Matokeo chanyA+ online




Saturday, June 19, 2021

BILIONI 17 KUTUMIKA KUSAMBAZA UMEME PEMBEZONI MWA JIJI LA DODOMA


 

 

 Na. Veronica Simba - REA

Serikali inatarajia kutumia kiasi cha Shilingi za Kitanzania takribani bilioni 17.3 kuwafikishia umeme wateja wa awali 4,609 kupitia Mradi wa Kusambaza Umeme Awamu ya Pili katika maeneo yaliyo pembezoni mwa jiji la Dodoma.

Waziri wa Nishati Dkt. Medard Kalemani alibainisha hayo jana, Juni 16, 2021 alipokuwa akizindua rasmi mradi huo katika hafla iliyofanyika katika kijiji na kata ya Chihanga, nje kidogo ya jiji la Dodoma.

Alisema kuwa Mradi huo utatekelezwa katika kata 16 za Mkoa wa Dodoma kwa kipindi cha miezi 12 ambapo fedha za utekelezaji wake zimetolewa na Serikali kwa asilimia 100.

“Tunawaomba wananchi watumie nishati ya umeme katika shughuli mbalimbali za uzalishaji mali ikiwa ni pamoja na kuanzisha viwanda vya kusindika mazao ya kilimo, mifugo, uvuvi na madini pamoja na kuboresha utoaji wa huduma za afya, elimu, maji, mawasiliano na kuboresha thamani za bidhaa za kilimo cha viwanda,” alitoa hamasa Waziri.

Aidha, Waziri Kalemani alibainisha kuwa Mradi huo hauna fidia hivyo akawataka wananchi ambao wako katika maeneo inakopita miundombinu husika, kutoa maeneo yao pasipo kudai fidia kama mchango wao katika miradi ya maendeleo.

Katika hatua nyingine, Waziri alisisitiza kuwa bei ya kuunganisha umeme wa njia moja kwa wateja wote nchi nzima iwe kijijini au mjini ni shilingi 27,000 tu kutoka shilingi 177,000 ya awali na kwamba kwa wenye kuhitaji kuunganishiwa umeme wa njia tatu, gharama yake ni shilingi 139,000 kutoka shilingi 912,000 iliyokuwa ikitozwa awali.

Akizungumza katika hafla hiyo, Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Anthony Mtaka aliwataka wananchi kutumia umeme huku wakiuunganisha na maendeleo pamoja na elimu.

“Nyumba tunazoweka umeme tufanye maendeleo. Tuone saluni pamoja na kufunga taa ili kuwawezesha watoto kujisomea na kukuza ufaulu mashuleni,” alisisitiza.

Kwa upande wake, Mbunge wa Dodoma Mjini, Anthony Mavunde, alimhakikishia Waziri kuwa wananchi wa Chihanga wako tayari kulipia shilingi 27,000 ili waunganishiwe huduma hiyo kwa ajili ya kuutumia katika kukuza kipato na kujiletea maendeleo.

Naye Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi wa Wakala wa Nishati Vijijini, Wakili Julius Kalolo alibainisha kuwa, Mradi huo uliozinduliwa na Waziri Kalemani ni sehemu tu ya mpango mkakati wa Wakala ambao umelenga kusambaza umeme katika maeneo yaliyo pembezoni mwa miji na majiji.

Wakili Kalolo aliongeza kuwa Mradi huo utatekelezwa katika mikoa mitatu ambayo ni Arusha, Mwanza na Dodoma ambapo utaongeza uwekezaji katika nyanja mbalimbali za maeneo yaliyo pembezoni mwa miji ikiwa ni pamoja na uanzishwaji wa viwanda na biashara mbalimbali.

Awali, Mkurugenzi Mkuu wa Wakala wa Nishati Vijijini (REA), Mhandisi Amos Maganga alieleza kuwa gharama za kutekeleza Mradi huo katika mikoa yote mitatu ya Arusha, Mwanza na Dodoma ni takribani shilingi bilioni 31.2 ambapo utatekelezwa kwa kipindi cha miezi 12.

