Matokeo chanyA+ online




Friday, June 4, 2021

RAIS SAMIA SULUHU HASSAN AKUTANA NA KUFANYA MAZUNGUMZO NA BALOZI WA CHINA ALIYEMALIZA MUDA WAKE HAPA NCHINI WANG KE

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan akizungumza jambo na Balozi wa China aliyemaliza muda wake hapa nchini Wang Ke wakati wakiagana mara baada ya mazungumzo yao Ikulu ya Chamwino mkoani Dodoma


Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan akimkaribisha Balozi wa China aliyemaliza muda wake hapa nchini Wang Ke mara baada ya kuwasili Ikulu ya Chamwino Mkoani Dodoma leo tarehe 4 Juni, 2021 


Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan akiwa katika mazungumzo na Balozi wa China aliyemaliza muda wake Wang Ke ambaye alifika Ikulu ya Chamwino kwa ajili ya kuaga mara baada ya kumaliza muda wake hapa nchini.


Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan akiwa katika picha ya kumbukumbu na Balozi wa China aliyemaliza muda wake Wang Ke ambaye alifika Ikulu ya Chamwino kwa ajili ya kuaga mara baada ya kumaliza muda wake hapa nchini.



Balozi wa China aliyemaliza muda wake hapa nchini Wang Ke akizungumza na Wanahabari mara baada ya mazungumzo yake na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan, Ikulu ya Chamwino Mkoani Dodoma.  

Rais Samia Suluhu Hassan leo tarehe 04 Juni, 2021 ameagana na aliyekuwa Balozi wa China hapa nchini Mhe. Wang Ke ambaye amemaliza kipindi chake.

Katika mazungumzo yaliyofanyika Ikulu Chamwino Mkoani Dodoma, Rais Samia amemshukuru  Wang Ke kwa jitihada zake za kuendeleza na kukuza uhusiano wa Tanzania na China ambao umewezesha kutekelezwa kwa miradi mbalimbali iliyofadhiliwa na China hapa nchini ikiwemo maktaba ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, jengo la Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki lililopo Jijini Dar es Salaam na msaada wa shilingi Bilioni 35 zilizoelekezwa katika miradi ya maendeleo.

Rais Samia pia amemshukuru kwa ufadhili wa China katika miradi mbalimbali ya ujenzi wa miundombinu na uboreshaji wa huduma za kijamii pamoja na ushirikiano wa kibiashara na uwekezaji ambao pamoja na kukuza pato la nchi umesaidia Watanzania wengi kupata ajira.

Rais Samia amepokea salamu za Rais wa China Rais Xi Jinping na amemtakia yeye na Wachina wote maadhimisho mema ya miaka 100 ya Chama cha Kikomunisti cha China (CPC) itakayotimia tarehe 01 Julai, 2021 na shukrani kwa uhusiano na ushirikiano mzuri kati ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) na CPC, na uhusiano na ushirikiano kati ya Tanzania na China uliodumu kwa miaka 56.

Ameeleza kuwa anatambua kazi kubwa iliyofanywa na CPC katika kuijenga China, kujenga na kuimarisha uhusiano wake na Mataifa mbalimbali ikiwemo Tanzania na amemhakikishia kuwa Tanzania itaendeleza na kukuza zaidi uhusiano na ushirikiano huo.

Kwa upande wake Mhe. Wang Ke amemshukuru  Rais Samia kwa ushirikiano mkubwa alioupata kutoka Serikalini wakati wote wa kipindi chake cha Ubalozi na amempongeza kwa kupokea kijiti cha Urais kutoka kwa aliyekuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Hayati Dkt. John Pombe Magufuli.

Amewasilisha salamu za Rais wa China  Xi Jinping ambaye amesema ana imani kubwa kuwa  Rais Samia atafanya mazuri na makubwa kwa Tanzania kutokana na dhamira yake ya kuendeleza kazi nzuri iliyofanywa na Hayati Dkt. Magufuli hususani uendelezaji wa miradi ya kimkakati, kuchukua hatua madhubuti za kuboresha mazingira ya kufanya biashara na kuchukua hatua za kisayansi za kukabiliana na janga la ugonjwa wa Korona (Covid-19).

Amesema China itaunga mkono juhudi zinazofanywa na  Rais Samia na ameshukuru kwa salamu za heri na pongezi kwa chama cha CPC kutimiza miaka 100 ambapo pamoja na kufanya mageuzi na kuleta maendeleo makubwa kwa China kimekua kutoka wanachama 50 hadi wanachama Milioni 92 na kwa sasa kipo katika mchakato wa mageuzi mengine ya mfumo wake wa ujamaa wenye misingi ya Kichina utakaojenga nchi ya kisasa zaidi na kutoa elimu ya historia ya China kwa vijana wake.

