Rais
wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli akizungumza
na Wachezaji wa timu ya Taifa ya Mpira wa Miguu Taifa Stars ambao
walifika Ikulu mara baada ya kufanikiwa kufuzu kushiriki Fainali za
michuano ya Mataifa ya Africa AFCON baada ya kuifunga Timu ya Taifa ya
Uganda The Cranes magoli 3-0 jijini Dar es Salaam.
Wachezaji
wa timu ya Taifa ya Mpira wa Miguu Taifa Stars waliopo upande wa kulia
pamoja na viongozi wengine wakionesha ishara ya magoli matatu ambayo
timu ya Taifa iliupata siku ya jumapili zidi ya Timu ya Taifa ya Uganda
The Craines na kufanikiwa kufuzu kucheza Fainali za michuano ya Mataifa
ya Africa AFCON nchini Misri baadae mwaka huu.
Sehemu
ya Wachezaji wa wa timu ya Taifa ya Mpira wa Miguu Taifa Stars waliopo
upande wa kulia pamoja na viongozi wengine wakiwa katika ukumbi wa
Mkutano Ikulu jijini Dar es Salaam.
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli
akisalimiana na mchezaji wa Timu ya Taifa Taifa Stars Shabani Iddi
Chilunda mara baada ya kumaliza kuzungumza na wachezaji hao.
Mwenyekiti
wa Kamati ya Uhamasishaji ya Timu ya Taifa Stars ambaye ni Mkuu wa Mkoa
wa Dar es Salaam Paul Makonda wanne kutoka kushoto waliokaa pamoja na
wachezaji Wachezaji wa wa timu ya Taifa ya Mpira wa Miguu Taifa Stars
waliopo upande wa kulia pamoja na viongozi wengine wakiwa katika ukumbi
wa Mkutano Ikulu jijini Dar es Salaam.
Bondia
wa Ngumi za kulipwa Hassan Mwakinyo kutoka Tanga akijitambulisha Ikulu
jijini Dar es Salaam mara baada ya kupewa nafasi ya kuzungumza kuhusiana
na mafanikio yake makubwa aliyoyapata katika ngumi za kulipwa pamoja na
kuitangaza nchi kimataifa.
Mfungaji wa goli la pili la Taifa Stars zidi ya Uganda Erasto Nyoni akijitambulisha Ikulu jijini Dar es Salaam.
Bondia wa Ngumi za kulipwa Hassan Mwakinyo kutoka Tanga akizungumza mara baada ya kupewa nafasi Ikulu jijini Dar es Salaam.
Rais
wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli akipiga
makofi wakati Bondia Hassan Mwakinyo alipokuwa akizungumza.
Mchezaji
wa Timu ya Taifa ya Tanzania Taifa Stars Jonas Mkude akifurahia jambo
wakati wakiwa Ikulu jijini Dar es Salaam pamoja na wachezaji wenzake.
Rais
wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli
akisalimiana na Kocha wa Taifa Stars Emanuel Amunike mara baada ya
kumaliza kuzungumza na wachezaji wa Timu ya Taifa.
Rais
wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli
akimsikiliza Mchezaji wa zamani wa Timu ya Taifa ya Tanzania Taifa
Stars Peter Tino ambaye alifunga goli moja lililoipeleka Tanzania kwa
mara ya kwanza katika michuano ya AFCON mwaka 1980 iliyofanyika nchini
Nigeria. Pia Rais Dkt. Magufuli amemsaidia mchezaji huyo wa zamani kiasi
cha Shilingi milioni tano.
Rais
wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli akiwa
anapata chakula cha mchana na viongozi pamoja na Wachezaji wa timu ya
Taifa ya Tanzania Taifa Stars Ikulu jijini Dar es Salaam.
