Matokeo chanyA+ online




Wednesday, February 15, 2023

SERIKALI YAWATAKA WATAALAMU NA WADAU WA MAZINGIRA KUIBUA MIRADI YA MAZINGIRA

Mkurugenzi wa Mazingira Ofisi ya Makamu wa Rais Dkt. Andrew Komba kwa niaba ya .. akifunga Warsha ya siku mbili ya Wadau na Wataalamu wa Mazingira iliyolenga kuainisha vipaumbele vya miradi ya mazingira na mabadiliko ya tabianchi inayosimamiwa na Mfuko wa Mazingira wa Dunia (GEF) na kufanyika jijini Dodoma Februari 13 hadi 14, 2023.




Mratibu wa Mfuko wa Mazingira wa Dunia (GEF) – Kanda ya Afrika Dkt. Ibrahima Sow akitoa neno wakati wa kufunga Warsha ya siku mbili ya Wadau na Wataalamu wa Mazingira iliyolenga kuainisha vipaumbele vya miradi ya mazingira na mabadiliko ya tabianchi inayosimamiwa na GEF na kufanyika jijini Dodoma Februari 13 hadi 14, 2023.


Washiriki mbalimbali wakiwa katika Warsha ya siku mbili ya Wadau na Wataalamu wa Mazingira iliyolenga kuainisha vipaumbele vya miradi ya mazingira na mabadiliko ya tabianchi inayosimamiwa na GEF na kufanyika jijini Dodoma Februari 13 hadi 14, 2023.





 Serikali imewataka wataalamu na wadau wa mazingira nchini kutumia vyema fursa za mafunzo yanayotolewa na wadau wa maendeleo ili kuibua ajenda na vipaumbele muhimu vya miradi ya mazingira na mabadiliko ya tabianchi.

Hayo yamesemwa Februari 14, 2023 na Katibu Mkuu Ofisi ya Makamu wa Rais, Bi. Mary Maganga wakati wa hotuba yake ya kufunga Warsha ya siku mbili ya Warsha ya siku mbili ya Wadau na Wataalamu wa Mazingira inayolenga kuainisha vipaumbele vya miradi ya mazingira na mabadiliko ya tabianchi inayosimamiwa na Mazingira wa Dunia (GEF).na kusomwa na Mkurugenzi wa Idara ya Mazingira, Dkt. Andrew Komba.

Bi. Maganga amesema Serikali kupitia Ofisi ya Makamu wa Rais kwa kushirikiana na GEF imeandaa warsha hiyo kwa ajili ya kuwakutanisha wataalamu na wadau wa mazingira ikiwa ni sehemu ya maandalizi ya utekelezaji wa miradi ya GEF mzunguko wa nane ambao unatarajia kutekelezwa katika kipindi cha miaka minne ijayo.

“Warsha hii ilikuwa na malengo makuu mawili ambayo ni kuanisha vipengele vya miradi ya GEF mzunguko wa nane na pia kupeana ujuzi na maarifa ya pamoja katika namna ya kukabiliana na athari za mazingira na mabadiliko ya tabia nchi” amesema Bi. Maganga.

Akifafanua zaidi Bi. Maganga amesema Serikali kwa kushirikiana na wadau wa maendeleo imekuwa ikiendesha mafunzo na warsha mbalimbali ili kuhakikisha kuwa wataalamu na wadau wa mazingira wanaongeza ujuzi na maarifa katika usimamizi wa miradi ya uhifadhi na usimamizi wa mazingira inayofadhiliwa na wadau wa maendeleo.

Aidha Bi. Maganga amewahakikishia wadau wa maendeleo ikiwemo GEF kuwa Serikali kupitia Ofisi ya Makamu wa Rais itaendelea kusimamia vyema miradi yote ya kimkakati inayoendelea kutekelezwa katika maeneo mbalimbali nchini ili kuhakikisha kuwa malengo ya miradi yanafikiwa kwa wakati.

Kwa upande wake Mratibu wa Mfuko wa GEF Kanda ya Afrika, Ibrahima Sow amewashukuru wadau na wataalamu wa mazingira walioshiriki warsha hiyo kwa kuwasilisha na kutoa maoni na mapendekezo yatakayoisaidia utekelezaji wa miradi ya GEF- mzunguko wa nane.

Warsha hii imetusaidia kuona utayari wa wataalamu na wadau wa mazingira na Serikali kwa ujumla katika namna ya kuanza utekelezaji miradi ya uhifadhi wa mazingira na mabadiliko ya tabia nchi awamu ya nane. Tutaendelea kushirikiana katika kuhakikisha malengo ya miradi hii inafikiwa” amesema Sow.

Maeneo matatu ya utekelezaji wa mradi wa GEF- mzunguko wa nane itajielekeza katika mradi wa usimamizi katika Maziwa Makuu na Mabonde ya Maji, fedha za kujenga uwezo kwa wataalamu wa miradi pamoja na usimamizi wa miradi katika nchi zinazoendelea. 