Aidha, Wang Ke amesema China ipo tayari kushirikiana na Tanzania katika kukabiliana na ugonjwa wa Korona.

Mazungumzo hayo yamehudhuriwa na Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Mhe. Mbarouk Nassor Mbarouk.

DKT. MAHENGE AIPONGEZA TARURA KUANZA KUTUMIA MFUMO WA KIELEKTRONIKI WA UKUSANYAJI MAPATO “TeRMIS”

Na. Bebi Kapenya

Mkuu wa Mkoa wa Singida, Mhe Dkt. Binilith Mahenge amepongeza Wakala wa Barabara za Vijijini na Mijini (TARURA) kuanza kutumia Mfumo wa Kielektroniki wa Ukusanyaji  wa  Mapato ujulikanao kama “TARURA e-Revenue  Management Information System” (TeRMIS) katika Mkoa wa Singida.

Hayo yamejiri wakati wa kikao kazi kilicholenga kuwapatia mafunzo viongozi wa Mkoa wa Singida wakiwemo Wajumbe wa Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Mkoa juu ya Mfumo wa Kielektroniki wa Ukusanyaji wa Mapato ujulikanao kama “TeRMIS”.

Mkuu wa Mkoa ameeleza kuwa lengo la mfumo ni kuboresha ufanisi wa ukusanyaji wa mapato ya Serikali yatakayosaidia maendeleo na maboresho ya miundombinu ya barabara, pia mfumo unalenga kumpunguzia mtumiaji wa maegesho kero ya kudaiwa ushuru kwani mteja atalipa mwenyewe kwa kutumia mtandao wowote wa simu ya mkononi, au kupitia Tawi la Benki ya NMB na CRDB au kupitia kwa Mawakala.

 

“Nitumie fursa hii kuwapongeza TARURA kwa kuleta mfumo huu katika Mkoa wetu kwani mfumo utaleta tija katika ukusanyaji mapato ya Serikali na utoaji wa huduma kwa wananchi”, alisema Dkt. Mahenge.

 

Aidha, Dkt. Mahenge amewataka TARURA kuhakikisha elimu ya matumizi ya mfumo inafika kikamilifu kwa wananchi ili wawe na uelewa wa pamoja ili kuepusha malalamiko mbalimbali kutoka kwa wananchi.

 

Pia, Mkuu wa Mkoa ametoa wito kwa wananchi kupokea mabadiliko hayo na kuanza kulipa wao wenyewe Ushuru wa Maegesho ili kuepuka adhabu na faini zisizo za lazima.

 

Kwaupande wake Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Singida, Mhe. Juma Kilimbah ameipongeza TARURA kwa kuanza kutumia mfumo huo kwani mapato ya Serikali yataongezeka kwakuwa kwa kutumia mfumo huo unalipa moja kwa moja serikalini na mapato hayo yatasaidia kuboresha miundombinu ya barabara katika Manispaa ya Singida.

 

Mfumo wa Kielektroniki wa Ukusanyaji Mapato yaani “TARURA e-Revenue Management Information System” (TeRMIS) unaosimamiwa na Wakala wa Barabara za Vijijini na Mijini (TARURA) umeanza kufanya kazi katika Mkoa wa Iringa na Singida na unatarajia kusambazwa nchi nzima.

BALOZI MULAMULA AKUTANA NA KUFANYA MAZUNGUMZO NA BALOZI WA CHINA NCHINI NA NAIBU KATIBU MKUU WA JUMUIYA YA AFRIKA MASHARIKI

 


Mheshimiwa Balazo Liberata Rutageruka Mulamula (Mb) Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki leo tarehe 3 Juni 2021 kwa nyakati tofauti amekutana na kufanya mazungumzo na Mhe. WANG Ke Balozi wa China nchini Tanzania na Mhandisi Steven Mlote, Naibu Katibu Mkuu wa Sekretariet ya Jumuiya ya Afrika Mashariki anayeshughulikia masuala ya Mipango, Miundombinu, Fedha na Utawala. 

Balozi WANG amemtembelea Balozi Mulamula kwa lengo la kumuaga baada ya kumaliza muda wake wa utumishi hapa nchini. Balozi WANG ameeleza furaha na kuridhishwa kwake na namna Wizara na Serikali kwa ujumla ilivyompa ushirikiano kwa kipindi chote alichokuwa nchini akitekeleza majukumu yake. Aidha, ameonyesha furaha yake juu ya namna mahusiano kati ya Tanzania na China yanavyoendelea kushamiri na hivyo kuchagiza maendeleo kwa Nchi zote mbili. 

