Matokeo chanyA+ online




Tuesday, September 14, 2021

ULEGA AAGIZA ZIUNDWE KAMATI ZA USULUHISHI MIGOGORO YA WAKULIMA, WAFUGAJI


Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Abdallah Ulega  akizungumza na wananchi wa Kijiji cha Nanjilinji kwenye mkutano uliofanyika katika Kijiji hicho Kilichopo Wilayani Kilwa, mkoani Lindi jana, akiwa katika mkutano huo aliwasiliana kwa njia ya simu na Mwenyekiti wa Chama cha Wafugaji  Tanzania ili aende kujadiliana kwa pamoja wakiwemo wafugaji na viongozi wa Kijiji hicho ili kuzipatia ufumbuzi kero zao.
Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Abdallah Ulega (kulia) akiteta jambo na Mkuu wa Wilaya ya Kilwa, Zainab Kawawa muda mfupi kabla ya kuanza ziara ya kutembelea Vijiji vya Nakiu na Nanjilinji vilivyopo wilayani humo jana.

Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Abdallah Ulega (kulia) akitoa maelekezo kwa Watendaji wa Serikali katika Mkutano uliofanyika katika Kijiji cha Nakiu Kilichopo Wilayani Kilwa, mkoani Lindi jana.Ulega alifanya ziara Wilayani humo kwa lengo la kusikiliza na kutatua kero za Wakulima na Wafugaji ambapo baada ya kusikiliza kero hizo  aliagiza kuundwa kwa kamati za maridhiano zitakzaokuwa zinashughulika migogoro hiyo mapema inapojitokeza. 


Na Mbaraka Kambona, Kilwa.


Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Abdallah Ulega amewataka viongozi wa  Serikali kuanzia ngazi za Vitongoji, Vijiji, Kata na Wilaya kuhakikisha wanaunda kamati za maridhiano kwa ajili ya kusuluhisha migogoro ya wakulima na wafugaji ambayo imekuwa ikijitokeza katika baadhi ya maeneo  na kuleta madhara kwa jamii.

Ulega alitoa agizo hilo kwenye ziara aliyoifanya katika Kijiji cha Nakiu Kilichopo Wilayani Kilwa, Mkoani Lindi jana baada ya kupokea kero zilizohusu migogoro mingi iliyoanza kujitokeza katika Wilaya hiyo inayowahusisha wakulima na wafugaji.

Katika Mkutano huo wananchi wa Kijiji hicho walililalamikia Jeshi la  Polisi katika Wilaya hiyo kwa  kutochukua hatua za haraka pale wanapopelekewa taarifa za wafugaji wanaolisha mifugo yao katika mashamba ya wakulima.

Wakulima hao walisema kuwa wafugaji wanaofanya vitendo hivyo wengi ni wahamiaji katika maeneo hayo na hivyo wamekuwa wakiwasababishia matatizo makubwa ikiwemo kuharibiwa kwa mazao yao na wanapotaka kufanya jitihada za kulinda mazao yao wanaishia kupata kipigo.

Kufuatia malalamiko hayo yaliyotolewa na sehemu kubwa ya wakulima hao, Waziri Ulega alitoa maelekezo kwa Watendaji wa Serikali kuanzia ngazi za chini kuanzisha kamati za usuluhishi ili ziwe zinashughulika na migogoro hiyo mapema kabla haijakuwa mikubwa na kuleta madhara.

Aliongeza pia kwa kulitaka Jeshi la Polisi Wilayani humo kuhakikisha wanatenda haki kwa kila mtu na kwa usawa ili kuondoka lawama zinazowakabili za kuonekana wanawapendelea wafugaji kuliko wakulima.

Vilevile,  aliwaekeza watendaji wa wilayani humo kuwa katika kamati hizo watakazoziunda waandae mpango mzuri wa kuweka njia kwa ajili ya kupitishia mifugo ili isiwe inapita katika mashamba ya wakulima.

Aidha, Waziri Ulega alitumia ziara hiyo pia kukemea vitendo vya kujichukulia Sheria mkononi vinavyofanywa na wakulima pamoja na wafugaji akisema kuwa kufanya hivyo ni kosa na ni miongoni mwa vitendo vinavyochangia uvunjifu wa amani. 