Aidha Warsha hiyo ilihudhuriwa na wataalamu wa uhifadhi na usimamizi wa mazingira kutoka Tanzania Bara na Zanzibar wakiwemo maafisa wa Serikali, Taasisi, Idara na Wakala wa Serikali na Taasisi binafsi.

Wadau wengine ni Shirika la Chakula na Kilimo la Umoja wa Mataifa (FAO), Shirika la Mazingira Duniani (UNDP), Benki ya Dunia (WB), Shirika la Uhifadhi wa Mazingira (WWF), Benki ya Maendeleo ya Afrika (AfDB), IFAD na IUCN. 

Tuesday, February 14, 2023

Konyagi Fusion Mpya imezinduliwa na Kampuni ya Tanzania Distilleries Limited


Meneja wa Chapa ya Konyagi Fusion, Pamela Kikuli

Mkurugenzi Mtendaji wa TDL, Timea Chogo






Na Mwandishi Wetu.

KAMPUNI ya Tanzania Distilleries Limited, ambao ni waanzilishi wa kinywaji cha Konyagi, imezindua aina mbili mpya za Konyagi ikiwa ni mwendelezo wa chapa hiyo zinazoitwa Konyagi Fusion. Konyagi Fusion zimekuja katika ladha mbili tofauti ikiwemo Konyagi Fusion ya ladha ya Tangawizi & Limao na Konyagi Fusion yenye Ladha ya Nazi. Uzinduzi ulianza katika ubao wa matangazo ambao ulikuwa n bomba la kutoa vinywaji hivyo kwa bure kabisa katika maeneo ya Coco Beach. Konyagi tayari imeshajulikana kwani ilianzishwa zaidi ya miaka 40 iliyopita na imekuwa moja ya kinywaji pendwa kwa wengi. 

Meneja wa Chapa ya Konyagi Fusion, Pamela Kikuli, anasema: “Tunayo furaha kutangaza kuwa leo tunazindua kinywaji kipya cha Konyagi. Kama mnavyojua Konyagi imekuwa na historia kubwa tangu ilipoanzishwa miaka ya 1968. Kwa sasa tumeleta Konyagi zenye ladha mbili tofauti kwa ajili ya vijana wa kisasa ambazo ni Konyagi ya Tangawizi na Limao, na nyingine ina ladha ya Nazi.

Aliongeza: “Tunataka wateja wetu wapate ladha tofauti na waliyoizoea. Konyagi Fusion ina asilimia 20% ya kilevi na kupatikana katika ujazo wa mililita 250. 
Mkurugenzi Mtendaji wa TDL, Timea Chogo, anaongeza “Wakati Tunafanya Uchunguzi, tuligundua kuwa mojawapo ya mitindo ya kimataifa ya vinywaji vya spirit ni kutumia ladha mbalimbali katika pombe kali. Na hivyo tukaamua kutumia kinywaji chetu cha kizalendo kutengeneza Kinywaji kipya kinachofuata mitindo ya Kimataifa. Konyagi Fusion zinatumia Ladha za kusisimua na pia kuburushisha zinazjulikana kama Konyagi Fusion, Ginger and Lemon and Konyagi Fusion, Coconut. Tuna imani kubwa wateja wetu watazipenda Ladha hizi mpya”. 

Konyagi Fusion rasmi itazinduliwa Februari 17, 2023 katika Ukumbi wa Tipsy Coco, Dar es Salaam. Tunatarajia wateja wetu watapata fursa ya kuburika zaidi kwani kwa mara ya kwanza zitaanza kupatikana chupa za milimita 250 kwa sh. 5,000 na zitakuwa zinapatikana katika maeneo yote Tanzania.

Balozi wa Denmark aipongeza Benki ya CRDB kwa Matokeo Mazuri ya Fedha

Balozi wa Denmark nchini, Mette Nørgaard Dissing-Spandet (wapili kushoto) katika picha ya pamoja na Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi Benki ya CRDB, Dkt. Ally Laay (wakwanza kushoto), Makamu Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi Benki ya CRDB, Prof. Neema Mori, na Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya CRDB, Abdulmajid Nsekela wakati walipomtembelea ofisini kwake kujadili uwekezaji wa DANIDA ndani ya benki hiyo na Mkakati mpya wa Miaka Mitano wa Biashara wa Benki ya CRDB wa 2023/2028.


Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya CRDB, Abdulmajid Nsekela (wakwanza kulia) akimwelezea Balozi wa Denmark nchini, Mette Nørgaard Dissing-Spandet (wapili kushoto) juu ya Mkakati mpya wa Miaka Mitano wa Biashara wa Benki ya CRDB wa 2023/2028 wakati ujumbe wa Benki hiyo ulipotembelea katika Ubalozi wa Denmark kujadili mafanikio ya uwekezaji wa DANIDA ndani ya benki hiyo. Ujumbe huo uliongozwa na Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi Benki ya CRDB, Dkt. Ally Laay (wapili kushoto), pamoja na Makamu Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi Benki ya CRDB, Prof. Neema Mori (hayupo pichani), Mkurugenzi wa Mawasiliano wa Benki ya CRDB, Tully Mwambapa (watatu kushoto), na Katibu wa Kampuni Benki ya CRDB, John Rugambo.