Balozi Mulamula kwa upande wake amempongeza na kumshukuru Balozi WANG kwa utumishi na mchango wake alioutoa katika kudumisha na kukuza mahusiano kati ya Tanzania na China. Sambamba na pongezi hizo Balozi Mulamula amemtakia kheri Balozi WANG katika maisha yake na utumishi. Vilevile Balozi Mulamula amemwakikishia Balozi WANG kuwa Tanzania itaendelea kudumisha na kukuza mahusiano mazuri yaliyopo kati ya Tanzania na China yaliyodumu kwa nyakati zote. 

Katika hatua nyingine Mheshimiwa Balozi Mulamula na Mheshimiwa Balozi Mbarouk Nassor Mbarouk (Mb), Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki kwa pamoja wamekutana na kufanya mazungumzo na Mhandisi Steven Mlote, Naibu Katibu Mkuu Sekretariet ya Jumuiya ya Afrika Mashariki anayeshughulikia masuala ya Mipango, Miundombinu, Fedha na Utawala. Mhandisi Mlote amefika Wizarani kwa lengo la kujitambulisha kwa Waziri Mulamula na Naibu Waziri Mbarouk na kuwapongeza kwa kuteuliwa kushika nyadhifa hizo. 

Balozi Mulamula na Balozi Mbarouk wamemweleza Mhandisi Mlote kuwa Wizara na Serikali kwa ujumla itaendelea kutoa ushirikiano kwa Sekretariet ya Jumuiya ya Afrika Mashariki katika shughuli zao za kuiletea maendeleo Jumuiya. Aidha, wameipongeza Sekretariet kwa kazi nzuri ya kutekeleza miradi ya kimkakati kama vile ujenzi barabara, miradi ya umeme na maji ambayo inaleta mchango mkubwa katika kukuza uchumi kwa Nchi wanachama. 
Mheshimiwa Balazo Liberata Rutageruka Mulamula (Mb), Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki akisisitiza jambo wakati wa mazungumzo na Mhandisi Steven Mlote, Naibu Katibu Mkuu Sekretariet ya Jumuiya ya Afrika Mashariki anayeshughulikia masuala ya Mipango, Miundombinu, Fedha na Utawala yaliyofanyika katika Ofisi za Wizara jijini Dodoma
Mheshimiwa Balazo Liberata Rutageruka Mulamula (Mb), Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki akimsikiliza Mhandisi Steven Mlote, Naibu Katibu Mkuu Sekretariet ya Jumuiya ya Afrika Mashariki

Mazungumzo yakiendelea


Mheshimiwa Balazo Liberata Rutageruka Mulamula (Mb), Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mheshimiwa Balozi Mbarouk Nassor Mbarouk (Mb), Naibu Waziri (kulia) na Mhandisi Steven Mlote,Naibu Katibu Mkuu Sekretariet ya Jumuiya ya Afrika Mashariki wakiwa katika picha pamoja baada ya mazungumzo yaliyofanyika katika Ofisi za Wizara jijini Dodoma.

Thursday, June 3, 2021

BALOZI MBAROUK AKUTANA NA KUFANYA MAZUNGUMZO NA MWAKILISHI WA KAMPUNI YA SHELL

 

Mheshimiwa Balozi Mbarouk Nassor Mbarouk (Mb), Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki leo tarehe 3 Juni 2021 amekutana na kufanya mazungumzo na Bw. Ahmed Salim anayeratibu Mahusiano kati ya Kampuni ya Shell na Serikali. Bw. Salim ameeleza ameeleza lengo la ziara yake Wizarani ni kuelezea dhamira ya Kampuni ya Shell ya kuwekeza katika Sekta ya Gesi (LNG) Nchini. 

Balozi Mbarouk licha ya kupongeza uamuzi wa Kampuni ya Shell ya kuwekeza nchini amemweleza Bw. Salim kuwa Wizara na Serikali ipo tayari kutoa ushirikiano kwa kampuni hiyo katika shughuli zao uwekezaji. Pia amweleza kuhusu dhamira ya Serikali ya kuendelea kuboresha mazingira ya uwekezaji na ufanyaji biashara nchini. 

Bw. Salim ameeleza kuwa Kampuni ya Shell inatarajia kufanya uwekezaji wenye thamini ya fedha za kitanzania zaidi shilingi bilioni 30.
Mheshimiwa Balozi Mbarouk Nassor Mbarouk (Mb), Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki akimkaribisha Bw. Ahmed Salim anayeratibu Mahusiano kati ya Kampuni ya Shell na Serikali alipowasili Wizarani jijini Dodoma.
Mheshimiwa Balozi Mbarouk Nassor Mbarouk (Mb), Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki akimweleza jambo Bw. Ahmed Salim anayeratibu Mahusiano kati ya Kampuni ya Shell wakati wa mazungumzo yaliyofanyika katika jijini Dodoma