Tuesday, June 15, 2021

TANZANIA YAJIPANGA KUWA KINARA WA MBOLEA, WAZIRI MKENDA AANZA MKAKATI WAKE


 
Waziri wa Kilimo, Mhe Prof. Adolf Mkenda akikagua sehemu inayotumika kupakuwa mbolea wakati alipofanya ziara ya kikazi ya siku moja katika bandari ya Dar es salaam tarehe 14 Juni 2021. (Picha Zote Na Mathias Canal)
Waziri wa Kilimo, Mhe Prof. Adolf Mkenda akizungumza na Menejimenti ya Bandari ya Dar es salaam wakati alipofanya ziara ya kikazi ya siku moja katika bandari ya Dar es salaam tarehe 14 Juni 2021 ili kujionea hali ya upakuaji wa mbolea inapowasili nchini.
Waziri wa Kilimo, Mhe Prof. Adolf Mkenda akizungumza na Menejimenti ya Bandari ya Dar es salaam wakati alipofanya ziara ya kikazi ya siku moja katika bandari ya Dar es salaam tarehe 14 Juni 2021 ili kujionea hali ya upakuaji wa mbolea inapowasili nchini.
Waziri wa Kilimo, Mhe Prof. Adolf Mkenda akizungumza na waandishi wa habari mara baada ya kukamilika kwa ziara yake ya kikazi ya siku moja katika bandari ya Dar es salaam tarehe 14 Juni 2021 ili kujionea hali ya upakuaji wa mbolea inapowasili nchini.
Waziri wa Kilimo, Mhe Prof. Adolf Mkenda akisisitiza jambo wakati akikagua ufanisi wa Bandari ya Dar es salaam katika upakuaji wa mbolea inayowasili nchini alipofanya ziara ya kikazi ya siku moja katika bandari ya Dar es salaam tarehe 14 Juni 2021 ili kujionea hali ya upakuaji wa mbolea inapowasili nchini.

Na Mathias Canal, Wizara ya Kilimo-Dar es salaam


Waziri wa Kilimo, Mhe Prof. Adolf Mkenda amesema Serikali ipo kwenye  mikakati wa  kuhakikisha Tanzania inakuwa kituo  cha kuingiza mbolea na kusambaza kwa nchi zenye uhitaji.

Ameyasema hayo tarehe 14 Juni 2021 wakati akiwa katika ziara ya kikazi katika Bandari ya Dar es Salaam kwa lengo la kuangalia shughuli ya upakuaji na uingizaji wa mbolea ndani ya nchi.

Amesema njia mojawapo ya kuhakikisha mbolea inashuka ni kuhakikisha mbolea nyingi inaingia nchini, na ili kufanikisha hilo lazima Tanzania iwe ni “HABU’’ ya kuagiza na kuingiza mbolea. 

“Kwa bahati mbaya hivi karibuni Zambia walikuwa wanaleta mbolea kupitia bandari yetu lakini sasa hivi wanaleta kupitia bandari nyingine, tunataka warudi waingize mbolea kupitia bandari ya Dar es Salaam. 

 “Tunapenda wafanyabiashara walete mbolea kwa wingi  hapa nchini, sisi tutaweka mfumo mzuri wa kuwarahisishia kuiondoa  mapema ili kuipeleka  Congo na Zambia  au nchi nyingine yoyote wanapotaka kwenda kuuza,” Amesema  

Waziri amesema kuwa hiyo ni hatua ya awali,  nyingine wanatarajia kuimarisha uzalishaji wa mbolea ili kufanikisha kupatakana kwa wingi nchini. 

“Kuna kiwanda kinajengwa Dodoma, yule wa Minjingu tumemwambia tutamlinda na aongeze ufanisi wa mbolea yake ili kazi iende mbele, hii itatusaidia sisi wakulima kupata mbolea kwa bei rahisi hivyo mazao yatauzwa pia kwa bei rahisi,” Amekaririwa Profesa Mkenda.

Amesema hatua hiyo inalenga katika  kuongeza ushindani wa kuingiza mbolea na  hiyo ndiyo sababu ya kuongeza muda wa zabuni ili kuwe na kampuni nyingi ambazo zitakuja kushindana kuleta mbolea. 

Akizungumzia kuhusu bei ya mbolea Waziri Mkenda amesema kuwa, Kwa sasa inaongezeka duniani na hata nchini imeshapanda ambapo kati ya Juni mwaka jana na Juni mwaka huu bei imeongezeka kwa asilimia 50.

“Mahitaji  ya mbolea nchini ni takribani Tani laki saba, wakati  uzalishaji wetu ni chini ya laki moja, tayari wameanza mazungumzo na leo muwakilishi wa balozi wa Saudi Arabia na Qutar. 

 “Ni mojawapo ya nchi ambazo zinazalisha mbolea kwa wingi, na nitaendelea kufanya mazungumzo na mabalozi wengi kuwashawishi kampuni zao kule zije kuwekeza nchini  hiyo itachangia  bei zipungue,” Amesema.

Kwa upande wake Mkurugenzi Mtendaji wa Mamlaka ya Udhibiti wa Mbolea Tanzania (TFRA), Dkt Stephan Ngailo amesema kuwa suala la vibali wameshaanza kuhakikisha wafanyabiashara wanaoomba vibali wanapatiwa kwa wakati.

“Tunataraji kuanza kuruhusu wafanyabiashara kuomba vibali kwenye  kuingiza mbolea, wanapata hati ya kulipia kwa njia ya mtandao na kibali pia.  

Amesema kuwa hiyo itarahisisha vibali kutolewa kwa wakati, hivyo itaongozeka ufanisi lengo kuhakikisha mkulima anapata mbolea bora  bei rahisi na kwa wakati uliokusudiwa.

Kwa upande wake  Mkurugenzi wa Bandari ya Dar es Salaam, Elihuruma Lema amemueleza  Waziri Mkenda kuwa TFRA imeboresha mfumo wa upakiaji wa mbolea unaofanywa kwa njia  ya kisasa   unaowezesha upakiaj kufanyika haraka.