Na Mwandishi Wetu

Uongozi wa Benki ya CRDB kupitia Mkurugenzi Mtendaji wake, Abdulmajid Nsekela umekutana na Balozi wa Denmark nchini, Mh. Mette Nørgaard Dissing-Spandet kujadili uhusiano baina ya Shirika la Kimataifa la Maendeleo la Denmark (DANIDA) na benki hiyo.

Hakuna wakati mzuri wa kujadili uhusiano huo wa kihistoria kama kipindi hiki ambacho benki hiyo kinara wa utoaji huduma za kifedha nchini, imetoka kupata faida kubwa kwa mwaka uliopita.

Ikiivunja rekodi yake yenyewe iliyoiweka kwa mwaka 2021 ya faida baada ya kodi ya takriban Sh268 bilioni na kufikia faida ya Sh353 bilioni kwa mwaka 2022.

Mafanikio hayo yanaelezwa kutokana na jitihada za makusudi za benki hiyo kukuza vyanzo vya mapato yasiyotokana na riba ambapo yaliongezeka kwa asilimia 13 mwaka hadi mwaka na kufikia kiasi cha Sh400 bilioni kutoka Sh354 bilioni.

Nsekela, akifafanua rekodi hiyo, alisema imechagiwa na ongezeko la ufanyaji miamala ya fedha hususan kupitia njia za kidijitali.

Kiujumla, wanahisa wa benki hii, DANIDA akiwa mmojawapo akishirikiana na Serikali ya Tanzania, wanaendelea kuona fahari ya kuwa sehemu ya uwekezaji wa benki inayofanya vizuri kwa kuwa wana uhakika gawio lao litaongezeka maradufu.

Balozi Dissing-Spandet akizungumza na viongozi wa Benki ya CRDB alisema amefurahishwa na matokeo mazuri ya Benki ya CRDB kwa 2022 na ni kiashiria kizuri kwa matokeo yajayo.

Historia ya DANIDA na Benki ya CRDB

Uhusiano wa DANIDA na Benki ya CRDB haujaanza leo, mizizi yake ilipandwa kupitia uhusiano wa kidiplomasia baina ya Tanzania na Denmark.

Tanzania imekuwa mnufaika wa misaada ya kimaendeleo kutoka kwa Denmark kupitia DANIDA kwa miongo kadhaa iliyopita ikitekeleza miradi ya afya, uchumi, utafiti, ujasiriamali nk.

Wakati Benki ya CRDB ikijulikana kama Cooperative Rural Development Bank, ilipitia nyakati ngumu kiasi cha kushindwa kujiendesha hatua iliyopelekea Serikali kuiomba DANIDA kupitia wake Mfuko wa Uwekezaji wa Denmark (DIF) kuinasua benki hiyo.

Kuingia kwa DIF kama mwekezaji kuliweza kuleta mageuzi katika benki hiyo ambayo ilipelekea kuzaliwa upya kama Benki ya CRDB. Miaka kadhaa baadaye Benki ya CRDB ilifikia hadhi yakuweza kuorodheshwa katika Soko la Hisa la Dar es Salaam (DSE).

Uwekezaji wa hisa na urudishaji kwa jamii

DIF ilianza kwa kuwekeza hisa 247,014 mwaka 2002 ambazo zimeongezeka na kufikia hisa 548,067,648 mwaka 2021 ambazo ni sawa na asilimia 21 ya hisa zote za Benki ya CRDB.

Katika upande wa gawio, DIF na Serikali ya Tanzania, zilipata kiasi cha Sh247 milioni mwaka 2002 na Sh19.7 bilioni mwaka 2021.

Uhusiano huu wa aina yake baina ya DANIDA, Serikali na Benki ya CRDB umekuwa na maana kubwa katika kuifanya benki hii kuendelea kufanya vyema kila mwaka na kupata faida katika biashara yake.

Serikali ya Denmark imeendeleza ushirikiano wake na Benki ya CRDB na sasa imewekeza kupitia Mfuko wake wa Uwekezaji unaoitwa Investment Fund for Developing Countries (IFU), kwenye Kampuni tanzu ya CRDB Bank nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo.

Kwa kuwa DANIDA ni mdau wa maendeleo nchini, inaelezwa kuwa Denmark ilikuwa miongoni mwa waasisi wa Fedha za Mfuko wa Afya wa Pamoja (HBF) mwaka 1999 na imekuwa ikiendelea kuchangia katika mfuko huo. Kwa mwaka huo pekee, ilichangia kiasi cha DKK 60 milioni.

Kupitia mchango wake katika fedha za mifuko ya afya ya pamoja kwa bara na visiwani, Danida imekuwa ikitumia fedha zake za uwekezaji kusaidia kuboresha mifumo ya afya, ubora wa huduma za afya, huduma za afya ya uzazi kwa wanawake na wasichana.