Mheshimiwa Balozi Mbarouk Nassor Mbarouk (Mb), Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki akimsikiliza Bw. Ahmed Salim anayeratibu Mahusiano kati ya Kampuni ya Shell na Serikali alipowasili Wizarani jijini Dodoma
Mazungumzo yakiendelea

WAZIRI MKENDA AFANYA MAZUNGUMZO NA RC SENDIGA AAHIDI KUVALIA NJUGA UWEZEKANO KUANZISHA VITALU VYA KUZALISHA MICHE YA PARACHICHI IRINGA

Waziri wa Kilimo Mhe Prof. Adolf Mkenda (Katikati) akiwa katika picha ya pamoja na Mkuu wa Mkoa wa Iringa Mhe Queen Sendiga (Kulia), Katibu Tawala wa Mkoa wa Iringa Bi Happiness Seneda (Kushoto) mara baada ya kumalizika kwa mazungumzo yaliyofanyika leo tarehe 3 Juni 2021 Ofisini kwake Jijini Dodoma. (Picha Zote Na Mathias Canal, Wizara ya Kilimo)
Waziri wa Kilimo Mhe Prof. Adolf Mkenda akisisitiza jambo wakati akizungumza na Mkuu wa Mkoa wa Iringa Mhe Queen Sendiga pamoja na Katibu Tawala wa Mkoa wa Iringa Bi Happiness Seneda leo tarehe 3 Juni 2021 Ofisini kwake Jijini Dodoma.
Katibu Tawala wa Mkoa wa Iringa Bi Happiness Seneda akisisitiza jambo wakati wa kikao kazi na Waziri wa Kilimo Mhe Prof. Adolf Mkenda pamoja na Mkuu wa Mkoa wa Iringa Mhe Queen Sendiga leo tarehe 3 Juni 2021 Ofisini kwake Jijini Dodoma.
Waziri wa Kilimo Mhe Prof. Adolf Mkenda akisisitiza jambo wakati akizungumza na Mkuu wa Mkoa wa Iringa Mhe Queen Sendiga pamoja na Katibu Tawala wa Mkoa wa Iringa Bi Happiness Seneda leo tarehe 3 Juni 2021 Ofisini kwake Jijini Dodoma.
Mkuu wa Mkoa wa Iringa Mhe Queen Sendiga pamoja na Katibu Tawala wa Mkoa wa Iringa Bi Happiness Seneda wakimsikiliza kwa makini Waziri wa Kilimo Mhe Prof. Adolf Mkenda akisisitiza jambo wakati leo tarehe 3 Juni 2021 wakati wakifanya mazungumzo Ofisini kwake Jijini Dodoma.

Na Mathias Canal, Wizara ya Kilimo-Dodoma

 

Kilimo cha parachichi kinaendelea kukua hasa katika nchi za Afrika Mashariki, Pia kilimo hichi hakihitaji fedha nyingi na subira ya ukuaji wa matunda haya mara nyingi huambatanishwa na faida kubwa wakati wa mavuno.


Kwa Tanzania, kilimo hichi kimeanza kushika kasi zaidi mwaka 2015 ambapo baadhi ya watu walijitokeza na kuelezea mafanikio waliyopata kutokana na kilimo cha parachichi.


Nchi za Ulaya kama Denmark, Ufaransa, Uingereza, Norway na Uholanzi zimeonyesha kufurahishwa na maparachichi yanayotoka nchi za Afrika Mashariki hususani Tanzania. Mikoa iliyojikita zaidi na uzalishaji wa zao hili ni Kilimanjaro, Mbeya, Njombe na Iringa, hii ni kutokana na hali ya hewa ya baridi iliyopo katika mikoa hiyo.

Kufuatia umuhimu huo wa zao la parachichi Waziri wa Kilimo Mhe Prof. Adolf Mkenda leo tarehe 3 Juni 2021 amekutana na kufanya mazungumzo na Mkuu wa Mkoa wa Iringa Mhe Queen Sendika Ofisini kwake Jijini Dodoma.

Katika mazungumzo yao Waziri Mkenda amemuhakikishia Rc Sendika kuwa Wizara ya Kilimo imejipanga kuimarisha sekta hiyo katika zao la Parachichi ambapo miongoni mwa mikoa ya kimkakati katika zao hilo ni pamoja na mkoa wa Iringa.


Kadhalika Waziri Mkenda amesema kuwa atafanya mashauriano na Taasisi ya Utafiti wa Kilimo Tanzania (TARI) ili kujua nini kinahitajika kwa ajili ya kuanzisha vitalu vya uzalishaji mbegu mkoani Iringa vitakavyorahisisha upatikanaji wa miche ya parachichi.