Lema amesema kuwa mashine ya awali ilikuwa na uwezo wa kuakia mifuko 1500 kwa saa 24 lakini hiyo ya kisasa ina uwezo wa kujaza mifuko 3000. 


MWISHO

RAIS SAMIA SULUHU HASSAN AMALIZA ZIARA YAKE YA SIKU 3 MKOANI MWANZA

 

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan akiagana na viongozi mbalimbali wa mkoa wa Mwanza, mikoa jirani, pamoja na Wabunge mara baada ya kumaliza ziara yake ya siku 3 na kuondoka mkoani Mwanza. 

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan akiagana na Mkuu wa Mkoa wa Mwanza Mhandisi Robert Gabriel Luhumbi wakati akiondoka mkoani Mwanza leo tarehe 15 Juni, 2021. PICHA NA IKULU




Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan akiangalia kikundi cha ngoma za asili cha mkoa wa Mwanza wakati akielekea kuagana na viongozi mbalimbali wa Serikali na Mkoa mara baada ya kumaliza ziara yake ya siku 3 mkoani Mwanza.

RAIS SAMIA SULUHU AWEKA JIWE LA MSINGI UJENZI WA RELI YA KISASA STANDARD GAUGE RAILWAY (SGR) KUTOKA MWANZA-ISAKA KM 341 MKOANI MWANZA

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan akionesha mfano wa kufukia majina ya viongozi mbalimbali walioshiriki kufanikisha kuanza kwa mradi wa Ujenzi wa Reli ya Kisasa Standard Gauge Railway (SGR) kutoka Mwanza hadi Isaka mkoani Shinyanga katika sherehe zilizofanyika Fela mkoani Mwanza  tarehe 14 Juni, 2021.

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan akivuta utepe kuweka jiwe la Msingi Ujenzi wa Reli ya Kisasa Standard Gauge Railway (SGR) kutoka Mwanza hadi Isaka mkoani Shinyanga katika sherehe zilizofanyika Fela mkoani Mwanza  tarehe 14 Juni, 2021.

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan akimsikiliza Mkurugenzi Mkuu wa TRC Masanja Kadogosa kuhusu ujenzi wa Reli ya Kisasa kipande cha kutoka Mwanza hadi Isaka km 341 mara baada ya kuweka jiwe la Msingi katika sherehe zilizofanyika Fela mkoani Mwanza  tarehe 14 Juni, 2021.

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan akiwa na Mkuu wa Mkoa wa Mwanza Mhandisi Robert Gabriel Luhumbi, Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi Dkt. Leonard Chamuriho, Mkurugenzi Mkuu wa TRC Masanja Kadogosa pamoja na viongozi wengine wa Chama, Serikali na Bunge, akikata utepe kuashiria uzinduzi wa ujenzi wa Reli ya Kisasa kipande cha kutoka Mwanza hadi Isaka km 341

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan akitembea kwenye mfano wa Reli ya Kisasa itakayojengwa kutoka Mwanza hadi Isaka mara baada ya kuweka jiwe la msingi katika sherehe zilizofanyika Fela mkoani Mwanza  tarehe 14 Juni, 2021.

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan akizungumza na viongozi mbalimbali pamoja na wananchi waliohudhuria sherehe za uwekaji wa Jiwe la Msingi jiwe la Msingi Ujenzi wa Reli ya Kisasa Standard Gauge Railway (SGR) kutoka Mwanza hadi Isaka mkoani Shinyanga katika sherehe zilizofanyika Fela mkoani Mwanza  tarehe 14 Juni, 2021.

Sehemu ya Wananchi waliohudhuria sherehe za uwekaji wa jiwe la Msingi mradi huo mkubwa wa ujenzi wa Reli  ya Kisasa SGR ambao utagharimu kiasi cha Shilingi za Kitanzania Trilioni 3.1

Viongozi mbalimbali pamoja na wananchi wa Mkoa wa Mwanza waliohudhuria sherehe za uwekaji wa jiwe la Msingi mradi huo mkubwa wa ujenzi wa Reli ya Kisasa SGR katika eneo la Fela mkoani Mwanza  tarehe 14 Juni, 2021.

Msanii wa Singeli Barobaro akitumbuiza huku viongozi mbalimbali wakimtunza katika Sherehe za uwekaji wa jiwe la Msingi mradi huo mkubwa wa ujenzi wa Reli ya Kisasa SGR katika eneo la Fela mkoani Mwanza leo tarehe 14 Juni, 2021.

PICHA NA IKULU

WAZIRI LUKUVI AITWA KUINGILIA KATI MGOGORO WA ARDHI MCHOMORO


Na Stephano Mango, Namtumbo

Wannachi  kutoka katika koo 16 wa Kijiji cha Mchomoro kilichopo katika Halmashauri ya Wilaya ya Namtumbo Mkoani Ruvuma wamemuomba Waziri wa ardhi , nyumba na maendeleo ya makazi William Lukuvi kuingilia kati utatuzi wa mgogoro wa ardhi yao zaidi ya heka 700 kati yao na Mkuu wa Wilaya hiyo Mstaafu Luckness Amlima ili waweze kuendelea na shughuli zao za kimaendeleo kuliko mateso ambayo wanayapa hivi sasa ya kufunguliwa kesi kila wanapoenda katika mashamba yao.

