Waziri
wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Prof.
Palamagamba Kabudi (Mb.) amekutana na kufanya mazungumzo na Balozi wa
Umoja wa Falme za Kiarabu (UAE) Mhe. Khalifa Abdulrahman Mohamed
Al-Marzooqi alipomtembelea katika ofisi ndogo za Wizara zilizopo Jijini
Dar es Salaam tarehe 20 Machi 2019. Mazungumzo hayo yalijikita katika
kujadili masuala mbalimbali ya namna ya kudumisha na kukuza uhusiano
baina ya Tanzania na UAE.
Waziri
Mhe. Kabudi akimsikiliza Balozi wa Falme za Kiarabu nchini Mhe.Khalifa
Abdulrahman Mohamed Al-Marzooqi walipokutana kwa Mazungumzo Jijini Dar
es Salaam
Mazungumzo yakiendelea.
Mhe.
Prof. Palamagamba John Kabudi (Mb.), Waziri wa Mambo ya Nje na
Ushirikiano wa Afrika Mashariki amekutana na kufanya mazungumzo na Mhe.
Khalifa Abdulrahman Al-Marzooqi, Balozi wa Umoja wa Falme za Kiarabu
(UAE) nchini.
Katika
mazungumzo yao yaliyofanyika tarehe 20 Machi 2019 kwenye ofisi ndogo za
Wizara zilizopo Dar es Salaam, Prof. Kabudi alimshukuru Mhe. Balozi
Al-Marzooqi kwa kupata fursa ya kukutana naye na kwamba, Tanzania
inathamini mahusiano na ushirikiano wa kidiplomasia uliopo kati ya
Tanzania na Umoja wa Falme za Kiarabu.
Aidha,
alimweleza Balozi huyo kuwa, Wizara chini ya uongozi wake itaendelea na
jitihada za kuhakikisha kuwa, mahusiano yaliyopo kati ya nchi hizi
mbili yanaimarishwa.
Kwa
upande wake, Mhe. Balozi Al-Marzooqi ametumia mazungumzo hayo
kumpongeza Mhe. Prof. Kabudi kwa kuteuliwa kuwa Waziri wa Mambo ya Nje
na Ushirikiano wa Afrika Mashariki na kumhakikishia ushirikiano wa
karibu ili kuhakikisha mahusiano yaliyopo yanaimarishwa.
Mhe.
Balozi Al-Marzooqi aliongeza kuwa, Umoja wa Falme za Kiarabu una nia ya
kuimarisha mahusiano yaliyopo na umepanga kufungua Ubalozi mdogo
(Consulate General) Zanzibar. Pia, Mhe. Balozi alimuarifu Mhe. Waziri
kwamba ana mpango wa kuutembelea Mkoa wa Dodoma ili pamoja na masuala
mengine, kujionea eneo walilopewa na Serikali kwa ajili ya ujenzi wa
ofisi za ubalozi na makazi kwa lengo la kujipanga kuliendeleza.
Kadhalika,
Prof. Kabudi na Mhe. Balozi Al-Marzooqi wamekubaliana kuendeleza
ushirikiano kwenye maeneo ya uwekezaji ambapo Balozi huyo ameonesha nia
ya kuendelea kushawishi wawekezaji kutoka nchini kwake kuja kuwekeza
nchini hususan kwenye sekta za utalii, hoteli, viwanda na utoaji wa
huduma. Pia ameahidi kuwashawishi wafanyabishara wakubwa na wadogo
kutoka UAE kuja nchini ili kujionea fursa za biashara zilizopo.
Prof.
Kabudi amemuhakikishia Balozi Al-Marzooqi kuwa, Tanzania ni eneo bora
la uwekezaji na biashara na kwamba, Wizara ya Mambo ya Nje na
Ushirikiano wa Afrika Mashariki kwa kushirikiana na Wizara zingine
zitaendelea kuweka mazingira mazuri ya kupokea wawekezaji na
wafanyabiashara kutoka maeneo yote duniani.
Imetolewa na:
Kitengo cha Mawasiliano ya Serikali,
Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki,
Dodoma.
20 Machi 2019
No comments:
Post a Comment