Kwa mantiki hiyo, ili DIF inayoshirikiana na Serikali, iweze kuendelea kusaidia upatikanaji wa huduma za afya katika jamii zenye uhitaji mkubwa inalazimika kutenga kiasi cha gawio litokanalo na faida ya uwekezaji wake kila mwaka kwa Benki ya CRDB kufanikisha jitihada hizo.

Kwa kuwa mfuko huo na mingine bado inategemea michango kutoka kwa wadau wa maendeleo, Benki ya CRDB inabaki kuwa tegemeo la wadau wengi ambao wanachangia katika mfuko huo kupitia gawio inaloligawa kila mwaka baada ya kuwekeza hisa zao.

Ni sahihi kusema kuwa benki hiyo imekuwa ikisaidia moja kwa moja katika HBF kupitia wanahisa wake wanaopata gawio kila mwaka, kwa mantiki hiyo, ina dhima kubwa ya kuendelea kuhakikisha inakuja na mikakati bora ya kuiwezesha benki kufanya vizuri kwa mwaka huu na inayofuata na wanahisa wake kuchangia zaidi.

Kwa mwaka wa fedha 2022/23, Waziri wa Afya, Ummy Mwalimu alisema kuwa wadau wa HBF walikubaliana kuchangia kiasi cha Sh98.1 bilioni kwa ajili ya kuboresha utoaji wa huduma za afya nchini.

“Fedha zinazoingizwa nchini kwa ajili ya kusaidia shughuli mbalimbali za afya tunapenda ziingizwe kwenye Mfuko wa Afya wa pamoja ili tuweke kushirikiana kufanya kazi pamoja na kupata matokea ya haraka kwa pamoja. Mapendekezo yetu wadau wengine wachangia kupitia mfuko huo kwani tumeona mafanikio makubwa" amefafanua Waziri Ummy Mwalimu.

Aidha Waziri Ummy Mwalimu amesema upo umuhimu kwa wadau wa maendeleo kuchanga fedha kwa pamoja na kuweka kwenye Mfuko wa Afya wa pamoja na kusema kuwa kufanya hivyo ni kuzingatia Mifumo na taratibu za Serikali za kutoa fedha kwa ajili ya Huduma za Afya nchini pamoja na kuwekeza fedha kwenye maeneo ya vipaumbele vya Serikali.

Monday, February 13, 2023

WAKULIMA RUVUMA WAINGIZA BILIONI 644 BAADA YA KUUZA KAHAWA NA KOROSHO

Shehana ya kahawa iliyokobolewa na nyingine ikiendelea kukobolewa katika kiwanda cha kukoboa kahawa cha DAE LTD mjini Mbinga



Katikati mwenye tabasamu ni Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma Kanali Laban Thomas alipotembelea na kukagua kiwanda cha kukoboa Kahawa cha DAE LTD mjini Mbinga

Wakulima Ruvuma waingiza bilioni 644 kwa kahawa na korosho

Wakulima mkoani  Ruvuma waingiza zaidi ya shilingi bilioni 644 baada  kuuza mazao ya kahawa na korosho kwenye  misimu mitano mfululizo.

Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma Kanali Laban Thomas amesema Mkoa wa Ruvuma kwa vipindi vya misimu ya kilimo mitano mfululizo kutoka msimu wa kilimo 2017/2018  hadi kufikia msimu 2020/2021 jumla ya kilo 77,664,927.75 za kahawazilikusanywa.

Amesema kilo hizo  ziliuzwa kwa watani wa bei sh. 4,638 na kuwapatia wakulima  wa kahawa zaidi ya shilingi bilioni  353.

Amebainisha kuwa kati ya fedha hizo,msimu wa mwaka 2016/2017  zilinunuliwa kilo  15,393.500 zilizowaingizia wakulima zaidi ya shilingi bilioni 66 na kwamba msimu wa 2017/2018 zilinunuliwa kilo 20,162,900 na kuwaingizia  wakulima zaidi ya shilingi bilioni 74.

Kwa mujibu wa Kanali Thomas katika msimu wa mwaka 2018/2019 zilinunuliwa kilo 15,675,100 zilizowaingiza  wakulima zaidi ya shilingi bilioni 64,msimu wa mwaka 2019/2022 zilinunuliwa kilo 12,676,844 zilizowaingiza wakulima zaidi ya shilingi bilioni 50  na kwamba mwaka 2020/2021  zilinunuliwa kilo 15,756,583.75 na kuwaingiza  wakulima zaidi ya shilingi bilioni 97. 

 

TANZANIA KUNUFAIKA NA BILIONI 120/- KUTOKA GEF KULINDA MAZINGIRA

Katibu Mkuu Ofisi ya Makamu wa Rais Bi. Mary Maganga akifungua Warsha ya siku mbili ya Wadau na Wataalamu wa Mazingira inayolenga kuainisha vipaumbele vya miradi ya mazingira na mabadiliko ya tabianchi inayosimamiwa na GEF jijini Dodoma  Februari 13, 2023.


