Rais
wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli ameagiza
kusitishwa mara moja kwa zoezi la kuviondoa vijiji na vitongoji vinavyodaiwa
kuwepo katika maeneo ya hifadhi na amewataka viongozi wa wizara zote
zinazohusika kukutana ili kubainisha na kuanza mchakato wa kurasimisha maeneo
ya vijiji na vitongoji hivyo.
Mhe.
Rais Magufuli ametoa agizo hilo Ikulu Jijini Dar es
Salaam alipokutana na Waziri wa Maliasili na Utalii Mhe. Dkt. Hamis
Kigwangallah, Katibu Mkuu Kiongozi Mhe. Balozi John Kijazi, Naibu Waziri wa
Mifugo na Uvuvi Mhe. Abdallah Ulega, Katibu Mkuu Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa
na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) Mhandisi Joseph Nyamhanga na Katibu Mkuu Wizara
ya Ardhi Bi. Dorothy Mwanyika.
Pamoja
na agizo hilo Rais Magufuli ametaka viongozi wa wizara husika kubainisha
maeneo ya hifadhi za wanyamapori na misitu ambayo hayana wanyamapori ama misitu
ili yagawiwe kwa wafugaji na wakulima ambao kwa sasa wanataabika kupata maeneo
ya kufugia wanyama na kuzalisha mazao.
Rais
Magufuli pia ameitaka Wizara ya Maliasili na Utalii kuangalia upya zoezi la
uwekaji wa mipaka ya hifadhi na makazi, na kutumia busara katika uwekaji wa
mawe ya mipaka hiyo ili kutowaondoa wananchi katika maeneo ambayo hayana
ulazima wa kuwaondoa.
“Mimi
sifurahii kuona wafugaji kila mahali wanafukuzwa, kama kuna eneo ambalo
tunafikiri lilikuwa hifadhi ya wanyama lakini halitumiki, tutabadilisha sheria,
tunalimega na tunaligawa kwa wafugaji, vivyo hivyo hata kwa wakulima kama kuna
eneo tunaona ni hifadhi lakini halina msitu wala wanyamapori, na lina rutuba,
na wakulima wanataka kulima nalo tunalimega tunawapa wakulima.
Baadaye
tutajua kabisa eneo hili ni la hifadhi, hili ni la mifugo, hili ni la wakulima,
hili ni la makazi. Kwa hiyo nyinyi Mawaziri na Makatibu Wakuu mkakae
mkatangulize maslahi ya hawa tunaowaongoza ambao ni wakulima, wafugaji, wavuvi
nakadhalika, lakini pia tunahitaji wanyamapori, sijasema sasa hifadhi zote za
wanyama tunazimaliza, hapana, hifadhi za wanyama lazima tuzihifadhi” amesisitiza
Mhe. Rais Magufuli.
Rais Magufuli ameagiza vijiji vyote 366 vilivyoainishwa kuwepo ndani ya maeneo ya
hifadhi hapa nchini visiondolewe katika maeneo hayo na badala yake ametoa mwezi
mmoja kwa viongozi wa wizara zote zinazohusika kubainisha maeneo ya vijiji
hivyo na kuanzisha mchakato wa mabadiliko ya sheria ili yawasilishwe katika
kikao kijacho cha Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Amefafanua
kuwa ni lazima Serikali ifanye maamuzi haya sasa kwa kuwa idadi ya Watanzania imeongezeka
hadi kufikia Milioni 55, idadi ya mifugo imeongeza hadi kufikia Milioni 35 na
hivyo kuna ongezeko kubwa la mahitaji ya maeneo ya ardhi ikilinganishwa na
wakati nchi inapata uhuru ambapo Watanzania walikuwa Milioni 9 na mifugo
ilikuwa Milioni 10.
Aidha, Rais Magufuli ameagiza sheria ya vyanzo vya maji pia iangaliwe upya ili
kutowazuia Watanzania wanaozalisha mazao kandokando mwa mito na ameelezea
kutofurahishwa kwake na vitendo vya kufyeka mazao ya wakulima kwa madai kuwa
wamelima ndani ya mita 60.
Halikadhalika
Mhe. Rais Magufuli ameipongeza Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi
kwa kuwasilisha kwake mapendekezo ya kufutwa kwa mashamba ambayo
hayajaendelezwa na ameagiza wizara hiyo iendelee kumpelekea mapendekezo ya
mashamba yote yaliyotelekezwa ili ayafute na wananchi wagawiwe kwa ajili ya
kuyatumia kwa uzalishaji wa mazao na mifugo.
Hata
hivyo, Rais Magufuli amesema maagizo hayo hayana maana kuwa sasa wananchi
waruhusiwe kuvamia maeneo ya hifadhi, na ametaka zoezi la uwekaji wa mipaka
lifanyike haraka na kwa uwazi.
No comments:
Post a Comment