Naye, Mkuu wa Wilaya ya Kilwa, Zainab Kawawa katika kuhakikisha maelekezo hayo ya Naibu Waziri yanafanyiwa kazi kwa haraka aliwaagiza Watendaji wake kuhakikisha kamati hizo zinaundwa ndani ya wiki moja.

kuhusu suala la kuweka njia za mifugo, Kawawa alitoa mwezi mmoja kwa wataalam mifugo kwa kushirikiana na wafugaji na wakulima kuhakikisha njia hizo zinawekwa ili kupunguza usumbufu wa mifugo katika mashamba ya wakulima.

Aidha, Mkuu wa Wilaya huyo pia aliwataka wafugaji kuchimba mabwawa ya maji kwa ajili ya mifugo yao na kwa kufanya hivyo kutasaidia kupunguza  migogoro ya mara kwa mara na wakulima.

Kabla ya ziara hiyo ya Waziri Ulega Wilayani humo, siku chache zilizopita wafugaji waliuwawa kutokana na migogoro hiyo hiyo ya wakulima na wafugaji katika Kijiji cha Nanjilinji.

Sunday, September 12, 2021

WAZIRI DKT.GWAJIMA AMTEMBELEA MAMA MWENYE WATOTO SITA WALIOKOSA FURSA YA KUPATA ELIMU


    

Na WAMJW- DSM

Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Dkt. Dorothy Gwajima amemtembelea Mama Zaina Khamis mwenye Watoto sita waliokosa fursa ya kupata elimu ingali umri wao wanastahili kuendelea na masomo anaeishi na wanae katika kata ya Bangulo Gongo la mboto, Jijini Dar es Salaam.

Familia hiyo ilikuwa ikiishi Tabata Kinyerezi, Jijini Dar es Salaam kabla ya kutelekezwa na kuamia Bangulo ili kupata hifadhi katika kipindi hiki wanachopitia hali ngumu ya maisha na changamoto ya uhusiano wa kifamilia.

Akiongozana na Mganga Mkuu wa Mkoa wa Dar-es-salaam Dkt. Mfaume pamoja na Wataalamu wa Maendeleo ya Jamii ngazi ya Mkoa Dkt. Gwajima ameagiza familia hiyo kupewa hifadhi katika makazi ya kulelea Watoto wenye uhitaji, huku taratibu za kuwapeleka shule Watoto wote zikiendelea.

Pia, amewaagiza Wataalamu wa Maendeleo ya Jamii kufuatilia mzazi mwenza wa Mama Zaina ili kujua ukweli kuhusu jambo hilo ikibidi kutatua changamoto zao ili kuinusuru familia hiyo.

WATU 50 WANAODHANIWA KULA CHAKULA CHENYE SUMU SINGIDA WARUHUSIWA KURUDI NYUMBANI


Mkuu wa Mkoa wa Singida Dkt.Binilith Mahenge akimjulia hali jana Mwanahamisi Shabani ambaye ni mjamzito mmoja wa wananchi ambaye amelazwa Hospitali ya Mkoa wa Singida akipatiwa matibabu akidhaniwa kula chakula kinachodhaniwa kuwa na sumu.
Mkuu wa Mkoa wa Singida Dkt.Binilith Mahenge akimjulia hali na kuzungumza na Sheikh wa Kata ya Unyambwa, Ramadhani Yusuf  (kulia) ambaye amelazwa  katika Hospitali hiyo akipatiwa matibabu akidhaniwa kula chakula kinachodhaniwa kuwa na sumu. Katikati ni Kamanda wa Polisi Mkoa wa Singida Kamishna Msaidizi (ASP) Stella Mutabihirwa.
Mkuu wa Mkoa wa Singida Dkt.Binilith Mahenge akiwajulia hali  wahanga wa tukio hilo alipo watembelea jana kabla ya kuruhusiwa..
Mkuu wa Mkoa wa Singida Dkt.Binilith Mahenge akiwajulia hali  wahanga wa tukio hilo alipo watembelea jana kabla ya kuruhusiwa..
Wahanga wa tukio hilo wakiwa hospitalini hapo kabla ya kuruhusiwa.
Wahanga wa tukio hilo wakiwa hospitalini hapo kabla ya kuruhusiwa.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Singida Kamishna Msaidizi (ASP) Stella Mutabihirwa, akizungumza na madaktari wa Hospitali wakati mkuu wa mkoa alipo watembelea wahanga wa tukio hilo. 


