Mchezaji wa zamani wa Timu ya Taifa ya Tanzania (Taifa Stars) Peter
Tino leo amekabidhiwa shilingi Milioni 5 alizopewa na Rais wa Jamhuri
ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli kwa kutambua
mchango wake kwa Timu ya Taifa ya mwaka 1980 ambayo ilifuzu kuingia
fainali Michuano ya Soka Barani Afrika (AFCON).
Mchezaji Peter Tino ndiye aliyefunga goli lililoiwezesha Tanzania
kuingia fainali hizo na tangu mwaka huo wa 1980 Tanzania haikuwahi
kufanikiwa tena kuingia hatua hiyo mpaka mwaka 2019 ikiwa ni miaka 39
imepita.
Peter Tino alialikwa Ikulu Jijini Dar es Salaam leo tarehe 25 Machi,
2019 wakati Rais Magufuli alipokutana na kuwapongeza wachezaji wa
Timu ya Taifa ya Tanzania (Taifa Stars) ambao jana waliifunga Timu ya
Taifa ya Uganda (The Cranes) na kufanikiwa kufuzu kucheza fainali za
AFCON 2019 zitakazofanyika baadaye mwezi Juni 2019 huko Misri.
Pamoja na kupatiwa shilingi Milioni 5, Peter Tino pia ameunganishwa
katika zawadi ya kupatiwa kiwanja Jijini Dodoma kwa kila mchezaji wa
Taifa Stars iliyotolewa na Rais Magufuli ambapo naye atapatiwa
kiwanja cha kujenga nyumba.
Peter Tino ameziweka pesa hizo katika akaunti yake ya Benki ya CRDB
aliyoifungua mara tu baada ya kutoka Ikulu na kukabidhiwa kadi yenye
taarifa zake za benki (ATM).
“Hakika Mungu ni mkubwa” amesema Peter Tino baada ya kupokea kadi yake
ya Benki kwa Meneja Biashara wa Tawi la CRDB la Azikiwe, Bw. George
Yatera, akishuhudiwa na Afisa kutoka kutoka TFF Bw. John Michael
Mashaka. “Hela hii sikuiota hata ndotoni na mradi Raisi wetu mpendwa
John Pombe Magufuli kanikumbuka hakika sintomwangusha. Yaani
nitakwenda kumalizia kibanda changu kule Morogoro, ” aliongezea.
Afisa wa Benki hiyo Bi. Gloria Kaale ndiye aliyemsajili mchezaji huyo
ambaye wadogo zake, Gebbo Peter na Emma Peter, nao walitikisa anga za
soka nchini kwa nyakati tofauti siku za nyuma kabla ya na wao
kustaafu. Familia yao kwa sasa inaishi Morogoro.
Kwa mujibu wa kumbukumbu zilizopo, ilikuwa ni Agosti 26,1979 wakati
timu ya soka ya Taifa, Taifa Stars ilipokuwa ikirudiana na timu ya
soka ya Taifa ya Zambia katika mechi ya michuano ya kuwania kufuzu
kucheza fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika za mwaka 1980
zilizofanyika nchini Nigeria.Pambano hilo lilichezwa mjini Ndola.
Mechi hiyo ilikuwa na umuhimu mkubwa kwa Taifa Stars kwa vile ilikuwa
ikihitaji sare ya aina yeyote ili iweke historia ya kufuzu kucheza
fainali hizo kwa mara ya kwanza , tangu ilipoanza kushiriki michuano
hiyo mwaka 1968. Katika mechi ya kwanza iliyochezwa wiki mbili nyuma
kwenye uwanja wa Taifa, Dar es Salaam, Taifa Stars iliishinda Zambia
bao 1-0. Bao hilo lilifungwa na kiungo Mohammed Rishard Adolph.
Ushindi huo ulipatikana kwa mbinde kiasi kwamba mashabiki wengi
hawakuwa na imani iwapo Taifa Stars ingeshinda ama kupata sare katika
mechi ya marudiano. Na hivyo ndivyo ilivyokuwa kwani Wazambia
walifanikiwa kupata bao la kuongoza dakika za mapema na kudumu nalo
kwa takriban dakika 86.
Zikiwa zimesalia dakika tatu pambano hilo kumalizika, mshambuliaji
mrefu mwenye kasi na mashuti makali, Peter Tino alibadili sura ya
mchezo na kufanya kile kilichokuwa kikisubiriwa kwa hamu kubwa na
mashabiki wa mchezo huo nchini.
Ilipigwa kona kwenye lango la Taifa Stars, kipa Juma Pondamali
akaupangua mpira kwa ngumi, ukamkuta kiungo Leodegar Tenga, aliyetoa
pasi ndefu kwa kiungo mwenzake, Hussein Ngulungu, ambaye naye alitoa
pasi ndefu kwa Tino.
Akiwa amezungukwa na mabeki watatu wa Zambia, Tino alilazimika kupiga
hesabu za haraka haraka. Aliwachomoka mbio mabeki nao na kukimbia na
mpira kwa kasi. Alipofika nje kidogo ya eneo la hatari la Zambia,
alifumua shuti kali la mguu wa kulia, lililompita kipa Shileshi wa
Zambia na mpira kutinga wavuni.Bao hilo lilipatikana baada ya pasi
tatu.