Kwa upande wake Mkuu wa Mkoa wa Iringa Mhe Queen Sendiga ambaye katika mazungumzo hayo aliambatana na Katibu Tawala wa Mkoa huo Bi  Happiness Seneda amesema kuwa Mkoa wa Iringa hutegemea miche ya Parachichi kutoka mikoa ya Njombe na Iringa hivyo jambo hilo huchelewesha kasi ya uzalishaji wa Parachichi.

Kufuatia changamoto hiyo Rc Sendika amemueleza Waziri Mkenda kuhusu uhitaji wa miche mingi ya Parachichi ikwiemo uwezekano wa kuanzisha vitalu vya kuzalisha miche hiyo kwa wingi mkoani Iringa.

Wapewe jicho la pekee kupatiwa miche na ikiwezekana kuwe na uzalishaji wa miche ya Parachichi Mkoani Iringa

Amesema kuwa wakulima wengi wanaojihusisha na kilimo hicho huuza katika soko la nje hivyo kuna umuhimu kwa serikali kuwezesha vijana nchini hasa wasio na kazi za kuajiriwa kujihusisha na kilimo hiki kwa kuwa hakina gharama.

Wednesday, June 2, 2021

SPIKA NDUGAI AKUTANA NA VIONGOZI WAKUU WA TAKUKURU JIJINI DODOMA



Spika wa Bunge, Job Ndugai (kushoto) akizungumza na Mkurugenzi Mkuu wa TAKUKURU, CP. Salum Hamduni (katikati) pamoja na Naibu Mkurugenzi wa TAKUKURU, Neema Mwakalyeye walipomtembelea Ofisini kwake Bungeni Jijini Dodoma, Juni 2, 2021
Spika wa Bunge, Job Ndugai (katikati) katika picha ya pamoja na Mkurugenzi Mkuu wa TAKUKURU, CP. Salum Hamduni (kulia) pamoja na Naibu Mkurugenzi wa TAKUKURU, Neema Mwakalyeye walipomtembelea Ofisini kwake Bungeni Jijini Dodoma, Juni 2, 2021
 
Spika wa Bunge, Job Ndugai (katikati) katika picha ya pamoja na ugeni kutoka TAKUKURU wakiongozwa na Mkurugenzi Mkuu wa TAKUKURU, CP. Salum Hamduni (watatu kulia) walipomtembelea Ofisini kwake Bungeni Jijini Dodoma, Juni 2, 2021, Watatu kushoto ni Naibu Mkurugenzi wa TAKUKURU, Neema Mwakalyeye

(PICHA NA OFISI YA BUNGE)

Tuesday, June 1, 2021

WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII AMKABIDHI ZAWADI NYOTA WA KLABU WA CRYSTAL PALACE, MAMADOU SAKHO

 

Nyota wa Klabu ya Crystal Palace na timu ya Taifa ya Ufaransa, Mamadou Sakho akizungumza na Vyombo vya habari katika mkutano wa Waandishi wa habari  uliofanyika Jijini Dodoma ambapo Nyota huyo ameahidi kuwaleta Mastaa wengi wa Soka kuja kutembelea vivutio vya Utalii nchini. Mamadou Sakho ni Balozi wa Hiari wa Utalii Tanzania.

Waziri wa Maliasili na Utalii, Dkt.Damas Ndumbaro akizungumza na  Nyota wa Klabu ya Crystal Palace na timu ya Taifa ya Ufaransa, Mamadou Sakho mara baada ya  mkutano na vyombo vya habari uliofanyika Jijini  Dodoma ambapo Nyota huyo Sakho  ameahidi kuwaleta Mastaa wengi wa Soka kuja kutembelea vivutio vya Utalii nchini. Mamadou Sakho ni Balozi wa Hiari wa Utalii Tanzania.

Waziri wa Maliasili na Utalii, Dkt.Damas Ndumbaro akimpa zawadi ya Tisheti kutoka Hifadhi ya Mamlaka ya Ngorongoro  Nyota wa Klabu ya Crystal Palace na timu ya Taifa ya Ufaransa, Mamadou Sakho akiwa na Mkewe Majda Sakho mara baada ya mkutano na vyombo vya habari uliofanyika Jijini Dodoma ambapo Nyota huyo ameahidi kuwaleta Mastaa wengi wa Soka kuja kutembelea vivutio vya Utalii nchini. Mamadou Sakho ni Balozi wa Hiari wa Utalii Tanzania.