Na Dotto Mwaibale, Singida

Watu 50 waliokuwa wamelazwa Hospitali ya Mkoa wa Singida wakipatiwa matibabu baada ya kunusurika kufa baada ya kula chakula kinachodhaniwa kuwa na sumu wameruhusiwa kurudi nyumbani baada ya afya zao kuhimarika.

Akizungumza mbele ya Mkuu wa Mkoa wa Singida Dkt.Binilith Mahenge alipowatembelea wananchi hao jana Mganga Mfawidhi wa Hospitali hiyo Banuba Deogratius alisema juzi walipokea juzi jumla ya wagonjwa 50, Wanawake 34 na Wanaume 16 ambapo hali hadi jana hali zao zilikuwa zikiendelea vizuri na baadhi yao wameanza kuwaruhusu kurudi nyumbani kuendelea na majukumu yao ya ujenzi wa Taifa.

Banuba alisema wakazi hao wa Kata ya Unyambwa Kijiji cha Kisasida katika Manispaa ya Singida mkoani hapa walifikishwa hospitalini hapo  baada ya hali zao kuwa mbaya kutokana na kula chakula kilichoandaliwa katika shughuli za ufunguzi wa Madrasa moja Katika kijiji hicho.

Akipokea taarifa hiyo  Mkuu wa Mkoa Singida Dkt Bilinith Mahenge aliwapongeza madaktari wa Hospitali hiyo kwa jitihada walizozifanya za kuhakikisha wananusuru maisha ya wananchi hao ambapo kwa sasa hali zao zinaendelea vizuri na kuipongeza Serikali kwa kuweka miundombinu mizuri ya huduma katika sekta ya afya.

Alitoa wito kwa viongozi wa Serikali na Dini kuwajibika kikamilifu katika kutoa elimu ya namna ya kuandaa chakula pamoja na kusimamia inapotokea sherehe mbalimbali kwenye maeneo yao ili kuepuka madhara ya namna hiyo yasije kutokea tena.

 Kamanda wa Polisi Mkoa wa Singida Kamishna Msaidizi (ASP) Stella Mutabihirwa alisema wanawashikilia watu saba kuhusika na tukio hilo.

" Tuna walishiriki watu saba ambao waliandaa chakula hicho na  uchunguzi ukikamilika tutatoa taarifa kamili kwa sasa tayari tumechukua mabaki ya chakula hicho kwa ajili ya kuyachunguza," alisema Mutabihirwa.

Alisema katika tukio hilo  mtoto mmoja mwenye umri wa miaka (7) aliye mtaja kwa jina la Fahad Masoud alifariki dunia kabla ya kufikishwa hospitali kwa ajili ya kupatiwa matibabu.

Friday, September 10, 2021

MWENYEKITI WA CCM NA RAIS WA TANZANIA SAMIA SULUHU HASSAN, AONGOZA KIKAO CHA KAMATI KUU YA CCM


 

 

Mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi CCM na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan, akiongoza kikao cha Kamati Kuu ya Halmashauri Kuu ya Taifa ya CCM kilichokutana leo  Sept,10,2021 Ikulu Chamwino Jijini Dodoma. 




TEA YAKAGUA MRADI WA KUKUZA UJUZI ULIOTEKELEZWA NA SIDO MKOANI SINGIDA


Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Elimu Sayansi na Teknolojia Prof.James Mdoe akizungumza na wajasiriamali waliopatiwa mafunzo na  Shirika la kuhudumia Viwanda Vidogo  (SIDO) ya kukuza ujuzi kupitia mradi wa kuongeza na kukuza ujuzi kwa Vijana na wanawake katika ziara yake ya kukagua utekelezaji wa mradi huo.

Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Elimu Tanzania Bahati Geuzye akizungumza kwenye ukaguzi huo.

Meneja wa Shirika la kuhudumia Viwanda vidogo (SIDO) Mkoa wa Singida Agnes Yesaya akizungumza kwenye ukaguzi huo.

Mjasiriamali Happy Francis akichangia jambo kwenye ukaguzi huo.

Afisa Mafunzo na Masoko kutoka SIDO  Singida,  Joel Tangai akiwasilisha taarifa ya utekelezaji wa mradi huo.

Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Elimu Sayansi na Teknolojia Prof.Mdoe, Mkurugenzi Mkuu Mamlaka ya Elimu Tanzania (TEA) Geuzye na Viongozi wengine wakisikiliza taarifa fupi ya Mradi kutoka SIDO

Wajasiriamali wakionesha bidhaa zao wanazozizalisha baada ya kupatiwa mafunzo ya kukuza ujuzi na SIDO.

Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Elimu Sayansi na Teknolojia Prof.Mdoe akikagua bidhaa za wajasiriamali.

Ukaguzi ukiendelea.
Picha ya pamoja.
Picha ya pamoja.
 

Boniphace Jilili na Dotto Mwaibale, Singida.

Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Elimu Sayansi na Teknolojia Profesa. James Mdoe ameliagiza Shirika la kuhudumia Viwanda vidogo (SIDO) Mkoa wa Singida kuangalia namna nyingine ya kuwawezesha mikopo wajasiriamali ili waweze kuongeza ufanisi kwenye biashara zao.

Prof.Mdoe alitoa wito huo leo alipolitembelea shirika hilo kwa lengo la kukagua utekelezaji wa mradi wa kuongeza ujuzi kwa Vijana na wanawake unaofadhiliwa na Benki ya Dunia.

Alilitaka shirika hilo kuongeza muda wa kurejesha mikopo ya wajasiriamali walionufaika na mradi huo ambao pia SIDO hutoa mkopo kwa ajili ya kuwawezesha wajasiriamali mbalimbali kukuza biashara zao badala ya miezi mitatu iwe zaidi ya hapo.

"Ni kweli mumewapa mikopo lakini huu muda wa miezi mitatu ni mfupi angalieni namna ya kuwaongezea muda." alisema Profesa Mdoe.

Alisema Wizara ina mradi wa kuongeza ujuzi kwa Vijana na wanawake kupitia Vyuo vya Veta, chuo cha maendeleo ya jamii na mashirika ya Umma kama SIDO kwa kupatiwa mafunzo yatakayo saidia kujiajiri na kwamba unasimamiwa na Mamlaka ya Elimu Tanzania (TEA) 

Aidha aliipongeza SIDO mkoani hapa kwa kuwawezesha wajasiriamali mbalimbali kwa kuwapatia mafunzo yatakayo wasaidia kuanzisha na kusimamia biashara wanazozianzisha ili ziwe na tija.

Alitoa wito kwa wanufaika hao kujiunga kwenye vikundi ili waweze kupata mikopo ambayo pia hutolewa na Halmashauri kuliko mtu mmoja mmoja kwani wengine hawatapata.

Akizungumzia mradi huo Mkurugenzi Mkuu Mamlaka ya Elimu Tanzania (TEA) ambao ndio msimamizi wa mradi huo Bahati Geuzye alisema lengo la Serikali ni kuwasaidia vijana wanaoshindwa kuendelea na elimu ya juu na wanawake kukuza ujuzi ili waweze kujiajiri wenyewe.

Alisema wao kama wasimamizi wa mradi huo wanatarajia kuona vijana na watu wengine wanakuza ujuzi wao kupitia mafunzo wanayoyapata katika mashirika ya Umma na Vyuo mbalimbali vya Veta na Maendeleo ya jamii ambayo mradi umewafikia.

Kwa upande wake Meneja wa Shirika la kuhudumia Viwanda vidogo (SIDO) Mkoa wa Singida Agnes Yesaya alisema wamepokea zaidi ya milioni mia moja thelathini kwa ajili ya kuwawezesha wajasiriamali 400 lakini mpaka sasa SIDO imewawezesha wajasiriamali 436 na hadi kufikia mwisho wa mradi itakuwa imewawezesha wajasiriamali 550 zaidi ya lengo.

