Naibu Waziri wa Afya, Maendeleo ya
Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Dkt. Faustine Ndugulile (Wakwanza
kushoto) akiwa katika kikao na Madaktari bingwa kutoka shirika la
Tokushukai kutoka nchi ya Japan baada yakufanikisha upandikizaji wa figo
kwa kushirikiana na Madaktari kutoka Hospitali ya Benjamin Mkapa Jijini
Dodoma.
Picha ya pamoja ikiongozwa na
Naibu Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto akiwa
na Madaktari bingwa kutoka shirika la Tokushukai kutoka nchi ya Japan na
Wataalamu kutoka Hospitali ya Benjamin Mkapa Jijini Dodoma baada
yakujionea upandikizaji wa figo wenye mafanikio.
Naibu Waziri wa Afya, Maendeleo ya
Jamii, Jinsia, Wazee na watoto Dkt. Faustine Ndugulile akiwa na Daktari
Bingwa wa magonjwa ya Figo kutoka Hospitali ya Benjamin Mkapa Dkt.
Charles Shija
…………………………
Na WAMJW – DOM
Hospitali ya Benjamin Mkapa
imefanikiwa kupandikiza Figo jumla ya Wagonjwa saba tangu ilipoanza
kufanya huduma hiyo kwa kushirikiana na Madaktari kutoka shirika la afya
la Tokushukai lilopo nchi ya Japan.
Hayo yamesemwa na Naibu Waziri
wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto wakati
alipofanya ziara ya kukagua hali ya utoaji huduma za kibingwa za
magonjwa ya Figo katika Hospitali ya Benjamin Mkapa Jijini Dodoma.
Dkt. Ndugulile amesema kuwa
Idadi ya wagonjwa waliokwishapandikizwa figo hapa nchini ni 43, ambapo
38 wamepatiwa huduma hiyo kwenye hospitali ya Taifa Muhimbili na
wagonjwa watano(5) hospitali ya Benjamin Mkapa
“Hivi navyoongea tayari
mgonjwa mmoja amekwishapandikizwa figo na ameshatoka salama, yupo
anaendelea kuangaliwa, lakini wana mpango wa kuwafanyia wengine wawili
tutapokuwa tumekamilisha hili tutakuwa na wagonjwa saba ambao
wamefanyiwa hospitali hii” alisema Dkt. Ndugulile.
Dkt. Ndugulile aliendelea
kusema kuwa, Serikali imelenga kuhakikisha kwamba inawajengea uwezo
Wataalamu wa ndani kufanya upasuaji wa kibingwa ili waweze kuwahudumia
Watanzania bila msaada kutoka Wataalamu wa nje.
“lengo na kusudio ni kuhakikisha kwamba tunajenga uwezo wa ndani wa kuweza kufanya upasuaji huu” Alisema Dkt. Ndugulile
Dkt. Ndugulile amesema kuwa
Serikali imeokoa zaidi ya kiasi cha shilingi bilioni 4.2 ambacho
kingetumika katika matibabu ya wagonjwa 80 mpaka 100 ambao wangepelekwa
nje ya nchi kwa ajili ya matibabu.
“Wagonjwa
waliokwishapandikizwa figo hapa nchini ni 42, kama tungewapeleka
wagonjwa nje ya nchi ingegharimu serikali kiasi cha shilingi bilioni
4.2 kwa idadi hiyo ya wagonjwa. 80 mpaka 100, wakati huduma hii hapa
nchini inagharimu kiasi cha shilingi milioni 21 kwa kila mgonjwa.”
alisema Dkt. Ndugulile
Aidha, Dkt. Ndugulile
amewashukuru Wataalamu kutoka shirika la Tokushukai kutoka nchi ya Japan
kwa kujitoa na kuja kuwajengea uwezo Wataalamu wa ndani hali
iliyosaidia kupunguza kiasi kikubwa cha fedha ambacho hutumika kwa ajili
ya matibabu kwa wagonjwa wanaoenda kutibiwa nje.
“Kwa niaba ya Serikali ya
Tanzania nimepita kuwashukuru na kuwapongeza, kwa sababu badala ya
kutusaidia sisi samaki, wenzetu wa Japan wameamua kutupatia sisi mishipi
na kutufundisha jinsi ya kujua naamini ujuzi huu utatusaidia sana ”
alisema Dkt. Ndugulile.
No comments:
Post a Comment