 

Waziri wa Maliasili na Utalii, Dkt.Damas Ndumbaro akimpa zawadi ya moja ya kikombe chenye nembo ya Hifadhi za Taifa, Nyota wa Klabu ya Crystal Palace na timu ya Taifa ya Ufaransa, Mamadou Sakho akiwa na Mkewe Majda Sakho mara baada ya mkutano na vyombo vya habari uliofanyika Jijini Dodoma ambapo Nyota huyo ameahidi kuwaleta Mastaa wengi wa Soka kuja kutembelea vivutio vya Utalii nchini. Mamadou Sakho ni Balozi wa Hiari wa Utalii Tanzania. Wa kwanza kushoto ni Katibu Mkuu wa Wizara ya Maliasili na Utalii, Dkt.Allan Kijazi

SERIKALI INAENDELEA KUBORESHA MAZINGIRA YA BIASHARA MPAKANI, WAFANYABIASHA ZINGATIENI SHERIA NA TARATIBU ZA KUFANYA BIASHARA

 

Na Eliud Rwechungura

Waziri wa Viwanda na Biashara, Prof. Kitila Mkumbo (Mb) amewahakikishia Wafanyabiashara kuwa Serikali inaendelea kuboresha mazingira ili kuhakikisha wanafanikiwa huku akiwahasa wafanyabiashara wa Tanzania na Kenya kuzingazia Sheria na taratibu zilizowekwa ndani ya Jumuiya ya Afrika Mashariki ili kuondokana na vikwazo ambavyo vimekuwa vikiwekwa  kutoka na kutozingatia Sheria na taratibu za kufanya biashara mipakani.

 

Prof. Mkumbo ameyasema hayo 30 Mei 2021 alipoambatana na Mawaziri wa Kenya na Tanzania kutembelea Mpaka wa Namanga kujionea jinsi biashara na shughuli za upitishaji wa bidhaa na huduma zinafavyofanyika katika Mpaka huo baada ya nchi hizo kukubalina kuondoa vikwazo 30 vya biashara visivyokuwa vya kiushuru.

 

“Rais wa Jamhuri ya muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan anataka kuona Maisha ya Watanzania yanaboreka na biashara zinafanyika vizuri, niwahakikishie wafanyabiashara wa Watanzania, Serikali yenu ipo na nyie na itaendelea kuwaunga mkono na kuwapa msaada ili kuona mnafanikiwa lakini kwa upande wenu tunaomba katika kufanya kwenu biashara mzingatie sheria na taratibu zilizopo kwasababu nchi zetu zinaongozwa na utawala wa sheria” ameeleza Prof. Mkumbo

 

Ameongeza kuwa, lengo la ziara hiyo ni utekelezaji wa maelekezo ya Waheshimiwa Marais wa Tanzania na Kenya ya kuhakikisha mahusiano ya wananchi wa nchi mbili yanaboreka lakini muhimu Zaidi biashara hazikwami ndo maana wamekutana Mawaziri kutatua mambo mengi yaliyokuwa yanakwamisha biashara ikiwemo changamoto ya mahindi hapa mpakani wameweza kuizungumzia  na anashukuru imetatuliwa na mambo mengine mengi yalikuwepo pande zote mbili za Tanzania na Kenya.

 

Aidha, Prof. Mkumbo amewapongeza wataalam wa pande zote mbili za Tanzania na Kenya kwa kazi kubwa wanayoendelea kuifanya huku akiwahasa kuendelea kuimalisha mahusiano mazuri kwa kukaa Pamoja na kujadiliana kwa kuzitatua changamoto kwasababu ni jambo kubwa na la muhimu viongozi wetu wanalotaka kuliona

 

Kwa upande wake, Waziri wa Viwanda, Biashara na Maendeleo ya Wajasiliamali nchini Kenya Mhe. Betty Maina amefurahishwa na kuona changamoto 30 kati ya 64 zimetatuliwa na hizo nyingine zilizobaki wamejiwekea muda wa miezi mitatu kuzifanyia kazi huku akiwataka wafanyabiashara wa pande mbili kuendelea kuzingatia sheria ambazo zimewekwa kwa pande zote mbili za Kenya Tanzania wakati wa ufanyaji biashara.

MAADHIMISHO YA WIKI YA MAZIWA YAANZA NA WENYE MAHITAJI MAALUM


 

Na. Edward Kondela

Bodi ya Maziwa nchini (TDB) imesema katika kuhakikisha wananchi wanakuwa na afya bora imeamua kugawa maziwa kwa watu wenye mahitaji maalum kutokana na virutubisho vilivyopo kwenye maziwa hayo ambavyo vitawasaidia kuimarisha afya zao.

Akizungumza leo (31.05.2021) mara baada ya kuhitimisha siku ya kwanza ya ugawaji maziwa ikiwa ni sehemu ya shughuli mbalimbali zinazofanywa na TDB katika maadhimisho ya wiki ya unywaji maziwa kitaifa yanayofanyika Mkoani Tanga, kuanzia tarehe 31 Mei hadi 04 Juni Mwaka 2021, Afisa Msindikaji wa Maziwa kutoka bodi hiyo Bw. Dotto Nkuba amesema katika siku ya kwanza bodi imetembelea shule tatu za msingi za Mkoa wa Tanga ambazo pia zinawahudumia watoto wenye mahitaji maalum ili kutoa kipaumbele kwa watoto hao kunywa maziwa na kuhamasisha jamii kuwa na utaratibu kwa kunywa maziwa ili kuimarisha afya zao.

