WazirI
Mkuu, Kassim Majaliwa akiwa ameshika kipande cha dhahabu mali
Mchimbaji Mdogo Bw. Christopher Thadeo (kushoto) chenye uzito wa gramu
141.01 kikiwa na thamani ya sh. 13,537, 439/= wakati alipofungua Soko
la Dhahabu mjini Geita, Machi 17, 2019. Katikati ni Mkuu wa Mkoa wa
Geita, Mhandisi Robert Gabriel. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu)
WAZIRI MKUU AWATAHADHARISHA WADAU WA MADINI
Waziri
Mkuu, Kassim Majaliwa ametoa tahadhari kwa wadau wote wa madini kuwa
atakayekamatwa anatorosha madini, atachukuliwa hatua za kisheria ikiwemo
utaifishaji wa madini atakayokuwa akiyatorosha.
Pia
amewataka viongozi na watendaji wote wa Serikali wasimamie kwa weledi,
uaminifu na uadilifu, sheria, kanuni na miongozo kuhusu sekta ya madini
kwa lengo la kudhibiti utoroshwaji wa madini hususan dhahabu kwenda nje
ya nchi.
Waziri
Mkuu ametoa tahadhari hiyo leo (Jumapili, Machi 17, 2019) wakati
akifungua soko la madini la Mkoa wa Geita. Ufunguzi wa soko hilo ni
utekelezaji wa agizo la Rais Dkt. John Magufuli alilotoa tarehe
22.01.2019 la kuitaka mikoa yote ianzishe masoko ya madini.
Waziri
Mkuu ameitakaWizara ya Madini, Tume ya Madini, Serikali ya Mkoa, Idara
na Taasisi nyingine za Serikali zinazohusika na maendeleo ya sekta ya
madini waheshimu mipaka ya majukumu yao ili waweze kulisimamia vizuri
soko hilo na kufanya kazi kama ilivyokusudiwa.
“Wizara
ya Madini ishirikiane na vyama na mashirikisho ya wachimbaji na
wafanyabiashara wa madini kuandaa mpango kazi mahsusi kwa ajili ya
utekelezaji wa majukumu ya soko hili ili lisigeuke kuwa kikwazo kipya
kwa wachimbaji na wafanyabishara wa madini”
Waziri
Mkuu ameviagizaVyombo vya Ulinzi na Usalama vihakishe soko hilo
linapata ulinzi wa kutosha muda wote ili watendaji, mali zitakazokuwemo,
vitendea kazi na miundombinu yote iwe salama muda wote. “Mkuu wa mkoa
na Wakuu wa vyombo vya ulinzi na usalama, nawaagiza hakikisheni Suala
hili mnaliandalia utaratibu haraka iwezekanavyo”.
Pia,
Waziri Mkuu ametumia fursa hiyo kuielekeza mikoa mingine yenye kiwango
kikubwa cha uzalishaji wa madini hususan ya metali na vito iharakishe
uanzishwaji wa masoko ya madini sanjari na miundombinu yote muhimu ili
masoko hayo yaanze kufanya kazi kabla ya kwisha kwa mwaka huu wa fedha
2018/2019.
Waziri
Mkuu, Kassim Majaliwa na Mkuu wa Mkoa wa Geita, Mhandisi Robert
Gabriel (kulia) wakifurahia baada ya Waziri Mkuu kufungua Soko la
Dhahabu mjini Geita, Machi 17, 2017. Kushoto ni Mwenyekiti wa CCM wa
Mkoa wa Geita, Alhaji Said Kalidushi. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu)
Amesema
anaamini kwamba, usimamizi mzuri wa soko hilo na masoko mengine ya
madini yanayoendelea kuanzishwa nchini utaimarisha makusanyo ya kodi za
Serikali na kuongeza mchango wa sekta hiyo kwenye pato la Taifa. Vilevile,
amesema wafanyabiashara wa madini, hususan kutoka nje ya nchi
wataongezeka kwa sababu tutakuwa tumewaepusha na matapeli na vikwazo
vingine vya kibiashara. “Uimara wa soko hili pia, utaboresha uhusiano
kati ya wadau wa biashara ya madini na Serikali”.
Waziri
Mkuu amesema Serikali imefuta baadhi ya tozo na kodi ambazo zilikuwa
kero kwa wafanyabiashara wa madini hususan wachimbaji wadogo. Miongoni
mwa tozo zilizofutwa ni Kodi ya Ongezeko la Thamani (VAT) na Kodi ya
Zuio ya asilimia tano ya mwisho (final withholding tax) inayotozwa
kwenye bei ya kuuzia madini ya aina zote.
Amesema
baada ya kufutwa kwa kodi na tozo hizo Serikali inatarajia kuwa
utoroshwaji wa madini utapungua, pia kutasaidia wachimbaji wadogo
kutambuliwa kupitia uanzishwaji wa masoko ya madini; kupunguza gharama
za uendeshaji wa shughuli za wachimbaji wadogo na kuongeza wigo wa
mapato kwa nchi.
