Waziri wa Nishati,
Dkt Medard Kalemani (kushoto) akikagua mitambo ya kisasa ya kuchenjulia madini
tani 10 kwa saa ambayo ipo katika Kijiji cha Shenda wilayani Mbogwe na kuahidi
kupeleka umeme hivi karibuni.
Na
Teresia Mhagama,
Wachimbaji wadogo
katika machimbo ya Nyakafuru yaliyo katika Kijiji cha Nyakafuru wilayani Mbogwe
wameonesha kufurahishwa na ahadi ya Waziri wa Nishati, Dkt Medard Kalemani ya
kufikisha umeme katika machimbo hayo ndani ya siku kumi.
Ahadi hiyo aliitoa
jana mara baada ya kufanya ziara ya kikazi wilayani Mbogwe mkoani Geita ambapo
akiwa katika machimbo hayo, wachimbaji hao walilalamika kuhusu gharama kubwa
wanazotumia katika kununua mafuta ya kuendesha mitambo mbalimbali ikiwemo ya
kuchenjulia ya madini.
Kwa nyakati tofauti
walieleza kuwa, mchimbaji mmoja anaweza kutumia zaidi ya shilingi milioni 1.5
kwa ajili ya mafuta ya kuendeshea mitambo suala ambalo linawafanya kutopata
faida inayostahiki katika shughuli zao.
Kutokana na hilo, Dkt
Kalemani alisema kuwa, “kutoka umeme unapoishia hadi hapa ni kilometa 1.5 tu,
na hapa kuna wachimbaji wadogo zaidi ya Elfu Nne na mashine za kuchenjulia
madini zaidi ya 200, hivyo nakuagiza Meneja wa TANESCO kuleta umeme hapa ndani
ya siku Kumi na pia muwafungie transfoma itakayohudumia eneo hili,”.
Waziri wa Nishati pia
alitembelea mitambo ya kisasa ya kuchenjulia madini tani 10 kwa saa ambayo ipo
katika Kijiji cha Shenda wilayani Mbogwe ambayo nayo uendeshaji wake unatumia
mafuta badala ya umeme.
Baada ya kukagua
mitambo hiyo, Dkt. Kalemani alimwagiza Meneja wa TANESCO wilayani Mbogwe
kuhakikisha kuwa, ifikapo tarehe 25 mwezi huu awe ameshafikisha umeme katika eneo hilo.
Akiwa wilayani
Mbogwe, Dkt Kalemani pia alikagua kazi ya usambazaji umeme katika Kijiji cha
Bulugala na kukuta nguzo zimesimikwa huku nyaya zikiwa bado hazijavutwa hivyo
alimuagiza mkandarasi wa umeme (kampuni ya Whitecity
Guangdong JV) kuwasha umeme katika Kijiji hicho kabla ya tarehe 5 mwezi ujao.
Katika ziara yake
wilayani Mbogwe pia aliwasha umeme katika Kijiji cha Kasosobe, Kitongoji
cha Mkolani ambapo awali alielezwa kuwa umeme huo bado haujafika katika maeneo
muhimu ya kijamii kama Shule na Nyumba za ibada pamoja na vitongoji vingine vya
Kijiji hicho.
Dkt Kalemani
alimuagiza mkandarasi wa umeme kufikisha umeme katika vitongoji vyote vya
Kijiji hicho ikiwemo ikiwemo Shule, na Nyumba za Ibada ndani ya siku 14.
Vilevile Dkt.Kalemani
alifanya ziara katika wilaya ya Bukombe mkoani Geita ambapo aliwasha rasmi
umeme katika Kijiji cha Ryobaika, kilicho katika Kata ya Uyovu na kutoa wasaa kwa
wananchi kulipia huduma ya umeme mapema na wataalam wa TANESCO pamoja na
mkandarasi kutokataa malipo ya wananchi kwa kisingizio chochote kile. |
No comments:
Post a Comment