwa masheha wa shehia za mkoa huo zenye thamani ya sh.milioni 26 ambapo alisema pikipiki hizo zitawarahisishia kazi.

Akizungumza mara baada ya kukabidhi pikipiki hizo Mbunge huyo alisema kuwa kitendo cha utoaji wa pikipiki umekuja baada ya kuona changamoto zilizojitokeza kipindi cha kampeni katika uchaguzi mkuu wa mwaka huu.

Alisema katika kipindi hicho cha kampeni masheha hao walikuwa hawana taarifa rasmi kutokana na kuwa kila mara taarifa zinabadilika na ndipo alipoona haja ya kuwapatia vitendea kazi hizo ili kuwawezesha kuzunguka kwenye maeneo yao yote ili kuwa na taarifa rasmi.

Mbunge huyo alisema pikipiki hizo zimetolewa kwa wilaya ambapo pikipiki tano zilitolewa kwa masheha wa wilaya ya Kaskazini 'A' na wilaya ya Kaskazini 'B' katika mkoa huo wa Kaskazini Unguja kutokana na kuwa maeneo yao ni makubwa na hawana vitendea kazi.

"Tunapohitaji taarifa zinazohusu shehia zao huwa zinachelewa au zimekuja bila ya uhalisia hivyo mategemeo yetu pikipiki hichi zitatufanya tupate taarifa kwa wakati," alisema

Alisema pikipiki hizo zitawapa nafasi za kufanya kazi na kupeleka kupata taarifa kwa wakati sambamba na kujenga mahusiano haina ya viongozi wa Chama na serikali.

"Masheha ni viongozi wa Serikali hivyo kutaweza kuwasaidia wananchi kwa ukaribu zaidi kwani masheha ni viongozi wa Serikali nasi tunawasaidia  katika kufanya kazi kwa ufanisi zaidi," alisema

Hata hivyo, aliwataka masheha hao kuzitumia kwa uangalifu kwa kuvaa kofia ngumu 'helmenti' na kuendesha kwa mwendo wa kawaida ili kuweza kuepusha ajali zilizokuwa si za lazima pamoja na kufuata sheria za barabarani ili kuepuka ajali zinazoweza kuepukika.

Naye, Mwenyekiti wa Jumuiya ya Wanawake wa Chama Cha Mapinduzi(UWT) Mkoa wa Kaskazini Unguja, Maryam Muharami Shomari, alisema kutolewa kwa pikipiki hizo, zinaonyesha wazi kuwa Mbunge huyo anatambua umuhimu wa masheha kutokana na  kumekuwepo kwa umuhimu wa sheha katika kufanya kazi zao kwa umakini.

Pia, aliwataka Wabunge wengine kuendeleza aliyoyaanza Mbunge huyo ili kuweza kukamilisha idadi ya masheha waliokuwepo katika Mkoa huo kupata vitendea kazi katika Mkoa na wilaya zao.

Naye sheha wa shehia ya Matemwe, Vuai Faraji Mcha, alisema amefarijika kupatiwa pikipiki hizo na kwamba kuahidi kuitumia pikipiki hizo kuwa lengo lilokusudiwa ili kuona hali ya kiutendaji inakwenda kama ilivyopangwa pamoja na kumuahidi mbunge huyo kufanya kazi kwa lengo la kupatiwa. 