Mradi huo ulioanza mwaka 2019 hadi 2022 unatarajiwa kutoa matokeo chanya kwa wanawake na vijana kwa kukuza ujuzi wao hivyo kupelekea kupunguza idadi ya ukosefu wa ajira.

Wednesday, September 8, 2021

DC HANANG AUNGANA NA WANANCHI KUTATUA KERO YA MAJI

Mkuu wa Wilaya ya Hanang.Janeth Mayanja (kulia) akishiriki kubeba matofali na wananchi wa Kijiji cha Lambo Kata ya Masakta mkoani Manyara wakati wakichimba mifereji jana kwa ajili ya kupitisha bomba za maji zitazoelekea katika kijiji hicho na kijiji cha jirani.
Mkuu wa Wilaya ya Hanang.Janeth Mayanja (katikati) akiwa na wakina mama wakati wa kazi hiyo ya kuchimba mifereji.
Mkuu wa Wilaya ya Hanang.Janeth Mayanja akichimba mifereji.
Mkuu wa Wilaya ya Hanang.Janeth Mayanja (katikati) akiwa na wakina baba wakati wa kazi hiyo ya kuchimba mifereji.
Kazi ikiendelea.
Mkuu wa Wilaya ya Hanang.Janeth Mayanja akichimba mifereji.
 

Na Mwandishi Wetu, Hanang.

 Changamoto  ya ukosefu wa maji iliyodumu kwa muda mrefu katika Kijiji cha Lambo Kata ya Masakta wilayani Hanang mkoani Manyara ina kwenda kukoma baada ya mkuu wa wilaya hiyo, Janeth Mayanja kuungana na wananchi wa kijiji hicho kuchimba mifereji kwa ajili ya kupitisha bomba za maji zitazoelekea katika kijiji hicho na kijiji cha jirani.

Wanakijiji wa eneo hilo wamemshukuru Mkuu wa Wilaya ya Hanang.Janeth Mayanja kwa kuamua kuungana nao kwa ajili ya kuhakikisha.maji yanapatikana ndani ya muda mfupi katika kijiji hicho kwani tangu kuanzishwa kwa kijiji hicho huduma ya maji ilikua inapatikana kwa tabu hadi kufikia wanakijiji kushindwa kupata huduma ya maji kwa ukaribu.

Akizungumza katika zoezi hilo Mayanja alisema kuwa  usambazaji wa maji katika eneo hilo lipo chini ya Mamlaka ya Maji Safi na Usafi wa Mazingira ( RUWASA) Wilaya ya Hanang ambapo alimtaka mkandarasi ahakikishe ndani ya miezi minne kijiji hicho kiwe kimepata maji.

Aidha Meneja wa RUWASA Wilaya ya Hanang Mhandisi Herbert Kijazi amewahakikishia wana kijiji wa eneo hilo pamoja na mkuu wilaya kuwa Ruwasa itahakikisha wanafanya kazi usiku na mchana na ndani ya miezi minne maji yatakuwa yanapatikana katika eneo hilo.

RAIS SAMIA AWASILI DODOMA AKITOKEA JIJINI MWANZA



Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan, akiwasili katika Uwanja wa Ndege wa Dodoma akitokea  Jijini Mwanza baada ya kusimikwa kuwa Mkuu wa Machifu wote Tanzania na kuitwa jina la Hangaya yani ni Nyota inayong`aa, katika Tamasha la Utamaduni (Mila na Desturi zetu) lililofanyika leo Sept,08,2021 katika Viwanja vya Redcross Kisesa Magu, Mkoani Mwanza.
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan, akisalimiana na Viongozi mbalimbali wa Serikali alipowasili katika Uwanja wa Ndege wa Dodoma akitokea  Jijini Mwanza baada ya kusimikwa kuwa Mkuu wa Machifu wote Tanzania na kuitwa jina la Hangaya yani ni Nyota inayong`aa, katika Tamasha la Utamaduni (Mila na Desturi zetu) lililofanyika leo Sept,08,2021 katika Viwanja vya Redcross Kisesa Magu, Mkoani Mwanza.

