Waziri Mkuu wa
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Kassim Majaliwa amesema kuwa mapendekezo ya
Bajeti ya Serikali yanazingatia Mpango wa Maendeleo wa Taifa sanjari na
utekelezaji wa Ilani ya uchaguzi.
Amesema hayo leo
Bunge jijini Dodoma alipokuwa akiwasilisha Hotuba ya Mapitio na Mwelekeo wa
kazi za Serikali na makadirio ya Mapato na Matumizi ya fedha za Ofisi ya Waziri
Mkuu na Ofisi ya Bunge kwa mwaka 2019/2020.
"Mpango wa
Maendeleo wa Taifa unatekelezwa sanjari
na maelekezo ya Ilani ya Uchaguzi ya Chama cha Mapinduzi (CCM) ya mwaka 2015 -
2020, ahadi za Mheshimiwa Rais wakati wa kampeni za Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2015
na zile alizozitoa katika hotuba yake ya kuzindua Bunge hili mwezi Novemba,
2015." amesema Waziri Mkuu Majaliwa.
Amesema, vipaumbele
vya mpango wa mwaka 2019/2020 ni kuendelea kuimarisha msingi wa uchumi wa
viwanda, kufungamanisha ukuaji wa uchumi na maendeleo ya watu, kuendelea
kuboresha mazingira wezeshi kwa uendeshaji
wa biashara na uwekezaji na kuimarisha usimamizi wa utekelezaji wa
mpango.
Aidha amesema kuwa, katika
Mpango wa Maendeleo na Bajeti ya mwaka 2019/2020, Serikali itaendelea
kutekeleza Mradi wa Umeme wa Maji wa Mto Rufiji (Stiegler's Gorge), ujenzi wa
miundombinu ya reli ya kisasa (SGR), barabara pamoja na kukuza sekta ya anga.
Utekelezaji wa miradi
hiyo ya miundombinu wezeshi ya kiuchumi una lengo la kufungamanisha ukuaji wa
sekta hizo na sekta nyingine hususan za biashara, kilimo na utalii.
Waziri Mkuu amesema
kuwa, kuimarika kwa sekta hizo kutachochea ukuaji wa uchumi na maendeleo ya
Wananchi kwa ujumla
Ameendelea
kusema, katika kipindi cha miaka mitatu ya uongozi wa Mhe. Dkt. John Pombe
Magufuli yamepatikana mafanikio mengi ambayo wananchi wanapaswa kufahamishwa.
Amesema,
Mhe. Rais Magufuli ameonesha dhamira ya dhati ya kisiasa katika kujenga msingi
wa uchumi wa kisasa wa Taifa linalojitegemea. Halikadhalika, ameweza
kuhakikisha dhamira hiyo ya kujenga uchumi imara usiyo tegemezi inaenea kwa
viongozi wengine, watendaji na wananchi kwa ujumla.
Miongoni
mwa mafanikio yaliyopatikana ni kuendelea kukua na kuimarika kwa uchumi ambao
unachochewa na jitihada za Serikali za kuwekeza kwenye miundombinu ya
usafirishaji ikiwemo ujenzi wa barabara, reli, viwanja vya ndege sanjari na
kutengemaa kwa upatikanaji wa nishati ya umeme.
Ameongeza
kuwa kuimarika kwa Shirika la Ndege Tanzania ni sehemu ya mafanikio hayo,
ambapo Serikali imefanikisha ununuzi wa ndege saba mpya ikiwemo Dreamliner
Boeing 787.
Ununuzi
wa ndege hizo umesaidia kuitangaza nchi, kuongeza mapato ya Serikali, fursa za
ajira kwa vijana na kuwa kichocheo kwa Sekta za ajira kwa vijana na kuwa
kichocheo kwa sekta nyingine kama vile kilimo, utalii, mifugo na uvuvi.
Vilevile,
mpango wa elimu msingi bila malipo umesaidia kuongezeka idadi ya wanafunzi
wanaoandikishwa kutoka wanafunzi milioni 1.57 mwaka 2015 hadi milioni 2.08
mwaka 2016 sawa na ongezeko la asilimia 35.2 kwa mwaka 2019 uandikishaji ulikuwa milioni 1.58.
Serikali
ya Awamu ya Tano imeendelea kuimarisha uchumi na mafanikio yanayoonekana,
ambapo katika kipindi cha Januari hadi Septemba 2018, Pato la Taifa lilikuwa
kwa asilimia 6.7 ikilinganishwa na ukuaji wa asilimia 6.2 katika kipindi kama
hicho mwaka 2017.
Ukuaji
huo wa uchumi umechangia kutoa ajira na kuongeza mapato ya Serikali
yaliyowezesha ujenzi na uboreshaji wa miundombinu kwa ajili ya shughuli za kiuchumi
na kijamii.
No comments:
Post a Comment