Wadau na Wataalamu wa Mazingira wakiwa katika Warsha inayolenga kuainisha vipaumbele vya miradi ya mazingira na mabadiliko ya tabianchi inayosimamiwa na GEF jijini Dodoma Februari 13, 2023.




Katibu Mkuu Ofisi ya Makamu wa Rais Bi. Mary Maganga (kulia) akiteta Mwakilishi wa Shirika la Mazingira la Umoja wa Mataifa (UNEP) anayeshughulikia Mfuko wa GEF, Bi. Christine Haffner-Sifakis (kushoto) wakati kifungua Warsha ya siku mbili ya Wadau na Wataalamu wa Mazingira inayolenga kuainisha vipaumbele vya miradi ya mazingira na mabadiliko ya tabianchi inayosimamiwa na GEF jijini Dodoma leo Februari 13, 2023. Katikati ni Naibu Katibu Mkuu Ofisi ya Makamu wa Rais (Mazingira) Dkt. Switbert Mkama
Mgeni rasmi Katibu Mkuu Ofisi ya Makamu wa Rais Bi. Mary Maganga (waliokaa katikati) akiwa katika picha ya pamoja na wadau mbalimbali walioshiriki Warsha ya Warsha ya siku mbili ya Wadau na Wataalamu wa Mazingira inayolenga kuainisha vipaumbele vya miradi ya mazingira na mabadiliko ya tabianchi inayosimamiwa na GEF jijini Dodoma leo Februari 13, 2023.

TANZANIA KUNUFAIKA NA BILIONI 120/- KUTOKA GEF

 

Tanzania inatarajia kunufaika na mradi wenye thamani ya Shilingi 120 Bilioni kwa ajili ya miradi ya uhifadhi wa mazingira na mabadiliko ya tabianchi kutoka Mfuko wa Mazingira wa Dunia (GEF).

 

Hayo yamesemwa leo Jumatatu (Februari 13, 2023) Jijini Dodoma na Katibu Mkuu Ofisi ya Makamu wa Rais Bi. Mary Maganga wakati akifungua Warsha ya siku mbili ya Wadau na Wataalamu wa Mazingira inayolenga kuainisha vipaumbele vya miradi ya mazingira na mabadiliko ya tabianchi inayosimamiwa na GEF.

 

Bi. Maganga amewashukuru washirika hao wa maendeleo kwa kuandaa mpango huo wa utoaji wa fedha hizo ambazo hadi sasa tayari zimekwishatolewa katika amwamu na kusema kuwa zitasaidia katika juhudi za kuimarisha uhifadhi na usimamizi wa mazingira nchini.

 

Aidha Bi. Maganga amewataka wadau na wataalamu hao kutumia vyema ujuzi na uzoefu walionao katika kuimarisha mapambano na changamoto za mazingira zilizopo kwa lengo la kuhakikisha maandalizi na utekelezaji wa miradi chini ya GEF- awamu ya  nane inatekelezwa kwa wakati.

 

“Tanzania ni nchi mnufaika wa miradi ya GEF ambayo inafadhiliwa kupitia mikataba mbalimbali ya kimataifa, hivyo Ofisi ya Makamu wa Rais imeona umuhimu wa kuita wadau na wataalamu kutoka wizara na taasisi za kisekta kutoka mashirika mbalimbali ili kuweka mikakati ya pamoja na kufanikisha ajenda ya mazingira,” alisema.

 

Aidha, Katibu Mkuu Maganga ametoa wito kwa wataalamu hao kuhakikisha wanafanya maandalizi ya haraka ya kuainisha maeneo ya kipaumbele ya miradi ya washirika wa maendeleo ili kuanza katika uliowekwa na kuikamilisha kwa wakati.

 

Kwa upande wake Mratibu wa GEF – Kanda ya Afrika Bw. Ibrahima Sow alisema kuwa Tanzania imetengewa mgao huo wa fedha za mzungumzo wa nane katika maeneo matatu ya mradi kwa kipindi cha miaka minne ijayo.

 

Alitaja maeneo hayo kuwa ni mradi wa usimamizi katika Maziwa Makuu na Mabonde ya Maji, fedha za kujenga uwezo kwa wataalamu wa miradi pamoja na usimamizi wa miradi katika nchi zinazoendelea. 

 

Naye Mkurugenzi wa Mazingira Ofisi ya Makamu wa Rais Dkt. Andrew Komba alisema kuwa katika eneo la kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabianchi, Serikali imeendelea kushirikiana na wadau mbalimbali na kuhimiza na kuhamasisha utunzaji wa mazingira.

 

Alisema kuwa mabadiliko ya tabianchi ni miongoni mwa matokeo ya kuongezeka kwa gesijoto duniani sambamba na uharibifu wa uoto asili na bioanuai, hivyo Serikali imeanzisha kampeni za upandaji miti ili kuhakikisha nchi inakabiliana na athari hizo.

