Naibu
Waziri, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora,
Mhe. Dkt. Mary Mwanjelwa (Mb) amewataka waajiri serikalini kuzingatia
kigezo cha ubunifu wanapotekeleza zoezi la ujumuishwaji wa masuala ya
kijinsia sehemu za kazi ili kuleta matokeo chanya na yenye tija katika
utekelezaji wa majukumu yao ya kila siku.
Mhe.
Dkt. Mwanjelwa (Mb) amesema hayo mapema leo, alipokuwa akifungua kikao
kazi cha siku mbili kinachohusu ujumuishwaji wa masuala ya kijinsia
mahala pa kazi kilichofanyika mjini Morogoro.
Mhe.
Dkt. Mwanjelwa amesema kuwa, endapo waajiri watazingatia kigezo cha
ubunifu na kuacha kufanya kazi kwa mazoea serikali itapata watendaji
kazi bora watakaoleta matokeo chanya katika maendeleo ya nchi kwani
watafanya kazi kwa uadilifu na kwa kuzingatia sheria, kanuni na taratibu
za utumishi.
Mhe.
Dkt. Mwanjelwa (Mb) ameongeza kuwa, ubunifu katika utendaji kazi
utawezesha watumishi kuondokana na mitazamo hasi juu ya dhana ya jinsia
ya kike kutegemea kupata kazi kutokana na jinsi yao badala yake watambue
kuwa vigezo na sifa za kiushindani ndiyo vinazingatiwa.
“Tunapodai
haki zetu kama wanawake tuwe na hoja zenye mashiko zitakazoendana na
sifa na vigezo husika, tusiseme kuwa sisi ni wanawake hivyo tupewe
nafasi” amesema Dkt. Mwanjelwa.
Dkt.
Mwanjelwa amewataka waajiri kuzingatia vigezo vya ubunifu wanapoajiri
wanawake na kutenga bajeti kwa ajili ya ujumuishwaji wa masuala ya
jinsia mahala pa kazi ili kuboresha utendaji kazi.
Aidha,
Dkt. Mwanjelwa amewaagiza watendaji katika Idara za Utawala na
Rasilimaliwatu kuwa kioo katika utekelezaji wa masuala ya kijinsia
mahala pa kazi ili kuepuka vitendo vya unyanyasaji wa kijinsia, rushwa
ya ngono, ubaguzi wa aina yoyote, upendeleo, ubadhilifu wa mali za umma
na uvujishaji wa siri za serikali.
Naye,
Mkurugenzi wa Idara ya Uendelezaji Sera, Ofisi ya Rais , Menejimenti ya
Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Bi. Agnes Meena amesema kuwa, ofisi
yake kama mratibu wa masuala ya anuai za jamii imeona umuhimu wa kuandaa
kikao cha ujumuishaji wa masuala ya kijinsia sehemu za kazi kwa
kushirikiana na wakurugenzi wa Idara ya Utawala na Usimamizi
Rasilimaliwatu kwa kuwa wao ndio wahusika katika usimamizi wa mipango ya
rasilimaliwatu na masuala yote ya kiutumishi.
Bi.
Meena amesema kuwa, kikao hicho kimefanyika kutokana na kuwapo kwa
mwitikio wa wastani katika utekelezaji wa masuala ya jinsia sehemu za
kazi unaosababishwa na kukosekana kwa utayari wa taasisi , mipango
katika taasisi, mitazamo hasi, unyanyapaa na ufinyu wa bajeji.
Akizungumza
kwa niaba ya washiriki wa kikao hicho, Mkurugenzi Msaidizi Idara ya
Utawala, Mahakama ya Tanzania, Bi. Wanyenda Kutta amekiri kuwapo kwa
changamoto katika utekelezaji wa masuala ya kijinsia mahali pa kazi na
kuahidi kuwa kikao hicho kitatoa maazimio yatakayoiwezesha serikali
kutekeleza masuala ya kijinsia ipasavyo mahali pa kazi.
Lengo
la kikao hicho ni kujadili fursa za masuala ya kijinsia katika utumishi
wa umma na kuweka mikakati itakayofanikisha Usawa wa Jinsia kwa
Maendeleo Endelevu.
Naibu
Waziri, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora,
Mhe. Dkt. Mary Mwanjelwa (Mb) akifungua kikao kuhusu ujumuishwaji wa
masuala ya kijinsia mahali pa kazi kilichofanyika katika ukumbi wa
Glonency Hotel, mjini Morogoro.
Mkurugenzi
Msaidizi Idara wa Utawala, Mahakama ya Tanzania, Bi. Wanyenda Kutta
akitoa neno la shukrani katika kikao kuhusu ujumuishwaji wa masuala ya
kijinsia mahali pa kazi kilichofanyika kwenye ukumbi wa Glonency Hotel,
mjini Morogoro.
Mkurugenzi
Idara ya Uendelezaji Sera, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa
Umma na Utawala Bora , Bi. Agnes Meena akimkaribisha Naibu Waziri, Ofisi
ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Dkt.
Mary Mwanjelwa (Mb) (hayupo pichani) kufungua kikao kuhusu Ujumuishwaji
wa masuala ya ya kijinsia mahali pa kazi kilichofanyika katika ukumbi wa Glonency Hotel, mjini Morogoro.
Mkurugenzi
Msaidizi, Sehemu ya Anuai za Jamii, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya
Utumishi wa Umma na Utawala Bora ,Bi. Leila Mavika akiwasilisha mada
katika kikao cha ujumuishwaji wa masuala ya kijinsia mahali pa kazi
kilichofanyika katika ukumbi wa Glonency Hotel, mjini Morogoro.
Baadhi
ya washiriki wa kikao kuhusu ujumuishwaji wa masuala ya Kijinsia mahali
pa kazi kutoka katika Wizara na Taasisi za serikali wakimsikiliza Naibu
Waziri, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora,
Mhe. Dkt. Mary Mwanjelwa (Mb) (hayupo pichani) wakati akifungua kikao
hicho kilichofanyika ukumbi wa Glonency Hotel, mjini Morogoro.
Naibu
Waziri, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora,
Mhe. Dkt. Mary Mwanjelwa (Mb) akiwa katika picha ya pamoja na washiriki
wa kikao kuhusu ujumuishwaji wa masuala ya kijinsia mahali pa kazi
kilichofanyika katika ukumbi wa Glonency Hotel, mjini Morogoro.
No comments:
Post a Comment