Tuesday, September 7, 2021

IBADA MAALUM KUFANYIKA KUWAENZI HAYATI BABA WA TAIFA MWL. NYERERE, BENJAMIN MKAPA NA DKT. JOHN POMBE MAGUFULI

Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Uratibu, Bunge, Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu) Mhe. Jenista Mhagama pamoja na Mkuu wa Mkoa wa Geita Mhe. Rosemary Senyamule .wakisaliana na Askofu wa Jimbo Katoliki Geita Mhashamu Flavian Kassala mara baada ya kuwasili katika ofisi za kanisa hilo Septemba 04,2021 kwa lengo la kuteta kuhusu maandalizi ya Kelele cha Mbio Maalum za Mwenge wa Uhuru kwa mwaka huu.
 

Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia masuala ya Sera, Uratibu, Bunge, Kazi, Vijana, Ajira na wenye Ulemavu Mhe. Jenista Mhagama ameleza uwepo wa ibada na sala maalum ya kuwaombea hayati Baba ya Taifa Mwl. Julius Kambarage Nyerere, Rais wa Awamu ya Tatu, Benjamin William Mkapa na aliyekuwa Rais wa Awamu ya Tano Dkt. John Pombe Magufuli ikiwa ni sehemu ya kuwaenzi tunapoelekea kuhitimisha Mbio Maalum za Mwenge wa Uhuru kwa Mwaka 2021.

 

Amesema hayo wakati wa ziara yake ya kikazi mwishoni mwa wiki alipoongozana na Waziri wa Nishati Dkt. Medard Kalemani kwa lengo la kukagua maandalizi ya kilele cha mbio hizo zitakazo hitimishwa katika Wilaya ya Chato Mkoani Geita tarehe 14 Oktoba, 2021.

 


Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Uratibu, Bunge, Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu) Mhe. Jenista Mhagama akizungumza wakati wa kikao na Askofu wa Jimbo Katoliki Geita Mhashamu Flavian Kassala katika ofisi zake Mkoani Geita.

 

Waziri Mhagama ameeleza umuhimu wa ibada hiyo, kwa kuzingatia michango ya viongozi hao katika Taifa na kusema ni sehemu ya kuwaenzi na kuonesha heshima kwa namna walivyolitumikia Taifa.

 

Aliongezea kuwa, Kanisa kwa kushirikiana na kamati ya maandalizi wana jukumu la kuiandaa ibada hiyo ya kipekee kulingana na heshima kubwa ya viongozi hao katika Taifa na kuonesha tunatambua michango yao kwa matendo.

 

“Ninatambua mchango wa kanisa katika nchi yetu, nikushukuru baba  Askofu Flaviana kwa kuonesha  uzalendo na utayari wa kuandaa ibada hii muhimu, nitoe rai muendelee kuiombea siku hiyo na Taifa kwa ujumla  ili kudumu katika Amani na Mshikano,”Mhe. Mhagama

 

Aliongezea kuwa, tukio hili ni muhimu kwa kuzingatia mbio za Mwenge kwa mwaka huu zimekua ni maalum kwani ni mara ya kwanza kuhitimishwa mbele ya Rais wa kwanza mwanamke nchini hivyo ni tukio la kihistoria.

 

“Mbio hizi ni maalum kwa kuzingatia maeneo muhimu matatu ikiwemo; Taifa kuondokewa na Rais wa Awamu ya Tano akiwa  madarakani, Taifa kuongozwa na Rais mwanamke wa kwanza na kuupa heshima mkoa wa Geita kuzingatia ni mkoa aliozaliwa na kuzikwa Rais wa Awamu ya Tano hayati Dkt. Johh Pombe Magufuli,” alisisistiza  Waziri Mhagama.