 

Naye Mwenyekiti wa Jukwaa la Wadau wa Mazingira Nchini Bw. Tumaini Marijani aliipongeza Serikali kwa namna inavyoratibu masuala ya uhifadhi na usimamizi wa mazingira nchini.

 

Tumaini, pamoja na kuhamisha wadau wakiwemo taasisi binafsi kushiriki shughuli za mazingira,  pia aliwataka watalaamu na wadau hao kushiriki zoezi la upandaji wa miti ili kuunga mkono juhudi za Serikali katika uhifadhi na usimamizi wa mazingira.

  

Warsha hiyo inatoa fursa kwa Tanzania na wadau wa ndani na nje ya nchi kujadili na kupeana uzoefu katika mafanikio na namna ya kutatua changamoto zilizopo na zinazoweza kutokea katika miradi iliyopita na inayoendelea kutekelezwa.

 

Sunday, February 12, 2023

WAZIRI CHANA : SERIKALI IMEWEKA MAZINGIRA WEZESHI KWA WAWEKEZAJI SEKTA YA UTALII

Waziri  wa Maliasili na Utalii, Balozi Dkt.Pindi Chana akizungumza  na  Chama cha Mawakala wa usafiri wa anga Tanzania (TASOTA) kwenye mkutano wao wa mwaka ambapo amewapongeza kwa kuwa wazalendo wa kuilinda na kutetea nchi kwa watalii wanaoitembelea Tanzania

Waziri  wa Maliasili na Utalii, Balozi Dkt.Pindi Chana akiwa na Mwenyekiti wa Chama cha Mawakala wa usafiri wa anga Tanzania (TASOTA) 
Moustafa Khataw ( wa kwanza kulia ) wakiwa kwenye mkutano wao wa kila  mwaka wakifuatilia burudani  Jijini Dar es Salaam


Waziri  wa Maliasili na Utalii, Balozi Dkt.Pindi Chana akiwa ameongozana  Mwenyekiti wa Chama cha Mawakala wa usafiri wa anga Tanzania (TASOTA) 
Moustafa Khataw ( wa kwanza kushoto) akiwa pamoja na Mkurugenzi Mkuu wa Bodi ya Utalii Tanzania ( TTB) Damas Mfugale mara baada ya kuwasili kaatika mkutano wa mwaka wa TASOTA uliofanyika jana usiku


Waziri  wa Maliasili na Utalii, Balozi Dkt.Pindi Chana akikabidhiwa tuzo iliyotolewa na na Mwenyekiti wa Chama cha Mawakala wa usafiri wa anga Tanzania (TASOTA) Moustafa Khataw ikiwa ni kutambua mchango wake katika wa kuhakikisha Wanachama wa TASOTA wanafanya kazi zao katika mazingira wezeshi ikiwemo kero zao kutatuliwa kwa wakati

Waziri  wa Maliasili na Utalii, Balozi Dkt.Pindi Chana akiwa kwenye picha ya pamoja na Wajumbe wa Bodi wa Chama cha Mawakala wa usafiri wa anga Tanzania (TASOTA) katika mkutano wa mwaka wa Chama hicho uliofanyika jana usiku Jijini Dar es Salaam

Baadi ya Wanachama wa  Chama cha Mawakala wa usafiri wa anga Tanzania (TASOTA) pamoja na wageni waalikwa wakimsikiliza Waziri  wa Maliasili na Utalii, Balozi Dkt.Pindi Chana ambapo amekipogeza Chama hicho kwa kazi kubwa inayofanya ya kutangaza vivutio vya utalii kwa watalii wanaokuja kuangalia vivutio vyetu

Mwenyekiti wa TASOTA, Moustafa Khataw akizungumza kabla hajamkaribisha Waziri wa Maliasili na Utalii,Balozi Dkt.Pindi Chana ambapo  ameishukuru Serikali kwa kutambua mchango wao wa kutangaza uzuri wa Tanzania







 Waziri  wa Maliasili na Utalii, Balozi Dkt.Pindi Chana amesema Serikali itaendelea kuweka mazingira wezeshi kwa Wawekezaji wa ndani na nje ya nchi wenye nia ya kutaka kuwekeza kwenye  sekta ya utalii nchini ili kuweza kutafsiri kwa vitendo maono ya Rais Samia kupitia filamu ya The Royal Tour


Ametoa kauli hiyo jana usiku Jijini Dare s Salaam wakati akizungumza  na  Chama cha Mawakala wa usafiri wa anga Tanzania (TASOTA) kwenye mkutano wao wa mwaka ambapo kila mwaka hukutana mara moja kwa ajili ya kujadili masuala mbalimbali kuhusu ustawi wa Chama chao.

Amesema  Serikali imepunguza ada ya kila mwaka kwa Mawakala  wa Usafiri wa anga nchini  ( TALA fee )  kutoka dola za Marekani 2,000 hadi dola 500

Pia ameeleza kuwa Serikali imejipanga kupunguza utitiri wa kodi katika sekta ya utalii  ili kuhamasisha Wawekezaji zaidi katika sekta hiyo ili iweze kutoa ajira nyingi zaidi.