Wakizungumza na waandishi wa habari waliofika katika kijiji hicho jana wawakilishi wa koo 16 zenye familia zaidi ya 68 walisema kuwa mgogoro huo umedumu kwa zaidi ya miaka mitano sasa na kwamba viongozi wa kijiji na Wilaya wamekuwa wakipuuzia mgogoro huo kwa sababu zao binafsi hali ambayo inaashiria kuwa ni kumpendelea mkuu huyo wa Wilaya mstaafu kwa kuwa alisaidiwa na baadhi ya viongozi kujimilikisha maeneo hayo kinyume na utaratibu

Akizungumza kwa niaba ya koo hizo Rashid Malamaye alisema kuwa mkuu huyo wa Wilaya amevamia katika maeneo yao ya asili ambayo wao walikuwa wanayatumia kwa shughuli za kilimo na ufugaji toka miaka mingi lakini cha kushangaza kwa sasa wanataka kudhulumiwa mashamba yao na mkuu huyo mstaafu

Malamaye alisema kuwa katika mashamba hayo kulikuwa na nyumba za nyasi lakini zimechomwa moto, mazao ya muda mrefu aina ya minazi, machungwa,migomba na mihogo lakini cha kushangaza mazao hayo yamefyekwa bila wao kujulishwa na kuwekwa walinzi ambao wamekuwa wakiwapiga wananchi ambao wanakwenda katika mashamba hayo na kuwafungulia mashataka mbalimbali kwa lengo la kuwanyanyasa

“Tumeshtushwa sana na kitendo hicho cha uharibifu wa mazao yetu na uvamizi wa mashamba hayo ambayo yapo katika maeneo ya mihane katika kitongoji cha Nyerere na mwekezaji ambaye aliwahi kuwa mkuu wa Wilaya bila sisi wenye maeneo kujulishwa na hata tulipolalamika kwenye uongozi wa kijiji na Wilaya hakuna hatua zinazochukuliwa dhidi yake”alisema Malamaye

Naye Issa Languka alisema kuwa mara baada ya kutokea kwa uvamizi huo walitoa taarifa katika uongozi wa kijiji na kwenye uongozi wa Chama cha Mapinduzi lakini majibu waliyoyatoa kuwa mwekezaji huyo yupo kihalali bila kufafanua sheria ipi au mkutano gani wa hadhara ambao ulihalarisha mwekezaji huyo kupewa heka zaidi ya 700 na kijiji kinyume na sheria za ardhi

Languka alisema kuwa inasikitisha sana kuona kuwa viongozi wa kijiji badala ya kulinda raia na mali zao wao wamekuwa chanzo cha kutengeneza migogoro kinyume na kiapo chao cha uadilifu ambacho waliapa na mara kadhaa wamekuwa wakitoa taarifa za uongo kuhusu mgogoro huo

Alifafanua kuwa hali iliyopo kwasasa sio nzuri kwani wenye mashamba wamekuwa wakienda kufanya shughuli zao wanakamatwa na kufunguliwa kesi mbalimbali katika kituo cha polisi Wilaya ya Namtumbo hali ambayo inazidisha uhasama kati ya wananchi na mwekezaji huyo.

Alisema kuwa kutokana na kitendo hicho tumemwandikia Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma Christine Mdeme kumjulisha madai yetu ili aweze kuchukua hatua stahiki kwani mwenendo wa viongozi wa Wilaya ya Namtumbo dhidi ya mgogoro husika hauridhishi na hatuna imani nao kwani ni zaidi ya mwaka wa nne sasa wameshindwa kuukomesha.

Kwa upande wake Mwenyekiti wa kijiji hicho Said Mohamed Mkalela alikili kuwepo kwa mgogoro huo na kusema kuwa hatua zinaendelea kuchukuliwa ingawa wananchi hao wamekuwa wakikosa imani kutokana na kuchelewa kumalizika kwa mgogoro huo

Mkalela alisema kuwa wao waliingia madarakani mwaka 2019 lakini nyaraka zinaonyesha mwekezaji huyo alipata eneo la heka 40 kihalali toka mwaka 2016 katika maeneo ya namambigi na sio mihane, lakini hatua za kutatua mgogoro huo zinaendelea ingawa wananchi wanateseka.

