RaisDkt. John Pombe Magufuli
amesema Serikali haina mpango wa kuongeza maeneo ya utawala ikiwemo kuanzisha mikoa
mipya na badala yake imejipanga kuimarisha huduma na mahitaji ya miundombinu
iliyopo ili kuwaletea maendeleo wananchi.
Akizungumza katika hafla ya
uzinduzi wa barabara ya Namtumbo-Kilimasera-Matemanga- Tunduru yenye urefu wa
kilometa 193 leo (Ijumaa April 5, 2019), Rais Magufuli alisema Serikali
imekusudia kutatua changamoto mbalimbali zinazowakabili wananchi ikiwemo ujenzi
wa miundombinu ya barabara, afya, maji, elimu n.k katika maeneo waliopo.
Aliongeza kuwa katika awamu yake
yake ya Uongozi, suala la kuongeza maeneo ya utawala halipo na badala yake
kuwataka Viongozi wa maeneo hayo wajipange katika kuwaletea maendeleo wananchi
badala ya fedha zilizopo kwenda katika kujenga ofisi mpya za Wakuu wa Mikoa mipya
na kuwalipa mishahara viongozi hao.
“Tumepanga kuleta maendeleo ya
kweli kwa wananchi wetu, tumechelewa kuleta Maendeleo hususani kwa wananchi
wetu wa mikoa ya kusini, Serikali ninayoiongoza haina mpango wa kuanzisha mikoa
mipya , badala yake pesa hizo tutazielekeza katika ununuzi wa madawa na
kuboresha miundombinu ya barabara, elimu na nishati’ alisema Rais Magufuli.
Aidha Rais Magufuli alisema bado yapo
baadhi ya maeneo mengi nchini yanakabiliwa na changamoto mbalimbali ikiwemo
barabara za lami, hivyo Serikali haitoweza kuleta Maendeleo katika sehemu moja
kwa kuwa fedha hizo hazipo kwa kuwa ina na mahitaji makubwa katika kuboresha
huduma mbalimbali za kijamii na kiuchumi katika maeneo mbalimbali ya nchi.
Kwa mujibu wa Rais Magufuli
alisema malengo ya Serikali ni kuhakikisha kuwa huduma muhimu na za msingi kwa Maendeleo
ya wananchi zinapewa kipaumbele ikiwemo ujenzi wa vituo vya afya na Zahanati,
kwa kuwa kukamilika kwake kutasaidia kupunguza vifo vya akina mama na watoto
ambavyo katika miaka ya nyuma vimekuwa vikisababisha vifo vya makundi hayo ya
kijamii.
Akizumgumzia kuhusu Sekta ya
Maji, Rais Magufuli alimtaka Waziri wa Maji, Prof. Makame Mbarawa kuwasimamia
wakandarasi wa miradi ya maji nchini, kwani Serikali imekuwa ikitenga kiasi
kikubwa cha cha fedha katika miradi ya Maendeleo pasipo na kupata matokeo
yaliyotarajiwa, na hivyo kuisababishia hasara Serikali.
“Kwa mujibu wa ripoti ya Wizara
ya Fedha na Mipango, miradi mingi ya maji imekuwa ikitumia fedha nyingi pasipo
na kupata matokeo yoyote na wataalamu wetu hasa wakandarasi wamekuwa wazito
kutoa tafsiri za nadharia za utaalamu na kuzileta katika nadharia halisi, na
mataifa ya nje yanashangwa tunaposhindwa kuvitumia vyanzo tulivyonazo ili
kuweza kuzalisha maji ya kutosha’ alisema Rais Magufuli.
Awali akizungumzia kuhusu ujenzi
wa barabara hiyo, Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Isack Kamwelwe alisema
kujengwa kwa barabara hiyo kutaimarisha mawasiliano katika ukanda wa kusini unaojumuisha
Mtwara, Mingoyo, Masasi, Mangaka, Tunduru hadi Mbamba Bay na hivyo kuzidi
kufungua fursa za kiuchumi nanchi jirani za Malawi na Msumbiji.
Alisema hadi kukamilika kwake barabara
hiyo imegharimu kiasi cha Tsh Bilioni 173, ambapo Shirika la Misaada la Japan
limetoa asilima 23.24, Benki ya Maendeleo ya Afrika asilimia63.32 na Serikali
ya Tanzania asilimia 13.35 ikiwemo kodi na kulipa fidia kwa wananchi
wanaostahili kwa mujibu wa sheria ya barabara ya mwaka 2007.
Naye Balozi wa Japan nchini
Tanzania, Shinichi Goto alisema Serikali ya Japan imekuwa mstari wa mbele
kuisaidia Tanzania kutekeleza miradi ya maendeleo ikiwemo barabara ya Namtumbo-Kilimasera-Matemanga- Tunduru
na itaendelea kusaidia miradi mingine ili kuhakikisha kuwa malengo ya Serikali
ya Awamu ya Tano ya kuondoa umaskini kwa wananchi wake yanafikiwa.
No comments:
Post a Comment