Na Josephine Majura, WFM, Dodoma
Serikali
imesema kuwa kwa sasa nchi haina tatizo la mzunguko mdogo wa fedha
katika soko kutokana na hatua mbalimbali ilizozichukua kukabiliana na
tatizo hilo ikiwemo kuongeza ukwasi kwenye uchumi.
Hayo
yameelezwa Bungeni mjini Dodoma na Naibu Waziri wa Fedha na
Mipango, Mhe. Dkt. Ashatu Kijaji (Mb), alipokuwa akijibu swali la msingi
la Mbunge wa Momba Mhe. David Silinde (Chadema), aliyetaka kujua sababu
za mzunguko mdogo wa fedha.
Dkt.
Kijaji alisema kuwa, katika kutatua changamoto ya kupungua kwa mzunguko
wa fedha katika soko, Serikali kupitia Benki Kuu ya Tanzania (BoT)
ilichukua hatua mbalimbali za kuongeza ukwasi kwenye uchumi ikiwemo
kushusha riba ya Benki Kuu (discount rate) kutoka asilimia 16 kwa mwezi
Machi, 2017 hadi asilimia 7, Agosti 2018.
“Benki
Kuu ilipunguza kiwango cha kisheria cha sehemu ya amana kinachotakiwa
kuwekwa Benki Kuu na mabenki ya biashara(Statutory Minimum Reserve
Requirement, (SMR)) kutoka asilimia 10 hadi asilimia 8 mwezi April 2017
pamoja na kuruhusu mabenki kutumia asilimia 10.0 ya sehemu ya SMR kama
chanzo kimojawapo cha kusaidia hali ya ukwasi kwenye uchumi”, alisema
Dkt. Kijaji.
Alisema
Benki Kuu ilianzisha utaratibu wa kutoa mikopo ya muda maalumu kwa
mabenki pamoja na kununua fedha za kigeni kutoka kwenye soko la jumla la
mabenki ili kuongeza ukwasi kwenye uchumi.
Alifafanua
kuwa mzunguko wa fedha katika uchumi unaendana na malengo pamoja na
mahitaji halisi ya shughuli za kiuchumi zizopo kwa sasa.
Aidha,
Dkt. Kijaji alisema Serikali kupitia Benki Kuu ya Tanzania inatekeleza
Sera ya Fedha inayolenga kusimamia mzunguko wa fedha unaoendana na
mahitaji halisi ya uchumi kwa lengo la kudumisha utulivu wa mfumuko wa
bei na hivyo kuweka mazingira mazuri ya ukuaji wa uchumi.
No comments:
Post a Comment