Mamlaka
ya Mapato Tanzania (TRA), imefanikiwa kukusanya jumla ya Shilingi
Trilioni 11.96 katika kipindi cha miezi Tisa ya mwaka wa Fedha 2018/19
ikiwa ni kuanzia Julai 2018 hadi Machi 2019.
Katika
robo ya tatu ya mwaka wa fedha 2018/19 TRA, ilifanikiwa kukusanya
Shilingi Trillioni 1.30 kwa mwezi wa Januari, Shilingi Trillioni 1.23
kwa mwezi wa Februari na kiasi cha Shilingi Trillioni 1.43 kwa mwezi wa
Machi, 2019.
Mamlaka
ya Mapato Tanzania inawashukuru walipakodi wote waliochangia makusanyo
hayo kwa kulipa kodi zao kwa hiari na kwa wakati na kuhimiza wale ambao
bado wanasuasua kujitokeza kulipa kodi hizo kwa wakati. TRA inaendelea
kuhimiza wananchi wote ambao wana changamoto za kikodi kutembelea ofisi
za TRA na kuonana na mameneja wa mikoa na wilaya kwa ufumbuzi wa
changamoto hizo.
Aidha,
katika kuongeza wigo wa kodi, TRA kwa sasa imeweka utaratibu wa
kurahisisha upatikanaji wa Namba ya Utambulisho wa Mlipakodi (TIN) kwa
kushirikiana na Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa (NIDA) ambapo TIN
inaweza kutolewa katika ofisi zote za TRA katika ngazi ya Mkoa na Wilaya
baada ya mwombaji kuwasilisha kitambulisho cha taifa au kwa kupata
namba ya kitambulisho wakati kitambulisho kikiendelea kushughulikiwa .
Sambamba na hilo TRA inaendelea kuhamasisha, kutoa elimu ya kodi na
kusajili walipakodi wapya katika mikoa, wilaya na vitongoji mbalimbali
nchini kote.
Wakati
huo huo, Mamlaka inapenda kuwakumbusha wamiliki wote wa majengo nchini
kujitokeza kulipia kodi za majengo haraka kuepuka usumbufu wa kulipa
mwishoni kwani kwa sasa viwango ni rafiki na vinalipika. Viwango hivyo
kwa mwaka ni Shilingi 10,000 kwa nyumba ya kawaida, Shilingi 50,000 kwa
kila sakafu nyumba ya ghorofa katika majiji, Manispaa na halmashauri za
miji na Shilingi 20,000 kwa jengo la ghorofa katika maeneo ya
halmashauri za wilaya.
Vile
vile, TRA inawaasa wale wote wanaojishughulisha na vitendo vya kughushi
risiti za kielektroniki za EFD nchi nzima kuacha mara moja kwa sababu
wakibainika watachukuliwa hatua za kisheria ikiwa ni pamoja na
kufikishwa mahakamani. Kila mwananchi na mfanyabiashara atambue wajibu
wake wa kudai risiti kwa kila manunuzi na kutoa risiti kwa kila mauzo.
Tunaendelea
kuwakaribisha wakazi wa Dar es Salaam kutembelea kituo cha ushauri kwa
walipakodi kilichopo katika makutano ya mitaa ya Samora na Bridge
katikati ya jiji, karibu na jengo TTCL. Pia wanaweza kupiga simu bure
namba 0800 750075 au 0800 780078 na kwa upande wa barua pepe tafadhali
tuandikie huduma@tra.go.tz. Vile vile, wanaweza kutuma ujumbe kupita
namba ya Whatsapp 0744 233 333.
Mkurugenzi
wa Huduma na Elimu kwa Mlipa kodi TRA, Richard Kayombo akitangaza
makusanyo ya yaliyopatikana kwa muda wa miezi 9 kwa waandishi wa habari
ambapo kiasi cha Trilioni 11.96 kimepatikana ikiwa ni makusanyo ya kodi
mbalimbali nchini mkutano huo umefanyika leo kwenye makao makuu ta TRA
Stesheni jijini Dar es Salaam.
Mkurugenzi
wa Huduma na Elimu kwa Mlipa kodi TRA, Richard Kayombo akifafanua jambo
kwa wanahabari leo wakati akitangaza makusanyo yaliyopatikana kwa muda
wa miezi 9 ambapo kiasi cha Trilioni 11.96 kimepatikana.(Picha na Emmanuel Massaka,MMG)
No comments:
Post a Comment