Matokeo chanyA+ online




Friday, February 15, 2019

UJENZI WA RELI YA KISASA DAR ES SALAAM – MOROGORO WASHIKA KASI

Benny Mwaipaja, WFM, Dar es Salaam
NAIBU Waziri wa Fedha na Mipango, Dkt. Ashatu Kijaji amesema kuwa Serikali imedhamiria kwa dhati kukamilisha mradi mkubwa wa Reli kwa kiwango cha Kimataifa (SGR), ambapo tayari kiasi cha zaidi ya shilingi trilioni 2 kimetolewa mpaka sasa kwa ajili ya ujenzi huo.

Dkt. Kijaji ametoa kauli hiyo baada ya kutembelea na kukagua maendeleo ya ujenzi wa Reli hiyo kutoka Dar es Salaam hadi eneo la Soga, umbali wa kilometa 53, na kujionea maendeleo makubwa ya ujenzi wa reli hiyo.

Ameelezea kuridhishwa kwake na kasi ya ujenzi wake na kumpongeza mkandarasi anaye jenga reli hiyo, Kampuni ya Yapi Merkezi, kwa kutekeleza ujenzi huo kwa viwango vya hali ya juu ambapo ameelezwa kuwa, treni ya kwanza kutoka Dar es Salaam kwenda Morogoro inatarajia kuanza safari zake Mwezi Novemba mwaka huu kama kila kitu kitakwenda kama kilivyopangwa.

"Ninampongeza sana Mhe. Rais Dkt. John Pombe Magufuli kwa jitihada zake kubwa na kuamua kwa dhati kutekeleza mradi huu mkubwa na miradi mingine, ukiwemo mradi wa kuzalisha umeme kwa njia ya maporomoko ya maji ya Mto Rufiji, ambayo kukamilika kwake kutachochea uchumi wa viwanda" alisema Dkt. Kijaji

"Tunakwenda kwenye Tanzania ya viwanda, tutakuwa na viwanda kila mahali, tumeanza ujenzi wa mradi wa umeme wa megawat 2,115, viwanda vitazalisha bidhaa ambazo zitahitaji miundombinu ya usafirishaji, reli hii itatumika na tunatarajia ifikapo mwaka 2025, Tanzania itakuwa ni nchi yenye kipato cha kati"  aliongeza Dkt. Kijaji


Kwa upande wake, Meneja wa Mradi wa Ujenzi wa Reli kwa Kiwango cha Kimataifa (SGR), kipande cha  kutoka Dar es Salaam hadi Morogoro, Mhandisi Machibya Masanja, amesema kuwa ujenzi wa reli hiyo umekamilika kwa asilimia 42.


"Mradi wetu unaenda vizuri na kwa wakati, zoezi la ujenzi na utandikaji reli tumeanza katika Jijini la Dar es Salaam umeanza na unaendelea vizuri ambapo ujenzi wa daraja hilo umekamilika kwa asilimia 55 na utandikaji wa reli katika Jiji hili utafikia kilometa 10 mwishoni mwa mwezi Februari" alifafanua Mhandisi Masanja.

na nguvu kubwa imeelekezwa katika ujenzi wa tuta na madaraja, zezi ambalo limefikia asilimia 55 hivi sasa" alifafanua Mhandisi Masanja

Ujenzi wa Reli kwa Kiwango cha Kimataifa kutoka Dar es Salaam, Morogoro, Dodoma hadi Mwanza, na baadae kuunganisha mtandao wake na nchi jirani za Kongo, Uganda, Burundi na Rwanda, unatarajia kugharimu zaidi ya shilingi trilioni 7.

Katika hatua nyingine, Naibu Waziri wa Fedha na Mipango, Dkt. Ashatu Kijaji, amezungumza na wakazi wa eneo la Guluka Kwalala, Gongo la Mboto, waliokuwa wakiendelea na taratibu zao za kulipwa fidia ambapo amewahakikishia kuwa Serikali itaendelea kuwaletea maendeleo.

