Mkuu wa Wilaya ya Nkasi Mh. Said
Mtanda (aliyeshika tofali) akitoa maelezo kwa Mkuu wa mkoa wa Rukwa Mh.
Joachim Wangabo wakati wa ziara fupi ya kuangalia maendeleo ya ujenzi wa
hospitali ya Wilaya hiyo ulioanza mapema mwaka huu na kutakiwa
kumalizika mwishoni mwa mwezi wa sita mwaka 2019.
Mkuu
wa Mkoa wa Rukwa Mh. Joachim Wangabo (rainboot za kijani) akiangalia
uimara wa matofali yaliyojengewa msingi katika moja ya majengo saba ya
hospitali ya wilauya ya Sumbawanga inayojengwa katika bonde la ziwa
Rukwa, kata ya Mtowisa. (mwenye shati ya kitenge) Mkuu wa Wilaya ya
Sumbawanga Dkt. Khalfan Haule.
Mkuu wa Mkoa wa Rukwa Mh. Joachim
Wangabo amewaagiza wakuu wa Wilaya za Mkoani Rukwa kuhakikisha wanakuwa
na utaratibu wa pamoja katika kutembeleana na kuelezana changamoto na
mafanikio katika maeneo ya mradi wa ujenzi wa hospitali za wilaya ili
kujenga hospitali hizo katika hadhi sawa na hatimae kupeana ujuzi wa
utekelezaji wa mradi huo.
Amepongeza ushirikiano
unaoonyeshwa na uongozi wa wilaya ya Nkasi unaoongozwa na Mkuu wa Wilaya
hiyo mh. Said Mtanda pamoja na wabunge, madiwani na mkurugenzi na
kusifu mafunzo waliyoyapata na kuyarekebisha wakati wa utekelezaji wa
ujenzi wa vituo vitatu vya afya katika wilaya hiyo na kuonyesha dalili
za kutojirudia kwa makosa waliyoyafanya wakati wakitekeleza ujenzi wa
vituo hivyo.
“Wakuu wa Wilaya waweke program ya
kutembeleana kwa pamoja ili kujifunza, wanakuja kwa mfano (wilaya ya)
Nkasi, wanakwenda wilaya ya Sumbawanga, Wanakwenda wilaya ya Kalambo
halafu watakaa chini wafanye tafakari ili waone ni namna gani wanweza
wakasimamia vizuri hizo hospitali zetu za wilaya kwasababu tunapaswa
tuwe na kitu bora, hospitali zote tatu ziwe bora ndani ya mkoa wetu,”
Alisisitiza.
Alisema kuwa halitakuwa jambo jema
kwa wilaya moja kuwa na ufanisi sana ilihali wilaya nyingine inakuwa na
changamoto na hivyo vyema wakaungana kama timu na kutembelea miradi
hiyo ya ujenzi wa hospitali za wilaya ili kila mmoja aweze kujifunza
kutoka kwa mwenzie.
Ameyasema hayo baada ya ziara yake
ya kutembelea ujenzi wa hospitali ya Wilaya ya Nkasi pamoja na ujenzi
wa hospitali ya Wilaya ya Sumbawanga ili kujionea changamoto mbalimbali
zinazoukabili mradi huo ambao unatakiwa kuisha mwishoni mwa mwezi wa
sita mwaka huu.
No comments:
Post a Comment