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli akiwa
na Makamu wa Rais Samia Suluhu Hassan, Waziri Mkuu Kassim Majaliwa,
Naibu Waziri wa Habari Utamaduni Sanaa na Michezo Juliana Shonza, Rais
wa TFF Walace Karia, Bondia wa Ngumi za kulipwa Hassan Mwakinyo wapili
kutoka kushoto katika picha ya pamoja na Wachezaji wa timu ya Taifa ya
Mpira wa Miguu Taifa Stars ambao walifika Ikulu mara baada ya kufanikiwa
kufuzu kushiriki Fainali za michuano ya Mataifa ya Africa AFCON baada
ya kuifunga Timu ya Taifa ya Uganda The Cranes magoli 3-0 jijini Dar es
Salaam. PICHA NA IKULU
======= ========= ========= ==========
Rais
wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli leo
tarehe 25 Machi, 2019 amekutana na kuwapongeza wachezaji wa Timu ya
Taifa ya Tanzania (Taifa Stars) kwa kufanikiwa kufuzu kucheza fainali za
michuano ya soka Barani Afrika kwa mwaka 2019 (AFCON-2019) na pia
amempongeza bondia Hassan Mwakinyo ambaye juzi alishinda pambano lake
dhidi ya bondia Sergio Gonzalez wa Argentina lililofanyika Jijini
Nairobi nchini Kenya.
Hafla
ya kuwapongeza wanamichezo hao imefanyika Ikulu Jijini Dar es Salaam na
kuhudhuriwa na Makamu wa Rais Mhe. Samia Suluhu Hassan, Waziri Mkuu
Mhe. Kassim Majaliwa Majaliwa, Viongozi wa Shirikisho la Mpira wa Miguu
nchini (TFF), Kamisheni ya Ngumi Tanzania (TPBRC) na Kamati ya Ushindi
ya Taifa Stars iliyoongozwa na Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam Mhe. Paul
Makonda.
Akizungumza
katika hafla hiyo Mhe. Rais Magufuli ameelezea kufurahishwa kwake na
matokeo ya mchezo wa jana ambapo Taifa Stars iliifunga Timu ya Taifa ya
Uganda (The Cranes) katika uwanja wa Taifa Jijini Dar es Salaam kwa
magoli 3-0 na ameahidi kuwa Serikali itaendelea kuunga mkono juhudi za
wanamichezo wote kwa kuwa mafanikio yao yanaliletea Taifa sifa na
heshima na pia yanatangaza fursa mbalimbali ikiwemo utalii, biashara na
uwekezaji.
Mhe.
Rais Magufuli amewapongeza wachezaji wa Taifa Stars, viongozi wa TFF,
Kamati ya Ushindi ya Taifa Stars na Watanzania wote kwa kuungana pamoja
kuishangilia timu yao katika mchezo wa jana bila kujali tofauti zao za
kidini, itikadi za kisiasa, makabila na kanda wanazotoka.
“Kwa
kweli jana nilifurahi sana jinsi mlivyokuwa mnacheza na jinsi
mlivyofunga magoli, Watanzania wanataka furaha, sio kufungwafungwa kama
mlivyofungwa kule Lesotho, ile iliniuma sana hadi nilipanga kuwa sitaita
tena timu kuja hapa Ikulu, lakini sasa safi.
Nataka
niwahakikishie Serikali ipo na nyinyi na ni matarajio yangu kuwa
mtajiandaa vizuri ili mkafanye vizuri katika michuano ya AFCON huko
Misri, sasa vita imeanza” amesema Mhe. Rais Magufuli.
Mhe.
Rais Magufuli ametoa changamoto kwa wadau wote wa michezo kuhakikisha
wanasimamia uboreshaji wa miundombinu ya michezo, wanajipanga vizuri kwa
michezo mbalimbali ya kuiwakilisha nchi, wanarekebisha dosari zote
zilizosababisha kusuasua kwa Tanzania katika michezo ya kimataifa na
ameipongeza TFF kwa kufanikiwa kurejesha mgao wa fedha za maendeleo
kutoka Shirikisho la Soka Duniani (FIFA).
Aidha,
ameiagiza Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo kufuatilia
uendeshaji wa uwanja wa Taifa ili kujiridhisha juu ya mapato na matumizi
ya fedha za uwanja huo pamoja na kuangalia ubora wake kutokana na
kuwepo kwa taarifa kuwa maeneo yanayoharibika hayafanyiwi matengenezo
inavyopaswa.
