Na Mwandishi wetu
Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania, Samia Suluhu Hassan amepongeza juhudi za Benki ya Maendeleo
ya Kilimo Tanzania (TADB) kwa kusaidia wakulima wadogo nchini hali
inayoongeza uzalishaji na kuwaongezea kipato wakulima hao.
Makamu wa Rais aliyasema hayo wakati
akikabidhi hundi ya mfano yenye thamani ya Shilingi 1.285 Billioni
zilizotolewa na TADB kwa ajili ya miradi ya kilimo cha Alizeti kwa
wakulima 458 waliochini ya vyama vya ushirika (AMCOS) mkoani Singida.
Aliongeza
kuwa wakulima waliopatiwa mkopo huo hawana budi kuutumia katika kuongeza
tija ya uzalishaji ili kuweza kufikia malengo ya mkopo huo ambao
umelenga kuchagiza kusaidia Sekta ya Mbegu za Mafuta nchini ili kutanzua
changamoto za ukosefu wa mafuta hapa nchini.
Makamu wa Rais alitumia fursa hiyo
kuwaagiza viongozi wa ushirika mkoani Singida kusimamia kwa makini mkopo
huo ili utumike kwa malengo yaliyokusudiwa na kuhakikisha unarudi kwa
wakati ili uweze kusaidia wakulima wengine.
“Nawasihi muwe waaminifu kwa kuutumia
mkopo huu vizuri na kuurudisha kwa wakati ili kuwawezesha wakulima
wengine nchini waweze kukopeshwa ili kuchagiza uzalishaji wa mazao ya
kilimo,” aliongeza.
Mapema akizungumza na hadhara mjini Itigi
ambapo mfano wa hundi hiyo ilipotolewa, Mkuu wa Mkoa wa Singida, Dkt.
Rehema Nchimbi alisema kuwa mkopo huo utachagiza hupatikanaji wa
malighafi kwa ajili ya viwanda 144 ya kusindika mafuta ya alizeti
vilivyopo mkoani humo.
“Kwa kipekee tunaishukuru TADB kwa kutoa
mkopo kwa AMCOS hizi saba mkopo ambao umelenga kuongeza tija ya
uzalishaji wa alizeti hali itakayochangia hupatikanaji wa malighafi ya
uhakika ya viwanda vyetu,” alisema.
Kwa upande wake, mwakilishi wa Mkurugenzi
Mtendaji wa Benki hiyo ambaye ni Mkurugenzi wa Mikopo na Biashara,
Augustino Matutu Chacha, alisema kuwa kwa msimu huu wa mwaka 2018/2019,
benki imeidhinisha mikopo ya jumla ya shilingi Bilioni 3.506 kwa miradi
ya Kilimo ya Mkoa wa Singida pekee, ambapo Shilingi 1.285 Billioni
zimetolewa kwa ajili ya miradi ya kilimo cha Alizeti kwa wakulima 458
waliochini ya vyama vya ushirika (AMCOS) na Shilingi 2.221 Billioni kwa
ajili ya ujenzi wa Kiwanda cha kusindika mbegu za mafuta ya alizeti
kitakachojengwa katika Halmashauri ya Wilaya ya Manyoni.
“Tunatambua Alizeti kama mojawapo ya
mazao ya kimkakati kwa uchumi wa taifa letu na hasa kwa wananchi wa
mikoa inayozalisha zao hili kwa wingi ikiwamo mkoa wa Singida. Zao hili
la Alizeti lina fursa kubwa ya kuliingizia taifa fedha za kigeni na pia
ni chanzo cha ajira kwa watu wapatao laki 3 na zaidi,” alisema.
Aliongeza kuwa Mkakati wa benki hiyo ni
kuendelea kusaidia wakulima kuongeza uzalishaji wa Alizeti zenye ubora
kwa ajili ya kusaidia viwanda vya ndani kupata malighafi.
Aliongeza kuwa benki imefanya mazungumzo
na inatarajia kukutana na wadau wasindikaji wa mafuta ya kula kwa lengo
la kuandaa mpango shirikishi wa kutoa huduma za pembejeo na mafunzo ya
kilimo bora kwa wakulima.
“Benki ina mkakati wa kuwaunganisha wakulima na wasindikaji kwa ajili ya kupata huduma nafuu za pembejeo za kilimo,” aliongeza.
Mmoja wa wanufaika wa mkopo huo, amabaye
ni Makamu Mwenyekiti wa Chama Kikuu cha Ushirika, Yahya Ramadhan alisema
kuwa ujio wa Benki ya Kilimo umerudisha ari ya wakulima wa zao la
alizeti mkoani Singida ambao kwa takribani miaka nane wameshindwa kulima
kwa tija kutokana na ukosefu wa fedha kwa ajili ya ununuzi wa pembejeo
za kilimo.
“Kwa hakika mkopo huu umerudisha ari ya
wakulima kwani unatuhakikishia hupatikanaji wa pembejeo na zana za
kilimo kwa wakati hali itakayoongeza uzalishaji wa alizeti,” alisema.
No comments:
Post a Comment