“Lengo la kutoa maziwa kwa watu wenye mahitaji maalum tunahimiza kunywa maziwa kutokana na virutubisho vitokanavyo katika maziwa na tumeangalia watoto wa shule kwa siku ya leo na hii haimaanishi watu wengine wasinywe maziwa bali wanywe kwa faida ya afya zao ila hatua hii itakuwa mwendelezo wa kuyafikia makundi mengine.” Amesema Bw. Nkuba

Ameongeza kuwa maadhimisho ya wiki ya unywaji maziwa kitaifa yanayofanyika Mkoani Tanga, yanalenga kuhamasisha wananchi kunywa maziwa kwa sababu ni chakula ambacho kina virutubisho vyote ambavyo ni muhimu kwa mwili wa binadamu hususan maziwa yaliyosindikwa ambayo yamekidhi ubora.

Aidha, amesema Bodi ya Maziwa nchini inahimiza wananchi kunywa maziwa kwa wingi ili kuwa na utamaduni wa kunywa maziwa na kuviwezesha viwanda vya kuchakata maziwa nchini kuuza bidhaa zao kwa wingi.

Kwa upande wake Kaimu Afisa Lishe Mkoa wa Tanga Bi. Sakina Mustapha, amesema wamekuwa wakifanya kazi kubwa ya kutoa elimu juu ya umuhimu wa unywaji maziwa kutokana na maziwa kuwa na madini na vitamini pamoja na maji ambavyo vyote hivyo vinajenga mwili, kulinda mwili, kuongeza ufanisi wa kujenga mifupa sambamba na meno, kupata sukari na nguvu mwilini pamoja na nguvu ya ziada ya kufanya kazi.

Bi. Mustapha amewaasa wananachi kwa ujumla kunywa maziwa walau kikombe kimoja kila siku ili kuuwezesha mwili kuongeza virutubisho muhimu vitokanavyo na maziwa.

Wanafunzi waliopatiwa maziwa leo na Bodi ya Maziwa nchini ni kutoka katika Shule za Msingi Chuda, Nguvumali na Usagara zilizopo jijini Tanga na zoezi la ugawaji litaendelea kwa kuyafikia makundi mbalimbali ya watu maalum.

Maadhimisho ya wiki ya unywaji maziwa kitaifa yanafanyika Mkoani Tanga kuanzia Tarehe 31 Mei hadi 04 Juni Mwaka 2021, katika viwanja vya Tangamano yakiwa yamebeba kauli mbiu “Kunywa Maziwa ya Kwetu, Ongeza Uzalishaji na Usindikaji, Kazi Iendelee.”

RAIS SAMIA AUSIMAMISHA KAZI UONGOZI WA SOKO LA KARIAKOO

 



Rais Samia Suluhu Hassan ausimamisha kazi Uongozi wa Soko la kariakoo na kusema kuwa serikali inafanya tathimini ya soko na kuvitaka vyombo vya serikali kufanya uchuguzi.

Amesema hayo leo alipotembelea sokoni hapo kujionea hali halisi na kusema kuwa hali iliyopo sokoni hapo hairidhishi " na tunakwenda kuchukua hatua zinazofaa lakini kwa wakati huu naomba muendelee na biashara zenu kwa salama bila vurugu Serikali ipo pamoja nanyi" Amesema Rais Samia 

Aidha Rais Samia amewataka wafanyabiashara kufuata sheria zilizopo kwani njia zote zimezingirwa na kujegwa vibanda kila mahali na kushindwa kupitika.

"Seriakli yetu hii kuanzia wakati wa Mpendwa Marehemu Magufuli yupo hadi leo lengo letu nia yetu ni kusaidia wafanya biashara wadogo wadogo sasa tuliyo yaona ndani nimeongea na wanawake wawili watatu na mwingine mwananume naona kama usaidizi wa wafanyabiashara wadogo wadogo haupo ila kuna kutengeneza faida kwa uongozi wa soko'' Rais Samia Suluhu Hassan


KAMATI YA BUNGE YATOA WITO WAKANDARASI WABOVU MIRADI YA REA WASIPEWE TENA KAZI

 





Veronica Simba na Zuena Msuya

Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini imetoa wito kwa Serikali kuwa wakandarasi ambao hawakutekeleza miradi ya umeme vijijini kwa kiwango kinachoridhisha katika awamu zilizopita, wasipewe tena kazi hiyo.