Katika mechi hiyo, Taifa Stars iliwakilishwa na kipa Juma
Pondamali,mabeki ni Leopard Tasso, Mohammed Kajole/ Ahmed Amasha,
Salim Amir, Jella Mtagwa, viungo ni Leodegar Tenga, Hussein Ngulungu
na washambulaji ni Omari Hussein, Peter Tino, Mohamed Salim na Thuweni
Ally.
Kikosi hicho kilikuwa chini ya Kocha Slowmir Work kutoka Poland,
akisaidiwa na Wazawa Joel Bendera na Ray Gama (ambao kwa sasa wote ni
marehemu), ndicho kilichoiwakilisha Tanzania katika fainali za kombe
hilo zilizofanyika nchini Nigeria.
Katika fainali hizo, Taifa Stars ilichapwa mabao 3-1 na wenyeji
Nigeria katika mechi ya ufunguzi, ilitoka sare ya mabao 2-2 na Ivory
Coast kabla ya kuchapwa mabao 2-1 na Misri na kutolewa hatua ya
makundi.
Hiyo ilikuwa ni miaka 39 iliyopita ambapo hivi sasa, baada ya kuichapa
Uganda mabao 3-0 Jumapili, kila Mtanzania ameweka matumaini kwenye
kikosi hicho kipya kilicho chini ya kocha kutoka Nigeria, Emmanuel
Amunike.
Mchezaji wa zamani wa Timu ya Taifa ya Tanzania (Taifa Stars) Peter
Tino akikamilisha kufungua akaunti ili aweke shilingi Milioni 5 leo
alizopewa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe
Magufuli kwa kutambua mchango wake kwa Timu ya Taifa ya mwaka 1980
ambapo goli lake liliiwezesha Tanzania kufuzu fainali ya Michuano ya
Soka Barani Afrika (AFCON). Wanaoshuhudia ni Meneja Biashara wa Tawi la
CRDB la Azikiwe, George Yatera na Afisa kutoka kutoka TFF John Michael
Mashaka. Kushoto ni Afisa wa Benki hiyo Bi. Gloria Kaale ambaye ndiye
aliyemfungulia akaunti nyota huyo wa zamani.
Mchezaji
wa zamani wa Timu ya Taifa ya Tanzania (Taifa Stars) Peter Tino
akielekezwa na Meneja Biashara wa Tawi la CRDB la Azikiwe, Bw. George
Yatera namna na kutumia kadi yake ya ATM baada ya kukamilisha kufungua
akaunti ili aweke shilingi Milioni 5 alizopewa na Rais wa Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli kwa kutambua mchango wake
kwa Timu ya Taifa ya mwaka 1980 ambapo goli lake liliiwezesha kufuzu
fainali ya Michuano ya Soka Barani Afrika (AFCON). Kushoto ni Afisa wa
Benki hiyo Gloria Kaale
Mchezaji
wa zamani wa Timu ya Taifa ya Tanzania (Taifa Stars) Peter Tino
akikabidhiwa kadi yake ya ATM kutoka kwa Meneja Biashara wa Tawi la CRDB
la Azikiwe, Bw. George Yatera baada ya kukamilisha kufungua akaunti ili
aweke shilingi Milioni 5 alizopewa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli kwa kutambua mchango wake kwa Timu ya
Taifa ya mwaka 1980 ambapo goli lake liliiwezesha kufuzu fainali ya
Michuano ya Soka Barani Afrika (AFCON). Wanaoshihudia ni Afisa kutoka
kutoka TFF Bw. John Michael Mashaka na Afisa wa Benki hiyo Bi. Gloria
Kaale ambaye ndiye.
Mchezaji
wa zamani wa Timu ya Taifa ya Tanzania (Taifa Stars) Peter Tino
akionesha kadi yake ya ATM baada ya kukamilisha kufungua akaunti ili
aweke shilingi Milioni 5 alizopewa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli kwa kutambua mchango wake kwa Timu ya
Taifa ya mwaka 1980 ambapo goli lake liliiwezesha kufuzu fainali ya
Michuano ya Soka Barani Afrika (AFCON).
Mchezaji wa zamani wa Timu ya Taifa ya Tanzania (Taifa Stars)
Peter Tino akimshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli kwa kumzawadia shilingi Milioni 5 kwa
kutambua mchango wake kwa Timu ya Taifa ya mwaka 1980 ambapo goli lake
liliiwezesha Tanzania kufuzu fainali ya Michuano ya Soka Barani Afrika
(AFCON) wakati Rais Magufuli alipokutana na kuwapongeza wachezaji wa
Timu ya Taifa ya Tanzania (Taifa Stars) ambao jana waliifunga Timu ya
Taifa ya Uganda (The Cranes) na kufanikiwa kufuzu kucheza fainali za
AFCON 2019 zitakazofanyika baadaye mwezi Juni 2019 huko Misri.
No comments:
Post a Comment