Ameongeza kuwa  Serikali imeendelea kuwekeza miundombinu bora katika maeneo ya Hifadhi ikiwemo barabara zenye uwezo wa kupitika muda wote pamoja na usimikaji wa mtandao wa intaneti katika mlima Kilimanjaro. 

Amesisitiza kuwa Wizara ya Maliasili na Utalii itaendelea kuweka mazingira wezeshi kwa sekta binafsi ili kuondoa vikwazo kwa wadau wenye nia ya kutaka kuwekeza hapa nchini.

Akizungumzia umahiri wa  TASOTA, Waziri Chana amesema Wanachama  hao  wamekuwa wazalendo na  Mabalozi wa  kutangaza vivutio vya utalii nchini kwa wageni wanaotaka kuja kujionea uzuri wa Tanzania 

" Najisikia fahari  kuona TASOTA, wakifanya kazi usiku na mchana ya kuilinda na kuitetea taswira ya nchi kwa kuratibu  na kupanga safari za watalii wanaotembelea Tanzania " 

Aidha, Dkt.Chana ameihaikikishia TASOTA kuwa yeye kama Waziri mwenye dhmama ataendelea kufanya kazi kwa ukaribu na jumuiya hiyo  ili sekta ya utalii iweze kuleta matokeo yaliyokusudiwa.

Naye Mwenyekiti wa TASOTA, Moustafa Khataw amesema anaishukuru Serikali kwa kutambua mchango wao wa kutangaza uzuri wa Tanzania

" Tumekuwa tukifanya kazi zetu kwa weledi wa hali ya juu katika tasnia hii  ya usafirishaji kwani ni biashara hii  haina njia za mkato wala haina ujanja ujanja inahitaji watu wazalendo  na wenye haiba nzuri katika kuwahudumia watalii wetu " amesema Mwenyekiti Khataw.

Rais Mhe. Samia Suluhu Hassan akutana na viongozi wa Shirikisho la Vyuo vya Elimu ya Juu Tanzania (TAHLISO) pamoja na ya Zanzibar (ZAHLIFE) na pia wale wanaowakilisha Serikali za Wanafunzi kutoka Taasisi za Elimu ya Juu kutoka Tanzania Bara na Zanzibar

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan akiwa na Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Mhe. Profesa Adolph Mkenda wakati akizungumza na Viongozi wa Shirikisho la Vyuo vya Elimu ya Juu Tanzania (TAHLISO) na ZAHLIFE kutoka Zanzibar mara baada ya kuwasili Ikulu Chamwino Mkoani Dodoma tarehe 11 Februari, 2023.


Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan akiwa na Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Mhe. Profesa Adolph Mkenda katika picha ya pamoja na Viongozi wa Shirikisho la Vyuo vya Elimu ya Juu Tanzania (TAHLISO) na ZAHLIFE kutoka Zanzibar mara baada ya mazungumzo, Ikulu Chamwino Mkoani Dodoma tarehe 11 Februari, 2023.



Viongozi mbalimbali pamoja na Wale wa Shirikisho la Vyuo vya Elimu ya Juu Tanzania (TAHLISO), ZAHLIFE wakimsikiliza Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan wakati akizungumza nao katika Viwanja vya Ikulu Chamwino Mkoani Dodoma tarehe 11 Februari, 2023.







Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan akizungumza na Viongozi wa Shirikisho la Vyuo vya Elimu ya Juu Tanzania (TAHLISO) na ZAHLIFE kutoka Zanzibar pamoja na Wale wanaowakilisha Serikali za Wanafunzi kutoka Taasisi za Elimu ya Juu, Tanzania Bara na Zanzibar kwenye Mkutano uliofanyika katika Viwanja vya Ikulu Chamwino Mkoani Dodoma tarehe 11 Februari, 2023.


 

Wataalamu wa JKCI Waadhimisha siku ya wapendanao kwa kufanya upasuaji wa moyo kwa watoto 15

Wataalam wa upasuaji wa moyo na mishipa ya damu kwa watoto wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) wakifanya upasuaji wa kuziba tundu la moyo katika kambi maalum ya matibabu ya siku tano inayofanywa na wataalamu wazawa wa Taasisi hiyo ambapo watoto 15 walifanyiwa upasuaji.


Wataalam wa upasuaji wa moyo na mishipa ya damu kwa watoto wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) wakifanya upasuaji wa kuzibua mshipa wa damu wa moyo uliokuwa umeziba wakati wa kambi maalum ya siku tano iliyofanywa na madaktari hao ambapo watoto 15 walifanyiwa upasuaji. 

10/02/2023 Watoto 15 wenye magonjwa ya moyo ya kuzaliwa nayo wamefanyiwa upasuaji mkubwa wa moyo katika kambi maalumu ya siku tano ya matibabu ya moyo inayofanywa na madaktari wazawa wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI)

 

Kambi hiyo maalum ya upasuaji wa moyo ilifanyika kwa lengo la kusherehekea siku ya wapendanao itakayofanyika duniani kote tarehe 14 Februari mwaka huu ambapo wataalamu hao wameiadhimisha kwa kuonesha upendo wao kwa watoto  wenye matatizo ya moyo ya kuzaliwa nayo ambayo ni matundu na mishipa ya damu ya moyo  kutokukaa katika mpangilio wake. 

