Matokeo chanyA+ online




Monday, February 18, 2019

MGOGORO WA KYORUBA NA KEBWEHE WAMALIZIKA WILAYANI TARIME

Katibu Mkuu Ofisi ya Rais TAMISEMI Mhandisi Joseph Nyamhanga akiwasihi wananchi wa vijiji vya Kyoruba na Kebwehe wilayani Tarime kuacha mapigano na kuendelea kuishi kwa amani na utulivu. Kulia kwake ni Mkuu wa Wilaya ya Tarime Mhe. Charles Kabeho

Katibu Mkuu Ofisi ya Rais TAMISEMI Mhandisi Joseph Nyamhanga amewasihi wananchi wa vijiji vya Kyoruba na Kebwehe kuacha mapigano kama ilivyoamriwa na Serikali hivi karibuni.
Mhandisi Joseph Nyamhanga amesema kuwa haina haja ya kupigana kwa silaha zozote kwa kuwa mgogoro huo umekwishapatiwa ufumbuzi kwa asilimia mia moja na badala yake wao wenyewe waamue na kukubaliana na maamuzi yaliyotolewa.
Nyamhanga amesema mgogoro huu ni wa muda mrefu na sasa lazima wananchi wote wafuate sharia zilizotumika kuutatua ambazo ni ramani iliyopo, kamati za mgogoro na sio kutumia mishale.
Aidha, wananchi walipoulizwa walisema wamekubali na watafuata sheria iliyowekwa na wataendelea kuishi kwa amani.
Mkuu wa Wilaya Tarime Mhe. Charles Kabeho amesema Mhe. Waziri Mkuu wa Tanzania Kassim Majaliwa alifika katika vijiji hivyo na kusuluhisha mgogoro huo na maamuzi ya mipaka iliwekwa kwa mujibu wa ramani na wananchi wa kila kijiji wanapaswa kufuata mipaka hiyo.
Naye mzee Rubeni mwenyeketi wa kijiji cha Kyoruba alisema mgogoro huo ni wa kihistoria ambapo baada ya kuhamishiwa katika vijiji mwaka 1974 uliibuka tena tarehe 2 Februari, mwaka 1981 na ulisuluhishwa na Mkuu wa wilaya wa wakati huo (DDC) na kwisha lakini uliibuka tena mwezi Julai, mwaka 2017 hivyo kwa maoni yake kwa wale ambao hawaridhiki na matokeo ya maamuzi ni vema wakafuata utaratibu wa kisheria bila ya kupigana.
Mapigano hayo yaliyotokea wilayani Tarime yanahusisha wanyabasi wa kijiji cha Kebwehe waliopigana dhidi ya wakira wa kijiji cha Kyoruba mgogoro ambao uliilazimu Serikali kuingilia kati na kurudisha hali ya amani na utulivu.

No comments:

Post a Comment