Naye Mkuu wa Wilaya mstaafu  Luckness Amlima alipotafutwa ili kuelezea mgogoro huo alisema yeye hautambui mgogoro huo bali waulizwe viongozi wa kijiji husika na sio yeye kwani yeye amepewa na viongozi wa kijiji hicho kwa kufuata utaratibu waliokubaliana

Amlima alipotakiwa kusema kuwa ni eneo lipi ambalo alipewa kisheria lakini aliendelea kusema kuwa yeye na wenzake 16 waliomba mashamba na walipewa na mkutano wa kijiji mwaka 2017 lakini yeye haelewi kuwa ni wapi ambapo alikabidhiwa hivyo wanao weza kujibu malalamiko hayo ni viongozi wa vijiji

Kwa upande wake Katibu Tawala wa Wilaya hiyo aden Nchimbi alikiri kuusikia mgogoro huo na kuagiza wahusika kwa kushirikiana na Afisa ardhi wa Halmashauri kukutana na kuumaliza mgogoro huo ili kuwaondolea kero wananchi

Kwa upande wake Mbunge wa Jimbo la Namtumbo Vita Kawawa alipotafutwa ili aweze kuzungumzia mgogoro huo alisema atafutwe baadae kwani kwasasa yupo kwenye shughuli za Bunge.

WAZIRI MKUU ATOA MAELEKEZO KUFANIKISHA KILIMO CHA ALIZETI


Waziri Mkuu Kassim Majaliwa akikagua mabanda ya wadau wa Wakala za Mbegu na Makampuni yaliyopo kwenye mnyororo wa uzalishaji kwenye kilimo cha zao la alizeti, alipozindua kampeni ya kitaifa ya kuhamasisha kilimo cha zao hilo mkoani hapa juzi kwa kuanza na mikoa ya Singida, Dodoma na Simiyu. 


Na Godwin Myovela, Singida

Waziri Mkuu Kassim Majaliwa ameagiza sehemu zote zinazolima zao la alizeti ikiwemo mikoa ya Singida, Dodoma na Simiyu kutumia asilimia 10 ya mikopo inayotengwa kwa makundi ya vijana, wanawake na wenye ulemavu kwa kuwapatia mitaji ya mbegu za zao hilo badala ya fedha ili kupanua wigo wa uzalishaji wake, sanjari na kukuza uchumi wa mtu mmoja mmoja kupitia kilimo.

Waziri Mkuu aliyasema hayo juzi mkoani hapa wakati akizindua kampeni ya kitaifa ya kuhamasisha kilimo cha alizeti alipokutana na wadau mbalimbali wa mnyororo wa thamani ya zao hilo kutoka mikoa ya Singida, Dodoma na Simiyu.  

"Toeni mitaji ya mbegu kwa makundi haya badala ya fedha. Mana hata wengine mnaowapatia mikopo ya fedha hizo hawarudishi, wapeni mbegu na wasimamieni hii italeta tija kubwa," alisema.

Waziri Mkuu aliweka bayana faida kubwa ambayo mkulima atanufaika nayo endapo atajikita kwenye kilimo cha alizeti, kuwa pamoja na mambo mengine, mkulima atakayelima ekari moja atatumia wastani wa shilingi 250,000 lakini atakwenda kupata takribani shilingi 1,350,000.

"Mathalani ukilima zao hili Kwa ekari moja utatumia mbegu kilo 2 kwa gharama ya elfu 70, utavuna magunia 15 ya takribani kilo 65 na kwa kila gunia utapata lita 18 za mafuta, na kila Lita Kwa bei ya soko ni shilingi 5000...kwaiyo unakuta unakwenda kupata takribani 1,350,000 ukitoa 250,000 za maandalizi ya shamba hadi kuvuna unajikuta na faida kubwa," Alisema Waziri Mkuu.

Alihamasisha wakulima kuchangamkia fursa hiyo ili kuinua hali ya vipato vyao lakini pia kutumia zao kama suluhisho la kukabiliana na uhaba wa mafuta ya kula nchini ambapo takribani tani 400,000 hulazimika kuagizwa nje ya nchi ili kutosheleza mahitaji.

Alisema uwezo wa nchi kwa sasa ni kuzalisha tani 290,000 pekee huku akisisitiza kiasi hicho ni sawa na asilimia 45 ya jumla ya tani zipatazo 650,000 zinazohitajika nchini.

"Nchi huagiza tani zipatazo 400,000 kufidia upungufu wa mafuta ya kula kwa gharama ya shilingi bilioni 474 kila mwaka kwa takwimu za sasa," Alisema Waziri Mkuu.

Alisema mkakati wa Serikali uliopo ni kuongeza uzalishaji wa mazao ya mafuta yakiwemo alizeti, chikichi, pamba, karanga na ufuta ili kujitosheleza na kuondokana ya adha ya uagizaji wa mafuta ya kula kutoka nje.

Kuhusu mkakati uliopo wa kuinua tija ya kilimo cha alizeti, pamoja na mambo mengine, Waziri Mkuu amewataka Wakuu wa Mikoa kuandaa mpango mkakati ikiwemo kutenga maeneo mahususi kwa ajili ya kilimo cha zao hilo.

Aidha, aliwaagiza wakuu hao wa Mikoa kuhakikisha kila Taasisi na mashule wanaweka mara moja utaratibu wa  kuanza kuzalisha alizeti, jambo ambalo anaamini litasaidia hata kuwajenga kiujuzi wanafunzi kuweza kutumia mafunzo hayo ili kujitegemea hapo baadaye.

