Waziri
wa madini Mhe Doto Mashaka Biteko akizungumza wakati akitoa taarifa ya
wizara ya madini kwenye mkutano wa uanzishwaji wa Masoko ya Madini
uliohudhuriwa na Wakuu wa Mikoa na Makatibu Tawala wa Mikoa Tanzania
Bara katika ukumbi wa Hazina Jijini Dodoma
(Picha Na Mathias Canal)
Waziri Mkuu Kassim Majaliwa, akiwahutubia Wakuu
wa Mikoa na Makatibu Tawala wa Mikoa Tanzania Bara, wakati akifungua mkutano
kwenye ukumbi wa Hazina jijini Dodoma.
Vipngozi
mbalimbali wakifatilia mkutano wa uanzishwaji wa Masoko ya Madini
uliohudhuriwa na Wakuu wa Mikoa na Makatibu Tawala wa Mikoa Tanzania
Bara katika ukumbi wa Hazina Jijini Dodoma, Mkutano huo ulifunguliwa na Waziri Mkuu Mhe Majaliwa Kassim.
Waziri
wa madini Mhe Doto Mashaka Biteko akizungumza wakati akitoa taarifa ya
wizara ya madini kwenye mkutano wa uanzishwaji wa Masoko ya Madini
uliohudhuriwa na Wakuu wa Mikoa na Makatibu Tawala wa Mikoa Tanzania
Bara katika ukumbi wa Hazina Jijini Dodoma.
Naibu
Waziri wa Madini Mhe Stanislaus Nyongo akifuatilia mkutano wa
uanzishwaji wa Masoko ya Madini uliohudhuriwa na Wakuu wa Mikoa na
Makatibu Tawala wa Mikoa Tanzania Bara katika ukumbi wa Hazina Jijini
Dodoma.
Na Mathias Canal, Dodoma
Wizara
ya Madini imeanza utekelezaji wa
Maagizo mbalimbali yaliyotolewa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania Mhe Dkt John Pombe Magufuli yenye lengo la kuboresha mchango wa
Sekta ya
Madini.
Tanzania ni moja kati ya nchi zenye uzalishaji mkubwa wa madini ya aina
mbalimbali ikiwemo dhahabu na vito; hata hivyo imeonekana kuwa sehemu ya madini
yanayozalishwa hapa nchini hutoroshwa na kuuzwa nje ya nchi bila ya kufuata
taratibu zilizowekwa na Serikali na hivyo kupelekea upotevu mkubwa wa mapato
yanayotokana na Sekta ya madini.
Hayo
yamesemwa na Waziri wa madini Mhe Doto Mashaka Biteko leo tarehe 26
Januari 2019 wakati akitoa taarifa ya wizara hiyo kwenye mkutano wa
uanzishwaji wa Masoko ya Madini uliohudhuriwa na Wakuu wa Mikoa na
Makatibu Tawala wa Mikoa Tanzania Bara katika ukumbi wa Hazina Jijini
Dodoma.
Alisema kuwa kwa sasa Wachimbaji na wafanyabiashara wa
madini hawana maeneo maalumu wanayoweza kufanyia biashara ya madini hali ambayo
imechangia kuwepo utoroshaji wa madini, hivyo kuikosesha Serikali mapato
stahiki.
Katika kukabililana na hali hiyo Serikali imekuwa ikichukua hatua
mbalimbali kudhibiti utoroshaji wa madini kwa kushirikiana na Vyombo vya Ulinzi
na Usalama. Hata hivyo, pamoja na njia hii bado ubunifu Zaidi unahitajika
katika kuziba mianya ya utoroshaji wa madini.
Mhe Biteko alisema kuwa Sheria ya Madini ya Mwaka 2010 iliyofanyiwa
marekebisho mwaka 2017, kupitia Sheria ya The
Written Laws (Miscellaneous Amendments) Act, 2017. Maeneo muhimu katika
marekebisho hayo ni pamoja na: hisa za
serikali katika uchimbaji wa madini (Kifungu Na.10)
Serikali kuwa na hisa
zisizolipiwa zisizopungua asilimia16 katika kila Leseni za Uchimbaji Madini (Special Mining Licence na Mining Licence)
na kuweza kupata hisa Zaidi hadi kufikia asilimia 55 kwa kuzingatia unafuu wa
kodi aliopewa Mchimbaji, kuanzishwa kwa
Tume ya Madini ili kusimamia utoaji wa leseni za utafutaji na uchimbaji wa
madini na biashara ya madini; kufanya ukaguzi katika maeneo ya utafiti na
uchimbaji madini; kusimamia hifadhi ya mazingira na usalama migodini.
Aidha, kuanzisha
Masoko ya Madini (Mineral and Gem Houses)
ambayo itajumuisha minada ya madini (Minerals
Auction Centers) Masoko ya Madini (Minerals
Exchange) na Vituo vya malipo na makabidhiano (Clearing House).
Vilevile, kuanzishwa kwa Akiba ya Taifa ya Madini
katika Benki Kuu ya Tanzania. Akiba hiyo itakuwa sehemu ya mrabaha kwa madini
yaliyosafishwa na madini yaliyokamatwa kwa mujibu wa sheria.
Biteko amesisitiza kuwa Maeneo mengine ambayo yameguswa na Marekebisho
ya sheria hiyo ni kuanzishwa kwa Maghala
ya Serikali kwa ajili ya kutunzia madini ya metali na vito yaliyozalishwa
nchini, ambayo inaeleza kwamba kila Mchimbaji kuwa na sehemu ya kutunzia madini
katika eneo la mgodi kwa ajili ya kuhifadhi madini anayozalisha na kuweka
kumbukumbu ya madini hayo.