KANISA LA MORAVIAN WATAKIWA KUTORIDHIKA NA MAENDELEO WALIONAYO


Mwenyekiti na Mchungaji Kiongozi wa Kanisa la Moravian Jimbo la Kusini Mchungaji, Yona Mwambeta, akihubiri Jumapili wakati akiongoza harambee kwa ajili ya ujenzi wa Kanisa la Moraviani Usharika wa Kijichi jijini Dar es Salaam.
Waumini wa kanisa hilo wakiwa katika ibada hiyo.
Ibada ikiendelea.
Ibada ikiendelea.
Mwenyekiti na Mchungaji Kiongozi wa Kanisa la Moravian Jimbo la Kusini Mchungaji, Yona Mwambeta (kushoto) na Mchungaji wa kanisa hilo Usharika wa Kijichi, Raphael Mwampagatwa wakiwa kwenye ibada hiyo.
Maombi yakiendelea.
Harambee ikiendelea. Kushoto ni mke wa Mwenyekiti na Mchungaji Kiongozi wa Kanisa la Moravian Jimbo la Kusini Mchungaji, Yona Mwambeta, Mchungaji Lilian Mwambeta akihesabu sh.550.000 walizotoa kama mchango wao wa ujenzi wa kanisa hilo.
Mchungaji Lilian Mwambeta, akimkabidhi fedha hizo Mwenyekiti wa harambe hiyo, Subilaga Mwambeta.
Waumini wa kanisa hilo na wachungaji wao wakiwa nje baada ya kuhitimisha harambee hiyo.


Na Dotto Mwaibale


Mwenyekiti na Mchungaji Kiongozi wa Kanisa la Moravian Jimbo la Kusini,  Mchungaji, Yona Mwambeta amelitaka kanisa hilo kutoridhika na badala yake waige makanisa mengine yaliyopiga hatua ya maendeleo kwa kujenga makanisa makubwa na kuanzisha miradi ya maendeleo nchini.

Mwambeta aliyasema hayo Jumapili wakati akiongoza harambee kwa ajili ya ujenzi wa Kanisa la Moraviani Usharika wa Kijichi jijini Dar es Salaam.

"Wamoravian tangu siku nyingi wao ni watu wa kuridhika na vitu vidogo nawaambieni badilikeni na kuiga wanavyofanya wenzetu wa makanisa mengine ambao wapo mbali kimaendeleo" alisema Mwambeta.

Alisema kazi ya ujenzi wa kanisa hilo si ya waumini wa kanisa hilo pekee bali ni ya Mungu hivyo uchache wao usiwakatishe tamaa ya kupata fedha za kujenga kanisa hilo.

Akitolea mfano kanisa la Itungi lililopo wilaya ya Kyela mkoani Mbeya alisema lilianza kujengwa na watu wachache lakini leo hii limekuwa ni kanisa la mfano.

Mwambeta aliwataka waumini hao wa Kanisa la Moravian Kijichi kujenga kanisa kubwa litakalo akisi miaka  100 ijayo bila kujali litachukua muda gani kukamilika ujenzi wake.

Aidha Mwambeta aliwataka waumini wa kanisa hilo kuwashirikisha watu mbalimbali bila ya kujali dini zao na madhehebu wanayotoka ili kulijenga kanisa la usharika huo.

Mwenyekiti wa ujenzi wa kanisa hilo Jackson Mwaisemba alisema harambee hiyo ni ya pili  na kuwa wataendelea kufanya nyingine ili kufikia malengo ya kupata sh.milioni 100 zitakazo saidia kuanza ujenzi wa kanisa  hilo.

Mchungaji wa kanisa hilo Usharika wa Kijichi, Raphael Mwampagatwa alimshukuru Mwambeta kwa kuendesha harambee na kuwapa ari na moto mpya waumini wa kuchangia ujenzi huo.

Mchungaji Mwampagatwa alitumia harambee hiyo kutoa namba ya Voda 5312023 na Tigo 0679-607003 kwa ajili ya makanisa mbalimbali, taasisi, mashirika, wafanya biashara na mtu yeyote ambaye atapenda kuchangia ujenzi wa kanisa hilo kiasi chochote cha fedha awe Dar es Salaam na maeneo mengine ndani na nje ya Tanzania na Mungu atawabariki.

Katika harambee hiyo fedha taslimu zilizopatikana zilikuwa ni sh.3,717,000, ahadi sh.4,685,000 na jumla ikiwa ni sh. 8,402,000.