Alisema mkulima, mwekezaji au yeyote kwenye mnyororo wa kilimo hicho anayehitaji kuwekeza kwenye alizeti serikali itamlinda na kumhakikishia kila aina ya ushirikiano.

Hata hivyo, aliwakumbusha Wizara ya Kilimo kuandaa kalenda ya kilimo cha zao hilo na kuisambaza kwa wakulima kabla ya msimu mwingine kuanza sambamba na kuongeza idadi ya maafisa ugani kwenye Vijiji na Kata ili kuongeza tija.

Waziri Mkuu pia aliwaagiza Wakuu wa Wilaya ambazo alizeti inalimwa kuandaa vitalu vya mashamba darasa ya mbegu bora kama mwendelezo wa uzalishaji wake baada ya Utafiti, ili kurahisisha upatikanaji wake.

Suala la mkoa husika kuwa na kanzi data (database) ya wakulima na hali halisi ya kilimo hicho ni miongoni mwa maagizo yaliyopewa mkazo lengo ni kufanya kilimo cha alizeti kuwa tegemeo, na hatimaye kuweza kusambaza uchumi wa mtu mmoja mmoja.

Agizo lingine ni kuanza kuunda vikundi vya ushirika ili kurahisisha usambazaji elimu ya mbinu bora za kilimo, lakini zaidi kupeleka huduma za kiugani kwa mkulima kwa wakati.

Pia aliwataka Wakuu wa Wilaya kuhakikisha kila Afisa Ugani anapimwa Kwa matokeo Kwa kupewa eneo na kulima yeye mwenyewe shamba lake la mfano kulingana na zao la mahali husika, ili wakulima wanaomzunguka waende kujifunza kwake, na endapo shamba hilo litashindwa kutoa matokeo mazuri basi aondolewe kwenye halmashauri husika.

Hata hivyo, Waziri Mkuu alizitaka Taasisi mbalimbali za Fedha, ikiwemo Benki ya Kilimo kujitambulisha kwa wakulima na kusambaza elimu ya namna ya kunufaika na mikopo ya kilimo suala ambalo wengi hawalifahamu.

Pia aliagiza Wizara ya Kilimo kuanza mkakati wa ujenzi wa maghala ya kuhifadhia alizeti sambamba na Wizara ya Viwanda kwenda mara moja kusikiliza kero mbalimbali zinazowakabili wenye viwanda vya ukamuaji mafuta ya zao hilo.

"Tutahakikisha mtandao wote wa wanaojihusisha na kilimo cha alizeti tunausimamia ipasavyo. Na naagiza kila kiongozi au taasisi itakayofanya mkutano wowote kwenye mikoa inayolima zao hili kuwe na ajenda ya kuhamasisha alizeti," alisema Waziri Mkuu na akaongeza;

"Kikao hiki sio mwisho nitarudi tena Kwa tathmini kabla ya msimu kuanza ili kuangalia je tulijipanga kwenye kuhamasisha?, pembejeo zimefika kwa wakati? je tuko tayari kulima?, tumeandaa ekari ngapi kwa kilimo hiki? ili tuone kama tutafikia shabaha yetu." Alisema kupitia kampeni hiyo ya Twende Tukalime Alizeti ina Faida.

Thursday, June 10, 2021

TANZANIA KUSHIRIKI MKUTANO WA 26 WA NCHI WANACHAMA WA MKATABA WA UMOJA WA MATAIFA KUHUSU MABADILIKO YA TABIANCHI






Tanzania inatarajiwa kushiriki Mkutano wa 26 wa Nchi Wanachama wa Mkataba wa Umoja wa Mataifa kuhusu Mabadiliko ya Tabianchi utakaofanyika kuanzia Novemba mosi hadi 12, 2021 mjini Glasgow nchini Uingereza.

Hayo yamebainika leo Juni10, 2021 wakati wa kikao kati ya Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira), Mhe. Selemani Jafo na Balozi wa Uingereza nchini Tanzania, Mhe. David Concar aliyemtembelea ofisini kwake jijini Dodoma leo Juni 10, 2021.

Waziri Jafo alisema kuwa mkutano huo utakaofanyika utatoa mchango mkubwa katika sekta ya mazingira kwani nchi mbalimbali zitakutana na kujadili namna gani ya kuchangia kupambana na mabadiliko ya tabianchi, kupunguza hewa ya ukaa duniani na ukataji wa miti.

Alimpongeza Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan kwa kukuza uhusiano wa kidiplomasia na nchi mbalimbali na ambazo zimekuwa zikitoa mchango katika hifadhi ya mazingira.

“Changamoto ya mazingira imekuwa ni kubwa kwa hiyo ni jukumu letu Ofisi ya Makamu wa Rais inayosimamia Sera na kuratibu shughuli zote za mazingira na kuhakikisha nchi yetu inakuwa kinara katika uhifadhi mazingira,” alisema Jafo.

