Serikali
kupitia wizara ya maji imejipanga kuleta utaratibu wa kuziwekea
mikataba ya utendaji kazi taasisi zilizopo chini ya wizara hiyo ili
kuimarisha usimamizi wa sekta ya maji katika ngazi mbalimbali nchini.
Hayo
yamezungumzwa Jijini Dodoma na Waziri wa Maji Prof. Makame Mbarawa
wakati alipokuwa akifungua mkutano uliowahusisha Makatibu Tawala wa
Mikoa nchini kwa ajili ya kujengeana uelewa wa pamoja kuhusu uendeshaji
mpya wa sekta ya maji kufuatia kupitishwa kwa sheria mpya ya Huduma ya
Maji na Usafi wa Mazingira Sheria Namba 5 ya mwaka 2019.
Prof.
Mbarawa amesema kuwa wizara imeamua kuja na mikataba hiyo itakayokuwa
na malengo maalum ya kuzipima taasisi kwa kila mwaka mmoja ambapo nia ya
serikali sio kumkomoa mtendaji bali ni kuhakikisha wananchi wanapata
huduma iliyokusudiwa.
“Mamlaka
hizi zikisimamiwa kwa malengo zitafanya kazi vizuri zaidi na zitakuwa
na uwezo mkubwa wa kujiendesha pia kupimana utendaji kazi ni jambo zuri
kwa sababu tukifanya kazi kimazoea mamlaka na taasisi zetu hazitoweza
kufanya kazi vizuri wala kuimarisha utoaji wa huduma za maji safi na
salama kwa wananchi wetu,” amesema Prof. Mbarawa.
Ameendelea
kusema kuwa, mkutano huo ni sehemu ya utekelezaji wa agizo la Mhe. Rais
Magufuli alilolitoa mwezi Mei, 2018 kuhusu mfumo wa uendeshaji wa sekta
ya maji ambapo aliagiza sekta ya maji isimamiwe na wizara moja ili
kurahisisha usimamizi na uwajibikaji wa watendaji.
Nae
Katibu Mkuu wa Wizara hiyo, Prof. Kitila Mkumbo amefafanua kuwa Sheria
ya Huduma za Maji na Usafi wa Mazingira Namba 12 ya mwaka 2009 imepitiwa
na kutungwa upya na kwa sasa inajulikana kama Sheria ya Huduma ya Maji
na Usafi wa Mazingira ya mwaka 2019 ambapo kikubwa katika sheria hiyo ni
kuanzishwa kwa Wakala wa Maji Vijijini.
“Haitawezekana
kukamilisha mipango ya sekta ya maji bila ushirikiano wa kutosha kutoka
kwa Mamlaka za Serikali za Mitaa hivyo kupitia mkutano huu Makatibu
Tawala watapata nafasi ya kupitia na kuielewa sheria mpya kwa kina na
kubaini nafasi zao katika usimamizi na uendeshaji wa sekta ya maji
kwenye sheria hii," amesema Prof. Mkumbo.
Kuanza
kutumika kwa sheria hiyo mpya kutaimarisha mfumo wa utoaji huduma za
maji na usafi wa mazingira nchini, kutaongeza ufanisi na uwajibikaji
katika kutoa huduma za maji, kutaimarisha ujenzi na usimamizi na
uendeshaji wa miradi ya maji, kutachochea utendaji katika sekta
nyingine na kuongeza mchango wa sekta ya maji katika uchumi wa nchi.
Katibu
Mkuu wa Wizara ya Maji, Prof. Kitila Mkumbo akizungumza na Makatibu
Tawala wa Mikoa nchini (hawapo pichani) walioshiriki katika mkutano wa
kujengeana uelewa wa pamoja kuhusu uendeshaji upya wa sekta ya maji
kufuatia kupitishwa kwa sheria mpya ya Huduma ya Maji na Usafi wa
Mazingira Sheria Namba 5 ya mwaka 2019. Ufunguzi huo umefanyika leo
Jijini Dodoma.
Waziri
wa Maji Prof. Makame Mbarawa akizungumza wakati akifungua mkutano
uliowahusisha Makatibu Tawala wa Mikoa nchini kwa ajili ya kujengeana
uelewa wa pamoja kuhusu uendeshaji upya wa sekta ya maji kufuatia
kupitishwa kwa sheria mpya ya Huduma ya Maji na Usafi wa Mazingira
Sheria Namba 5 ya mwaka 2019. Ufunguzi huo umefanyika leo Jijini Dodoma.
Mwenyekiti
wa Makatibu Tawala wa Mikoa nchini, Mama Rehema Madenge akitoa neno la
shukrani baada ya Waziri wa Maji Prof. Makame Mbarawa kufungua mkutano
huo.
Baadhi ya Makatibu Tawala wa Mikoa nchini na wafanyakazi wa Wizara ya Maji waliohudhuria katika mkutano huo.Na Jacquiline Mrisho - MAELEZO
No comments:
Post a Comment