Wito huo ulitolewa jana, Mei 31, 2021 jijini Dodoma na Mwenyekiti wa Kamati hiyo, Dustan Kitandula alipokuwa akitoa majumuisho ya hoja mbalimbali zilizotolewa na baadhi ya Wajumbe, katika semina iliyoandaliwa na Wizara ya Nishati, ikilenga kuijengea Kamati hiyo uelewa wa kazi zinazoendelea kutekelezwa na sekta husika.

Alisema, baadhi ya wakandarasi wamekuwa wakikwamisha jitihada na dhamira njema ya serikali inayolenga kuwafikishia umeme wananchi wote walioko vijijini, kutokana na kuchelewesha kukamilisha miradi hiyo na wengine kutekeleza chini ya kiwango kinyume na mikataba yao.

Aliutaka Uongozi wa Wizara ya Nishati na Taasisi zake, hususan Wakala wa Nishati Vijijini (REA) na Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO), kutoa kipaumbele kwa wakandarasi waliotekeleza kazi zao kwa umahiri katika awamu zilizopita.

Akizungumza kwa niaba ya Uongozi mzima wa Wizara na Taasisi zake, Waziri wa Nishati Dkt. Medard Kalemani aliwahakikishia Wajumbe wa Kamati hiyo kuwa, Serikali itazingatia maelekezo yote yaliyotolewa.

Akifafanua, Waziri Kalemani alieleza kuwa tayari Serikali ilikwishachukua hatua za kuachana na wakandarasi wabovu ambapo alibainisha kuwa katika utekelezaji wa mradi wa usambazaji umeme vijijini, awamu ya tatu, mzunguko wa pili ambao unaendelea hivi sasa, wakandarasi wote wazembe hawakupewa kazi.

Katika hatua nyingine, Dkt. Kalemani aliieleza Kamati hiyo kuwa, Wizara yake imeamua kutumia nguzo za zege katika maeneo korofi hususan yenye ardhi inayohifadhi maji ili kutatua changamoto ya kuharibika kwa nguzo za miti ndani ya kipindi kifupi.

Pia, aliahidi kuwa Wizara ya Nishati itaendelea kusimamia kikamilifu suala la uzalishaji nguzo za miti zenye ubora, unaofanyika ndani ya nchi ili kuhakikisha zinakidhi viwango vya kimataifa. Aliongeza kuwa, lengo ni kuepusha hasara katika miradi ya usambazaji umeme inayotekelezwa kote nchini, ambapo Serikali inatumia nguzo hizo baada ya kuacha kuagiza kutoka nje ya nchi.

Awali, akiwasilisha mada kuhusu miradi mbalimbali inayotekelezwa na REA, Mkurugenzi wake Mkuu, Mhandisi Amos Maganga alibainisha kuwa Wakala umejiwekea malengo ya kufikisha miundombinu ya umeme kwenye vijiji vyote Tanzania Bara, ifikapo Desemba, 2022.

Aidha, alieleza kuwa REA imejipanga kuhakikisha hali ya upatikanaji wa huduma za umeme inafikia asilimia 100 ifikapo mwaka 2030.

Kwa upande wa mafanikio, Mhandisi Maganga alibainisha kuwa ni pamoja na kufikisha na kusambaza umeme katika Makao Makuu ya Wilaya zote za Tanzania Bara. Vilevile alisema, kupitia REA, Serikali imewezesha hali ya upatikanaji wa umeme maeneo ya vijijini kuongezeka kutoka asilimia mbili mwaka 2007 hadi kufikia asilimia 69.6 mwaka 2020.

Alitaja mafanikio mengine kuwa ni kuwezesha taasisi za afya, elimu na maji kufikiwa na huduma za umeme hivyo kuboresha na kuongeza ufanisi katika utoaji huduma. Pia, kuwezesha uboreshwaji wa kilimo cha umwagiliaji katika mashamba.

Semina hiyo ilifanyika katika Ofisi ndogo za Wizara zilizopo Kikuyu Dodoma. Viongozi wengine wa Serikali walioshiriki ni pamoja na Naibu Waziri wa Nishati Stephen Byabato, Katibu Mkuu Mhandisi Leonard Masanja, Naibu Katibu Mkuu Kheri Mahimbali na Wataalamu mbalimbali wa Wizara, REA na TANESCO.

Taasisi nyingine zilizowasilisha mada katika semina hiyo ni kutoka TANESCO iliyowasilishwa na Mkurugenzi wake Mtendaji, Dkt. Tito Mwinuka pamoja na kampuni yake tanzu ya uendelezaji jotoardhi (Tanzania Geothermal Development Company - TGDC), iliyowasilishwa na Meneja Mkuu, Mhandisi Kato Kabaka.