“Nitoe
wito kwa wachimbaji wote wadogo kwamba endeleeni kushirikiana na
mamlaka mbalimbali za Serikali katika kutekeleza majukumu yenu kwa
kufuata taratibu, sheria, kanuni na miongozo mbalimbali inayotolewa na
Serikali”. AmesemaSerikali inachukua hatua zote hizo si
kwa lengo jingine bali kuziba mianya ambayo imekuwa chanzo cha
utoroshwaji wa madini, ukwepaji kodi, na hivyo, kusababisha biashara
nzima ya madini kufanyika kiholela katika maeneo mengi ya nchi yetu.
Waziri
Mkuu amesema Serikali imejipanga vema katika kuhakikisha vikwazo vyote
vilivyomo katika mnyororo wa biashara ya madini vinaondolewa kwa lengo
la kukuza sekta hiyo na kuwanufaisha wananchi na Taifa kwa ujumla. Amesema
Serikali imeamua kutoa mwelekeo mpya katika usimamizi na maendeleo ya
sekta ya madini. “Utekelezaji wa dhamira hii unakwenda sambamba na
kuweka mazingira mazuri na miundombinu itakayowezesha kuimarika kwa
sekta ya madini nchini”.
Waziri
Mkuu, Kassim Majaliwa akipongezwa na Waziri wa Madini, Dotto Biteko
baada ya kufungua Soko la Dhahabu mjini Geita, Machi 17, 2019. Kulia
ni Mkuu wa Mkoa wa Geita, Mhandisi Robert Gabriel na kushoto ni
Mwenyekiti wa CCM wa mkoa wa Geita, Alhaji Said Kalidushi. (Picha na
Ofisi ya Waziri Mkuu).
Kadhalika,
Waziri Mkuu amesema wachimbaji wadogo wamekuwa wakilalamikia ukosefu wa
masoko ya uhakika ya madini ambao umekuwa sababu ya utoroshwaji madini,
hivyo kuanzishwa kwa soko hili kunawahakikishia wachimbaji wadogo
masoko na kukua kwa kipato kutokana na shughuli za madini.
Waziri
Mkuu amesema kwa muda mrefu sasa, kumekuwepo na malalamiko ya
kudhulumiwa au kupunjwa kutoka kwa baadhi ya wachimbaji wadogo, vitendo
hivyo vimekuwa vikiwahusisha wafanyabiashara wa madini wasiokuwa
waaminifu. “Ndugu wachimbaji wadogo, soko hili linakwenda
kuwa mwarobaini wa tatizo hilo kwani litasheheni vifaa vya kupimia uzito
na ubora wa madini kabla hayajauzwa. Naielekeza Tume ya Madini,
isimamie ipasavyo vifaa na taratibu za vipimo kwenye soko hili na
kuhakikisha hakuna manung’uniko juu ya utendaji kazi wa vifaa hivyo”.
Waziri
Mkuu ameongeza kuwa soko hilo pia litaondoa uwezekano wa wanunuzi wa
madini kuibiwa na wajanja wachache wanaojifanya kuwa na madini wakati
hawana. “Nawasihi wanunuzi wa madini kulitumia soko hili kikamilifu ili
kuepuka udanganyifu na matapeli”.
Pia
ameiagiza Tume ya Madini kuratibu bei za madini ndani ya soko hilo na
ihakikishe mchimbaji anapata stahiki zake, Serikali inapata mapato yake
na mfanyabiashara naye ananufaika. “Tunaimani kabisa tatizo la
kudhulumiana na kupunjana linaenda kwisha kabisa. Na kwa kweli ikitokea
mtu amepunjwa, atakuwa amejitakia mwenyewe”.
“Ndani
ya soko hili kutakuwa na huduma zote muhimu kwa mfanyabiashara ikiwemo
huduma za Tume ya Madini, Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), Mabenki na
nyinginezo, hivyo kuokoa muda na gharama nyingine katika kuendesha
biashara hii ya madini.
Amesema
soko hilo litasaidia sana katika ukusanyaji wa mapato ya Serikali na
takwimu za biashara ya madini. Hivyo, niwasihi wachimbaji wa madini
kulitumia soko hili na kuacha vitendo vya utoroshaji wa madini. Serikali
kwa upande wake, haitomvumilia mtu yeyote yule atakaye jihusisha na
utoroshaji wa madini.
Ufunguzi
huo umehudhuriwa na Waziri wa Madini, Doto Biteko, Waziri wa Nishati
Dkt. Medard Kalemani, Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Costantine
Kanyasu, Katibu Mkuu wa Wizara ya Madini, Profesa Simon Msanjila,
Wabunge wa mkoa wa Geita, Mkuu wa Mkoa wa Geita, Mhandisi Robertt
Gabriel, wakuu wa mikoa jirani na maafisa wa Serikali.
No comments:
Post a Comment