Baadhi ya washiriki wa Mkutano wa Mwaka wa Maafisa Ustawi wa Jamii wa
Mikoa na Halmashauri zote Tanzania Bara wakimshangilia Waziri Mkuu,
Kassim Majaliwa wakati alipoingia kwenye ukumbi wa Mikutano wa Jakaya
Kikwete jijiniDodoma kufungua mkutano huo, Januari 29, 2019.
Waziri
Mkuu, Kassim Majaliwa akimsikiliza mtoto, Hussein Jailal (kushoto)
wakati alipotoa ushuhuda kwa niaba ya watoto wanaoishi katika mazingira
hatarishi katika Mkutano wa Mwaka wa Maafisa Ustawi wa Jamii wa Mikoa na
Halmashauri zote Tanzania Bara, uliofunguliwa na Waziri Mkuu kwenye
ukumbi wa Jakaya Kikwete jijini Dodoma, Januari 29, 2019.
Waziri
Mkuu, Kassim Majaliwa akifungua Mkutano wa Mwaka wa Maafisa Ustawi wa
Jamii wa Mikoa na Halmashauri zote Tanzania Bara, kwenye Ukumbi wa
Mikutano wa Jakaya Kikwete jijini Dodoma, Januari 29, 2019. (Picha na
Ofisi ya Waziri Mkuu)
Baadhi
ya washiriki wa Mkutano wa Mwaka wa Maafisa Ustawi wa Jamii wa Mikoa na
Halmashauri zote Tanzania Bara wakimsikiliza Waziri Mkuu, Kassim
Majaliwa wakati alipofungua Mkutano huo kwenye ukumbi wa Jakaya Kikwete
jijini Dodoma, Januari 29, 2019.
Waziri
Mkuu, Kassim Majaliwa akimkabidhi cheti cha kuzaliwa mtoto, Faisal
Rashidi Haroun kabla ya kufungua Mkutano wa Mwaka wa Maafisa Ustawi wa
Jamii wa Mikoa na Halmashauri zote Tanzania Bara, Kwenye ukumbi wa
Mikutano wa Jakaya Kikwete jijini Dodoma, Januari 29, 2019. Kushoto ni
Mama Mzazi wa mtoto huyo, Habiba Mohammed.
Waziri
Mkuu, Kassim Majaliwa akimpongeza, Fundi Mkuu wa Karakana ya Vifaa
Visaidizi vya Wenye Ulemavu iliyopo eneo la Sabasaba jijini Dodoma, Bw.
Mwita Marwa Maki baada ya kuvutiwa na baiskeli za magurudumu matatu
zilifungwa mota ambazo zimebuniwa na zinatengenezwa na karakana hiyo.
Tukio hilo lilifanyika kwenye viwanja vya Ukumbi wa Mikutano wa Jakaya
Kikwete jijini Dodoma, kabla ya Waziri Mkuu kufungua Mkutano wa Mwaka wa
Maafisa Ustawi wa Jamii wa Mikoa na Halmashauri zote Tanzania Bara,
Januari 29, 2019. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu)
*Awataka wajiepushe na rushwa wafanye kazi kwa bidii, weledi na uadilifu
WAZIRI
MKUU, Kassim Majaliwa amewataka Maafisa Ustawi wa Jamii katika
Sekretarieti za Mikoa na Mamlaka za Serikali za Mitaa watekeleze
majukumu yao kwa bidii, weledi, uadilifu na wasijihusishe na vitendo vya
rushwa.
Amesema
maafisa hao wanatakiwa watumie mbinu shirikishi ambazo zinahusisha
jamii yenyewe na wataalamu ambao ni watoa huduma ngazi ya jamii
(Community Case Worker) ili kurahisisha utekelezaji wa majukumu yao.
Waziri
Mkuu ametoa maagizo hayo leo (Jumanne, Januari 29, 2019) kwenye Mkutano
wa Mwaka wa Kiutendaji wa Maafisa Ustawi wa Jamii katika Sekretarieti
za Mikoa na Mamlaka za Serikali za Mitaa, jijini Dodoma.