Baadhi ya wakazi hao, pamoja na kuiomba Wizara ya Ardhi na Makazi iwasaidie kupata viwanja kwa ajili ya kujenga makazi yao baada ya kulipwa fidia kupisha ujenzi wa mradi huo wa Reli ya Kisasa, wamempongeza Mheshimiwa Rais Dkt. John Pombe Magufuli kwa kusimamia ustawi na maendeleo ya nchi na kuahidi kuendelea kumuunga mkono.
 Mwenyekiti wa Bodi ya Shirika la Reli Tanzania (TRC) Prof. John Kondoro (kulia) akitoa maelezo ya utekelezaji wa Ujenzi wa Reli ya Kisasa yenye Kiwango cha Kimataifa (SGR) inayoanzia Dar es Salaam hadi Morogoro kwa awamu ya kwanza kwa Naibu Waziri wa Fedha na Mipango Mhe. Dkt. Ashatu Kijaji (Mb) (katikati), wakati wa ziara ya Naibu Waziri huyo ya  kukagua maendeleo ya mradi huo.
 Meneja wa Kampuni ya Ujenzi wa Reli Kanda ya Afrika Mashariki wa Kampuni ya Yapi Merkezi ya Uturuki Mhandisi  Abdullah Kilic, akititoa maelezo ya maendeleo ya ujenzi wa SGR kutoka Dar es Salaam hadi Morogoro, kwa Naibu Waziri wa Fedha na Mipango Mhe. Dkt. Ashatu Kijaji (Mb) (kulia), alipotembelea Karakana ya kutengeneza vifaa vya ujenzi wa Reli hiyo Jijini Dar es Salaam, wa pili kulia ni Mhandisi wa  mradi wa ujenzi wa  Reli  hiyo anayesimamia kipande cha Dar es Salaam hadi Morogoro, Machibya Masanja .
 Naibu Waziri wa Fedha na Mipango Mhe. Dkt. Ashatu Kijaji (Mb) (wa pili kulia), akifurahia jambo alipokua akiangalia ramani ya mradi wa Reli ya Kisasa yenye Kiwango cha Kimataifa (SGR) inayoanzia Dar es Salaam hadi Morogoro kwa awamu ya kwanza, ambapo tayari takribani cha Sh. Trilioni 2 zimetolewa na Serikali na ujenzi wa kipande hicho umefikia asilimia 42.
 Naibu Waziri wa Fedha na Mipango Mhe. Dkt. Ashatu Kijaji (Mb) akitoa maelekezo kwa Mhandisi wa ujenzi wa Reli ya Kisasa yenye Kiwango cha Kimataifa (SGR) inayoanzia Dar es Salaam hadi Morogoro ambaye ni Meneja wa Kampuni ya Ujenzi wa Reli Kanda ya Afrika Mashariki wa Kampuni ya Yapi Merkezi ya Uturuki Mhandisi Abdullah Kilic (kulia) kuhakikisha anamaliza kazi kwa wakati uliopangwa kwa kuwa fedha za mradi huo zipo.
 Muonekano wa mradi wa Reli ya Kisasa yenye Kiwango cha Kimataifa (SGR) unaotekelezwa na Kampuni ya Yapi Merkezi ya Uturuki katika eneo la Karume Jijini Dar es Salaam.
Naibu Waziri wa Fedha na Mipango Mhe. Dkt. Ashatu Kijaji (Mb) (katikati) akiwa katika Karakana ya kutengeneza mataluma ya Reli ya Kisasa kutoka Dar es Salaam hadi Morogoro eneo la Soga Mkoani Pwani ambapo alimtaka Mkandarasi wa mradi huo kuongeza kasi ya utekelezaji wa mradi kwa kuwa tayari fedha za fidia kwa wakazi waliokuwa katika eneo la ujenzi zimelipwa na Serikali.

(Picha na Peter Haule, Wizara ya Fedha na Mipango)

No comments:

Post a Comment