Matokeo chanyA+ online




Tuesday, April 23, 2019

JAJI MKUU AFUNGUA MKUTANO WA MWAKA WA KUTATHMINI UTENDAJI WA MAHAKAMA YA RUFANI

Majaji wa mahakama ya Rufani wametakiwa kuzingatia sheria na katiba katika kutoa haki, na pia kutosahau kutumia tabia za utamaduni ambazo hazijaandikwa mahali popote katika kusaidia utoaji wa haki.

Amesema, tabia ya  uvivu, uchonganishi, ulalamishi na ubishi usioeleweka ni moja kati ya tabia za kibinadamu zinazochangia  kutotolewa kwa haki kwa wakati. Jaji Mkuu wa Tanzania, Profesa Ibrahim Juma ameyasema hayo leo Aprili 23, 2019, jijini Dar es Salaam, wakati akifungua mkutano wa mwaka wa kutathmini utendaji wa Mahakama ya Rufani.

 Jaji Profesa Juma amesema,  majaji wana wajibu mkubwa wa kutoa haki kwa mujibu wa sheria na kutoa uamuzi hata katika mambo yasiyo na sheria na kwamba tabia za kutotoa haki kwa wakati ni pamoja na uvivu, uchonganishi, ubishi usioeleweka na ulalamishi kwani mambo haya yakiingia katika mfumo wa utoaji haki yanachelewesha.

Amesema pamoja na kutakiwa kutegemea sheria na katiba, yapo mambo ya kiutamaduni na tabia ambazo hazijaandikwa sehemu yoyote hivyo wanapaswa kuyazingatia katika kutoa haki.

"Mnatakiwa kuwa na uelewa wa sheria kwani wananchi wanategemea watapata haki kwa wakati, pia tuwe na ujuzi wa sheria na msisahau kuelewa tabia za watu  mbalimbali hususani majaji waliostaafu ili isije kuwa kikwazo katika utoaji haki," alisisitiza.

Amesema,  mkakati wa miaka mitano wa mahakama unajenga tabia ya kutoa haki  kwa kutumia utamaduni na kuwa hakuna mahali ambapo pameandikwa kuwepo kwa uharakishaji wa utoaji haki, lakini majaji wanapaswa kutambua suala hilo kwani wananchi wanawategemea kuendana na karne ya 21.

Jaji Profesa Juma amesema, kutumia tamaduni nzuri za nchi husika ni sehemu mojawapo inayosaidia utoaji wa haki, hivyo kama mahakama watazitumia tamaduni zetu, basis itasaidia sana kwani yapo mambo mengi ya kuwezesha utoaji haki kwa wakati ambayo hayakuandikwa.

Ameongeza kiwa, ongezeko la Majaji wa Rufani kutoka 15 tuliowazoea hadi 21,  imeongeza nguvu kwa mahakama na lengo ikiwa  kuondoa mashauri yaliyokuwa yakichelewa kwani ni Lazima tuwasaidie wananchi kupata suluhu ya haraka katika masuala ya uchumi na jamii.

Katika mkutano huo wa mafunzo wa siku mbili ulioandaliwa na chuo cha mafunzo ya uongozi Lushoto,  Majaji wa Mahakama ya Rufani watapata mafunzo ya namna ya kuendesha majopo mahakamani yatakayowawezwsha utoaji wa haki kwa wakati.
Jaji Mkuu wa Tanzania, Profesa Ibrahim Juma akifungua  mkutano wa mwaka wa kutathmini utendaji wa Majaji wa Mahakama ya Rufani na Majaji wastaafu unaofanyika kwa siku mbili jijini Dar es Salaam.
Baadhi ya Majaji wa Mahakama ya Rufani na Majaji wastaafu wakimsikiliza Jaji Mkuu wa Tanzania, Profesa Ibrahim Juma alipokuwa akifungua  mkutano wa mwaka wa kutathmini utendaji wa mahakama ya Rufani unaofanyika kwa siku mbili jijini Dar es Salaam
Jaji Mkuu wa Tanzania, Profesa Ibrahim Juma akiwa kwenye picha ya pamoja na baadhi ya Majaji wa Mahakama ya Rufani na Majaji wastaafu  mara baada ya kufungua mkutanowa mwaka wa kutathmini utendaji unaofanyika kwa siku mbili jijini Dar es Salaam.

No comments:

Post a Comment