Hata hivyo, Mchimbaji anatakiwa kuhamisha madini hayo
kwenye maghala ya Serikali ndani ya siku tano kwa ajili ya kusubiri kusafishwa
(refined) kuuzwa au kusafirishwa nje ya nchi. Madini yote kutakiwa kuongezewa
thamani kabla ya kusafirishwa au kuuzwa nje ya nchi, kampuni zinazojihusisha na
utafiti na uchimbaji wa madini kununua bidhaa na kutumia huduma zinazopatikana
hapa nchini na kuajiri raia hasa kwa kada ambazo Watanzania wapo.
Kadhalika, kampuni
hizo zinatakiwa kutoa fedha kwa ajili ya miradi ya maendeleo na huduma za jamii
kama vile shule na hospitali kwa jamii inazozizunguka Kampuni hizo zinatakiwa
kupanga mipango ya kuchangia miradi ya maendeleo na huduma za jamii kwa
kushirikiana na Halmashauri husika. Halmashauri zinatakiwa kutoa miongozo ya
kutoa huduma hizo kwa Kampuni.
"Marekebisho hayo yaliyofanyika Mwaka 2017
katika Sheria ya Madini ya Mwaka 2010 ili kuweza kulinda maslahi ya taifa letu
na kuhakikisha kwamba Sekta ya Madini inachangia ipasavyo katika kukuza na
kuimarisha mchango wa Sekta hii katika Pato la Taifa" Alikaririwa Mhe Biteko
Aidha, mbali na marekebisho hayo ya Sheria,
tarehe 25 Februari, 2018, Mhe. Stanslaus Nyongo aliunda Kamati maalum kuangalia
namna bora ya kudhibiti utoroshwaji wa madini na uanzishwaji wa soko la madini.
Katika taarifa ya kamati hiyo ilionekana kuwa
moja ya sababu kuu inazosababisha utoroshaji wa madini ni kukosekana kwa Soko
la uhakika kwa wazalishaji wa Madini hapa nchini. Pamoja na taarifa hiyo, kwa
nyakati tofauti Mhe. Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania amekuwa akitoa
maagizo ya kuanzisha masoko hayo. Kati ya siku alizotoa maagizo hayo ni pamoja
na alipokuwa akiniapisha kuwa Waziri wa Madini na siku alipofungua Mkutano wa
Wachimbaji Wadogo na Wadau wa Biashara ya Madini uliofanyika jijini Dar es
Salaam tarehe 22 Januari, 2019. Kwa mara nyingine alirudia kauli hiyo.
Alisema Ili kukabiliana na changamoto ya Masoko ya
Madini, Wizara ya Madini iliunda kamati iliyojumuisha wajumbe kutoka katika
taasisi mbalimbali za Serikali zikiwemo Ofisi ya Rais - Ikulu, Ofisi ya Rais - TAMISEMI,
Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Wizara ya Madini, Wizara ya Fedha,
Wizara ya Viwanda na Biashara, Benki kuu na Tume ya Madini. Kamati hiyo
iliundwa ili kuandaa rasimu ya Kanuni za kuanzisha na kusimamia Masoko ya
Madini Nchini.
"Kamati ilianza kutekeleza majukumu yake tarehe
15 Januari, 2019 ambapo nilikutana nayo, na pia, Mwanasheria Mkuu wa
Serikali-Mhe. Adelardus Kilangi. Kwa pamoja tuliwaeleza Wajumbe umuhimu wa
kanuni za kuanzisha na kusimamia masoko ya madini Nchini" Alisema na kuongeza kuwa
"Katika kikao hicho cha kamati nilisisitiza kufanya
marejeo katika taarifa za Kamati iliyoundwa na Mhe. Stanslaus Nyongo, Naibu
Waziri wa Madini na taarifa ya ziara ya mafunzo katika Nchi za India na Falme
za Kiarabu kuhusiana na uanzishwaji wa masoko ya bidhaa za madini pamoja na
Sheria za Madini.
Mafunzo hayo yalihusisha Watendaji wa Wizara na
Wataalam wengine ndani ya Serikali. Aidha,
nilielekeza mambo ya kuzingatia katika uandaaji wa rasimu hiyo kuwa ni umiliki
wa madini, ukusanyaji wa kodi na tozo mbalimbali, upatikanaji wa mitaji kwa
wachimbaji wadogo na namna ya ushiriki wa wachimbaji wadogo katika masoko hayo.
Vile vile, nilisisitiza kuwa msingi wa kanuni hizo ni kifungu cha 27C (1) cha Sheria ya Madini ya 2010."
Katika kuandaa kanuni hizo, jina la Kanuni linalopendekezwa
ni The
Mining (Mineral and Gem Houses) Regulations, 2019. Rasimu ya Kanuni ina sehemu kuu tano ambazo zitaelezwa wakati wa
kutoa mada hii.
Waziri Biteko amewaomba Wakuu wa Mikoa, Makatibu Tawala wa
Mikoa, Maafisa Madini Wakaazi wa Mikoa na Wadau kwa ujumla kufanya kazi kwa
pamoja ili kutimiza ndoto za muda mrefu za Wachimbaji wadogo,
wafanyabiashara wa Madini, Wadau na Watanzania wote kwa ujumla.
Mhe
Biteko amesisitiza, viongozi hao kuendelea kumuunga mkono kwa juhudi na
bidii kubwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ambaye anataka
kuona Sekta
hiyo inawanufaisha Wachimbaji wadogo na Watanzania wote kwa ujumla.
Mkutano huo umefunguliwa na Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe Kassim Majaliwa.
No comments:
Post a Comment