Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii,
Jinsia, Wazee na Watoto Mhe. Ummy Mwalimu amesema Serikali itaendelea
kusimamia na kudhibiti matumizi ya kemikali ili kuhakikisha hazileti
madhara kwa afya za wananchi na Mazingira.
Waziri Ummy
ameyazungumza hayo leo jijini Dar es Salaam wakati akifungua Mkutano na
wadau wanaojishughulisha na shughuli za kemikali ulioandaliwa na Mamlaka
ya Maabara ya Mkemia Mkuu wa Serikali kwa lengo la kujadili namna ya
kuboresha mazingira ya kufanya biashara ya kemikali nchini.
“Kemikali zisipodhibitiwa vizuri zinaweza
kuleta madhara katika afya, mazingira pamoja na kuhatarisha usalama wa
nchi, ipo haja ya kuweka mazingira mazuri ya kusimamia na kudhibiti
uingizaji na matumizi ya kemikali nchini ili zisilete madhara,” alisema
Ummy.
Mkemia Mkuu wa Serikali, Dkt. Fidelice Mafumiko (kushoto) akifafanua jambo kwa Mheshimiwa Ummy Mwalimu, wakati wa Mkutano na Wadau leo. |
Alifafanua kuwa takwimu za Shirika la
Afya Duniani (WHO) za mwaka 2014 zinaonyesha vifo milioni 12.6
vilitokana na mazingira duni ya kuishi, mojawapo ya kichocheo ni athari
za kemikali ambazo zimekuwa zikisababisha magonjwa na vifo.”
Waziri Ummy aliongeza kuwa kemikali
zimekuwa na athari kubwa kwa binadamu kwa kusababisha magonjwa zaidi ya
mia moja yakiwemo magonjwa ya moyo, saratani, ngozi, athari katika
mifumo ya fahamu, upumaji pamoja na chakula kuathiri zaidi wananchi
wengi.
“Tukubali kuwa kemikali zina madhara kwa
wananchi lakini sasa tuwe na mazingira mazuri ya kuzidhibiti, Serikali
itaendelea kuboresha mazingira mazuri kwa wafanya biashara ya kemikali
nchini,” Ummy aliongeza.
Aidha, Waziri Ummy amezitaka Taasisi ya
Mamlaka ya Maabara ya Mkemia Mkuu wa Serikali (GCLA) pamoja na Mamlaka
ya Chakula na Dawa nchini (TFDA) kuangalia upya tozo zinazotozwa kwa
wafanyabiashara wa kemikali nchini pamoja na kupunguza changamoto zisizo
za lazima ili kuwawekea mazingira rafiki wafanya biashara za kemikali.
Amezitaka Taasisi hizo kutokuwa na
vikwazo kwa uwekezaji na biashara, kikwazo cha kushamiri na kukua kwa
uwekezaji nchini na badala yake wawe mawakala wa kukuza biashara na
uchumi nchini ili kuvutia wawekezaji kwa kuweka mazingira rafiki kwa
biashara.
Katibu Mkuu wa Chama cha Mawakala wa Forodha Tanzania (TAFFA), Mhandisi Anthony Swai akichangia mada |
Mfanyabiashara Bw. Azim Dewji akichangia mada wakati wa Mkutano. |
No comments:
Post a Comment