Pia aliwaomba wadau mbalimbali na wananchi kwa ujumla kuungana kwa pamoja na kuifanya Tanzania kuwa ya mfano katika mapambano dhidi ya mabadiliko ya tabianchi yanayoikabali nchi yetu.

Katika mazungumzo yao, Balozi Concar alipongeza juhudi mbalimbali zinazofanywa na Serikali ya Tanzania kupitia Ofisi ya Makamu wa Rais hususan katika kuhakikisha suala la uhifadhi na usafi wa mazingira linakuwa endelevu.

Balozi huyo aliahidi kuwa nchi yake itaendelea kutoa ushirikiano kwa Tanzania katika kupambana na mabadiliko ya tabianchi ambayo yamekuwa yakisababisha madhara kwa binadamu yakiwemo ukame na mafuriko.

Alisema mkutano huo utakaofanyika Uingereza utakuwa na mchango mkubwa kwa kuwa nchi mbalimbali zitakutana na kujadili namna gani ya kuchangia katika kupambana na mabadiliko ya tabianchi na kupunguza hewa ya ukaa duniani na ukataji wa miti.

Kikao hicho kilichohudhuriwa pia na Mkurugenzi wa Mazingira, Dkt. Andrew Komba pamoja na Mkurugenzi Msaidizi Idara ya Mazingira, Bi. Catherine Bamwenzaki Akizungumza na Balozi Concar.

 


 

RAIS SAMIA AKUTANA NA KUFANYA MAZUNGUMZO NA RAIS WA BOTSWANA DKT. MASISI IKULU JIJINI DAR ES SALAAM


Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan akisalimiana na mgeni wake Rais wa Jamhuri ya Botswana Dkt. Mokgweetsi Eric Keabetswe Masisi mara baada ya kuwasili Ikulu Jijini Dar es Salaam leo tarehe 10 Juni 2021


Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan akimkabidhi Zawadi za Picha Rais wa Jamhuri ya Botswana Dkt. Mokgweetsi Eric Keabetswe Masisi mara baada ya kuwasili Ikulu Jijini Dar es Salaam leo tarehe 10 Juni 2021.

 


Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan akipokea na kuiangalia zawadi ya picha aliyopewa na Rais wa Jamhuri ya Botswana Dkt. Mokgweetsi Eric Keabetswe Masisi mara baada ya kuwasili Ikulu Jijini Dar es Salaam leo tarehe 10 Juni 2021.

 

Wednesday, June 9, 2021

RC SINGIDA AZITAKA HALMASHAURI KUSIMAMIA VYANZO VYA MAPATO

Mkuu wa Mkoa wa Singida Dkt.Binilith Mahenge akizungumza na Watendaji na Watumishi wa Halmashauri ya Wilaya ya Iramba jana, wakati akikagua jengo la maabara ya Hospitali ya wilaya iliyopo Old Kiomboi katika ziara yake ya kikazi ya kukagua miradi ya maendeleo.
Mkuu wa Mkoa wa Singida Dkt.Binilith Mahenge, akisisitiza jambo wakati akizungumza na Watendaji na Watumishi wa Halmashauri ya Wilaya ya Iramba jana.
Mkuu wa Wilaya ya Iramba, Emmanuel Luhahula, akisoma taarifa ya miradi mbalimbali ya maendeleo ya wilaya hiyo.

Kikao kikiendelea.
Kikao kikiendelea.
Baadhi ya watumishi wa Wilaya ya Iramba wakiwa kwenye kikao hicho.
Kikao kikiendelea.
Makofi yakipigwa kwenye kikao hicho.
Kikao kikiendelea.
Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Iramba,  Innocent Msengi akizungumza kwenye kikao hicho.
Dkt.Mahenge (katikati) akipokea taarifa ya ujenzi wa Maabara ya Hospitali ya Wilaya ya Iramba kutoka kwa Mganga Mkuu wa hospitali hiyo, Hussein Sepako (kushoto)  wakati alipofika kuona maendeleo ya ujenzi huo. 
Baadhi ya wauguzi wa hospitali hiyo wakiwa nje wakati wa ziara hiyo.
Mhasibu wa mapato wa wilaya hiyo, Optatusy Ottolikiliwike, akitoa maelezo ya ukusanyaji wa mapato kwenye mnada wa Igumo.
Mkuu wa Mkoa wa Singida Dkt.Binilith Mahenge akizungumza na wananchi alipotembelea Mnada wa Igumo. Kushoto ni Mkurugenzi wa Wilaya ya Iramba, Linno Mwageni na kulia ni Mkuu wa Wilaya ya Iramba, Emmanuel Luhahula.
Mkazi wa Iramba, Lutha Nathaniel, akimpongeza mkuu wa mkoa kwa kufanya ziara katika wilaya hiyo.
Mkuu wa Mkoa wa Singida Dkt.Binilith Mahenge akizungumza na  Mjasiriamali  alipotembelea Mnada wa Igumo. Kulia ni Mkuu wa Wilaya ya Iramba, Emmanuel Luhahula.
Mkuu wa Mkoa wa Singida Dkt.Binilith Mahenge akizungumza na watendaji wa wilaya hiyo  alipotembelea Mnada wa Igumo. Kulia ni Askari Polisi wakiimarisha ulinzi eneo hilo. Katikati ni Mkurugenzi wa Wilaya ya Iramba, Linno Mwageni.
Mkuu wa Mkoa wa Singida Dkt.Binilith Mahenge, akipata maelezo ya Mradi wa Maji uliopo Kijiji cha Kyalosangi Kinampanda..