 

Akizungumza wakati wa kambi hiyo Mkurugenzi wa Idara ya Upasuaji wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Dkt. Angela Muhozya alisema kambi hiyo imefanyika mahususi kwa watoto wenye magonjwa ya moyo ili kuwapa upendo na kurejesha tabasamu kwao kwani watoto hao hupitia maumivu makali kutokana na maradhi waliyonayo.

 

Dkt. Angela ambaye pia ni daktari wa usingizi alisema Idadi ya watoto wenye magonjwa ya moyo inaongezeka kila siku kwani watoto huendelea kuzaliwa, hivyo Idara ya upasuaji ikaona ni vizuri kufanya kambi hiyo huku lengo likiwa kupunguza idadi ya watoto hao wanaosubiria huduma ya upasuaji.

 

“Sisi kama madaktari pia ni wazazi na tumebarikiwa kuwa na watoto, tunaelewa mtoto anapokuwa mgonjwa wazazi wanakuwa kwenye wakati mgumu na  kupelekea baadhi ya mambo kwenye familia kusimama ndio maana tumeona ni vizuri kufanya kambi hii ili kupunguza idadi ya watoto wanaosubiri matibabu pamoja na kuwapa furaha”, alisema Dkt. Anjela .

 

Naye Daktari wa bingwa wa upasuajiwa moyo na mishipa ya damu kwa watoto wa JKCI Godwin Sharau alisema katika kambi hiyo walifanya upasuaji wa  kuziba matundu kwenye moyo, kuachanisha mishipa iliyokaribiana pamoja na kuzibua mishipa iliyoziba.

 

“Tumewafanyia upasuaji mkubwa wa moyo watoto ambao mioyo yao ina matundu pamoja na wale ambao mishipa yao ya damu imeziba haipeleki damu vizuri kwenye moyo”,.

 

“Upasuaji tulioufanya katika  kambi hii tumekuwa tukiufanya sisi kama wataalamu wazawa lakini kwa kufanya kambi maalumu tumewafikia watoto wengi zaidi kwa kipindi cha muda mfupi”, alisema Dkt. Sharau.

 

Daktari huyo bingwa wa upasuaji wa moyo kwa watoto alisema uzoefu wa madaktari wazawa wa upasuaji wa moyo kwa watoto umeongezeka kwani hapo awali kuna baadhi ya upasuaji kama wazawa walikuwa hawawezi kufanya lakini sasa wamebobea katika matibabu hayo bila hata ya kuwa na uangalizi kutoka kwa wenzao wa nchi mbalimbali ambao wamekuwa wakifanya nao upasuaji huo.

 

Dkt. Sharau alisema kutokana na ufinyu wa wodi ya watoto wenye magonjwa ya moyo idadi ya watoto waliohudumiwa imekuwa chache lakini kama wodi hiyo ingekuwa kubwa watoto wengi zaidi wangefanyiwa upasuji huo.

 

“Watoto tuliowafanyia upasuaji wanaendelea vizuri na wengine wameshatoka katika wodi ya uangalizi maalum (ICU) na kupelekwa wodini kwa ajili ya kuendelea na matibabu ikiwa ni pamoja na kufanya mazoezi”, alisema Dkt. Sharau.

 

Kwa upande wa wazazi ambao watoto wao wamefanyiwa upasuaji katika kambi hiyo waliishukuru JKCI kwa matibabu waliyayatoa kwa watoto wao na kuomba kambi kama hizo ziwe zinafanyika mara kwa mara ili watoto wengi zaidi waweze kutibiwa kwa muda mfupi.

 

Rehema Yacob ambaye mtoto wake alizaliwa na tundu kwenye moyo pamoja na mshipa mmoja wa damu kutokupeleka damu vizuri kwenye moyo  alisema kama JKCI isingekuwepo hapa nchini asingeweza kumpeleka mtoto huyo nje ya nchi kutokana na kipato chake kuwa kidogo hivyo kushindwa kumudu gharama za matibabu.

 

“Kutokana na ugonjwa huu wa moyo mtoto wangu alichelewa kutembea, lakini pia baada ya kutembea alikuwa akichoka mapema hivyo kushindwa kujumuika na wenzake kufanya michezo mbalimbali. Baada ya kufanyiwa upasuaji naona mabadiliko kwani sasa amechangamka na anafanya mazoezi”,. 

 

“Kupitia changamoto za mwanangu niliona umuhimu wa kuwa na bima ya afya hivyo kutafuta bima hiyo ambayo imenisaidia kupata matibabu kiurahisi, nawashauri wazazi wenzangu kuwakatia watoto wao bima ya afya kwani matatizo huja ghafla”, alisema Rehema.