Mhe.
Rais Magufuli amempongeza bondia Hassan Mwakinyo kwa ushindi alioupata
hapo juzi baada ya kumpiga kwa knockout bondia Sergio Gonzalez wa
Argentina katika pambano lisilo la ubingwa lilifanyika Jijini Nairobi
nchini Kenya, pamoja na mapambano mengine ambayo alishinda na amemtaka
kuendelea kufanya vizuri katika mapambano mengine ili kuipatia sifa
Tanzania.
“Nafahamu
kuwa unazo changamoto nyingi ambazo hukusema hapa, lakini nakupongeza
sana, juzi umemtandika yule jamaa mpaka akakaa chini na huwa nakuona
unavyofanya mazoezi makali kwa kutumia matairi, wewe ni kijana safi
sana” amesema Mhe. Rais Magufuli.
Mhe.
Rais Magufuli ameipongeza kampuni ya Serengeti Breweries Limited ambayo
ni wadhamini wa timu ya Taifa Stars na SportPesa ambao ni wadhamini wa
bondia Hassan Mwakinyo kwa mchango wao mkubwa wa kuendeleza michezo.
Katika
hafla hiyo Mhe. Rais Magufuli amekubali maombi yaliyotolewa na Wizara
ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo ya kusaidiwa maandalizi ya
michuano ya AFCON kwa vijana wa chini ya miaka 17 iliyopangwa kuanza
tarehe 14 Aprili, 2019 hadi tarehe 28 Aprili, 2019 Jijini Dar es Salaam
huku Tanzania ikiwakilishwa na timu ya Serengeti Boys, ambapo amesema
Serikali itatoa shilingi Bilioni 1 kusaidia maandalizi hayo.
Halikadhalika
Mhe. Rais Magufuli ametoa zawadi ya kiwanja kimoja cha kujenga nyumba
Jijini Dodoma kwa kwa kila mchezaji wa Taifa Stars, Bondia Hassan
Mwakinyo, mchezaji wa zamani na Nahodha wa Taifa Stars Leodgar Tenga na
mchezaji wa zamani na mfungaji wa bao lililoiwezesha Tanzania kucheza
robo fainali ya AFCON mwaka 1980 Peter Tino ambaye pia amezawadiwa
shilingi Milioni 5.
Kwa
upande wao wachezaji wa Taifa Stars ambao wameongozwa na Nahodha
Msaidizi Himid Mao na bondia Hassan Mwakinyo wamemshukuru Mhe. Rais
Magufuli na Serikali kwa ushirikiano mkubwa walioupata hadi kufikia
mafanikio hayo na wamemuahidi kuendelea kufanya vizuri katika michezo
inayofuata.
Rais
wa TFF Bw. Wallace Karia na Mwenyekiti wa Baraza la Michezo la Taifa
(BMT) Bw. Leodgar Tenga wamesema baada ya kufuzu kucheza fainali za
AFCON sasa Taifa Stars inaelekeza nguvu zake kujiandaa na michuano hiyo
mikubwa Barani Afrika na pia wameelezea matumaini makubwa ya Tanzania
kufanya vizuri katika michuano ya AFCON kwa vijana wa chini ya miaka 17
ambapo Tanzania itawakilishwa na timu ya Serengeti Boys, michuano ya
AFCON kwa wanawake ambapo Tanzania inawakilishwa na Twiga Stars na
kufanya vizuri kwa timu ya Taifa ya Soka chini ya miaka 20 (Ngorongoro
Heros) ambayo tarehe 31 Machi, 2019 itacheza na Eritrea Mjini Asmara.
Pamoja
na kuwapongeza wachezaji wa Taifa Stars na Bondia Hassan Mwakinyo Mhe.
Rais Magufuli amekula chakula cha mchana na wachezaji hao.
Gerson Msigwa
Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, IKULU
Dar es Salaam
25 Machi, 2019
No comments:
Post a Comment