 Meneja wa Wakala wa Majisafi na Usafi wa Mazingira Vijijini (RUWASAWilaya ya IrambaMhandisi Ezra Mwacha, akitoa taarifa ya mradi huo kwa mkuu wa mkoa.

Mwonekano wa tenki la maji la mradi huo.
Mkuu wa Mkoa wa Singida Dkt.Binilith Mahenge, akiagana na Watendaji na Watumishi wa Halmashauri ya Wilaya ya Iramba baada ya kumaliza ziara yake hiyo.

 

Na Dotto Mwaibale, Singida 

MKUUwa Mkoa wa Singida Dkt. Binilith Mahenge amewataka watendaji wa halmashauri kusimamia ipasavyo vyanzo vya mapato vilivyopo kwenye maeneo yao.

Mahenge alitoa agizo hilo jana wilayani Iramba mkoani hapa katika muendelezo wa ziara zake za kutembelea halmashauri zote kwa ajili ya kukagua miradi ya maendeleo na kuzungumza na watumishi, watendaji na wananchi.

Alisema anataka viongozi hao hasa watendaji kujua kuwa kupata mapato makubwa sio lazima kuwa na vyanzo vikubwa kama madini na miradi ya mashamba bali ni  hivihivi vidogo vilivyopo ambapo vikisimamiwa vizuri vitazifanya  halmashauri kupata mapato yakutosha.

"Nataka watendaji na viongozi wenzangu wajue kwamba mnada ni chanzo kizuri sana cha mapato hivyo kitiliwe maanani, kuna dhana kuwa ili kupata mapato makubwa ni lazima kuwepo na miradi mikubwa na vitu vingine vinavyofanana na hivyo hapana hivi hivi vidogo vikisimamiwa vitafanya mambo makubwa," alisema Mahenge.

Dkt.Mahenge alisema katika ziara yake hiyo wilayani humo aliamua kutembelea mnada ikiwa ni chanzo mojawapo cha mapato ambacho kimsingi kinajumuisha watu wengi sana.

Aliyata makundi hayo ya watu kuwa ni wachoma nyama, wauza nguo,mifugo na makundi mengine na kuwa alichojifunza ni kutokuwepo kwa usimamizi mzuri wa ukusanyaji wa mapato licha ya kuwepo kwa makundi hayo.

" Nimejifunza hatuna usimamizi mzuri na kuwa chanzo hicho  kipokipo tu kwa sababu hayupo mtu anaye hakiki upatikanaji wa mapato kama yamepanda au kushuka na kwanini makusanyo yana kuwa yale yale kila wakati.

Alisema katika minada aliyoitembelea amebaini kutokuwepo kwa utaratibu wa kuwa sajili wanunuzi wa mifugo kwenye eneo moja badala yake kila mtu anafanya kivyake jambo linalosababisha upotevu wa mapato.

Dkt. Mahenge alisema kukosekana kwa usimamizi mzuri wa mapato katika maeneo hayo kunasababishwa na baadhi ya watendaji wa serikali ambao sio waaminifu ambao wamechangia kutotumika kwa maeneo yaliyotengwa kwa shughuli za ununuzi na uuzaji wa mifugo na badala yake kwa kushirikiana na wanunuzi hao wamekuwa wakifanyia shughuli hizo nje ya maeneo hayo.

Aidha alisema jambo kubwa analolihitaji ni usimamizi mzuri wa ukusanyaji wa mapato kwenye mifugo na kwa wafanyabiashara wengine ambao wanafanya shughuli za kibiashara kwenye eneo hilo la mnada ambao wengi wao hawana vitambulisho vya ujasiriamali hivyo ametaka kuongezwa kasi ya utoaji wa vitambulisho hivyo kwani wananchi wako tayari lakini hawajapa fursa ya kuvipata. 

Alizitaka timu za ukusanyaji wa mapato za halmashauri kunapokuwa na minada kwenda kujionea ukusanyaji wa mapato badala ya kumuachia mtu mmoja ambaye anaweza kurubuniwa na kusababisha upotevu wa mapato. 

Dkt.Mahenge katika ziara yake alitembelea na kukagua ujenzi wa jengo la maabara hospitali ya wilaya ambapo hakuridhishwa na gharama halisi zilizotumika kwa ujenzi huu kuanzia msingi hadi hatua ya linta na kumwagiza mkuu wa wilaya hiyo kufanya uchunguzi.

Aidha alikagua ukusanyaji wa mapato katika Mnada wa Igumo na mradi wa maji uliopo Kijiji cha Kyalosangi.