Hata
hivyo, Waziri Mkuu amewataka maafisa hao wahakikishe kwamba haki za
msingi za makundi hayo zinapatikana kwa mujibu wa Sheria, Kanuni na
Miongozo iliyopo katika kutoa huduma ya taaluma yao.
Amesema
taaluma ya Ustawi wa Jamii imepewa dhamana ya kuwa mlinzi wa mtoto,
kumhudumia na kusimamia haki zake, hivyo amewatakawazuie na watokomeze
aina zote za ukatili kwa watoto, wazee na wenye ulemavu.
Waziri
Mkuu amesema jukumu hilo pia linahusisha watoto waliopo kwenye
mazingira hatarishi na wanaoishi na kufanya kazi mitaani, wazee,
wanawake wasio na uwezo na watu wenye ulemavu.
Amesema
pamoja na mafanikio makubwa ambayo Serikali ya Awamu ya Tano imeyapata
ni muhimu wakaendelea kuongeza nguvu na weledi ili kutorudi nyuma katika
kujenga msingi wa kuimarisha ustawi wa makundi maalumu.
Pia,
Waziri Mkuu amewaagiza maafisa hao wakasimamie utekelezaji wa mkakati
wa Mkono kwa Mkono, Familia kwa Familia, Kaya kwa Kaya kupitia huduma
ya kuzuia ukatili ngazi ya familia wenye lengo la kuzuia ukatili ndani
ya familia ili ulete matokeo tarajiwa.
“Tambueni
umuhimu wenu na kwamba jamii inawategemea kutekeleza majukumu yenu
kikamilifu ili kupunguza matatizo ya kijamii kwa wale wenye uhitaji
wakiwemo watoto, watu wenye ulemavu, wazee, familia zenye migogoro na
akina mama wanaonyanyaswa na makundi mengine.”
Katika
hatua nyingine, Waziri Mkuu amewashukuru wadau wa maendeleo kwa namna
wanavyoshirikiana na Serikali katika kusukuma mbele gurudumu la
maendeleo likiwemo suala la uimarishaji wa huduma za ustawi wa jamii
nchini.
Amesema
anatambua mchango mkubwa kutoka kwa shirika la UNICEF, USAID, UN WOMEN,
UNFPA, John Snow Inc, Pact, HelpAge International, World Vision, Save
the Children, Plan International na wengine wote ambao kwa namna moja au
nyingine wameendelea kushirikiana na Serikali kuinua kiwango cha utoaji
huduma za ustawi wa jamii nchini.
“Ninapenda
kuwahakikishia kuwa Serikali ya Awamu ya Tano, inayoongozwa na
Mheshimiwa Dkt. John Magufuli, ipo tayari kufanya kazi pamoja nanyi ili
tuweze kufikia malengo ya maendeleo endelevu ifikapo 2030.”
Kauli
mbiu ya mkutano wa mwaka huu ni “Uadilifu, Weledi na Uwajibikaji katika
Utoaji wa Huduma za Ustawi wa Jamii Ngazi ya Mamlaka za Serikali za
Mitaa ni Nguzo katika kuelekea Uchumi wa Kati wa Viwanda.”
Waziri
Mkuu amepongeza kwa kuanzisha utamaduni huo wa kukutana Watendaji wa
Sekta ya Ustawi wa Jamii kwa kuwa hiko ni kiashiria kwamba kuna
mabadiliko katika utendaji kwa kuzingatia kuwa mkutano huu haujawahi
kufanyika toka mwaka 2006.
Mkutano
huo wa siku tatu unajumuisha Maafisa Ustawi wa Jamii 164 kutoka mikoa
yote Tanzania Bara, wadau wa maendeleo, wawakilishi wa wazee, watoto
waishio katika mazingira hatarishi waliohitimu mafunzo ya VETA pamoja na
watoto waliokuwa wakiishi mitaani ambao kwa sasa wameunda kikundi cha
burudani.
No comments:
Post a Comment