Na ASP Lucas Mboje, Mbeya
Kamishina
Jenerali wa Magereza nchini, Phaustine Kasike amesema kuwa Jeshi la
Magereza limeanza utekelezaji wa mpango wa miaka mitano wa kuelekea
kujitosheleza kwa chakula cha wafungwa magerezani katika magereza kumi
(10) ya kimkakati likiwemo Gereza Songwe, lililopo Mkoani Mbeya ambalo
limelima hekari 750 za zao la mahindi.
Akizungumza
na wanahabari leo mara baada ya kukagua mashamba ya mahindi katika
Gereza la Kilimo Songwe, Kamishna Jenerali wa Magereza, Phaustine Kasike
amesema kuwa lengo la ziara yake ni kujionea hali halisi ya
ufanikishaji wa jukumu walilopewa na Serikali katika kuhakikisha kuwa
wanazalisha chakula kwa wingi cha wafungwa waliopo magerezani.
Amesema
kuwa Mkoa wa Mbeya ni miongoni mwa mikoa ambayo imeingizwa katika
utekelezaji wa mpango huo wa uzalishaji chakula cha wafungwa ambapo kila
Gereza la kimkakati limepangiwa malengo ya kulima mazao mbalimbali ya
chakula cha wafungwa ikiwemo mahindi, maharage na mpunga.
“Mpango
huu ni lazima tuufanikishe, hivyo tayari tumekwishajipanga na nguvu
kazi ya wafungwa inatumika ipasavyo katika kufanya kazi katika magereza
hayo kama mlivyojionea leo hapa Gereza Songwe, pia tunajitahidi
kusimamia rasilimali nyinginezo tulizonazo katika maeneo yetu ya
magereza ili tuweze kutekeleza ipasavyo maelekezo ya Serikali”.
Alisisitiza Jenerali Kasike.
Aidha,
Jenerali Kasike ameongeza kuwa kwa sasa Jeshi hilo linakusanya
rasilimali zilizopo na kutoa kipaumbele katika magereza yakimkakati,
ambapo katika kukidhi mahitaji ya nguvu kazi ya wafungwa, tayari
wafungwa kutoka sehemu mbalimbali nchini wamehamishiwa katika magereza
yenye mkakakati ili kuongeza nguvu kazi yakutosha katika maeneo hayo
yenye uzalishaji.
Akisoma
taarifa ya Magereza Mkoa kwa Kamishna Jenerali wa Magereza nchini, Mkuu
wa Magereza Mkoani Mbeya, SACP. Luhende Makwaia amesema kuwa Mkoa huo
una jumla ya magereza matano ambayo yanatekeleza shughuli mbalimbali za
maendeleo ikiwemo miradi ya kilimo, likiwemo Gereza Songwe.
Kuhusu
msongamano wa wahalifu, SACP. Luhende Makwaia amesema kuwa magereza
yote ya mkoa wa mbeya yanakabiliwa na tatizo la msongamano wa wafungwa
na mahabusu kutokana na ongezeko la uhalifu unaotokana na kuongezeka kwa
idadi ya watu pamoja na kukosekana kwa gereza moja la wilaya katika
mkoa huo.
Mkoa
wa Mbeya una jumla ya wilaya sita(6) ambazo ni Mbeya mjini, Mbeya
Vijijini, Chunya, Rungwe, Mbarali, na Kyela. Katika wilaya hizo ni
wilaya tano(5) tu zina magereza, wilaya moja(1) ya chunya hakuna gereza
hali inayochangia uwepo wa msongamano wa wahalifu katika mkoa. Aidha,
katika magereza matano yaliyopo hupokea na kuhifadhi wafungwa na
mahabusu katika mkoa huo.
Kamishna
Jenerali wa Magereza nchini, Phaustine Kasike akisalimiana na Mkuu wa
Gereza Songwe, SSP. Peter Anatory alipowasili katika Gereza la Kilimo
Songwe leo Januari 25, 2019 kwa ziara ya kikazi ya kukagua utendaji kazi
wa Jeshi hilo pamoja na kukagua mashamba ya kimkakati katika kuelekea
kujitosheleza kwa chakula cha wafungwa magerezani.
Kamishna
Jenerali wa Magereza nchini, Phaustine Kasike akikagua moja ya mashamba
ya mahindi ya Gereza Songwe alipofanya ziara ya kikazi katika Gereza
hilo kabla ya kuendelea na ziara yake Mkoani Rukwa leo Januari 25, 2019.
Kamishna
Jenerali wa Magereza nchini, Phaustine Kasike akitoa maelekezo kwa
Maafisa Waandamizi wa Magereza Mkoani Mbeya alipotembelea na kukagua
mashamba ya mahindi ya Gereza Songwe.
Muonekano wa mashamba ya mahindi katika Gereza la Kilimo yakiwa yamestawi kama inavyoonekana katika picha.
Kamishna
Jenerali wa Magereza nchini, Phaustine Kasike akiangalia zao la mhindi
ambalo linakaribia kukauka katika eneo la mradi wa Kilimo cha
umwagiliaji cha Gereza Songwe.
Kaimu
Katibu Tawala wa Mkoa wa Mbeya, Bw. Jeremia Minja (katikati) akiwa
katika picha ya pamoja na Kamishna Jenerali wa Magereza nchini,
Phaustine Kasike(wa pili toka kulia) pamoja na wajumbe wa Kamati ya
Ulinzi na Usalama ya Mkoa wa Mbeya.(Picha zote na Jeshi la Magereza).
No comments:
Post a Comment