 

Kwa upande wake Mkuu wa Mkoa wa Geita Mhe. Rosemary Senyamule alieleza Mkoa umejipanga kuhakikisha sherehe za Mbio za Mwenge zinafana na kuzingatia wamebakiza siku chache na kuahidi kuendelea kushirikirikiana na Ofisi ya Waziri Mkuu pamoja na wadau wote katika kuifikia siku hiyo.

 

 “Mkoa utaendelea kufanya maandalizi muhimu katika ubora unaoendana na hadhi ya Mkoa wa Geita na kuzingatia heshima tuliyopewa na Serikali yetu ya Awamu ya Sita,"alisema Rosemary

 

Naye Waziri wa Nishati Dkt.Medarn Kalemani alimshukuru Waziri Mhagama kutenga muda kutembelea na kukagua maendeleo ya maandalizi ya sherehe za kilele cha Mbio hizo na kuendelea kuwaasa wananchi wa Chato kuonesha ushirikiano wao kwa Serikali ili kufanikisha tukio hilo.

 

 Akitoa neno la shukran Askofu wa Jimbo Katoliki Geita Mhashamu Flavian Kassala amesema wataendelea kuliombea Taifa na kuhubiri upendo, amani na mshikamano ili kuendelea kuwa na Taifa lenye utulivu.

 

 “Sisi viongozi wa dini tunaungana nanyi kuifanikisha siku hiyo katika kujiandaa na ibada hiyo maalum na nitaliwasilisha katika baraza kulinga na uzito wake”Alieleza Askofu Kassala

RC SINGIDA AKAGUA MIRADI YA MAJI AWATAKA SUWASA KUONGEZA KASI YA UKUSANYAJI MAPATO


Mkurugenzi Mtendaji Maji Safi na Mazingira  (SUWASA) Mkoa wa Singida Mhandisi Patrick Nzamba (kushoto) akimuonesha Mkuu wa Mkoa Singida Dkt. Binilith Mahenge tenki la kuchanganyia 'chlorine powder' ambayo hutumika kutibu maji endapo umeme unakuwa umekatika. Kawaida SUWASA hutibu Maji kwa kutumia gesi ya klorini.
Ukaguzi wa miradi ya maji ukiendelea.
Mkuu wa mkoa alipata maelezo kutoka kwa Mkurugenzi Mtendaji SUWASA Mhandisi Patrick Nzamba.
Wageni walioambatana na Mkuu wa mkoa walipotembelea chanzo cha maji Mwankoko katika kituo cha kusukuma maji.
Mkuu wa mkoa pamoja na msafara wake wakielekea visimani Mwankoko.
Tanki la juu la Mandewa lenye lita 500,000 linalopokea maji kutoka chanzo cha maji Mwankoko. Pembeni ni tenki la chini lenye ujazo wa Lita milioni 2.5
Tenki la Somoku linavyoonekana na mradi wake umefikia 90%. Mradi huo una gharama ya milioni 755 ambapo kuna shughuli mbalimbali ikiwemo ujenzi wa tenki hilo, kulaza mtandao 13km kuunganisha wateja 500 na manunuzi ya pampu.

 
Na Mwandishi Wetu, Singida

Mamlaka  ya Maji Safi na Mazingira Mkoa wa Singida (SUWASA) wametakiwa kutumia mbinu mbadala kuongeza ukusanyaji wa mapato ili waweze kuendeleza miundombinu na kupunguza upotevu wa maji.

Hayo yamesemwa na Mkuu wa Mkoa wa Singida Dkt. Binilith Mahenge wakati akizungumza na watumishi wa  SUWASA  baada ya kutembelea miradi mbalimbali ya maji iliyojengwa na mamlaka hiyo.

 "Ukusanyaji wa mapato ukisimamiwa vizuri utasaidia kuongeza mapato na kukarabati miundombinu na usambazaji wa maji maeneo mengi zaidi kwa kutumia fedha za ndani,". alisema Mahenge.

Aidha Dkt. Mahenge amebainisha kwamba kiasi cha maji yanayopotea kwa Mkoa wa Singida ni asilimia 33.4 ambayo ni kiasi kikubwa kikilinganishwa na asilimia 22 ya upotevu inayokubalika hivyo kuwataka SUWASA kuhakikisha upotevu unapungua.

