Rais Dkt. John Pombe Magufuli ameshuhudia utiaji saini wa makubaliano kati ya Serikali ya
Tanzania na kampuni ya Bharti Airtel ya India juu ya umiliki wa hisa za kampuni
Airtel Tanzania na maslahi mengine ya Tanzania kutokana na biashara ya kampuni
hiyo.
Hafla
ya utiaji saini makubaliano hayo imefanyika Ikulu Jijini Dar es Salaam ambapo
Waziri wa Katiba na Sheria Prof. Palamagamba Kabudi ametia saini kwa niaba ya
Serikali ya Tanzania na Mwenyekiti wa Bharti Airtel Bw. Sunil Mittal ametia
saini kwa niaba ya kampuni ya Bharti Aitel.
Waziri
wa Katiba na Sheria Prof. Kabudi amesema katika makubaliano hayo kampuni ya
Bharti Airtel imekubali kupunguza umiliki wa hisa zake za kampuni ya simu za
mkononi ya Airtel Tanzania kutoka asilimia 60 hadi 51 na hivyo kuongeza hisa za
Serikali kutoka asilimia 40 hadi 49 bila malipo yoyote kutoka Serikalini.
Prof. Kabudi amebainisha maeneo mengine ya makubaliano kuwa ni Serikali kupata gawio
la kila mwaka kutokana na umiliki wake wa asilimia 49 ambapo inakadiriwa
itakuwa ikipata shilingi Bilioni 10, kufutwa kwa madeni yote ya kampuni ya
Airtel yaliyokuwa yamefikia shilingi Trilioni 1, Bharti Airtel itatoa shilingi
Bilioni 1 kila mwezi kwa kipindi cha miaka 5 kuanzia Aprili 2019 ili kuonesha
nia njema na Bharti Airtel itatoa shilingi Bilioni 2.3 kwa ajili ya kuchangia
huduma za kijamii.
Maeneo
mengine ya makubaliano ni Bodi ya Wakurugenzi wa Airtel Tanzania kuundwa na
wajumbe 7 ambapo Serikali ya Tanzania itawakilishwa na wajumbe 3 (akiwemo Mwenyekiti atakayeteuliwa na
Serikali) na Bharti Airtel itawakilishwa na wajumbe 4,
Menejimenti ya Airtel Tanzania itaongozwa na Bharti Airtel lakini Afisa Mkuu wa
Ufundi atateuliwa na Serikali ya Tanzania, pande zote mbili zitashirikiana
kuandaa upya nyaraka muhimu za kusaidia uendeshaji wa kampuni, pande zote mbili
zitashirikiana kuongeza tija na ufanisi wa Airtel Tanzania na pande zote mbili
zitashirikiana kutumia miundombinu ya Shirika la Simu Tanzania (TTCL) ikiwa kuna
hoja za kibiashara.
Kwa
upande wake Bw. Sunil Mittal amesema amefurahishwa na kufikiwa kwa makubaliano katika
mazungumzo hayo na amebainisha kuwa awali aliona kuna ugumu wa kufikia
makubaliano lakini baadaye alielewa kuwa lengo la Mhe. Rais Magufuli ni
kuhakikisha anaweka mwelekeo mzuri wenye manufaa kwa Tanzania.
Bw.
Mittal ameongeza kuwa makubaliano hayo yameandika historia mpya kwa hisa nyingi
kumilikiwa na Watanzania katika kampuni ya Airtel Tanzania na kwamba anatarajia
kuwa Airtel Tanzania itaendelea kufanya vizuri katika soko la Tanzania ambayo
ni nchi yenye uwekezaji mkubwa wa Bharti Airtel Barani Afrika.
No comments:
Post a Comment