Hata hivyo Dkt. Mahenge ameipongeza SUWASA kwa kuanzisha miradi mingi ya maji ambayo imejengwa kwa kutumia fedha za ndani na kwa viwango vinavyokubalika .

RC ameishukuru serikali kwa kutoa fedha zaidi ya shilingi bilioni 3.07 ili kutekeleza miradi ya maji iliyopo Manispaa ya Singida, Wilaya ya Iramba na Ikungi Nawapongeza sana kwa kazi nzuri milofanya Miradi mingi iliyojengwa ina viwango vinavyokubalika kwa fedha za ndani hii inaonesha ubunifu mkubwa mliutumia katika kutekeleza miradi hii, niwaombe muendelee kusimamia vizuri makusanyo ili muweze kuanzisha miradi mingine, alisema Dkt. Mahenge.

Aidha ametoa wito kwa wananchi wote mkoani hapo wanaotumia huduma ya maji kuhakikisha wanalipia huduma hiyo kwa wakati ili kusaidia Mamalaka kuendelea kusambaza huduma kwa watu wengine .

Naomba muandae orodha ya Taasisi na watu wote wanao daiwa nizipate ofsini kwangu,
lazima mtu aliyepatiwa huduma ya maji na akayatumia alipe, nitoe wito kwa yeyote
anayejua kwamba ana deni la maji alipe kabla orodha hiyo haijanifikia, alisisitiza 
Mahenge.

RC Mahenge amewakumbusha watumishi wa SUWASA kuhakikisha kwamba hakuna udanganyifu unaofanyika katika usomaji wa mita na kuacha ukadiriaji kwa mteja.
Akimalizia hotuba yake Dkt. Mahenge amewaagiza watumishi kufanya ukaguzi wa kawaida utakaobaini ubora wa maji katika visima binafsi vinatoa huduma kwa wananchi na kuyapima ili kulinda afya za watu.

Mkurungenzi Mtendaji wa Mamlaka ya Maji safi na mazingira Mkoani Singida (SUWASA) Mhandisi Patrick Nzamba amesema mkoani hapo wametekeleza jumla ya miradi ya maji saba 7 inayogharimu kiasi cha shilingi bilioni 3.075 katika Kata za Unyambwa, Minga, Mungu maji na Vijiji vya Misigiri na Ulemo.

Aidha amebinisha kwamba Mamlaka ina mpango wa kuongeza uzalishaji wa maji kwa
kuchimba visima 11 kupitia fedha za miradi 28 ya maji lengo likiwa ni kuhakikisha wananchi wengi wanapata maji.

Mhandisi Patrick amefafanua kwamba SUWASA kwa kushirikiana na RUWASA watakarabati miradi nane (8) pembezoni mwa mji katika maeneo ya Unyamikumbi A, Mtamaa B,  Manga, Ititi, Uhamaka,Unyianga Mtamaa A na Mwankoko A ambayo kwa sasa haitoi huduma  ya maji.

Ameendelea kusema kwamba wameweka mkakati wa kuhakikisha wanaongeza mtandao wa maji kwa kusambaza mabomba yenye urefu wa zaidi ya Kilometa 10 katika maeno ambayo hayana huduma hiyo.

Hata hivyo ameongeza kwamba changamoto kubwa katika utoaji wa huduma ya maji ni uhaba wa mitandao ya majitaka ambayo huathiri mazingira na tayari mipango ya uanzishwaji wa mradi huo umekamilika.

Changamoto chingine ni kupungua kwa uwezo wa visima kuzalisha maji na vingine kuwa na maji chumvi pamoja na uwepo wa mtandao wa mabomba ya zamani wenye urefu wa kilometa 40 ambayo husababisha upotevu wa maji. Alisema Mhandisi Patrick.

Aidha Mhandisi Patrick amemueleza RC kwamba baadhi ya wateja wamekuwa kikwazo kwa kuwa hawalipi madeni yao kulingana na huduma ya maji wanayoipata hivyo kusababisha deni la shilingi milioni 581.32 ambapo taasisi za Serikali pekee zinadaiwa kiasi cha shilingi milioni 305.